SEHEMU YA PILI – NDOA (inaendelea)

KUTENGENEA KWA FAMILIA YAKO, NDIO KUTENGENEA KWA JAMII NA TAIFA LAKO”

Sifa njema zote ni haki yake Allah; Muumba wa viumbe vyote na Mpangaji wa mambo na taratibu zote, asemaye katika Kitabu chake Kitukufu:: “Na kwamba Yeye ndiye aliye umba jozi; dume na jike. Kutokana na mbegu ya uzazi inapo miminwa”. Tunamuhimidi na kumshukuru Yeye aliye tukuka kwa kutupa neema ya dini hii inayo chukuzana na maumbile ya mwanaadamu. Na Rehema na Amani zimshukie Bwana wetu Muhammad, ambaye amewafundisha watu kheri kupitia kauli, matendo na hali zake. Na ambaye yeye ndiye ruwaza yetu njema katika kila kitu na jambo. Na pia ziwashukie Aali na swahaba zake wote.

Ni kwa neema, fadhila na ukarimu wake Allah; Mola Muumba wetu tunakutana tena katika jukwaa letu hili la kila wiki. Tumuombe atuwezeshe kumshukuru kwa neema zake zote nyingi ikiwemo hii ya kupata fursa ya kukumbushana, asaa tukapata kukumbuka na kunufaika na ukumbusho.

Juma hili katika jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu, tutaongozwa na somo lenye anuani isemayo:

  1. Malengo/Makusudio ya ndoa:

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-endelea kufahamu na kukubali ya kwamba ndoa ni kifungo (mkataba) kitukufu kilicho barikiwa na Allah Mola Muumba dume na jike katika kila kitu. Kilicho barikiwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie; mbora wa walio oa wote. Hali kadhalika kina baraka za wazazi wanao furahi pindi mtoto wao anapo oa ama kuolewa na wanachukia na kuumizwa moyo na hisia pindi mtoto wao anapo kwenda kombo, akazini na kupata watoto katika njia hiyo ya haramu.

Kifungo hicho cha ndoa, Allah Mtukufu amekifanya kuwa sheria kwa waja wake kwa maslahi na manufaa yao mengi ili kiwafikishe kwenye makusudio na malengo mema mazuri. Malengo na makusudio hayo ndio tunaweza kuyataja kama “Hekima/Falsafa ya ndoa”, tukipenda. Na kwa kuyachanganya pamoja, malengo na makusudio hayo ya ndoa yanaweza kuangukia katika mafungu makuu matatu, kama ifuatavyo:

  1. Kupata watoto na kuendeleza kizazi cha jamii ya wanaadamu (kuzaana):

Uislamu umeifanya ndoa kuwa ndio iwe njia/sababu ya kupata watoto watakao nasibishwa na wanandoa husika na pia iwe ndio kiwanda kinacho zalisha na kuendeleza kizazi cha jamii ya wanaadamu. Kwa eleweko hilo basi, tunasema kwa kinywa kipana kabisa ya kwamba kuzaana kwa mwanaadamu ni lazima kupitie katika ndoa sahihi kwa maana na nukta zote za kisheria. Na kizazi kilicho patikana kupitia ndoa, hicho ndicho ambacho Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-atakacho jifakharisha nacho mbele ya umma nyingine siku ya Kiyama. Na tunaposema kuzaana, tunaikusudia na kuilenga ile natija ya kimaumbile itokanayo na kukutana kimwili kwa jinsia mbili; ile ya kiume na ile ya kike na hilo ni tendo la kibaiolojia ambalo mwanaadamu anashirikiana na hayawani wengine. Tofauti yao ni kwamba tendo hilo kwa mwanaadamu huhalalishwa kwa kufungwa ndoa na huiandamia ndoa, lakini kwa hayawani wengine hutendwa tu pasina ndoa. Hivyo ndio kusema mwanaadamu anaye tenda tendo la ndoa nje ya ndoa; kabla ya kuoa/kuolewa, huyo huwa amejifananisha na hayawani asiye na akili. Na huyo huwa amekwenda kinyume na utaratibu alio wekewa na Mola Muumba wake.

Na Uislamu umehimiza na kushajiisha watu kuzaana kwa utungo wenye tija, ndipo hapo ukahalalisha kuoa mke zaidi ya mmoja na ukapendelea mtu kuoa mwanamke mwenye uzazi mwingi. Na ukaharamisha kutoa mimba/kuua watoto kwa kuogopea umasikini.

Naam, kwa yeyote aliye fikia umri wa kuoa au kuolewa ili kuanzisha familia yake na kuendeleza ukoo wao, lengo lake la kwanza katika ndoa liwe ni kupata mtoto mwema atakaye mpwekesha na kumuabudu Allah na atakaye muombea pale atakapo tangulia mbele ya Mola. Mtoto atakaye uhifadhi utajo wake baina ya watu na kuendeleza kizazi chake.

Imepokewa kutoka kwa Anas bin Maalik-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akituamrisha kuoa na akikataza vikali useja akisema: “Oeni mwanamke mzazi sana na mwenye kupendwa, kwani hakika mimi nitajifakharisha nanyi mbele ya umati nyingine siku ya Kiyama”.

Na lengo hilo kubwa la ndoa, ndilo linalo dokezwa na kauli yake Allah Yeye aliye Mtukufu: “… na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu…” An-Nahli [16]:72

Pia katika kauli yake Yeye aliye Mtukufu: “… Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Allah…”. Al-Baqarah [02]:187

Wamesema Wanazuoni wa fani ya Tafsiri-Allah awarehemu-katika kuelezea muradi/mapendeleo ya kauli hiyo ya Mola: Ya kwamba kutaka aliyo yaandika Allah, ni kutaka mtoto. Kwa maana ya kwamba na liwe lengo mama la kukutana kimwili, ni kupata mtoto na si tu kukidhi matamanio ya kimwili.

Na hali kadhaalika linadokezwa na kauli yake Allah Mtukufu: “Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu…”. Al-Baqarah [02]:223

Wanatafsiri-Allah awarehemu-wamesema katika kuifafanua kauli hiyo yake Allah Yeye aliye Mtukufu: Ya kwamba kheri anayo itangulizia mtu nafsi yake, ni mtoto ambaye ndiye natija ya kuchanganyika katika mahala ambapo panapo otesha mmea. Napo ndipo pale mahala pa kimaumbile pa maingiliano ya kijinsia, anamtanguliza ili awe muombezi wake siku ya Kiyama.

Na umbile la mwanaadamu alilo umbiwa nalo na Allah Mola Muumba wake, ni kupenda kupata/kuwa na watoto, hivyo ni kwa sababu Allah Mtukufu amewapambia watu kupenda watoto, kama alivyo sema Yeye aliye Mtukufu: “Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana …”. Aali Imraan [03]:14

Hali kadhaalika mwanaadamu anapenda watoto kwa sababu Allah amewafanya hao watoto kuwa ni pambo la maisha ya dunia, kama alivyo sema Yeye aliye Mtukufu: “Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia…”. Al-Kahfu [18]:46

Ewe ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tambua na ufahamu ya kwamba mara nyingi hutokezea mwanaadamu akazidiwa na mapenzi makubwa aliyo nayo kwa watoto wake akatumbukia ndani ya fitna, akamuasi Mola wake kwa sababu yao. Hilo ndilo analo litaja Allah na kututahadharisha kupitia kauli yake tukufu: “Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio (mtihani/fitna). Na kwa Allah upo ujira mkubwa”. At-Taghaabun [64]:15

Fitna/mtihani wa watoto utakapo mtawala na kumuhemeza mwanaadamu hata ukamsukuma kutenda yale yaliyo ya haramu kama vile kuchuma chumo la haramu ili apate kuwaridhisha kwa kukidhi matashi yao. Au ukampelekea kuacha yale yaliyo wajibu juu yake mithili ya kuacha kwenda kwenye jihadi kwa kuwahofia watoto wake. Basi watoto katika hali/mazingira hayo, wanakuwa ni mithili ya adui ambaye ni wajibu kutahadhari naye na hilo ndilo analo tuambia Allah Mtukufu kupitia kauli yake Yeye aliye Mtukufu: “Enyi mlio amini! Hakika mingoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao. Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Allah ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu”. At-Taghaabun [64]:14

Imepokewa katika kutaja sababu ya kushuka kwa aya hii, hadithi kutoka kwa Abdillah bin Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: Ilishuka aya hii (isemayo): Hakika mingoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao…”. (Ilishuka) kwa kaumu ya watu wa Makka walio silimu, wakang’ang’aniwa na wake zao na watoto wao (hata wakashindwa kuhama kumfuata Mtume, Madina). Na siku walipo fika kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-Madina, wakawakuta watu walio watangulia kuhama tayari wamekwisha kuwa weledi wa dini yao. Basi wakataka kuwaadhibu (wake na watoto wao), ndipo Allah Mtukufu akateremsha (kauli yake): “… Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Allah ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu”. Tirmidhiy, Al-Haakim & wengineo-Allah awarehemu.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

﴿… رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا٧٤ [الفرقان: 74]

Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachaMngu”. Al-Furqaan [25]:74

Ewe Mola wa haki! Kwa uwezo wako, tunakuomba utuwezeshe kuwa miongoni mwa wale walio nyenyekea kwa ajili yako, ukawanyanyua daraja. Wakaishi kila hatua ya maisha yao kama utakavyo na kuridhia Wewe na si kama watakavyo wao. Utuwezeshe kuwa miongoni mwa wale walio jikurubisha kwako, ukawakurubisha, walio kuomba ukawapa. Utuwezeshe kuifanya Qur-ani na Mtume wako kuwa ndio muongozo wa malezi ya familia zetu. Hakika Wewe ndiye Mpokeaji wa dua. Aamin!

Haya ndiyo tuliyo jaaliwa kuyaandaa kwa ajili ya kuzungumzia familia ya Kiislamu juma hili, tumuombe Allah atuwezeshe kwa rehema zake kuwa miongoni mwa wenye kukumbuka pindi wanapo kumbushwa na aturuzuku akili itakayo tuongoza kuzijenga na kuzilea familia zetu katika misingi ya Uislamu wetu.

Wakati tukiendelea kumuomba Allah atukutanishe tena juma lijalo tukiwa na afya ya mwili, roho na akili, si vibaya tukiizingatia na tukiitafakari kauli yake Allah Yeye aliye Mtukufu na Muumba wetu: “…basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivyo ndio kutapelekea msikithirishe wana”. An-Nisaa [04]:03

Tukutane juma lijalo katika muendelezo wa jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *