SEHEMU YA KWANZA

HII NDIYO DAWA, PONYO (POZO) LIKO WAPI?

Allah Mola Mwenyezi anasema:

“SOMA ULIYOLETEWA WAHYI KATIKA KITABU (hiki ulicholetewa) NA ISIMAMISHE SWALA. BILA SHAKA SWALA (ikiswaliwa vilivyo) HUMZUILIYA HUYO (mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU, NA KWA YAKINI KUMBUKO (utajo) LA ALLAH (lililomo ndani ya swala) NI JAMBO KUBWA KABISA (la kumzuilia mtu na mabaya) NA ALLAH ANAJUA MNAYOYATENDA”. [29:45]

Huenda ukajiuliza: Mbona/kwa nini yameamrishwa mambo mawili katika kauli hii ya Allah; kusoma kitabu (Qur-ani) na kusimamisha swala?

Jawabu sawia kwa swali lako hilo ni kuwa yameamrishwa mambo mawili hayo. Kwa kuzingatia kwamba ibada inayotekelezwa na mja imegawanyika katika vigawanyo (sehemu) vikuu vitatu:-

IBADA YA MOYO: Hii inahusisha itikadi ya haki na kweli juu ya Allah Mola Muumba wa ulimwengu na vyote vilivyomo; tuvijuavyo na tusivyovijua.

IBADA YA ULIMI: Hii inahusisha kumdhukuru Allah na kumsifia kwa utajo (dhikri) mwema.

IBADA YA KIWILIWILI: Hii inajihusisha na utendaji wa amali (matendo) njema kwa mujibu wa itikadi iliyomo moyoni mwa mja.

Katika mgawanyiko huu wa ibada, itikadi kwa maana ya imani ndio ibada pekee isiyojikariri na kujirudiarudia.

Hii ni kwa sababu mtu akiitakidi kitu/jambo, haiingii akilini kuliitakidi/kuliamini kwa mara nyingine tena.

Kwani itikadi (imani) ile ya mwanzo huendelea kuishi na kudumu moyoni, akilini na katika fikra zake.

 Kwa mantiki hii itikadi ni kitu cha mara moja, kikishakita mizizi moyoni ndio kimekita.

Pamoja na kukubali kuwa itikadi (imani) ni kitu kisichohitaji kurudiwarudiwa. Lakini hatuna budi kuukubali ukweli kuwa imani (itikadi) huzidi/hukua au hupungua/hudumaa.

Hapa sasa ndio tunabakiwa na vitu viwili; dhikri (utajo) ambayo ni ibada ya ulimi na ibada ya kiwiliwili.

Ibada mbili hizi ndizo zinazokubali zoezi la kujirudiarudia, kama lilivyo wazi hili kwa kila mmoja wetu.

Hii ndio sababu/falsafa ya kutajwa mambo mawili haya tu; kusoma kitabu (ibada ya ulimi) na kusimamisha swala (ibada ya kiwiliwili) katika aya hii.

Maswahaba Ibn Masoud na Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-wamesema: Ndani ya swala kuna kinga na kizuizi kinachomzuia mja kumuasi Allah.

Basi mtu ambaye swala yake haimuamrishi kufanya mema na wala haimkatazi kufanya maovu. Swala yake hiyo haimzidishii ila kuwa mbali zaidi na Allah na kuwa ni msiba na janga kwake yeye.

MARADHI YA MOYO/ROHO:

Elewa na ufahamu ewe muislamu kwamba kama ambavyo mwili huugua na kupatwa na maradhi mbali mbali.

Ambayo pengine husababisha kifo kwa mwili huo au udhaifu wa mwili, kama maradhi hayo hayakudirikiwa kwa tiba muafaka.

Hivi ndivyo zilivyo roho za wanadamu ambazo uhai wa kiwiliwili unazitegemea, kwani bila ya roho kiwiliwili hakina uhai.

Roho nazo hushambuliwa na maradhi ya kiroho, kinafsi na kimoyo.

Maradhi haya ni kathiri (mengi) katika roho (nafsi) za wanadamu kuliko tunavyoweza kufikiri na kuwaza.

Kuna maradhi ya unyonge, dharau, unafiki, kibri na riyaa. Kadhalika roho/nyoyo zinaugua maradhi ya ubakhili, hasadi, wivu mbaya, choyo, uroho, tamaa (uchu) wa mali na madaraka na mengi mengineyo.

Yote haya ni maradhi ambayo huyafanya maisha ya mwanadamu kuwa mithili ya Jahanamu isiyokalika hata kwa sekunde moja.

Unaitazamia vipi nafsi ( roho) ya mnafiki kupata neema ya kutulia kupumzika wakati ambapo lengo la unafiki ni fisadi na uharibifu?!

Vipi itapata utulivu na makini nafsi ya mtu bakhili wakati ambapo maisha yake yamezungukwa na kutoa na kutumia.

Na yeye hupenda kukusanya na kulimbikiza bila ya kutaka kutoa wala kutumia?! I wapi basi dawa ya maradhi haya hatari, maovu na machafu yanayouangamiza utu wa mwanadamu?

Aya tukufu tuliyoifungulia somo letu hapo juu inatueleza na kutupa dawa na tiba pekee na sahihi ya maradhi haya chukivu kwa Allah.

Lakini wapi, yu wapi mwanadamu wa kuitumia dawa hii imponye na kumkinga na maradhi haya yanayomvua ubinadamu wake na kumvika unyama.

Sote tumeghafilika na dawa hii kama kwamba hatuihitajii na tutaishi milele katika ulimwengu huu.

Tambua na ujue kuwa muislamu kamili, mwenye akili timamu ni yule anayeweza kuiepusha na kuitakasa nafsi yake na maradhi haya hatari ya moyo (roho).

Atafanya hivyo kwa kukisoma kitabu kitukufu cha Mola wake mara kwa mara na kuyatekeleza yote yaliyomo ndani yake kivitendo.

Kwa kuzisimamisha swala tano kama itakiwavyo sambamba na kumtaja (kumdhukuru) Bwana Mlezi wake.

Na kumtakia rehema na amani Mtume wake (kumswalia) asubuhi, mchana, jioni na usiku.

 Hakika Qur-ani Tukufu na dhikri (utajo) ya Allah ni mizizi mitatu ambayo kwa pamoja hutengeneza dawa mujarabu ya kiroho.

Ambayo hutoa tiba isiyo shaka kwa maradhi yote ya moyo/roho.

Ikiwa hivi ndivyo hebu na tujiulize: Kwa nini leo dawa hii imepoteza nguvu yake miongoni mwetu na haiwatibu ila wachache tu, pamoja naukweli kuwa tupo wagonjwa wengi tuihitajiayo?!

Ni kwa nini leo, dawa hii haina athari kwetu, haitutibu pamoja na kuitumia kwetu japo kimatatizotatizo?!

 Leo tuna wasomaji wazuri tu wa Qur-ani ambao wamehifadhi sehemu kubwa tu ya Qur-ani kama si Qur-ani nzima.

Mbona hawa hawana tofauti na watu wengine katika mwenendo, matendo na kauli na kuzama katika ulimwengu?!

Huzioni kabisa adabu za Qur-ani waisomayo au kuihifadhi katika utendaji wao wa kila siku, uwe ni ule wa kibinafsi au wa kijamii.

Ni nadra sana kumuona fundi, mfanyakazi, mfanyabiashara na…na…, swala yake imemzuilia na ghushi (udanganyifu/utapeli).

Uvunjaji wa ahadi, viapo vya uongo na utendaji mbaya wa majukumu yake.

Wala hatujamshuhudia mtu mwenye mwenendo mbaya akiingia msikitini kuswali, kisha akatoka akiwa kabadilika kwa kuuacha mwenendo mbaya huo.

Swala ikamfunganisha na Allah Muumba na Mruzuku wake, akamcha na kumuogopa kutokana na mwenendo wake huo mbaya na akarudi katika njia ya haki na sawa.

Tunawaona watu wengi wakitenga wakati maalumu wa mchana nausiku wao kwa ajili ya dhikri, nyiradi na kusoma Qur-ani.

Hulipupia hili sambamba na kuchunga utekelezaji wake bila kuchelewa wala kuzembea.

Wako pia wanaokwenda na kurudi katika halaqah (daira/vikao) za dhikri na elimu. Kisha pamoja na juhudi zao zote hizi, bado ibada zao hizi haziwapi nafuu ya kuyaepa na kuyaepuka maasi.

Kwa upande mmoja wanaonekana wanamtii Mola wao na kwa upande mwingine wanamuasi bila ya haya wala soni.

Ni kwa nini basi watu hawa hawanufaiki na ibada zao hizi wanazozifanya usiku na mchana?!

Wana nini wagonjwa hawa, dawa wanatumia lakini hawaponi bali pengine maradhi yao ndio huzidi! Wamepata dawa lakini wamenyimwa kupona!

Ni kweli kuwa dawa kazi yake ni kuponya, lakini vipi umtazamie kupona mtu atumiaye dawa bila ya kupata virutubisho vyote muhimu vihitajikavyo mwilini!

Ni wazi kuwa dawa hii itageuka na kuwa sumu, kwa hivyo badala ya kutibu itaua tu na si vinginevyo.

Hali kadhalika ibada na twaa zote haziwezi kumfikisha muhusika katika lengo lililokusudiwa. Ambalo ni kumpa manufaa na kumuondoshea madhara kama hazikutekelezwa kwa usahihi kwa mujibu wa muongozo na sheria.

Utekelezaji sahihi wa ibada kama alivyoamrisha Allah na kufundishwa kimatendo na kauli na Mtume wake.

Ndio chakula kinachotakiwa kitumike pamoja na dawa ili mgonjwa aweze kupona. Kwa hivyo linalodhihirika ni kwamba hao Dhaakirina (wenye kumdhukuru Allah), waswaliji na wasomaji wa Qur-ani.

Wao wenyewe ndio wamejidhulumu faida (dawa) na matunda ya ibada zao. Kwa nini, kwa sababu ya utekelezaji wao mbovu, kuacha adabu na mambo ya wajibu (msingi) katika ibada zao.

Maadamu msomaji wa Qur-ani hajishughulishi na kukifahamu akisomacho na kisha kukifanyia kazi.

Vipi Qur-ani hii itakuwa dawa ya kumponya maradhi yake ya roho/nafsi! Na muda wa kuwa swala leo imekuwa kwa watu wengi ni ada na mazoezi tu ya viungo kuliko kuwa ibada.

Leo utamuona mtu akiswali haraka haraka, amejawa na fadhaa, hana utulivu wala unyenyekevu.

Akirukuu, kusujudu na ilhali kichwa chake kimejaa wasiwasi na shughuli zake. Hafahamu na wala hazingatii anachokisema ndani ya swala yake. Ni vipi basi mtu huyu aingiaye ndani ya swala kwa mwili wake tu, na moyo na akili yake vikiwa nje ya swala.

Kisha swala hii ndio iwe dawa na tiba kwa mtu huyu?!

Ni vipi swala hii iliyokosa roho yake, imkanye na kumkinga mwenye kuiswali na mambo maovu na machafu?!

Unaitazamia vipi swala hii iwe ni kiungo baina ya mja na Mola wake? Hali ni hii kwa dhikri inayofanywa kwa ulimi tu na moyo na akili vikawa mbali na dhikri hiyo. Dhikri ya namna hii ni: “…NI KAMA MAVUMBI YALIYOTAPANYWA (yaliyotawanywa)”. [25:23]

Yana faida gani basi mavumbi hayo isiyokuwa madhara!

Hivi ndivyo zilivyo ibada zote, ziwe ni za fardhi au zile za suna, zote zinatakiwa ziwe na kiwiliwili na roho.

Ama kiwiliwili cha ibada ni zile harakati (matendo) zake za kimaumbile zinazoambatana na kanuni/misingi ya Fiq-hi katika kutengenea na kusihi kwake.

Na roho ya ibada yo yote ile ni moyo kuwa hadhiri kiasi cha kumuona au kuwa na hisia kuwa Allah yu mbele yake.

Akili izingatie na kujua yote yasemwayo na kutendwa kwa muongozo na amri yake. Kwa hivyo utaona kiwiliwili hakikamiliki bila ya kuwa na roho na roho pia ili iweze kutambulika inahitajia kiwiliwili.

Muislamu analazimika kutambua anapoinua mikono yake na kuleta Takbiratul-Ihraamu ambayo huashiria kuwemo ndani ya swala.

Atambue kwamba kitendo chake hicho kinamaanisha kuitupa nyuma ya mgongo wake dunia na vyote vilivyomo ndani yake.

Na kwamba amekuja mbele ya yule ambaye ni Mtukufu na Mkubwa kuliko vitu vyote. Muumini atambue kwamba swala haikuitwa “swala” ila ni kutokana na kuwa kwake “swila”-kiungo cha mawasiliano baina ya mja kiumbe na Mola Muumba wake.

Faida na matunda ya swala yatakuja kwa kadri ambavyo mja anavyoijua swala na jinsi anavyozitekeleza nguzo, sharti na suna zake.

Sambamba na kujiepusha na yenye kuibatilisha na kuifisidi. Mja hapati jazaa ya swala yake ila kwa kadri atakavyokuwemo ndani ya swala.

FAIDA YA SWALA: SEHEMU YA KWANZA

HII NDIYO DAWA, PONYO (POZO) LIKO WAPI?

Allah Mola Mwenyezi anasema:

“SOMA ULIYOLETEWA WAHYI KATIKA KITABU (hiki ulicholetewa) NA ISIMAMISHE SWALA. BILA SHAKA SWALA (ikiswaliwa vilivyo) HUMZUILIYA HUYO (mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU, NA KWA YAKINI KUMBUKO (utajo) LA ALLAH (lililomo ndani ya swala) NI JAMBO KUBWA KABISA (la kumzuilia mtu na mabaya) NA ALLAH ANAJUA MNAYOYATENDA”. [29:45]

Huenda ukajiuliza: Mbona/kwa nini yameamrishwa mambo mawili katika kauli hii ya Allah; kusoma kitabu (Qur-ani) na kusimamisha swala?

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *