“MANDHARI NA MUONEKANO WA WATENDA MAASI SIKU YA KIYAMA”
Kuhimidiwa na kutukuzwa kunamstahikia Allah; Mola Mlezi wa viumbe wote, ambaye ndiye aliye muambia Mtume wake: “Na waonye siku inayo kurubia, wakati nyoyo zitakapo fika kooni, nao wamejaa huzuni. Madhaalimu hawatakuwa na rafiki, wala mwombezi wa kuitikiwa”. Na Rehema na Amani zimuendee Bwana wa ulimwengu; Mtume wetu Muhammad. Na ziwaendee pia Aali na swahaba zake kila mara na kila wakati.
Ama baad,
Mpendwa mwana-jukwaa letu.
Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!
Jukwaa hili halipungui kuwa ni neema ambayo sote tunalazimika kumshukuru Allah kwa kutukirimu neema hii. Hivyo basi ni wajibu wa kila mmoja wetu kuitumia vema neema hii, kwa kuwa tayari kukumbushwa na kisha akayatendea amali yale aliyo kumbushwa kwa ajili ya maslahi na manufaa yake mwenyewe katika dini, dunia na akhera yake.
Haya sasa karibu tuendelee na jukwaa letu la juma hili, ambalo bado liko chini ya maudhui mama yenye anuani isomekayo:
Mandhari na muonekano wa watenda maasi/dhambi.
Kwa uwezeshi wake Mola wetu Mtukufu, ni juma jingine tena bado tunaendelea kuishi na kuyaangalia yale madhambi yatakayo mletea mja kujuta na kusaga meno siku ya Kiyama, na kama tulivyo tangulia kusema juma la jana, lengo la kuyataja madhambi hayo ni ili tupate kuyahepa na kujitenga nayo, asaa kesho mbele ya Mola wetu Mkarimu na Mrehemevu mno, tukasalimika na adhabu iliyo chungu, kali na kubwa mno kuweza kuhimiliwa na mwanaadamu aliye dhaifu kwa kila hali.
Na leo chini ya mada kuu hiyo hapo juu, tutaishi na kuiangalia dhambi:
Wale wasio toa zaka (kutokutoa zaka):
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tunaamini kila mmoja wetu anaiona hali ya jamii yetu leo. Kila mmoja anaamini ya kwamba kile anacho kimiliki amekipata kwa sababu ya elimu yake, nguvu zake, juhudi zake, ujanja wake au akili zake.
Na yule asiye na kitu basi jamii inamuona kuwa ni mjinga, hana elimu, mvivu, hana akili na hataki kufanya kazi. Ni imani, mawazo na fikra hizo ndizo zimetufikisha kusahau ya kwamba si juhudi, ujanja, nguvu wala akili zetu ndizo zinazo tupa riziki iwe nyingi au kidogo.
Kwani ni wangapi wana elimu kuliko sisi, wana nguvu kuliko sisi, wana juhudi kuliko zetu, lakini wote hao hawana mali au kipato kikubwa kama tulicho nacho sisi bali wengine tumewaajiri sisi katika miradi yetu. Tumesahau kabisa ya kwamba: “Hakika Allah ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti”. Ad-Dhaariyaat [51]:58
Pia tumesahau au tumejisahaulisha kabisa ya kwamba:
“Allah ni Mpole wa waja wake. Humruzuku ampendaye. Naye ni Mwenye nguvu, Mtukufu”. As-Shuura [42]:19
Sasa basi, ni kujighafilisha huko ndiko kumetupelekea kuwa na ubakhili, unyimi na uchoyo hata tukaona si wajibu kutoa sehemu kiduchu katika vile alivyo turuzuku Mola wetu kuwapa waja wake alio tuamrisha kuwapa.
Ni kweli kabisa, kutokutoa zaka na kuacha kuitekeleza nguzo ya tatu hiyo ya Uislamu; ambayo ni nguzo pacha na swala, kwani kila ilipo tajwa swala pametajwa pamoja nayo zaka, limekuwa ni jambo la kawaida kabisa. Na wala mtu hajui kwamba hiyo ni dhambi, tena ni dhambi itakayo mpelekea kujuta mno siku ya Kiyama.
Wapo wengine wanao toa zaka, lakini wanasahau ya kwamba zaka ni ibada na kama ni ibada basi ni lazima itekelezwe kama alivyo amrisha Mola na kufundishwa na Mtume wake.
Wanasahau ya kwamba kila aliye miliki mali ni faradhi juu yake kujifunza na kuijua elimu ya zaka ili aweze kutoa zaka kama itakiwavyo na Allah. Kwani kutoa zaka kwa mujibu wa matashi, fikra na akili zako, hakupungui kuwa ni dhambi.
Na pia wanasahau ya kwamba wao wenyewe ni milki na watumwa wa Allah, mali waliyo nayo ni riziki kutoka kwa Allah, aliye wawajibishia kutoa sehemu ndogo mno katika mali hiyo ni Allah na hao wanao takiwa kuwapa ni waja wake Allah.
Basi tunawakumbusha ndugu zetu hao watambue ya kwamba kuacha kutoa zaka ni:
- Janga na majuto makubwa siku ya Kiyama,
- Kukhalifu na kuipinga amri ya Mwenye mali yake,
- Kujenga chuki baina ya masikini na matajiri,
- Kuongeza vitendo vya uhalifu na hata mauaji katika jamii, na
- Kuongeza ombwe la walio nacho na wale wasio nacho.
Hali kadhalika wakumbuke ya kwamba kutoa zaka kwa namna aitakayo Mola, ni mojawapo ya njia za:
- Kutokomeza umasikini miongoni mwa jamii,
- Kujenga mapenzi na huruma baina ya wanajamii,
- Kujenga mshikamano na moyo wa kusaidiana miongoni mwa wana jamii,
- Kupunguza kama si kutokomezaa kabisa uhalifu katika jamii, na
- Kuitekeleza amri yake Allah.
Naam, ewe ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-hebu sasa na tuitupie jicho mandhari ya majuto kwa wale wasio toa zaka, ziko nyingi lakini katika darsa yetu hapa tutaziangalia mbili tu miongoni mwa hizo nyingi.
Ama mandhari ya kwanza ni ile inayo elezewa na Allah Atukukiaye katika kauli yake: “… Na wanao kusanya (jilimbikizia) dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika njia ya Allah, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu. Siku zitapo tiwa katika moto wa Jahannamu, na kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa: Haya ndiyo mlio jilimbikia nafsi zenu, basi onjeni mliyo kuwa mkilimbika”. At-Taubah [09]:34-35
Eeh! Mandhari hatari iliyoje! Sasa swali hapa ni kwa nini Allah amechagua katika mwili wa mzuia zaka kipaji, mbavu, mgongo kuwa ndivyo vitakavyo chomwa moto na si viungo vingine vya mwili?!
Jawabu la swali hilo ikiwa litakupitia, ni kwamba duniani masikini alipo kuwa akienda kwa tajiri kumuomba ampe katika kile alicho pewa na Allah, tajiri alikuwa akimkunjia masikini huyo paji la uso wake.
Masikini akiendelea kuomba, tajiri alikuwa akimpa ubavu kwa kugeukia upande mwingine na masikini akiendelea kung’ang’ania na kushikilia kuomba, hapo tajiri humpa kisogo akamgeuzia mgongo.
Ndipo Allah Mtukufu akavichagua viungo hivyo vitatu vilivyo kuwa vikitumiwa na tajiri katika kumnyanyapaa masikini, viadhibiwe kwa mali yake mwenyewe aliyo kuwa akimnyima masikini. Mali yake itatiwa ndani ya moto wa Jahannamu hata ilipo yeyuka ikachukuliwa akabandikwa nayo kwenye viungo hivyo.
Na hayo pia ndiyo aliyo yaeleza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-pale alipo sema: “Hapana mtu mwenye (aliye miliki) dhahabu wala fedha, hatoi katika (mali) hiyo zaka, ila itakapo kuwa siku ya Kiyama, (mali hiyo) itageuzwa kuwa mbati za moto, zikatiwa kwenye moto wa Jahannamu, kisha zikachomwa kwazo mbavu zake, paji lake na mgongo wake. Kila zitakapo poa (mbati hizo), zitatiwa tena motoni (akachomwa tena) katika ile siku ambayo kadiri yake imekuwa ni miaka hamsini elfu. Hata pakisha hukumiwa baina ya waja, ataiona njia yake; ima ya kwendea peponi au ya kwendea motoni”.
Pakaulizwa: Ewe Mtume wa Allah! Na ngamia je? Akajibu: “Wala mwenye ngamia ambaye hatoi haki (zaka) yake. Ila itakapo kuwa siku ya Kiyama atatandaziwa na kukunjuliwa (mifugo yake) kwenye ardhi tambarare, kamili kama ilivyo kuwa (duniani) hakosekani hata yule mwana ngamia aliye achishwa kunyonya. Wamkanyage kanyage kwa kwato zao na kumng’ata kwa meno yao, kila wanapo pita wale wa mwanzo wake, anawarudishia wengine (wapite kumkanyaga) katika ile siku ambayo kadiri yake imekuwa ni miaka hamsini elfu. Hata pakisha hukumiwa baina ya waja, ataiona njia yake; ima ya kwendea peponi au ya kwendea motoni”. Muslim kutoka kwa Abu Huraira.
Pakaulizwa: Ewe Mtume wa Allah! Na ng’ombe na mbuzi/kondoo? Akajibu: “Wala mwenye ng’ombe wala mwenye mbuzi/kondoo asiye toa haki (zaka) yake, ila itakapo kuwa siku ya Kiyama atatandaziwa na kukunjuliwa (mifugo yake) kwenye ardhi tambarare, hakikosekani chochote katika mifugo hiyo. Hakuna (katika kundi hilo) mwenye pembe zilizo pinda, wala asiye na pembe wala yule aliye vunjika pembe (wote wana pembe kamili na nzima). Wampige kwa pembe zao na wamkanyage kwa kwato zao, kila wanapo pita wale wa mwanzo wake, anawarudishia wengine (wapite kumkanyaga) katika ile siku ambayo kadiri yake imekuwa ni miaka hamsini elfu. Hata pakisha hukumiwa baina ya waja, ataiona njia yake; ima ya kwendea peponi au ya kwendea motoni”. Muslim [SAHIH MUSLIM 02/680]. Rejea JAAMI’UL-USWUUL 04/554 – Allah awarehemu.
Ama mandhari ya pili, ni kwamba mwenye mali ambaye hakuwa akitoa zaka duniani, mali yake itageuzwa na kuwa joka lenye upara, liitwalo “Shujaa”, lenye mabato mawili meusi juu ya macho yake.
Litazungusha shingo lake na kumkamata mtu wake (huyo mzuia zaka) kwa mifupa ya taya zake ilhali likimwabia: Mimi ndio ile mali yako (ambayo hukuwa ukiitolea zaka), mimi ndio ile hazina yako (uliyo kuwa ukiilimbikiza pasina kutoa haki yake).
Imepokewa katika SAHIH BUKHAARIY kutoka kwa Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakaye pewa mali na Allah na asitoe zaka yake, (mali yake hiyo) siku ya Kiyama itageuzwa kuwa joka lenye upara, lenye mabato mawili meusi juu ya macho yake. Limkamate, kisha limwambie: Mimi ndio ile mali yako (ambayo hukuwa ukiitolea zaka), mimi ndio ile hazina yako (uliyo kuwa ukiilimbikiza pasina kutoa haki yake). Kisha akasoma: “Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika aliyo wapa Allah katika fadhila zake kuwa ni kheri yao. Bali hiyo ni shari kwao. Watafungwa kongwa za yale waliyo yafanyia ubakhili siku ya Kiyama…”. Aali Imraan [03]:180
Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:
رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١
“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41
Mola wetu Mtukufu kwa rehema zako tunakuomba utupe Amani, Salama na Uokovu katika ile siku ambayo uliyo sema ya kwamba:
“Utawaona hao madhaalimu wanavyo kuwa na khofu kwa sababu ya waliyo yachuma, nayo yatawafika tu. Na walio amini na wakatenda mema watakuwamo katika mabustani ya peponi. Humo watapata wayatakayo kwa Mola wao Mlezi. Hiyo ndio fadhila kubwa”. As-Shuura [42]:22
Jukwaa letu la juma hili linakomea hapa, tunatumai kwa uwezo wake Allah utakuwa umeongeza maarifa yako kuhusiana na madhambi yatakayo mletea mja majuto makubwa siku Kiyama, na utakuwa unajitahidi kwa kadiri ya uwezo wako kuyaepuka ili ukapate salama na uokovu katika ile siku iliyo nzito na ngumu kuwahi kukupitia.
Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine chini ya anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.
Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.
Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo.
Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:
Kila mmoja wetu na ajiulize, itakuwaje hali yangu: “Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye. Na mama yake na babaye. Na mkewe na wanawe. Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha”. ‘Abasa[80]:34-37