Hii ni rukhsa inayompa msafiri nafasi ya kuzijumuisha swala mbili na kuziswali katika wakati wa mojawapo ya swala mbili hizo.
Ushahidi na dalili juu ya rukhsa hii ya kujumuisha unapatikana katika hadithi nyingi miongoni mwake ni hadithi hii:-
Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas–Allah awawiye radhi-amesema:
“Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akijumisha baina ya swala ya adhuhuri na ile ya alasiri anapokuwa safarini na akijumuisha baina ya Maghribi na Ishaa”. Bukhaariy
Ujumuishaji swala umegawanyika migawanyiko miwili kama ifuatavyo:-
A/. UJUMUISHAJI WA KUTANGULIZA
Hili ni zoezi la kuzijumuisha swala mbili; swala ambayo umeingia wakati wake na ile ambayo haujaingia wakati wake bado na kuziswali swala mbili hizo pamoja katika wakati wa swala hii ambayo umeingia wakati wake.
Mathalan kuzijumuisha swala za Adhuhuri na Alasiri ukaziswali zote mbili katika wakati wa Adhuhuri.
Kwa kujumuisha huku utakuwa umetanguliza kuiswali Alasiri kabla ya kuingia wakati wake na huo ndio ‘ujumuishaji wa kutanguliza’.
B/. UJUMUISHAJI WA KUAKHIRISHA
Hili pia ni zoezi linalohusisha ujumuishaji wa swala mbili. Swala ya kwanza tayari umetoka wakati wake na ya pili umeingia wakati wake.
Ukaziswali swala mbili hizi katika wakati wa swala hii ya pili. Mathalan kuzijumuisha swala za Adhuhuri na Alasiri, ukaziswali swala mbili hizi katika wakati wa Alasiri .
Kwa kujumuisha huku utakuwa umeakhirisha kuiswali swala ya Adhuhuri katika wakati wake na kuiswali wakati wa Alasiri. Hiyo ndio maana ya ‘ujumuishaji wa kuakhirisha’.
Ujumuishaji huu wa kutanguliza na ule wa kuakhirisha unatokana na kitendo cha Mtume. Imepokelewa kutoka kwa Muaadh–Allah amridhie–kwamba Mtume–Rehema na Amani zimshukie–alikuwa katika vita vya Tabuuk.
“Anapoanza msafara kabla jua halijapanda huiakhirisha adhuhuri ili aijumuishe na Alasiri na kuziswali pamoja (ujumuishaji wa kuakhirisha).
Na unapoanza msafara baada ya kupinduka jua, huswali Adhuhuri na Alasiri pamoja (katika wakati wa Adhuhuri), kisha ndio huenda zake (ujumuishaji wa kutanguliza).
Na alikuwa anapoanza msafara kabla ya Magharibi, huiakhirisha swala ya Magharibi ili aiswali pamoja na Ishaa. Na anapoanza msafara baada ya Magharibi, huiharakisha swala ya Ishaa, akaiswali pamoja na Magharibi”. Abuu Daawoud, Tirmidhiy & wengineo.
SWALA ZINAZORUHUSIWA KUJUMUISHWA
Swala zinazoguswa/zinazohusika na rukhsa hii ya kujumuisha miongoni mwa swala tano za fardhi ni hizi zifuatazo:-
Adhuhuri na Alasiri, na
Magharibi na Ishaa tu.
Hizi ndizo swala ulizopewa rukhsa ya kuzijumuisha ukitaka kufanya hivyo.
Ni mamoja kuwe kujumuisha huko ni kwa kutanguliza au kwa kuakhirisha kama alivyofanya Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie.
Kwa hivyo basi haisihi kisheria kuijumuisha swala ya Sub-hi (Alfajiri) na swala iliyo kabla yake ambayo ni Ishaa.
Au kuijumuisha na swala iliyo baada yake ambayo ni Adhuhuri. Kadhalika hakuna kujumuisha baina ya swala ya Alasiri na Magharibi.
SHARTI ZA KUJUMUISHA
Kila ujumuishaji; ujumuishaji wa kutanguliza na ujumuishaji wa kuakhirisha una sharti zake ambazo inatakikana zichugwe ili ujumuishaji usihi. Hebu sasa na tuzitaje sharti za kila ujumuishaji tukianzia na:-
a) SHARTI ZA UJUMUISHAJI WA KUTANGULIZA:
UTARATIBU BAINA YA SWALA MBILI HIZO
Mjumuishaji wa swala mbili anatakiwa aanze kuiswali swala ya mwanzo yaani swala ya wakati ule. Kisha ndio aiswali ile nyingine ambayo siyo ya wakati ule.
Kwa mfano mtu ameamua kuitumia rukhsa ya kujumuisha kwa kuzijumuisha swala za Adhuhuri na Alasiri katika wakati wa Adhuhuri.
Kiutaratibu anatakiwa aanze kuiswali swala ya Adhuhuri, kwani ndio swala ya wakati ule. Baada ya kumaliza ndio aswali Alasiri ambayo wakati wake haujaingia bado.
NIA YA KUJUMUISHA KABLA YA KUMALIZIKA KWA SWALA YA MWANZO:
Mjumuishaji anapaswa kunuia kuijumuisha swala ya pili (Alasiri) na hii ya mwanzo (Adhuhuri) kabla hajatoa salamu kuashiria kumalizika kwa swala hii ya mwanzo aliyoanza kuiswali. Lakini inapendelewa kuwa nia hiyo ya kujumuisha pamoja na Takbira ya kuhirimia swala ya mwanzo.
KUFULULIZA BAINA YA SWALA MBILI HIZO.
Mjumuishaji hapaswi kuacha mwanya mkubwa baina ya swala mbili hizi anazozijumisha kwa kuleta dua au kuswali suna katikati yake.
Bali anatakiwa baada ya kutoa salamu ya swala ya mwanzo, ainuke na kuanza kuswali swala ya pili. Angalia ikiwa ataacha mwanya mkubwa na ukubwa wa mwanya utarejea katika ada.
Au iwapo ataichelewesha swala ya pili bila ya sababu yo yote (dua/suna) utabatilika ujumuishaji wake huo na kutamuwajibikia kuiakhirisha swala hiyo ya pili mpaka uingie wakati wake na aiswali ndani ya wakati wake huo na sio sasa.
Haya yote ni kwa kumfuata Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar–Allah awawiye radhi– amesema:
Nilimuona Mtume–Rehema na Amani zimshukie– anapokuwa na safari ya haraka huiakhirisha swala ya Magharibi na kuiswali rakaa tatu (kama kawaida), kisha hutoa salamu.
Halafu hakai kitambo kirefu ila hukimu (Iqaamah) Ishaa na kuiswali rakaa mbili (Qaswru), kisha hutoa salamu”. Bukhaariy
KUWEMO SAFARINI MPAKA KUVAANA NA SWALA YA PILI.
Ni sharti swala mbili zote zinazojumuishwa ziswaliwe na il-hali mjumuishaji angali safarini, hii ni kutokana na kufungamana kwa rukhsa ya kujumuisha na safari.
Yaani rukhsa hii hutumika safarini, kwa mantiki hii basi isitokee mojawapo ya swala jumuisho kuswaliwa safarini na nyingine nje ya safari.
b) SHARTI ZA UJUMUISHAJI WA KUAKHIRISHA:
Kujumuisha swala kwa kuakhirisha kunatawaliwa na sharti mbili zifuatazo:-
KUNUIA KUJUMUISHA SWALA YA MWANZO NDANI YA WAKATI WAKE.
Msafiri anayekusudia kuzijumuisha swala za Adhuhuri na Alasiri
mjumuisho wa kuakhirisha, mathalani. Inamapasa kutia nia ya kuijumuisha swala hii ya mwanzo inayoakhirishwa (Adhuhuri) ili iswaliwe pamoja na Alasiri ndani ya wakati wa Alasiri.
Atie nia ya kuijumuisha Adhuhuri ndani ya wakati wake, yaani wakati wa Adhuhuri. Angalia ikiwa hakutia nia ya kujumuisha Adhuhuri na Alasiri kwa kuakhirisha mpaka ukatoka wakati wa Adhuhuri na kuingia Alasiri.
Swala hii ya Adhuhuri itakuwa katika dhima yake kwa njia ya “kadhaa” inayoambatana na dhambi ya kuiswali nje ya wakati wake.
KUWEMO SAFARINI MPAKA KUMALIZA KUZISWALI SWALA ZOTE MBILI PAMOJA
Kama tulivyotangulia kueleza kuwa rukhsa hii ya kujumuisha inafungamana na safari.
Ni sharti swala mbili hizi zinazojumuishwa kwa kuakhirishwa ziswaliwe zote ndani ya safari.
Katika ujumuishaji huu wa kuakhirisha haikupokelewa sharti ya utaratibu, bali mjumuishaji ana khiyari ya kuanza na swala yo yote miongoni mwa mbili hizo aitakayo.