SOMO LA KUMI NA SABA

MANDHARI NA MUONEKANO WA WAKANUSHAJI NA MAKAFIRI.

Ashukuriwe na ahimidiwe Allah ambaye: “Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha akakuhukumieni ajali, na muda maalumu uko kwake tu. Tena baada ya haya nyinyi mnatia shaka”. Na rehema na amani zimshukie Mtume Muhammad; aliye mwisho wa Mitume na Manabii, na ziwaendee pia Aali zake, maswahaba wake na jamia ya wafuasi wao walio wafuata, wanao wafuata na watakao wafuata kwa wema hadi siku ya Kiyama.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Yaa Rabbi! Kama ulivyo tujumuisha tena katika jukwaa letu juma hili kwa uweza wako, tunakuomba kwa uweza wako huo uibariki milango yetu ya fahamu ili tuweze kuyafahamu na kukumbushika na haya uliyo tujaalia kukumbushana.

Mandhari ya wakanushaji na makafiri.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo hapo juu, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kukiangalia kipengele kingine kisomekacho:

  • Viza juu ya viza.

Naam, juma hili tena kwa kupitia Televisheni Qur’ani tunaendelea kuitazama na kuiangalia Mandhari ya wakanushaji na makafiri namna itakavyo kuwa hali yao tangu pale watakapo jiwa na Malaika wa mauti ili kuzitwaa roho zao na kurejeshwa kwa Mola Muumba wao wapate kulipwa kutokana na ukanushaji na ukafiri wao. Namna watakavyo toka makaburini mwao na watakavyo kuwa katika ardhi ya makusanyo mbele ya Mola Muumba wao waliye mkana na kumpinga hapa duniani.

Kila mmoja wetu sisi kusanyiko la Waislamu, anapaswa kuamini ya kwamba shida/matatizo yatakayo wapitia na kuwakumbuka makafiri hayatakuwa na ukomo aslan. Adhabu itawaganda na wala haitawabanduka abadan tangu kile kipindi watakacho jiwa na Malaika wa mauti mpaka pale watakapo vurumishwa ndani ya moto wa Jahannamu. Allah atuepushe sisi na nyinyi wadau wa jukwaa letu hili na adhabu chungu ya moto, itikia “Aaamin!”. Haya sasa,

  • Watazame hao wao makafiri wanatoka makaburini mwao katika hali ngumu sana ya udhalili na unyonge kama anavyo waelezea Allah aliye Mtukufu: “Siku watakapo toka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo. Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndio Siku waliyo kuwa wakiahidiwa”. Al-Ma’arij [70]:43-44
  • Si hivyo tu, bali wao watapiga mayowe ya kuangamia pale litakapo pulizwa parapanda na wakainuka kutoka makaburini, anasema Allah Ataadhamiaye: “Na litapulizwa baragumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi. Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume”. Yaasin [36]:51-52
  • Haya hao watazame wapo kwenye uwanja wa makusanyo wamekodoa macho na nyoyo zao zikiwa zimejaa utisho na shida zinazo wazunguka kwa pande zote, anasema Yeye aliye Mtukufu: “Wala usidhani Allah ameghafilika na wanayo yafanya madhaalimu. Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku yatapo kodoka macho yao. Nao wako mbioni, vichwa juu, na macho hayapepesi, na nyoyo zao tupu”. Ibraahim [14]:42-43
  • Na watakapo hudhurishwa mbele ya Allah, wataletwa katika hali ngumu sana ya udhalili na wakiwa wadogo mno, wamepigwa pingu, wamevikwa nguo za lami na nyuso zao zimegubikwa na moto, anasema Allah aliye Mtukufu: “Siku itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine, na mbingu pia. Nao watahudhuria mbele ya Mungu Mmoja, Mwenye nguvu. Na utaona wakhalifu siku hiyo wamefungwa katika minyororo. Nguo zao zitakuwa za lami, na moto utazigubika nyuso zao”. Ibraahim [14]:48-50
  • Siku ya Kiyama kafiri atajuta kwa ukafiri wake na umri wake alio upoteza kwenye shirki badala ya kuutumia katika neema ya Tauhidi na Imani, anasema aliye na utukufu na ukarimu: “Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume! Ee ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki. Amenipoteza, nikaacha ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli shetani ni khaini kwa mwanaadamu”. Al-Furqaan [25]:27-29
  • Siku hiyo kafiri atatamani Allah amuhilikishe na amfanye kuwa mchanga: “Siku hiyo walio kufuru na wakamuasi Mtume watatamani ardhi isawazishwe juu yao. Wala hawataweza kumficha Allah neno lolote”. An-Nisaa [04]:42

… na kafiri atasema: Laiti ningelikuwa udongo”. An-Nabaa [78]:40

  • Hali itazidi kuwa mbaya mno pale ambapo kafiri atakuta amali zake zimekuwa ni mavumbi yapeperushwayo na upepo, kama alivyo sema Allah Ataadhamiaye: “Na tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika”. Al-Furqaan [25]:23

Angalia basi, matendo ya makafiri yanagawanyika makundi mawili haya:

  1. Matendo ya batili yaliyo fisidika ambayo haitarajiwi kwayo kheri/manufaa yoyote, basi hayo ni viza juu ya viza, kama alivyo sema Allah aliye Mtukufu: “Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Allah hakumjaalia kuwa na nuru hawi na nuru”. An-Nuur [24]:40
  2. Matendo mazuri kama vile kutoa misaada, kuacha huru mtumwa, kuunga udugu na mengineyo kama hayo. Lakini matendo hayo mema hayatamfaa kwa sababu ule ukafiri wake umeyapomosha matendo yote hayo mema. Ni kwa ajili hiyo basi, ndio Allah akayashabihisha na mazigazi ambayo hayana hakika, Allah Mtukufu anasema: “Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Allah hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Allah ni Mwepesi wa kuhisabu”. An-Nuur [24]:39

Na mahala pengine akayafananisha matendo yao na majivu yanayo tapanywa na upepo kwa kiasi ambacho mwenye majivu yake hawezi kuyakusanya tena, akasema Yeye aliye na utukufu na ukarimu: “Mfano wa walio mkufuru Mola wao Mlezi – vitendo vyao ni kama jivu linalo peperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya mdharba. Hawawezi kupata chochote katika waliyo yafanya. Huko ndiko kupotelea mbali!”. Ibraahim [14]:18

Na mahala pengine akayamithilisha na upepo mkali wenye baridi kali, ambao unavumia kwenye mimea na matunda ukaviangamiza vyote, akasema Ataadhamiaye: “Mfano wa vile wanavyo vitoa katika uhai wao wa duniani ni kama upepo ambao ndani yake ipo baridi ya barafu, ukalisibu shamba la watu walio dhulumu nafsi zao, ukaliteketeza. Na Allah hakuwadhulumu, bali wao wenyewe wanadhulumu nafsi zao”. Aali Imraan [03]:117

Basi hao watakuja siku ya Kiyama nao wakidhania ya kwamba amali zao njema zitawanufaisha, mara tahamaki wanakuta matendo yao hayo yamekuwa ni mithili ya mavumbi peperushwa. Na wa mbele wao hao makafiri yarukao patupu matendo yao mema na kadhalika baadhi ya wale walio jinasibisha na Uislamu ambao walio mshirikisha Allah, anasema Allah Mwenye utukufu na ukarimu: “Sema: Je, tukutajieni wenye khasara mno katika vitendo vyao? Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri. Hao ni wale walio zikanusha ishara (Aya) za Mola wao Mlezi na kukutana naye. Kwa hivyo vitendo vyao vimepotea bure, na wala Siku ya Kiyama hatutawathamini kitu. Hiyo Jahannamu ni malipo yao kwa walivyo kufuru na wakafanyia kejeli ishara zangu na Mitume wangu”. Al-Kahfu [18]:103-106

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Yaa Allah! Wewe ndiye Mola Muumba wetu, uliye tuumba kwa uwezo wako na ukatukadiria umri wa kuishi katika hii ardhi yako. Tunakuomba kwa uwezo wako huo ulio tukuka, uturuzuku umri mrefu wenye siha njema katika kutenda mema yatufae leo kabla ya kesho tutakapo rudi kwako. Utupe mapenzi ya kweli katika kumpenda kipenzi chako Mtume Muhammad, turuzuku kumuiga na kumfuata haki ya kumfuata na tuwezeshe kuwapenda Aali Beit wake. Ewe Mwenye kujibu dua za waja wako, tutakabalie dua yetu!

Haya ndio tuliyo wezeshwa na Allah kukumbushana kwa juma hili, tulilo patia ni kwa uwezeshi wake Allah Mola Muwezeshi na tulilo kosea linatokana na mapungufu ya kibinaadamu, kwani ukamilifu ni wake Allah pekee. Tumuombe Allah atudumishie jukwaa letu hili, ili tuendelee kukumbushana kwa lengo la kupata nusura siku hiyo ya Kiyama.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine katika anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

Enyi mlio amini! Tubuni kwa Allah toba iliyo ya kweli. Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati yake, siku ambayo Allah hatamdhalilisha Nabii na walio amini pamoja naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za kulia, na huku wanasema: Mola wetu Mlezi! Tutimizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu”. At-Tahreem [66]:08

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *