SOMO LA KUMI NA NANE-01

MANDHARI NA MUONEKANO WA WATENDA MAASI SIKU YA KIYAMA”

Sifa zote njema zimuendee Mola Mlezi wetu kwa Hidaya zake za wazi na zilizo fichikana azitoazo wakati wote, ambaye ni Yeye ndiye: “Anaye samehe dhambi na anaye pokea toba, Mkali wa kuadhibu, Mwenye ukarimu, hakuna Mungu ila Yeye; marejeo ni kwake”. Na Baraka na Amani zimuendee Nabii wake Muhammad, Aila yake na Maswahaba wake ambao walijitolea kwa mali na nafsi zao katika kuitumikia Dini ya Allah na wote walio wafuata wao mpaka siku ya Kiyama.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Naam, ni juma jingine tena Allah Mtukufu, Muumba uhai na umauti, kwa ukarimu na fadhila zake anakutanisha tena katika ukumbi wetu huu ambao malengo na madhumuni yake makuu ni kukumbushana. Tunamshukuru kwa neema hii ya kutukutanisha katika jambo hili la kheri, na tunamuomba azidi kuyakunjua maarifa na ufahamu wetu ili tuzidi kuitekeleza amri yake ya kukumbushana. Pia tunamuomba aibariki juhudi yetu hii na aijaalie iwe ni kwa ajili tu ya kutaraji radhi zake.

Kuanzia juma na majuma kadhaa baada ya leo, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mkarimu, katika jukwaa letu hili, tutaishi na maudhui inayo beba anuani hii:

Mandhari na muonekano wa watenda maasi/dhambi.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-bado tunaendelea kuiangalia siku ya Kiyama na hali za watu katika siku hiyo ngumu, kupitia televisheni Qur’ani. Kupitia onyesho letu la juma hili na kuendelea mpaka pale litakapo malizika, litatuonyesha ya kwamba sote sisi tunapaswa kujua kwa yakini hakuna dhambi yoyote atakayo itenda mwanaadamu ila mwisho wake utakuwa ni majuto duniani na akhera. Katika makala hizi tutayatupia macho baadhi ya madhambi ambayo yatamletea mtendaji wake majuto siku ya Kiyama. Lengo la kuyataja madhambi hayo ni ili tupate kutahadhari nayo na kuyahepa leo duniani tukapate salama na kusalimika na majuto katika siku ya Kiyama.

Anasema Imamu Abu Haamid-Allah amrehemu-katika kitabu chake (KASHFU ILMUL-AAKHIRAH): “Wako watu watakao fufuliwa wakiwa na fitina zao za duniani, wako walio kuwa wamefitinika na upigaji wa udi/kinanda (muziki) maisha yao yote. Basi mmojawapo atakapo inuka kutoka kaburini mwake atakichukua kinanda chake kwa mkono wake wa kulia, akitupe na aseme (kukiambia): Uangamie mbali! Umenishughulisha na dhikri ya Allah. Basi kinanda kitamrudia na kimwambie: Mimi ni mwenzako (nitaambatana nawe) mpaka atakapo hukumu Allah baina yetu na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu. Na hali kadhalika mlevi atafufuliwa akiwa amelewa, mpiga zumari na zumari yake na kila mmoja atakuwa katika hali/jambo lililo mzuilia na njia (dini) ya Allah.

Akasema (Imamu): Na ni mithili ya hadithi iliyo pokewa kwenye Bukhaariy ya kwamba mnywaji wa pombe atafufuliwa na kuguduria/chupa (ya pombe) ikiwa imetundikwa shingoni mwake na bilauri mkononi mwake. Naye akinuka harufu mbaya kuliko mizoga yote iliyo juu ya ardhi na atalaaniwa na kila kiumbe anaye pita karibu yake”. [Nukuu kutoka kwenye kitabu AT-TADHKIRAH cha Imamu Qurtubiy 01/395]-Allah amrehemu.

Naam, haya sasa na tuanze kuyaangalia hayo baadhi ya madhambi yatakayo mtia mtendaji wake majuto siku ya Kiyama, tukianza na:

  • Anaye ua pasina haki.

Hakika siku ya Kiyama atakuwa na majuto yasiyo mithilika kila ambaye aliye muua mtu pasina haki; kwa dhulma, kwani Allah Mtukufu amekwisha sema: “Na mwenye kumuua muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na Allah amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa”. An-Nisaa [04]:93

Na akasema tena Yeye aliye Mtukufu: “Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote…”. Al-Maaidah [05]32

Ama majuto ya muuaji pasina haki kesho akhera, hayo yamekwisha elezwa na yule aliye Mkweli Muaminifu-Rehema na Amani zimshukie: “Wachukivu mno kuliko watu wote kwa Allah ni mbeya (aina/makundi) tatu – na akataja miongoni mwao – na mwenye kutaka damu ya mtu mwingine pasina haki ili apate kuimwaga damu yake”. Bukhaariy [SAHIH AL-JAAMI’I 40]-Allah amrehemu.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-ujue na utambue kupitia kauli za Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-muuaji kwa dhulma ni mtu anaye chukiwa mno miongoni mwa watu duniani na akhera. Ama taswira ya pili ya majuto ya muuaji dhaalimu siku ya Kiyama, anatusawirishia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa kusema: “Muuliwa (kwa dhulma) atakuja na muuaji wake siku ya Kiyama ilhali akiwa ameshika utosi na kichwa chake mkononi na mishipa yake ya shingo ikichuruzika damu, aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Hebu muulize huyu aliniua kwa sababu gani? Mpaka amlete karibu na Arshi”. Tirmidhiy & Nasaai [SAHIH AL-JAAMI’I 8031]-Allah amrehemu.

Amesema Imamu Ibnu Al-Arabiy-Allah amrehemu: “Yamethibiti makatazo na makamio (ya adhabu) katika kumuua mnyama pasina haki. (Ikiwa hali ni hiyo kwa mnyama), itakuwaje kwa kumuua mwanaadamu?! Itakuwaje ikiwa mwanaadamu huyo ni muislamu na itakuwaje ikiwa mwanaadamu huyo ni mtu mchaMngu aliye mwema!”. [FAT-HUL-BAARIY 12/196]-Allah amrehemu.

  • Wale wanao kula riba.

Eeh! Majuto yaliyoje siku ya Kiyama kwa mtu aliye acha biashara ya halali na badala yake akajitumbukiza kwenye miamala ya riba aliyo iharimisha Allah Mwenye utukufu na ukarimu. Ama majuto yake duniani, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anayaelezea kwa kauli yake: “Allah amemlaani mla riba, mlisha riba, mashahidi wake na muandishi wake, wao wote katika madhambi ni sawa sawa”. Muslim & Ahmad [SAHIH AL-JAAMI’I 5090]-Allah amrehemu.

Na akasema Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Dirham moja ya riba anayo ila mtu ilhali akijua, (dhambi zake) ni kubwa mno mbele ya Allah kuliko zinaa thelathini na sita”. Ahmad & Twabaraaniy [SAHIH AL-JAAMI’I 3375]-Allah amrehemu.

Na amesema: “Riba ina milango sabini na mbili, wa chini yake (madhambi yake) ni kama mtu kulala na mama yake mzazi. Na hakika riba kubwa kuliko zote, ni mtu kufanya uadui katika heshima ya ndugu yake”. Twabaraaniy [SAHIH AL-JAAMI’I 3537]-Allah amrehemu.

Si hivyo tu, bali riba itakapo tangaa na kuenea katika jamii, bila ya shaka jamii hiyo imekwisha jihalalishia yenyewe kufikwa na adhabu ya Allah Mola Muumba wao, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Itakapo dhihiri zinaa na riba katika kitongoji, hakika bila ya shaka (watu wa kitongoji hicho) wamekwisha jihalalishia adhabu ya Allah”. Twabaraaniy [SAHIH AL-JAAMI’I 679]-Allah amrehemu.

Naam, ama majuto ya mla riba kaburini, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema katika sehemu ya hadithi ndefu: “…Basi tukaenda tukafika kwenye mto – nadhania yeye alikuwa akisema: “(mto huo) ni mwekundu mithili ya damu” – tahamaki mtoni humo yumo mtu anaogelea. Na tahamaki ukingoni mwa mto kuna mtu amekusanya mawe mengi. Yule muogeleaji ataogelea kiasi atakacho ogelea, kisha atamuendea yule aliye kusanya mawe, ataachama mdomo, yule (mwenye mawe) atamrushia jiwe. Ataondoka zake akiogelea kisha atarudi (tena) kwake (yule mwenye mawe) na kila akirudi huachama mdomo wake, na yule akamsokomeza jiwe”.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo uliza: Ni kina nani wawili hawa? Akajibiwa: “Ama yule mtu uliye mpitia akiogelea mtoni na akisokomezwa jiwe , hakika huyo ni mla riba”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Hiyo ndio adhabu yake kaburini. Ama kuhusiana na adhabu na majuto yake siku ya Kiyama, Allah amesema: “Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama yule aliye zugwa na shetani kwa kumgusa…”. Al-Baqarah [02]:275

Yaani: Hakika walaji wa riba siku ya Kiyama watainuka kutoka makaburini mwao kama mtu aliye pagawa kutokana na kukumbwa na shetani. Anasema Ibnu Abbas-Allah amuwiye radhi: “Mla riba atafufuliwa siku ya Kiyama akiwa mwendawazimu anaye jikaba shingo”.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Mola wetu Mtukufu kwa rehema zako tunakuomba utupe Amani na Salama katika:

Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru, nao watapata laana, na watapata makaazi mabaya kabisa”. Al-Ghaafir [40]:52

Jukwaa letu juma hili linatamatia hapa ili kutoa fursa kwa kila mwenye moyo wa kukumbuka, akumbuke, awaidhike na kisha aanze kujiandaa na siku iliyo ahidiwa ya Kiyama kwa kufuata maamrisho ya Mola wake na kuyaacha yale makatazo.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine chini ya anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

Na likumbuke jina la Mola walo Mlezi asubuhi na jioni. Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati mrefu”. Al-Insaan [76]:25-26

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *