SOMO LA KUMI NA NANE

MANDHARI NA VITISHO VYA SIKU YA KIYAMA.

Ametukuka ambaye mkononi mwake umo ufalme wote, na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha”. Na swala na salamu zimshukie Mtume wetu Muhammad bin Abdillah, jamaa zake na maswahaba wake na wote walio ufuata mwendo wake mpaka siku ya Kiyama.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Kabla ya lolote, tuendelee kuzielekeza shukurani za dhati zenye kusuhubiana na taadhima pamoja na unyenyekevu mkubwa kwa Allah ambaye Yeye ndiye anaye tuwezesha kuungana nawe katika ukumbi wetu huu ili tupate kukumbushana. Tumuombe Allah atudumishie neema hii na atuwezeshe kuishukuru kwa kuyatendea amali yale anayo tuwafikisha kukumbushana, kwani hiyo ndio namna bora kabisa ya kuishukuru neema.

Naam, jukwaa letu la leo, litaendelea kuongozwa na anuani mama kama inavyo someka mbele yetu:

Mandhari na vitisho vya siku ya Kiyama.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kuishi na kukiangalia kipengele kingine kinacho someka:

  • Ujio/kuletwa kwa Jahannamu.

Hebu ewe ndugu yetu-Allah akurehemu-itafakari kwa kina hali ya watu wakiwa wamesha kimwa na kutaabishwa na vitisho na vitetemeshi vya Kiyama kwa kiasi kikubwa. Sasa wakati wao wakiwa kwenye taabu hiyo, hali ya kuwa wamesimama wakisubiri kujua hatima yao na wakitamani kupata uombezi wa waombezi ili asaa wakapata msamaha wa Allah. Ni katika hali hiyo tahamaki wakosefu/watenda dhambi watazungukwa na viza vyenye mapande matatu na watafunikwa na moto wenye mwako mkali na watausikia ukitoa muungurumo wa kutosha kabisa kutoa roho kabla hata ya kutiwa humo. Hapo ndipo wale watu wakosefu watayakinisha kuwa sasa tumekwisha/tumeangamia na watapiga magoti ya mtu aombaye kusamehewa. Ni katika kitatange hicho atatoka mmojawapo wa Mazabania (Malaika wa adhabu) aulize: Yuko wapi fulani bin fulani ambaye hakutenda amali njema duniani kwa sababu ya mipango yake mingi ya muda mrefu na akaupoteza umri wake katika kutenda matendo maovu? Basi hapo Mazabania watamrukia na marungu ya chuma na kumpeleka kwenye adhabu chungu na kumvurumishia kwenye kina cha Jahannamu na wamwambie: “Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu!”. Ad-dukhaan [44]:49

Basi wapewe maskani kwenye nyumba iliyo finyu na yenye kiza, wakae humo milele wakiwa wafungwa. Wawashiwe humo moto, kinywaji chao humo ni maji ya moto yenye kutokota na makaazi yao ni ndani ya moto wa Jahimu wakishushiwa kipondo cha nguvu na Mazabania. Humo wao hawatatoka wala kuachiliwa, miguu yao ikiwa imefungwa kwenye tosi zao, nyuso zao zikipiga weusi kutokana na kiza cha madhambi. Basi wapige mayowe na ukelele kutokana na ukali wa adhabu, waseme: Ewe Mfalme wa siku hii ngumu! Yametuthibitikia makamio yako, yametuhemeza marungu ya chuma, zimechomeka hadi kuiva ngozi zetu, tunaomba ututoe humu na hatutarudia tena kukuasi. Wajibiwe na Mazabania: Aaah wapi! Li mbali mno hilo mliombalo! Nyinyi hamna kutoka kwenye nyumba hiyo ya udhalili. Basi hawataokolewa na majuto wala hawatasaidiwa na sikitiko lao, bali wao wataghariki ndani ya moto, humo chakula chao ni moto, maji yao ni moto, mavazi yao ni moto na malalo yao ni moto. Moto uwachemshe mchemsho wa vyungu na kila watakapo omba bora wafe, watamiminiwa juu ya vichwa vyao maji yanayo chemka, kwa maji hayo vitayayushwa viliomo matumboni mwao, na ngozi zao pia. Na ni yao humo marungu ya chuma, yapasuliwe kwa marungu hayo mapaji yao, uchimbuke usaha kutoka vinywani mwao na maini yao yakatike katike kutokana na ukali wa kiu. Na kila zitakapo iva ngozi zao kutokana na ukali wa moto, watabadilishiwa ngozi nyingine ili waendelee kuonja adhabu chungu. Hizo ni baadhi tu ya hali za watu wakosefu; watu walio muasi Mola Muumba wao katika nyumba hii ya mpito, watu wa motoni. [IHYAAU ULUUMID-DIIN 04/563-564]

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Italetwa Jahannamu ikiwa na hatamu sabini elfu, kila hatamu ina malaika sabini elfu wanao ikokota (hiyo Jahannamu)”. Muslim [SAHIH AL-JAAMI’I 8001]-Allah amrehemu.

Heeh! Mandhari na mtazamo uogofyao ulioje! Mandhari inayo zitatua tatua nyoyo. Hapo itakapo letwa Jahannamu, hatobakia Malaika mkurubishwa wala Nabii mtumilizwa ila atakita magoti chini na aseme: Ewe Mola wetu Mlezi! Tunaomba salama, salama yako. Allah Ataadhamiaye anasema: “Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande. Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu. Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini? Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu!”.

Hebu tuyazingatie pamoja majuto hayo makubwa kwa kila aliye chupa mipaka katika haki ya Allah na akaiona Jahannamu, hakika atapiga kelele na atasema: (Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu), hilo ni neno atakalo lisema kila aliye:

  • Puuzia swala, akaacha kumsujudia Mola wake.
  • Wakata pande na kuwaasi wazazi wake.
  • Wadhulumu waja wa Allah kwa aina iwayo ya dhulma.
  • Acha hijabu, akatoka nje kichwa wazi, akionyesha mapambo yake, akiisahau kauli yake Allah Ataadhamiaye: “Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Allah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu”. Al-Ahzaab [33]:59

Na akilisahau neno lake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Mbeya (aina) mbili za watu bado sijaziona; watu wenye bakora kama mikia ya ng’ombe, wanawapiga watu kwazo. Na wanawake walio vaa lakini wako uchi, wenye kupondosha (wanaume), walio pinda kitabia. Vichwa vyao ni kama nundu za ngamia (kutokana na mitindo yao ya kuunga nywele) zilizo inamia nyuma. Hao hawataingia peponi na wala hawatainusa harufu yake na hakika harufu yake inapatikana kutokea umbali wa mwendo kadha na kadha”. Muslim [SAHIH AL-JAAMI’I 3799]-Allah amrehemu.

Eeh! Ewe dada yangu, hivi bado tu haujafika wakati wewe:

  • Kuvaa hijabu yako ili ikawe ni kinga yako itakayo kuepusha na adhabu ya moto?!
  • Kuvaa nguo za sitara na zenye staha na kujiepusha na machafu?!
  • Kufuata amri za Allah Mola Muumba wako na Mtume wa Allah ili uepuke kuwa miongoni mwa watu wa motoni ambao Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amewataja katika hadithi tuliyo kunukulia hapo juu?!

Hakika maneno haya tunayaelekeza kwenye sikio la kila binti wa Kiislamu ambaye anamuamini Allah na siku ya mwisho. Eeh! Ewe dada yangu wee! Iokoe nafsi yako kutokana na moto kabla hujapiga mayowe na kusema: (Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu). Bado hujachelewa, muda wa kuwa u hai bado unayo fursa, ipatilize fursa hiyo kabla haijakupita. Rejea kwa Mola wako sasa, tubia kwa makosa na madhambi yote uliyo kwisha yatenda, chapusha hatua kuelekea kwake na ulimi wa hali yako useme kama alivyo sema Nabii Musa-Amani imshukie: “… Na nimefanya haraka kukujia Mola wangu Mlezi, ili uridhie”. Twaaha [20]:84

Na usujudu mbele ya Mola wako na umuombe maghufira na rehema zake, kwani kumbuka ni Yeye ndiye anaye sema: “Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu!”. Al-Hijri [15]:49-50

Eeh! Ewe ambaye unaye wadhulumu na kuwaonyesha umwamba waja wa Allah, unawaambia kwa kinywa kipana kabisa: Unajua mimi nani? Wewe nitakupoteza! Weee usinichezee, nitakupoteza! Unaonyesha umwamba na hata kudhulumu kupitia mali/madaraka uliyo nayo. Acha mara moja na wala usiisahau ile mandhari ya kuogofya siku ile itakapo letwa Jahannamu. Rudi kwa Mola wako na utubie na urejeshe ulivyo wadhulumu watu na uwaombe wakusamehe leo kabla haijafika siku hiyo ukapiga mayowe na kusema: (Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu). Ukajuta, wakati ambao majuto hayatafaa kitu na wala hayatakuondoshea adhabu chungu ya Mola Muumba wako.

Ewe ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-ni dhana yetu kwamba kwa maelezo yetu haya na nassi tulizo kunukulia, utakuwa umekiona kitisho, kishindo na timbwili la ujio wa Jahannamu na shida/dhiki zitakazo wagubika watu. Sasa basi pamoja na yote hayo, litakuwepo pote tukufu litakalo kuwa chini ya jivuli la Arshi ya Ar-Rahmaan – Mwingi wa rehema. Pote hilo ndilo analo litaja Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kupitia kauli yake hii: “Mbeya saba za watu, Allah ataziweka chini ya kivuli chake katika siku ambayo hapatakuwa na kivuli ila kivuli chake (tu);

  1. Imamu muadilifu,
  2. Kijana aliye inukia katika kumuabudu Allah,
  3. Mtu ambaye moyo wake umefungamana na msikiti atakapo toka humo mpaka arudi tena,
  4. Watu wawili walio pendana kwa ajili ya Allah, wamekutana kwa ajili hiyo na wametengana kwa hilo,
  5. Mtu aliye mdhukuru Allah faraghani, yakafurika machozi macho yake,
  6. Mtu aliye itwa na mwanamke mtukufu na mrembo (kutenda naye zinaa), akasema: Hakika mimi ninamuogopa Allah; Mola Mlezi wa walimwengu wote, na
  7. Mtu aliye toa sadaka kwa uficho mkubwa kiasi cha mkono wake wa kushoto kutokujua kilicho tolewa na mkono wa kulia”. Bukhaariy & Muslim [SAHIH AL-JAAMI’I 3603] – Allah awarehemu.

Faida: Tufahamu sote kwamba huko kuwekwa chini ya kivuli cha Allah hakukomelei tu kwa mbeya hizo saba za watu zilizo tajwa na Hadithi hiyo tuliyo inukuu punde tu. Katika hadithi nyingine Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amewataja watu wengine ambao watakao kuwa chini ya kivuli cha Arshi ya Allah, akasema:

  • Hakika Allah Ataadhamiaye atauliza siku ya Kiyama: Wako wapi wale walio pendana kwa utukufu wangu, leo nitawaweka chini ya kivuli changu katika siku ambayo hapana kivuli chochote ila kivuli changu (tu)”. Muslim & Ahmad [SAHIH AL-JAAMI’I 1915]-Allah awarehemu.
  • Atakaye mpa mtu mtwefu (aliye haribikiwa na mambo; hana kitu) muda (wa kulipa deni alilo kopa kwake) au akamfutia kabisa deni, (huyo) siku ya Kiyama Allah atamuweka chini ya kivuli cha Arshi yake, siku ambayo hapatakuwepo na kivuli chochote ila kivuli chake Yeye (tu)”. Ahmad & Tirmidhiy [SAHIH AL-JAAMI’I 6107]-Allah awarehemu.
  • Yeyote atakaye mpa muda (muongezea muda wa kulipa deni) mdeni wake au akamfutia deni, (huyo) atakuwa chini ya kivuli cha Arshi siku ya Kiyama”. Muslim & Ahmad [SAHIH AL-JAAMI’I 6576]-Allah awarehemu.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-jua la Kiyama si mchezo, watu wataogelea kwenye jasho lililo vuja miilini mwao kwa kiasi cha madhambi waliyo yatenda. Nafasi ya kuokoka na jua hilo bado ingalipo muda wa kuwa u hai, uchaguzi ni wako wewe, chagua kundi kati ya hayo uvuke nalo.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Ewe ambaye uliye mpa mwanaadamu matashi na hiari ya kutenda na kutotenda! Ewe ambaye uliye mpa mwanaadamu akili ya kutambua zuri na baya! Tunakuomba kwa uwezo wako huo mkuu, utuwezeshe kutenda yale unayo yaridhia na kuyaepuka yale unayo yachukia. Utubarikie katika maisha yetu yote na kila ulicho tumilikisha kwa ukwasi na utajiri wako. Yaa Rabbi tutakabalie dua!

Jukwaa letu kwa juma hili linakomea hapa. Ukamilifu ni wake Mola Muumba ikiwa mmenufaika nalo, na mapungufu ni yetu sisi waja kwa kushindwa kufikia malengo. Tuendelee kumuomba Allah alibariki jukwaa letu, lifikie malengo ya kuanzishwa kwake, kwani Yeye tu ndiye Muwezeshaji Mkuu.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine katika anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

سَابِقُوا إِلَى مَغْفِرَةٍ مِنْ رَبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا كَعَرْضِ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أُعِدَّتْ لِلَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّهِ وَرُسُلِهِ ذَلِكَ فَضْلُ اللَّهِ يُؤْتِيهِ مَنْ يَشَاءُ وَاللَّهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ٢١ [الحديد: 21]

Kimbilieni msamaha wa Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyo wekewa walio muamini Allah na Mitume wake. Hiyo ndio fadhila ya Allah, humpa amtakaye. Na Allah ni Mwenye fadhila kuu”. Al-Hadiid [57]:21

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *