SOMO LA KUMI NA NANE -02 , Wale wanao kula mali ya yatima kwa dhulma

Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Allah! Ambaye amesema na kauli yake ni haki: “Leo kila nafsi italipwa kwa iliyo yachuma. Hapana dhulma leo. Hakika Allah ni Mwepesi wa kuhisabu”.  Na amani ishuke juu ya waja wake alio wateua miongoni mwa Mitume, Aali zao, Wafuasi wao na jamia waja wema mpaka siku watakapo simamishwa waja mbele ya Mola kwa ajili ya hisabu, hukumu na jazaa sawia.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Wapendwa wana jukwaa wenziwetu, sote kwa pamoja tunao wajibu wa kumshukuru Allah Mtukufu aliye tujumuisha tena pamoja katika ibada hii ya kukumbushana ndani ya jukwaa hili la kila juma.

Kuanzia juma na majuma kadhaa baada ya leo, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mkarimu, katika jukwaa letu hili, tutaishi na maudhui inayo beba anuani hii:

Mandhari na muonekano wa watenda maasi/dhambi. 

Kwa uwezeshi wake Mola wetu Mtukufu, juma hili tena bado tunaishi na kuyaangalia yale madhambi yatakayo kuwa ni sababu ya mja kujuta na kusaga meno siku ya Kiyama, na kama tulivyo tangulia kusema juma la jana, lengo la kuyataja ni ili tupate kuyaepuka na kukaa mbali nayo, asaa tukapata salama kesho mbele ya Mola wetu Mkarimu na Mrehemevu mno. Na leo chini ya mada kuu hiyo hapo juu, tutaishi na kuiangalia dhambi:

  • Wale wanao kula mali ya yatima kwa dhulma:

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-ni kheri kwetu sote ikiwa tutajua na kufahamu ya kwamba katika jumla ya madhambi yatakayo mletea mja majuto siku ya Kiyama ni kula mali ya yatima alio fanywa yeye kuwa msimamizi wao, kisha yeye akaila mali yao kwa njia ya dhulma. Tumuombe Allah atuhifadhi na dhambi hiyo.

Allah Mwenye utukufu na ukarimu anasema: “Hakika wanao kula mali ya yatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia motoni”. An-Nisaa [04]:10

Imamu Ibnu Kathiir-Allah amrehemu-amesema katika kuitafsiri kauli hiyo tukufu ya Allah aliye Mtukufu: “Yaani analo kusudia kulisema hapa Allah ni kwamba watakapo kula mali za mayatima pasina sababu, hapo hakika bila ya shaka yoyote wanakula moto utakao vurumia matumboni mwao siku ya Kiyama”. MUKHTASAR TAFSIIR IBNI KATHIIR [01/356]-Allah amrehemu.

Na amesema mwanachuoni As-sadiy-Allah amrehemu: “Siku ya Kiyama mla mali ya yatima atafufuliwa na ilhali miale ya moto inatoka kinywani mwake, masikioni mwake, puani mwake na machoni mwake. Kila atakaye muona atajua ya kwamba yeye ni mla mali ya yatima”. AL-KABAAIR cha Imamu Ad-Dhahabiy [Sah. 118]-Allah amrehemu.

Kwa mukhtasari hiyo ndio hali ya yule anaye jiona leo mjanja na akaitumia fursa ya utoto wa mayatima akaila mali yao kwa dhulma, huo anao uona leo kuwa ni ujanja utakuwa ni majuto na moto siku ya Kiyama mbele ya Allah anaye muona pale anapo fanya hila ya kuwadhulumu watoto yatima. Allah atuhifadhi na dhambi hiyo inayo leta majuto mbele ya Mola; majuto ambayo hayatamnufaisha mjutaji kwa chochote. Haya na tuendelee kuiangalia dhambi nyingine miongoni mwa dhambi zitakazo kuwa ni sababu ya kumletea mtendaji wake majuto siku ya Kiyama, nayo ni:

  • Taariku swalaa (mtu asiye swali):

Kutokuswali leo limekuwa ni jambo la kawaida kwa wengi wetu, mtu anaona akiswali ni sawa na asipo swali hajakosea. Hapana, kuacha swala ni dhambi kubwa, kwani swala ndio ibada pekee ambayo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikabidhiwa na Mola pasina wasita (ukaa kati) wa Malaika Jibrilu-Amani imshukie. Bali alimuita mwenyewe mja wake mbinguni akamkabidhi usiku ule wa Israa na Miiraji, hali kadhalika ndio ibada ya mwanzo atakayo hisabiwa kwayo mja siku ya Kiyama, ikitengenea basi hapana haja ya kukaguliwa amali zake nyingine, ndio keshafuzu huyo. Ama ikikutwa na makosa, basi atakaguliwa na amali zake nyingine zote.

Hebu muone huyo muacha swala pale ambapo itakapo mfunukia hakika na uhalisia wa hali na akayaona dhaahiri shaahiri yale yote aliyo kuwa akiambiwa duniani, hapo sasa ndio atataka kumsujudia Allah lakini kila atakapo jaribu kusujudu atajikuta hawezi. Hilo ndilo analo litaja Allah Ataadhamiaye katika kauli yake, pale alipo sema: “Siku utakapo wekwa wazi muundi, na wataitwa kusujudu, lakini hawataweza. Macho yao yatainama chini, fedheha itawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa wasujudu walipo kuwa wazima”. Al-Qalam [68]:42-43

Katika kuitafsiri kauli hiyo yake Mola, Mwanachuoni Said Ibnu Al-Musayyab-Allah amrehemu-amesema: “Walikuwa wakisikia (wakati kukiadhiniwa) {Hayya alas-swalaah! Hayya alal-falaah!} – Njooni kwenye swala! Njooni kwenye kufaulu! Basi hawakuuitika wito huo (wa swala) na ilhali wao ni wazima walio salimika. Basi kila ambaye alihifadhi (alidumu na) swala duniani, huyo ndiye ataweza kumsujudia Allah akhera. Ama yule aliye iacha swala duniani, huyo Allah atamnyang’anya neema ya kusujudu akhera”. 

Imamu Ahmad-Allah amrehemu-amepokea kwa ‘sanadi jayidi’ ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisema kuizungumzia swala: “Atakaye ihifadhi (swala), itakuwa kwake ni nuru, hoja na uokovu siku ya Kiyama. Na yule ambaye hakuihifadhi, haitakuwa kwake nuru, wala hoja wala uokovu na siku ya Kiyama atakuwa pamoja na Qaarun, Firaun, Haamaana na Ubayyu bin Khalaf”. 

Baadhi ya Wanazuoni-Allah awarehemu-wamesema: Hakika si vinginevyo, muacha swala atafufuliwa na wanne hao, kwa kuwa yeye hakika si kwa jenginelo ima aliiacha swala kwa sababu ya kushughulika na mali yake, au ufalme/utawala/uongozi wake, au wizara/kazi yake, au biashara yake. Angalia, basi ikiwa aliacha swala kwa sababu ya mali yake, huyo atafufuliwa pamoja na Qaaruun. Na ikiwa aliacha kuswali kwa sababu ya ufalme/utawala/uongozi wake, huyo atafufuliwa pamoja na Firauni. Na ikiwa aliacha swala kwa sababu ya uwaziri/umeneja/kazi yake, huyo atafufuliwa pamoja na Haamaana. Na ikiwa aliacha swala kwa sababu ya biashara yake, huyo atafufuliwa pamoja na Ubayyu bin Khalaf; tajiri wa makafiri wa Makka”. AL-KABAAIR cha Imamu Dhahabiy [Sah. 49]

Na imepokewa ya kwamba, wa mwanzo ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi tii siku ya Kiyama, ni waacha swala na kwamba ndani ya Jahannamu kuna jangwa linalo itwa “Lamlam”, ndani ya jangwa hilo yamo majoka. Kila joka moja lina uzito sawa na shingo ya ngamia, urefu wake ni mwendo wa mwezi mzima, joka hilo litamgonga muacha swala, basi sumu yake itachemka mwilini mwake miaka sabini. Kisha inapukutika nyama yake. 

Eeh! Ni majuto yaliyoje hayo! Jihurumie ewe ndugu yangu masikini, adhabu ya Allah ni chungu, kali na kubwa kuliko ustahamilivu wako. Anza leo kuswali, msujudie Mola wako aliye kuumba katika umbile bora na akakutukuza kuwa ni mwanaadamu. Acha upasito, mlaani shetani na pambana na nafsi yako ambayo: “…Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu…”. Yuusfu [12]:53  

Anza kumuabudu Mola wako kupitia ibada tukufu kuliko zote ambayo ndio kontena la kubebea amali zako nyingine. Na si uswali wewe peke yako tu, bali: “Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchaMngu”. Twaha [20]:132 

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe: 

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١ 

“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41 

Mola wetu Mtukufu kwa rehema zako tunakuomba utupe fungu katika dua ya Malaika wako watukufu kwa waja wako Waumini pale walipo sema:

“Mola wetu Mlezi! Umekienea kila kitu kwa rehema na ujuzi. Basi wasamehe walio tubu na wakaifuata njia yako, na waepushe na adhabu ya Jahannamu. Mola wetu Mlezi! Na waingize katika bustani za milele ulizo waahidi. Na uwape haya pia walio fanya mema miongoni mwa wazee wao na wake zao na dhuriya zao. Hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Na waepushe na maovu, kwani umwepushaye maovu siku hiyo, hakika umemrehemu; na huko ndiko kufuzu kukubwa”. Al-Ghaafir [40]:07-09

Jukwaa letu juma hili linatamatia hapa ili kutoa fursa kwa kila mwenye moyo wa kukumbuka, akumbuke, awaidhike na kisha aanze kujiandaa na siku iliyo ahidiwa ya Kiyama kwa kufuata maamrisho ya Mola wake na kuyaacha yale makatazo.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu. 

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

“Basi ama yule aliye zidi ujeuri. Na akhiari maisha ya Dunia. Kwa hakika Jahannamu ndio makaazi yake. Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuia nafsi yake na matamanio. Basi huyo, Pepo itakuwa ndio makaazi yake”. An-Nazi’aat[79]:37-41

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *