SOMO LA KUMI NA NANE-04

“MANDHARI NA MUONEKANO WA WATENDA MAASI SIKU YA KIYAMA”

Sifa zote njema ni zake Allah; Mola Mlezi wa viumbe vyote, sifa zinazo kidhi neema zake na kutosheleza ziada zake. Allah ambaye: “Yeye ndiye anaye huisha na anaye fisha. Akihukumu jambo liwe, basi huliambia: Kuwa! Likawa”. Na Rehema na Amani zimuendee aliye mwisho wa Mitume na kiongozi wao; Bwana wetu Muhammad mwana wa Abdallah. Na Allah awawiye radhi maswahaba wake na wote walio wafuata kwa wema mpaka siku ya jazaa na malipo.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Ndugu mwana jukwaa letu-Allah akurehemu. Kwa msaada na uwezeshi wake Mola tumekutana tena katika ukumbi wa jukwaa kumbushi letu la kila juma, tumepewa tena fursa hii ili tuendelee kukumbushana kuhusiana na siku inayo tujongelea mno; siku ya Kiyama.

Tukumbushane chini ya kivuli cha maneno ya yule mwanaadamu aliye Mkweli Muaminifu kwa lengo lile lile la kuwaidhika na kujiandaa kwa kutenda amali njema ili tupate salama na nusra katika siku hiyo.

Haya sasa karibu tuendelee na jukwaa letu la juma hili, ambalo bado liko chini ya maudhui mama yenye anuani isomekayo:

Mandhari na muonekano wa watenda maasi/dhambi

Kwa uwezeshi wake Mola wetu Mtukufu, ni juma hili tena bado tunaendelea kuishi na kuyaangalia yale madhambi ambayo hayo ni sababu ya majuto kwa mja siku ya Kiyama, sababu kuu ya kuyataja madhambi hayo kwanza tupate kuyajua na kisha baada ya kuyajua tuyaache kama tulikuwa tunayafanya au tuyaepuke kama bado hatujayafanya.

Kwani ni kwa hayo mawili tu; kuyaacha au kutokuyafanya ndio tukasalimika na adhabu ya Mola, adhabu iliyo chungu, kali na kubwa mno ambayo hawezi yeyote kuihimili. Na leo chini ya mada kuu hiyo hapo juu, tutaishi na kuiangalia dhambi:

Kuficha elimu; hatamu za moto ni za yule aliye ificha elimu

Hili la kuficha elimu ndilo linalo tajwa na kauli yake Allah aliye Mtukufu: “Hakika wale wanao ficha tuliyo yateremsha-nazo ni hoja zilizo wazi na uwongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu kitabuni-hao anawalaani Allah, na wanawalaani kila mwenye kulaani”. Al-Baqarah [02]:159

Na amesema Yeye Mwenye utukufu na ukarimu: “Hakika wale wafichao aliyo yateremsha Allah katika Kitabu, wakanunua kwacho thamani ndogo, hao hawali matumboni mwao isipo kuwa moto, wala Allah hatawasemeza Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa. Nao watapata adhabu chungu. Hao ndio walio nunua upotofu badala ya uwongofu, na adhabu badala ya maghfira. Ama wavumilivu wa moto watu hawa!”. Al-Baqarah [02]:174-175

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakaye ulizwa kuhusiana na elimu, akaificha, siku ya Kiyama Allah atamvisha lijamu (hatamu) za moto”. Ahmad & Al-Haakim [SAHIH AL-JAAMI’I 6284]-Allah awarehemu.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-kupitia kauli hizo zake Mola Muumba wetu ambaye Yeye ndiye aliye mfundisha mwanaadamu kila anacho kijua, na kauli hiyo ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ambaye amelisisitiza mno suala la kusoma.

Kwa kauli zao hizo tunatambua na kujua ya kwamba kumbe kuficha kile alicho kufunulia Allah; ukaona choyo wenzako nao kukijua kupitia kwako.

Na ukasahau ya kwamba elimu uliyo nayo ni amana uliyo pewa na Allah na pia anakutahini kupitia elimu hiyo aone na ilhali Yeye ni Mjuzi mno, utaitumia kwa ajili ya kutafuta radhi zake au kwa ajili ya kupatia maslahi ya mpito ya dunia duni hii.

Kitendo chako hicho cha kuficha elimu, au ukaacha kuibainisha haki kwa kumchelea mtawala au kumuudhi mfadhili wako, hakipungui kuwa ni dhambi itakayo kuletea majuto makubwa siku ya Kiyama.

Mwenye elimu yake hatazungumza nawe, hatakutakasa na utapata adhabu kali na chungu ambayo huna uwezo wa kuihimili. Allah atuhifadhi na atuwezeshe kuiepuka dhambi hiyo kwa fadhila, ukarimu na rehema zake.

Naam, tuendelee kuiangalia dhambi nyingine miongoni mwa dhambi zinazo wajibisha mtu kupata majuto siku ya Kiyama, nayo ni:

Usengenyi

Kwanza kabisa tunapaswa kujua ya kwamba usengenyi ni dhambi ambayo Allah ameikataza na kuikemea vikali kabisa na akaifananisha kuwa ni sawa na mtu kula nyama ya ndugu yake aliye kufa, pale alipo sema ndani ya Kitabu chake kitukufu: “… wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! …”. Al-Hujuraat [49]:12

Katika aya hiyo Allah Ataadhamiaye anatukataza kumtaja muislamu mwenzetu kwa jambo ambalo akilisikia ataudhika na kuchukia hata kama jambo hilo ni la kweli; analo, analifanya au amelisema.

Tusimseme pembeni bali tukitaka basi tukamwambie usoni pake kwa njia ya kumnasihi. Angalia, ikiwa jambo hilo tunalo msema hana au halifanyi, basi hapo tutakuwa tumemzulia/tumemsingizia na hiyo ni dhambi kubwa.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ambaye ndiye mfasiri mkuu wa Qur-ani, anaumithilisha usengenyi na riba, anasema: “Riba ina milango sabini na mbili; mdogo kabisa ni mithili ya mtu kulala na mama yake mzazi na mkubwa kuliko yote ni mtu kumfanyia uadui mwenzake katika heshima yake (kumvunjia heshima, akaitangaza aibu yake na akamfedhehesha)”. Twabaraaniy [SAHIH AL-JAAMI’I 3537]-Allah awarehemu.

Ama kuhusiana na majuto atakayo kuwa nayo akhera, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema kuyaelezea majuto hayo: “Siku Mola wangu Mlezi alipo nipandisha mbinguni (katika ule usiku wa Israa na Mi’iraji), niliwapitia watu wenye kucha za shaba wanajipara kwazo nyuso zao na vifua vyao. Nikauliza: Ni kina nani hao, ewe Jibrilu? Akajibu: Hawa ndio wale ambao wanao kula nyama za watu (wanawasengenya) na wanawavunjia heshima”. Ahmad & Abu Daawoud [SAHIH AL-JAAMI’I 5213]-Allah awarehemu.

Amesema At-twayyibiy-Allah amrehemu: “Kwa kuwa kujipara makucha uso na kifua, kumekuwa ni sifa (mambo) ya wale wanawake wenye kuomboleza, ndio Allah akakufanya kuwa ndio jazaa na malipo ya wale wanao vunja heshima za waislamu ili kuonyesha ya kwamba mawili hayo (kupara makucha uso na kifua) sio katika sifa za wanaume, bali (hayo) ni katika mambo ya wanawake yaliyo katika hali mbaya na sura kirihi (inayo chukiza na kuchefua)”.

Na imepokewa katika Hadithi iliyo tajwa na Abu Huraira-Allah amuwiye radhi: “Atakaye kula nyama ya ndugu yake duniani (atakaye msengenya), atasogezewa nyama hiyo siku ya Kiyama na aambiwe: Ile akiwa amekufa kama ulivyo ila akiwa hai. Basi ataila atakunja uso (kama mtu alaye kitu kichungu na kikali) na atapiga ukelele mkubwa (kutokana na uchungu na ukali huo)”. Ibnu Hajar [AL-FAT-HI 10/485]-Allah amrehemu.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-ni kweli iliyo dhaahiri shaahiri mbele ya kila mmoja wetu kwamba leo usengenyi limekuwa ni jambo la kawaida mno na limetangaa sana miongoni mwa watu wa zama za leo.

Watu leo hawaogopi na wala hawajali hata kidogo kumsengenya mtu kiasi cha kufikia kuwa ni mtindo au sehemu ya maisha; bila ya kusengenya mtu haoni raha.

Tena usengenyi nao haukuachwa nyuma na maendeleo ya sayansi na teknolojia, watu leo wanavitumia vyombo vya tasnia ya habari na mawasiliano kuwasengenya wenzao kwa sura mbaya zaidi; si tu kwa sauti bali wanafikia hata kuweka picha au video za watu ili kuwavunjia heshima na kuwafedhehesha mbele ya jamii.

Tena wakati mwingine video au sauti hizo za walengwa huwa zimehaririwa ili tu kupoteza ukweli na kufikia lengo la hao wasengenyaji. Jamani hiyo ni dhambi kubwa na yenye athari kuwa katika jamii, tuiacheni jamani ili tusije patwa na majuto makubwa kesho mbele ya Allah.

Tumuombe Allah kwa unyenyekevu mkubwa atukinge na dhambi hii ya usengenyi, sisi na vizazi vyetu.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Yaa Allah! Wewe ndiye Mola Muumba wetu, uliye tuumba kwa uwezo wako na ukatukadiria umri wa kuishi katika hii ardhi yako. Tunakuomba kwa uwezo wako huo ulio tukuka, uturuzuku umri mrefu wenye siha njema katika kutenda mema.

Utupe mapenzi ya kweli katika kumpenda kipenzi chako Mtume Muhammad, turuzuku kumuiga na kumfuata haki ya kumfuata na tuwezeshe kuwapenda Aali Beit wake. Ewe Mwenye kujibu dua za waja wako, tutakabalie dua yetu!

Mpaka hapa jukwaa letu hili limetamatia, kwa uwezo wake Allah tunatumai utakuwa umejifunza kitu kupitia utajo wa madhambi hayo yenye kuleta majuto makuu kwa mja katika siku ile iliyo ngumu na nzito; siku ya Kiyama. Na kwa hivyo utakuwa umetafakari na kuanza kuchukua hatua za ama kuyaacha au kutoyafanya.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine chini ya anuani yetu mama hiyo ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo.

Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

“Ewe mwanaadamu! Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu? Aliye kuumba, akakuweka sawa, akakunyoosha. Katika sura yoyote aliyo ipenda akakujenga”. Al-Infitwaar [82]:06-09

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *