SOMO LA KUMI NA NANE-03, Mutakabirina; Wanao fanya kiburi, majivuno na jeuri

Himda na shukrani zote njema ni stahiki yake Allah; Mwenye utukufu na ukuu, Mstahiki wa himda na sifa zote za ukamilifu, azali na milele. Ambaye Yeye ndiye: “Anajua khiyana ya macho na yanayo ficha vifua (nyoyo)”. Rehema na Amani yake imshukie aliye Bwana wa Mitume wote, ziwashukie pia Aali, Swahaba na jamia ya ummati wake mpaka ile siku ya hukumu.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Kabla ya lolote, tuendelee kuzielekeza shukurani za dhati zenye kusuhubiana na taadhima pamoja na unyenyekevu mkubwa kwa Allah ambaye Yeye ndiye anaye tuwezesha kuungana nawe katika ukumbi wetu huu ili tupate kukumbushana. Tumuombe Allah atudumishie neema hii na atuwezeshe kuishukuru kwa kuyatendea amali yale anayo tuwafikisha kukumbushana, kwani hiyo ndio namna bora kabisa ya kuishukuru neema.

Haya sasa karibu tuendelee na jukwaa letu la juma hili, ambalo bado liko chini ya maudhuimama yenye anuani isomekayo:

Kabla ya lolote, tuendelee kuzielekeza shukurani za dhati zenye kusuhubiana na taadhima pamoja na unyenyekevu mkubwa kwa Allah ambaye Yeye ndiye anaye tuwezesha kuungana nawe katika ukumbi wetu huu ili tupate kukumbushana. Tumuombe Allah atudumishie neema hii na atuwezeshe kuishukuru kwa kuyatendea amali yale anayo tuwafikisha kukumbushana, kwani hiyo ndio namna bora kabisa ya kuishukuru neema.

Haya sasa karibu tuendelee na jukwaa letu la juma hili, ambalo bado liko chini ya maudhui mama yenye anuani isomekayo:

Mandhari na muonekano wa watenda maasi/dhambi. 

Kwa uwezeshi wake Mola wetu Mtukufu, ni juma jingine tena bado tunaendelea kuishi na kuyaangalia yale madhambi yatakayo mletea mja kujuta na kusaga meno siku ya Kiyama, na kama tulivyo tangulia kusema majuma kadhaa yaliyo kwisha tupa kisogo, lengo na madhumuni ya kuyataja madhambi hayo ni ili tupate kuyahepa na kujitenga nayo. Asaa kesho mbele ya Mola wetu Mkarimu na Mrehemevu mno, tukasalimika na adhabu iliyo chungu, kali na kubwa mno kuweza kuhimiliwa na mwanaadamu aliye dhaifu kwa kila hali. Na leo chini ya mada kuu hiyo hapo juu, tutaishi na kuiangalia dhambi:

Mutakabirina; wanao fanya kiburi, majivuno na jeuri:

Eeh! Mandhari ya kutisha iliyoje ya mutakabirina ambao waliijaza dunia kiburi, majivuno, jeuri, ukaidi na kujikweza. Hao ndio wanao zuiliwa na aya za Allah duniani; kuzizingatia, kuzisikiliza, kuzinyenyekea, kuzifuata na kuzitendea amali, kama anavyo sema Allah Ataadhamiaye: “Nitawatenga na ishara (Aya) zangu wale wanao fanya kiburi katika nchi bila ya haki. Na wao wakiiona kila ishara hawaiamini. Wakiiona njia ya uwongofu hawaishiki kuwa ndio njia; lakini wakiiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndio njia. Hayo ni kwa sababu wamezikanusha ishara zetu, na wameghafilika nazo”. Al-A’araaf [47]:146

Mandhari ya mutakabirina haiishii hapo, bali akhera nako watakuwa katika hali ngumu mno; watafufuliwa wakiwa dhalili na wanyonge mno. Hiyo ndiyo hali yao Akhera kama alivyo ielezea Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-katika kauli yake: “Mutakabirina watafufuliwa siku ya Kiyama mfano wa sisimizi katika sura ya watu, wakifunikwa na udhalili kotekote, wataswagwa kupelekwa kwenye gereza lililomo ndani ya Jahannamu, liitwalo Bulisi. Watafunikwa na moto wa mioto na wakinyweshwa usaha wa watu wa motoni”. Ahmad, Tirmidhiy [SAHIH AL-JAAMI’I 8040]-Allah awarehemu.

Eeh! Adhabu kali iliyoje! Na hekima ya kufufuliwa wakiwa watu katika umbo dogo la sisimizi na si kiumbe mwingine, ni kwamba mdudu sisimizi ni kiumbe ambaye watu hawamjali; wanapo tembea hawachukui tahadhari pale wanapo weka miguu yao, bali humkanyaga pasina kuhisi kama wamekanyaga kitu.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-epuka kiburi, kwani hiyo ni dhambi itakayo kuathiri kwanza hapa duniani na kesho akhera itakuweka mahala pabaya. Kwani ukiwafanyia waja wa Allah kiburi, jeuri, majivuno na ukajikweza juu yao, unapata nini au kinazidi nini kwako ila khasara tupu! Acha kiburi ili usalimike duniani na akhera, Allah atakupenda na waja wake watakupenda pia. 

Haya na tuendelee kuangalia madhambi mengine ambayo ni sababu ya majuto akhera:

Hawa hawatatazamwa na Allah siku ya Kiyama kwa jicho la rehema na wala hatazungumza nao:

Fahamu ewe ndugu mwema-Allah akurehemu-ya kwamba katika jumla ya watu ambao Allah atawaghadhibikia siku ya Kiyama; hatazungumza nao na wala hatawatakasa na wana wao adhabu chungu. Hao ni wale ambao wanao ivunja ahadi ya Allah baada ya kwisha ifunga na wanao uza viapo vyao kwa thamani ndogo; wanaapa viapo vya uwongo ili kupata maslahi duni ya dunia. Allah Ataadhamiaye anasema kuhusiana na watu hao: “Hakika wanao uza ahadi ya Allah na viapo vyao thamani ndogo, hao hawatakuwa na sehemu ya kheri yoyote katika Akhera, wala Allah hatasema nao wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao watapata adhabu chungu”. Aali Imraan [03]:77

Imamu Ibnu Kathir ametaja mlolongo wa hadithi nyingi zinazo fungamana na aya hiyo, miongoni mwazo ni ile iliyo pokewa kutoka kwa:

  • Abu Dhari-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Watu wa aina tatu Allah hatazungumza nao na wala hatawatazama kwa jicho la rehema siku ya Kiyama, wala hatawatakasa na wanayo wao adhabu chungu”. Nikauliza: Ewe Mtume wa Allah! Ni kina nani hao? Wamekula khasara na wameruka patupu. Akasema (Mpokezi): Na Mtume wa Allah akayakariri maneno hayo mara tatu. Akasema: “Mburuta nguo (kwa kiburi na jeuri), muuza bidhaa yake kwa kiapo cha uwongo na msimbuliaji (anapo toa)”. Muslim, Asw-haabu As-sunan & Ahmad-Allah awaremu.
  • Abdullah-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakaye apa kiapo na ilhali yeye kwenye kiapo hicho ni muovu (muongo, anaapa) ili apate kujichukulia mali ya mtu muislamu, (huyo) atakutana na Allah na ilhali Yeye amemghadhibikia”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
  • Abdillah bin Abi Aufaa ya kwamba mtu mmoja aliweka bidhaa yake sokoni, akaapa ya kwamba amenunua kwa kiasi kadhaa kiasi ambacho hakununua hivyo, (akaapa hivyo) ili apate mfanya mtu mmoja katika waislamu ainunue. Hapo ndipo ikashuka aya: “Hakika wanao uza ahadi ya Allah na viapo vyao thamani ndogo…”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Si hao tu, bali Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amezitaja mbeya (makundi) nyingi za watu ambao Allah hatawatazama kwa jicho lake la rehema siku ya Kiyama na wala hatawatakasa na watapata wao adhabu iliyo chungu mno. Akasema-Rehema na Amani zimshukie:

  • “Mbeya tatu za watu Allah hatazungumza nao siku ya Kiyama na wala hatowatazama kwa jicho la rehema; mtu anaye apa kwenye bidhaa yake kwamba amenunua ghali kuliko alivyo uza na ilhali yeye ni muongo. Na mtu aliye apa yamini ya uwongo baada ya Laasiri ili tu apate kunyakua kwacho (kiapo hicho) mali ya mtu muislamu. Na mtu aliye zuia ziada ya maji yake, basi Allah atasema: Leo na Mimi nitakunyima fadhila zangu kama wewe ulivyo zuia ziada ya kile ambacho haikukitengeneza mikono yako”. Bukhaariy & Muslim [SAHIH AL-JAAMI’I 3066]-Allah awarehemu.
  • “Mbeya tatu za watu Allah hatazungumza nao siku ya Kiyama na wala hatawatakasa, wala hatawatazama kwa jicho la rehema na watapata wao adhabu yenye uchungu mkubwa; mzee mzinifu, mfalme (raisi/kiongozi/mtawala) muongo na masikini jeuri”. Muslim & Nasaai [SAHIH AL-JAAMI’I 3069]-Allah awarehemu.
  • “Mbeya tatu za watu Allah hatazungumza nao siku ya Kiyama; mwenye kuwaasi wazazi wake, mwanamke mwenye kujishabihisha na wanamume na dayuthi (asiye na ghera kwa mkewe). Na watu watatu hawataingia peponi; mwenye kuwaasi wazazi wake, mwenye kudumu na ulevi na mwenye kusimbulia kwa anacho kitoa”. Ahmad & Nasaai [SAHIH AL-JAAMI’I 3071]-Allah awarehemu.
  • “Hakika yule ambaye anaye muingilia mke wake katika tupu yake ya nyuma, Allah hatamtazama kwa jicho la rehema”. Al-Baihaqiy [SAHIH AL-JAAMI’I 1691]-Allah awarehemu.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-chaguo ni lako wewe sasa, ikiwa unataka kutazamwa na Allah kwa jicho lake la rehema siku ya Kiyama, unataka Allah azungumze nawe na akutakase, nafasi unayo leo kabla hujarejea kwake. Ikiwa kweli unayataka hayo, basi ukiwa na mojawapo ya hayo aliyo yataja Allah Mwenyewe na Mtume wake, komeka na uyaogope kama unavyo muogopa simba katika maisha ya ulimwengu huu. Fahamu ya kwamba kuyaepuka madhambi hayo, ndiko pekee kutakako kuhakikishia fursa ya kuzungumzishwa na Mola Muumba wako, akutazame kwa jicho la rehema na akutakase. Allah atupe nguvu za kuyaepuka madhambi hayo, kwa fadhila zake kuu na rehema zake zilizo kienea kila kiumbe chake.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe: 

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١ 

“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41 

Mola wetu Mtukufu kwa rehema zako, ukarimu wako na fadhila zako, tunakuomba utupe Amani, Salama na Uokovu katika ile siku ambayo unasema kuwaambia waja wako:

“Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika”. Az-Zukhruf [43]:68

Tunatumai kwa uwezo wake Allah, tutakuwa tunaendelea  vizuri pamoja na utakuwa unaendelea kuyajua madhambi yatakayo mletea mja majuto makuu siku ya Kiyama. Kujua ambako kutakusaidia kuyaepuka madhambi hayo na kukaa mbali nayo ili usije angukia kwenye majuto. Allah atuhifadhi na madhambi hayo na baki ya madhambi mengine, kwani sisi waja wake dhaifu hatuna uwezo wala ujanga wa kuyahepa madhambi ila tu ni kwa kuwezesha naye.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine chini ya anuani yetu mama hiyo ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu. 

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

“Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu”. Al-Anbiyaa [21]:47

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *