SOMO LA KUMI NA TISA

MANDHARI YA WAKANUSHAJI NA MAKAFIRI.

Kila sifa kamali zinamstahikia Allah Mtukufu, aliye sema katika kitabu chake kitukufu: “Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na dini ya haki, ili aitukuze juu ya dini zote. Na Allah anatosha kuwa Shahidi”. Na tunamuombea Rehema na Amani Bwana wetu mpenzi; Mtume Muhammad, Bwana aliye tufunza namna bora ya kuhubiri Dini ya Allah. Hali kadhalika tunawaombea Rehema na Amani jamaa zake, maswahaba wake na jamia ummati Muhammad mpaka siku ya hisabu na jazaa.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Ndugu mwana jukwaa letu-Allah akurehemu. Kwa msaada na uwezeshi wake Mola tumekutana tena katika ukumbi wa jukwaa kumbushi letu la kila juma, tumepewa tena fursa hii ili tuendelee kukumbushana kuhusiana na siku inayo tujongelea mno; siku ya Kiyama. Tukumbushane chini ya kivuli cha maneno ya Allah na yale ya yule mwanaadamu aliye Mkweli Muaminifu kwa lengo lile lile la kuwaidhika na kujiandaa kwa kutenda amali njema ili tupate salama na nusra katika siku hiyo.

Hili ndilo somo litakalo tuongoza leo katika kuendelea kujuzana yale yanayo fungamana na siku ya Kiyama:

Mandhari ya wakanushaji na makafiri.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaanza kuishi na kukiangalia kipengele kifuatacho:

  • Mushirikina na mandhari ya majuto:

Ni ukweli, tena ni ukweli mtupu, na kisha ni ukweli usio pingika kwamba siku ya Kiyama kila aliye ondoka duniani ilhali akiwa anamshirikisha Allah Ataadhamiaye, atakuwa kwenye majuto, majuto yanayo bebwa na dhana nzima ya neno hilo. Huyo mushiriki ni yule ambaye alikuwa akiomba na kutaka msaada kwa wanaadamu wenzake; hajapata mtoto, hana kazi, maradhi yamemuegama anaenda kwa mganga ampe toto, ampe kazi, amponye. Akimuacha Mola Muumba wake ambaye Yeye ndiye huwapa waja wake watoto, tumsikilize akilitangaza hilo: “Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Allah; anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza”. As-shuura [42]:49-50

Akamuacha Mola Muumba wake ambaye Yeye ndiye Mtoa riziki kwa viumbe wake wote: “Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Allah. Naye anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha”. Huud [11]:06

Mushirikina atakaye kuwa na majuto yasiyo faa kwa chochote wala lolote siku ya Kiyama, huyo ni yule ambaye anamchinjia mzimu/jini/mti/pango mnyama aliye ruzukiwa na Allah eti ili apate ponyo la maradhi yake kutoka kwake, au apate ajira, apate mume/mke na… na… Na huyo ndiye yule anaye kwenda kuweka nadhiri pangoni/mzimuni au kwa jini ya kwamba akipata analo litaka, basi atamfanyia mzimu/jini huyo kadha wa kadha. Huyo ni yule ambaye anaitakidi kabisa ya kwamba kuna kiumbe anaye weza kumnufaisha au kumdhuru bila ya iraada ya Allah. Huyo ni yule ambaye anaye itakidi kwamba kuna mungu mwingine pamoja na Allah, au kuna mungu mwana, mungu baba na roho mtakatifu, au mungu ana mtoto, akaishi maisha yake yote hapa ulimwenguni katika itikadi hiyo hata mauti yakamkuta naye akiwa hivyo hivyo. Akawa amejivua mwenyewe vazi la Imani alilo umbiwa nalo na mahala pake akajivika vazi la upingaji na ukafiri. Huyo ndiye mtu ambaye atakaye ikosa neema ya kuwa karibu na Ar-Rahman – Mwingi wa rehema na ataishi maisha ya udhalili na unyimwa hata kama utamuona ana utajiri/madaraka. Hakika hayo ni majuto yaliyoje pale watakapo toka washirikina makaburini mwao wakiwa na hali hiyo tunayo sawirishiwa na Qur’ani: “Siku watakapo toka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo. Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndio Siku waliyo kuwa wakiahidiwa”. Al-Ma’arij [70]:43-44

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Allah atawakusanya watu siku ya Kiyama katika uwanda mmoja. Kisha Mola Mlezi wa viumbe wote atawachomozea na kuwaambia: Ehee! Kila mtu akifuate alicho kuwa akikiabudu. Basi mtu wa msalaba atamithilishiwa msalaba wake (akauabudu), muabudu sanamu naye atamithilishiwa sanamu lake (akaliabudu) na muabudu moto naye atamithilishiwa moto wake (akauabudu). Basi wavifuate walivyo kuwa wakiviabudu na (hapo) watabakia Waislamu, awachomozee Mola Mlezi wa viumbe wote…”. Tirmidhiy [SAHIH AL-JAAMI’I 8025]-Allah awarehemu.

Baada ya hapo, washirikina wataiita miungu yao hiyo waliyo kuwa wakiiabudu, ili iwasaidie basi haitawajibu wala kuwaitika: “Na siku atakapo sema (Allah): Waiteni hao mlio dai kuwa ni washirika wangu. Basi watawaita, na wao hawato waitikia. Nasi tutaweka baina yao maangamio. Na wakhalifu watauona moto na watajua ya kwamba wao lazima wataingia humo; wala hawatapata pa kuuepuka”. Al-Kahfi [18]:52-53

Na hatima yake, moto wa Jahannamu utawakusanya hao washirikina na miungu yao, kama anavyo sema Allah aliye Mtukufu: “Hakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya Allah ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu. Lau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote watadumu humo. Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia (jenginelo)”. Al-Anbiyaa [21]:98-100

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Allah atakapo wakusanya wale wa mwanzo (kuumbwa) na wale wa mwisho (kuletwa duniani) katika ile siku isiyo na shaka ndani yake, ataita mwenye kuita (aseme): Yeyote aliye mshirikisha mwingine katika amali aliyo itenda kwa ajili ya Allah, basi na aende akatafute thawabu zake kwake huyo. Kwani hakika Allah ni Mkwasi mno wa washirika kushirikishwa naye”. Ahmad & Tirmidhiy [SAHIH AL-JAAMI’I 482]-Allah awarehemu.

Na akasema tena: “Hakika ninacho kiogopea mno kwenu kuliko vingine ni shirki ndogo; riyaa. Pale Allah atakapo walipa watu jazaa ya amali zao siku ya Kiyama, atasema: Nendeni mkachukue jazaa yenu kwa wale mlio kuwa mkiwaonyesha matendo yenu duniani, katizameni je mtapata kwao hayo malipo”. Ahmad [SAHIH AL-JAAMI’I 1555]-Allah amrehemu.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Mola wetu Mtukufu kwa rehema zako tunakuomba utupe Amani na Salama katika:

يَوْمَ يَجْمَعُ اللَّهُ الرُّسُلَ فَيَقُولُ مَاذَا أُجِبْتُمْ …١٠٩ [المائدة: 109]

Ile siku ambayo Allah atapo wakusanya Mitume awaulize: Mlijibiwa nini?…”. Al-Maaidah [05]:109

Hapo tulipo fikia, ndio mwisho wa tuliyo jaaliwa kukuletea katika jukwaa letu juma hili. Tumuombe Allah; Mola Mtukufu aturuzuku uhai na uzima ili tuweze kukutana tena juma lijalo tupate kuendelea na makumbusho haya, asaa akapatikana mwenye kukumbuka.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine katika anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱتَّقُواْ ٱللَّهَ وَلۡتَنظُرۡ نَفۡسٞ مَّا قَدَّمَتۡ لِغَدٖۖ وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَۚ إِنَّ ٱللَّهَ خَبِيرُۢ بِمَا تَعۡمَلُونَ ١٨ وَلَا تَكُونُواْ كَٱلَّذِينَ نَسُواْ ٱللَّهَ فَأَنسَىٰهُمۡ أَنفُسَهُمۡۚ أُوْلَٰٓئِكَ هُمُ ٱلۡفَٰسِقُونَ ١٩

Enyi mlio amini! Mcheni Allah, na kila nafsi iangalie inayo yatanguliza kwa ajili ya kesho. Na mcheni Allah. Hakika Allah anazo khabari za mnayo yatenda. Wala msiwe kama wale walio msahau, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio wapotovu”. Al-Hashri [59]:18-19

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *