“RAMADHANI IMESHA KWENDA ZAKE, SASA NI FURSA YA KUFAIDIKA NA MAFUNDISHO YAKE”

RAMADHANI IMESHA KWENDA ZAKE, SASA NI FURSA YA KUFAIDIKA NA MAFUNDISHO YAKE”

Hakika sifa zote njema ni stahiki na milki yake Allah ambaye Yeye ndiye Mkusudiwa wa kila jambo, hakuzaa wala hakuzaliwa wala hana anaye fanana naye hata mmoja. Na Baraka, Rehema na Amani zimuendee Nabii wake Muhammad, Aila yake na Maswahaba wake ambao ulizidi mno uchaMngu wao baada ya Ramadhani na wote walio ufuata mwendo wao huo mwema mpaka siku ya Kiyama.

Ama baadu,

Wapendwa ndugu zetu katika Imani.

Assalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

Kwa namna ya kipekee na kwa mara nyingine tena, tuseme himda na sifa zote njema zimuendee Allah ambaye ametuneemesha kuishi ndani ya Ramadhani, tukafunga na hatimaye tumeikamilisha ibada tukufu ya funga kwa uwezo, ukarimu na fadhila zake kuu. Ewe Mola wa haki! Tujaalie kuwa miongoni mwa wenye kuzishukuru neema zako na wenye kuzikumbuka fadhila zako. Tusamehe dhambi zetu hali ya kuwa Wewe ndiye Mbora wa kusamehe. Na utuwezeshe kuendelea kukuabudu hata baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhani mpaka yatukute mauti nasi tukiwa katika ibada.

Mpendwa ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu!

Ni jambo lisilo hitaji dalili/ushahidi kwamba ni siku chache tu zimepita tangu kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na tayari tumesha sherehekea Eidil-Fitri katika kuishukuru neema ya Ramadhani tuliyo tunukiwa na Allah. Baada ya kumalizika kwa Ramadhani ambayo panapo majaaliwa yake Allah itarudi tena mwakani lakini mimi na wewe hatuna dhamana ya kuwa hai mpaka tutakapo jiwa na Ramadhani ya mwakani. Ikiwa tunaukiri na kuukubali ukweli huo, basi sasa ni wakati muwafaka na munasibu kwetu sote kila mmoja wetu ajiulize:

  • Hali yangu ikoje baada ya Ramadhani?

Ni fursa yetu sasa kulinganisha hali zetu zilivyo kuwa ndani ya Ramadhani na hali zetu sasa hivi baada tu ya Ramadhani, je bado tunayo harufu ya Ramadhani?! Ndani ya Ramadhani tulikuwa:

  • Tunaijaza misikiti yetu hadi ikatutapika katika swala za jamaa, je bado hilo linapatikana kwetu?
  • Tunaamka kuswali usiku ili kujikurubisha kwa Mola Muumba wetu na tukamkabidhi yetu ambayo Yeye anayajua mno kuliko sisi, je zoezi hilo bado linaendelea kwetu?
  • Tunasoma sana Qur’ani si tu misikitini bali hata ndani ya vyombo vya usafiri na mahala petu pa kutafutia riziki zetu, je bado tunaishi na Qur’ani?
  • Tunafanya dhikri sana katika hali zetu zote; tukiwa tumesimama, tumekaa au tunatembea. Je, bado ndimi zetu zi majimaji katika kumdhukuru Allah?
  • Tunaomba dua sana, tunaonesha uhitaji wetu mkubwa kwa Allah na kwamba bila ya Yeye hatuna letu jambo. Je, bado tunamkabidhi Mola wetu haja na shida zetu?
  • Tunatoa sadaka kwa wingi kwa kingi na kichache tulicho ruzukiwa na Mola wetu, je moyo huo wa ukarimu bado unaishi miongoni mwetu?
  • Tunawaunga ndugu zetu, tunawahurumia na kuwasaidia wajane, mayatima, wagonjwa na wale wasio jiweza miongoni mwetu. Je, ukarimu huo bado unaifunika jamii yetu? Na ….. Na …..

Mpendwa ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu!

Hakuna mwenye ujasiri wala uthubutu wa kuhoji au kupinga kwamba ndani ya Ramadhani, sote sisi tulionja utamu na ladha ya imani na tuliijua hakika ya funga. Kama ambavyo tulionja ladha ya chozi linalo dondoka katika kumuomba Allah msamaha kutokana na madhambi tuliyo yatenda na utamu wa kunong’ona na Allah faraghani katika usiku ule mwingi ambapo utamu wa usingizi unakolea, wakati ambao dunia iko kimya, ni mja tu na Mola wake. Tulikuwa tunaswali swala ya mtu ambaye tuo na raha yake imewekwa ndani ya swala, tulikuwa tunafunga swaumu ya mtu aliye uonja utamu na ladha ya ibada hiyo. Tulikuwa tukitoa katika kuwasaidia wenzetu utoaji wa mtu asiye ogopa kuishiwa kwa sababu ya kutoa na tulikuwa … tulikuwa …. tukiyatenda mengi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ulio kwenda zake na makontena ya bidhaa zetu hizo, kuyapeleka kwenye bandari ya haki ili kila mmoja wetu alipwe kutokana na thamani ya bidhaa zake.

Namna hivyo ndivyo tulikuwa tunazunguka katika medani ya matendo mema ya kheri kiasi cha kufikia mmoja wetu kutamani kufa akiwa katika hali bora hiyo kutokana na utamu wa imani na ladha ya utii iliyomo ndani yake.

Mpendwa ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu!

Naam, ni kweli Ramadhani imekwenda zake na hazijapita siku nyingi tangu kuondoka kwake, huenda kwa masikitiko na majonzi makubwa yule aliye ingizwa msikitini na Ramadhani na akawezeshwa na Allah kuswali swala tano, tena katika jamaa. Huenda amesha itupa mkono ibada mama hiyo ambayo ndio amali ya kwanza atakayo ulizwa mja siku ya Kiyama, ibada ambayo kutengenea kwake ndio kutengenea kwa baki ya ibada nyingine. Huenda yule mla riba aliye kemewa na utukufu wa funga ya Ramadhani, akaacha riba, huenda masikini mja huyo kwa hasara ya nafsi yake mwenyewe amesha rejea tena kwenye maisha yake machafu ya ulaji riba. Huenda pia yule aliye upa talaka muziki ndani ya mwezi wa Ramadhani, tayari amesha viondoa viwambo vya masikio yake na sasa analala na kuamka na muziki, Laa haula walaa quwwata illa billaah! Huenda yule aliye uheshimu mwezi wa Ramadhani, akaacha ulevi wa pombe, sigara, mirungi na pengine madawa ya kulevya, akawa mtu mzuri, huenda mja huyo tayari amesha yarudia maisha yake hayo ya kabla ya Ramadhani. Huenda yule mzinifu aliye agana na mzinifu mwenzake kuipisha Ramadhani, tayari amesharudiana na mchafu mwenzake huyo kuendelea na uchafu na uovu wao huo. Na … Na …. Hebu sasa tuwaombe ndugu zetu hao kwa mapenzi makubwa na huruma ya kweli kwao, kila mmoja wao ajiulize:

  • Mpaka lini nitajenga nyumba na kisha kuibomoa, ni lini nitakamilisha ujenzi wa nyumba yangu hiyo na kuishi ndani yake?!
  • Mpaka lini nitaendelea kumuasi Mola wangu, nini utakuwa mwisho wa uasi wangu huu na tangu nimeasi nimefaidika nini?!
  • Mpaka lini lile nililo katazwa na Mola wangu ndilo ninalitenda na lile nililo amrishwa silitendi?!
  • Huku kuasi kwangu kunamdhuru Mola Muumba wangu au kunanidhuru mimi mwenyewe na jamii inayo nizunguka?!

Ewe mwanaadamu! Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu?” Al-Infitwaar [82]:06

Naam, tunalo kusudia lifahamike na kueleweka na kila mmoja wetu ni kwamba sisi hatusemi baada ya Ramadhani tuwe kama tulivyo kuwa ndani ya Ramadhani vile vile, hilo hatuliwezi kwa sababu baraka zilizomo ndani ya Ramadhani ambazo ndizo zinatusaidia kuwa vile tulivyo kuwa, hazipatikani nje ya Ramadhani. Lakini tunacho kusudia kusema ni kwamba tusiache ibada baada ya kuondoka kwa Ramadhani, tukaacha kutenda matendo mema. Bali tuendelee kwa kadiri ya uweza wetu kuswali swala za faradhi jamaa misikitini, kuamka kuswali usiku, kutoa sadaka kwa kidogo au kikubwa tulicho nacho, kuwahurumia na kuwasaidia wajane, mayatima, wagonjwa na wale wasio jiweza miongoni mwetu. Tusiache kufunga mpaka Ramadhani ya mwakani, bali tuendelee kufunga funga za Sunna na ndio sababu tukawekewa funga ya siku sita za Shawwali (Mfunguo Mosi), funga ya Jumatatu na Al-Khamisi, funga ya siku nyeupe, funga ya siku tisa za Dhul-Hijja, funga ya Ashura na nyingi nyinginezo.

Mpendwa ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu!

Ramadhani imekuja na tayari imesharejea kwa Mola wa Ramadhani, sisi tulio letewa fursa hiyo Ramadhani, tujiulize: Tumefaidikaje nayo?

Naam, tayari tumekwisha iaga Ramadhani; mwezi wenye baraka, mwezi wa Qur’ani, mwezi wa uchaMngu, mwezi wa subira, mwezi wa jihadi, mwezi wenye rehema, mwezi wa msamaha wa dhambi, mwezi wa kuachwa huru na moto. Basi ni kipi tulicho kichuma katika matunda yake mabivu na matamu mno? Tujiulize:

  • Je, tumeupata uchaMngu ambalo ndilo lengo mama la ibada ya swaumu ya Ramadhani?
  • Je, tumehitimu katika chuo cha Ramadhani na tumefaulu kupata shahada ya uchaMngu?
  • Je, tumejifunza ndani ya chuo hicho subira kwa pande zake mbili; subira katika kuyaacha maasi na subira katika kutenda mema?
  • Je, tumezilea ndani yake nafsi zetu katika jihadi kwa aina zake zote?
  • Je, tumepambana na nafsi zetu na matamanio yake hata tukayashinda au sisi ndio tumepigwa mweleka na mazoea na mambo mabaya ya kuiga?
  • Je, ndani ya Ramadhani tulikwenda mbio kutenda yale ambayo ndio sababu inayo pelekea kupata rehema, maghufira na kuachwa huru na moto au tulibweteka tu hata Ramadhani ikaondoka?
  • Na je, ………….. Na je …………… Maswali ni mengi, mengi mno yanayo pita moyoni na fikrani mwa kila muislamu aliye mkweli ambayo yanahitaji majibu ya kweli. Na majibu hayo ndio kipimo cha ufaulu au ufeli wako katika chuo cha Ramadhani.

Naam, ndugu Muislamu-Allah akurehemu-jiulize tena: Umefaidika nini na Ramadhani?

Ni haki yako, na ni wajibu wako kufaidika na Ramadhani. Kwa sababu hiyo Ramadhani ni chuo cha Kiimani, ni kituo cha kiroho ambapo muislamu huchukua masurufu ya mwaka mzima; miezi kumi na moja baada ya Ramadhani. Hali kadhalika ni khasara yako, kutofaidika na Ramadhani. Basi ni lini utawaidhika, utazingatia na kufaidika na Ramadhani?! Kama haikuwa Ramadhani hii iliyo kwenda zake, ni lini basi utaubadilisha mtindo wako wa maisha ukawa kama vile ulivyo kuwa ndani ya Ramadhani hata kama ni kwa thumni (1/8) yake?!

Ewe ndugu yetu ambaye Ramadhani haikuwa ni sababu ya kukubadilisha kutoka kwenye uovu/uasi kukupeleka kwenye wema/utii, ni dhahiri kuwa bado hujaijua Ramadhani ni nini au hukufunga vile itakiwavyo hasa. Kwa hivyo basi, unapaswa kuwaendea wanawazuoni ukae kitako wakufundishe ibada ya swaumu, uijue ili upate kufunga kwa namna aliyo fundisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Ni kwa kufanya hivyo tu, ndio utaithamini Ramadhani na utafunga ndivyo ndivyo na hapo ndipo utapata kufaidika nayo. Na kama si hivyo, Ramadhani zitakuja na kuondoka na kukuacha kama zilivyo kukuta. Tambua, ufahamu na ujue kwamba Ramadhani imekusudiwa kuwa ni chuo cha mabadiliko ya kiroho kwa waumini, athari ya mabadiliko hayo ya kiroho iendelee kuonekana baada ya Ramadhani na hivyo hasa ndivyo ilivyo kusudiwa. Mabadiliko hayo yakikoma mara tu baada ya kuswaliwa kwa swala ya Eid, hilo halipungui kuwa ni riyaa na kufuru, kwani yule Mungu aliye kuwa akiabudiwa ndani ya Ramadhani ndiye huyo huyo tunatakiwa kuendelea kumuabudu nje ya Ramadhani. Ramadhani ni mwezi wa mabadiliko, tunatakiwa baada ya kuondoka kwake tuwe tayari tumeshakuwa na mabadiliko katika matendo yetu, tabia zetu, silka zetu, ada zetu, uneni wetu na hata ufikiriaji wetu na mabadiliko kwanza tuyatake na tuyaanze sisi, kisha ndipo Allah ataleta taufiki yake, tuzingatie: “… Hakika Allah habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo nafsini mwao…”. Ar-ra’ad [13]:11

Mpendwa ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu!

  • Wala usiwe kama mwanamke anaye uzongoa uzi wake baada ya kwisha usokota ukawa mgumu.

Angalia, ukiwa wewe ni miongoni mwa wale walio faidika na Ramadhani na ukawa umepambika na sifa za wachamNgu wanao zalishwa na Ramadhani. Ukaifunga Ramadhani kikweli, vile itakiwavyo na Mola na kwa namna iliyo fundishwa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Na ukaamka kuswali usiku kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mola wako na ukajipinda katika kupambana na nafsi yako ili iache kutenda yale machafu inayo yapenda na badala yake itende yale mema mazuri isiyo yapenda. Ikiwa hivyo ndivyo ulivyo kuwa ndani ya Ramadhani, basi muhimidi na umshukuru Allah na tena usichoke kumuomba akuwezeshe kuthibiti na kuendelea na hali hiyo mpaka pale atakapo kufisha baada ya kumalizika kwa muda alio kukadiria kuishi tangu azali.

Ogopa, tena epuka na tahadhari kabisa kuuzongoa (kuufumua na kuunyambua nyambua) ule uzi ulio taabika kuusokota ndani ya kipindi chote cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Unaonaje na uwe mkweli katika maono yako hayo. Utamuonaje na kumfikiriaje yule mwanamke aliye pigiwa mfano ndani ya Qur’ani katika Surat An-Nahli [16] aya ya 92. Mwanamke huyo alisokota nyuzi kisha akafuma kutokana na nyuzi hizo nguo, baada ya nguo kukamilika, ikampendeza na kuyafurahikia matokeo ya kazi yake hiyo ya ufumaji. Tahamaki akachukua mkasi na kuanza kuikata kata nguo ile nzuri vipande vipande pasina sababu. Unaonaje na unafikiri watu na wewe ukiwa miongoni mwao, watasemaje kuhusiana na mwanamke huyo?! Bila ya chembe ya shaka watasema: Mwanamke huyo anahitaji kufanyiwa uchunguzi wa akili yake, kwani hapungui kuwa ni mwendawazimu, mwehu au punguani.

Mfano wa mwanamke huyo, ndio hali ya yule mtu aliye funga Ramadhani na kuwa mtaabadi mno ndani yake, kisha mtu huyo baada ya Ramadhani akarejea kwenye maasi, ufuska na akaacha kumtii Mola wake katika maamrisho na makatazo yake na akaacha amali njema kubwa yao ikiwa ni swala. Baada ya kuneemeka kwa neema ya twaa ndani ya Ramadhani na ladha ya kunong’ona na Mola wake katika ibada za faragha/siri; ibada za usiku, kisha tena mtu huyo baada ya Ramadhani anarejea kwenye moto wa maasi na uovu!! Ni kweli kuwa mtu huyu anataka achukuliwe na ahesabiwe kuwa miongoni mwa wale watu wabaya waovu ambao hawamkumbuki na wala hawamjui Allah Mola Muumba wao ila ndani ya Ramadhani tu?! Kwa nini basi ewe masikini mja wa Allah, unajichagulia mwenyewe, tena kwa hilaki yako mwenyewe, halafu ni kwa hasara yako mwenyewe, unajichagulia kuwa katika wale ambao baada tu ya Ramadhani:

  • Ameitupa swala za jamaa misikitini baada tu ya kuswali swala ya Eid, hapo ndio amepeana mkono wa kwaheri na misikiti. Huyo haswali tena mpaka Ramadhani ya mwakani panapo majaaliwa yake Mola. Hasara iliyoje kwa waja wa Allah, ndani ya Ramadhani misikiti ilikuwa ikijaa watu katika swala ya Tarawehe ambayo hiyo ni swala ya Sunna. Baada ya Eid tu misikiti inakonda, swala za jamaa; swala tano hazina tena waswaliji, ajabu iliyoje hizi swala za faradhi zimetupwa wakati ile ya Sunna ilikimbiliwa?!
  • Amerejea tena kule kule kwenye nyimbo na muziki aliko kuwa kabla ya Ramadhani na huyo ndiye yule aliye jiweka mbali na muziki ndani ya kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kutambua ya kwamba hiyo ni kazi ya shetani na haimpendezi Allah. Lakini mara tu baada ya kuswali Eid, anarudi kule kule kwenye kile anacho kiita mwenyewe starehe yake au “hobby” yake.
  • Amelitupa vazi la stara alilokuwa akilivaa ndani ya kipindi cha mwezi wa Ramadhani kutokana na utukufu wa mwezi huo, na vazi hilo lilimbadilisha hata baadhi ya tabia zake. Lakini huyo huyo baada tu ya kuswali swala ya Eid, akalivua vazi hilo la stara na kuyarudia mavazi yake yenye kuleta ushawishi wa maovu kwa kila amuonaye.
  • Na … Na … Wote hawa tunawaomba waizingatie pamoja nasi kauli yake Allah:

Basi ama yule aliye zidi ujeuri. Na akakhiari maisha ya dunia. Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake. Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuiliya nafsi yake na matamanio. Basi huyo, Pepo itakuwa ndio makaazi yake”. Al-Anaziat [79]:37-41

Mpendwa ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu!

Tambua na ufahamu ya kwamba Ramadhani ni neema yako uliyo tunukiwa na Mola wako, ikiwa unalikubali hilo, basi neema haishukuruwi kwa kuyatupa na kuyaacha yale yaliyo letwa kwako na neema hiyo. Na wala neema hiyo Ramadhani, haisindikizwi na kuhitimishwa kwa kurejea tena kule kule iliko kutoa neema hiyo. Na wala Allah aliye muwezesha mja wake kufunga na kusimama kuswali usiku ndani ya mwezi wa Ramadhani, hashukuriwi kwa kuitupa ibada na kurejea kwenye maasia. Kufanya hivyo ni alama ya wazi ya kutokukubaliwa kwa amali za mja huyo alizo zitenda ndani ya Ramadhani, ni ishara ya kufeli vibaya mno katika mafunzo ya chuo cha uchaMngu. Kila mmoja wetu anapaswa kujitathimini ili apate kujua, anakwama na kukosea wapi. Kwa nini, mara tu baada ya Eid anarejea tena kule aliko tolewa na Ramadhani. Kwa nini anamkimbilia shetani ambaye siku ya Kiyama atamkana: “Na shetani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Allah alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini, lakini sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Allah. Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu chungu”. Ibraahim [14]:22

Ewe masikini, huyo ndiye shetani unayemkimbilia baada ya Ramadhani huku unamkimbia Mola wako ambaye amekuandalia msamaha na ujira mkubwa: “Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na watiifu wanaume na watiifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoa sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru Allah kwa wingi wanaume na wanawake, Allah amewaandalia msamaha na ujira mkubwa”. Al-Ahzaab [33]:35

Kwa nini anaukimbilia moto ambao kuni zake ni watu na wanaadamu: “Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allah kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa”. At-Tahrim [66]:06 Na anaikimbia pepo ambayo anaambiwa kuhusiana nayo: “Kimbilieni msamaha wa Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyo wekewa walio muamini Allah na Mitume wake. Hiyo ndio fadhila yake Allah, humpa amtakaye. Na Allah ni Mwenye fadhila kuu”. Al-Hadid [57]:21

Naam, kutengana na ibada na kuiacha ile hali njema ya uchaMngu aliyo kuwa nayo mtu ndani ya Ramadhani, hilo halipungui kuwa ni utovu wa shukrani kwa Mola wa Ramadhani na ni kuikanusha na kuipinga neema ya Ramadhani. Inamkinikaje mtu aliye bahatika kuidiriki Ramadhani na akafunga, akajizuia na yale yaliyo halali yake, kisha tena mtu huyo huyo baada tu ya swala ya Eid akavaana na yale aliyo harimishiwa?! Hapana, haimkiniki, huyo kiuhalisia hakufunga swaumu ya Ramadhani bali aliacha kula na kunywa tu. Tunasema hivyo kwa sababu mtu aliye funga swaumu ya hakika; iliyo kidhi matakwa na vipengele vyote vya kisheria, huyo ndiye hufurahia kufungua swaumu siku ya Eid, akamuhimidi na kumshukuru Mola wake kwa kumuwezesha kuikamilisha ibada hiyo ya funga. Pamoja na furaha yake hiyo, mtu huyo hukaa peke yake akalia kwa kuchelea kuwa huenda Allah hajaikubali swaumu yake. Hivyo ndivyo walivyo kuwa waja wema walio tangulia (Salafu), wao hao walikuwa wakilia na kumbembeleza Allah miezi sita baada ya Ramadhani awatakabalie swaumu na ibada zao alizo wawezesha kuzitenda ndani ya Ramadhani. Na tambua ewe ndugu yetu mwema, ya kwamba katika jumla ya alama na kipimo cha kukubaliwa na kupokelewa kwa amali za mja, ni mja huyo kuwa katika hali bora zaidi baada ya Ramadhani kuliko ile aliyo kuwa nayo kabla ya Ramadhani. Na kumuona mja huyo akiyakimbilia na kuyaendea mbio mambo ya twaa.

Mpendwa ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu!

  • Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni, na mkikufuru basi adhabu yangu ni kali”.

Ramadhani ni neema, ikiwa tunakubaliana na hilo, basi kila aliye idiriki Ramadhani kwa mapenzi yake Mola anao wajibu wa kumshukuru Mneemeshaji kwa tunu hiyo. Lau kuwa mja atamshukuru Mola wake haki ya kumshukuru kila anapo mtunukia neema, basi utamuona mja huyo anazidi katika kutenda kheri na kumtii Muumba wake. Si hivyo tu, bali utamuona akijitenga mbali na maasia na shukrani ya kweli ni mtu kuacha kutenda maasia na wala sio kuyakimbilia. Kwa mantiki hiyo basi, tunaweza kusema na si kusema tu bali kusema kwa kinywa kipana kabisa ya kwamba mtu aliye wafikiwa na Allah kuidiriki Ramadhani, na si kuidiriki tu bali akaweza kufunga na kusimama usiku. Huyo katu na aslan, hawezi kuikimbia ibada na matendo ya kheri baada tu ya Eid bali ndio huzidi mno katika twaa na wema, kwa nini inakuwa hivyo ni kwa sababu ya kumshukuru kwake Mola Mneemeshaji hivyo naye anamzidishia mja wake huyo mwenye kumshukuru kama inavyo sema aya hapo juu.

Ndugu yetu uliye mwema-Allah akurehemu-na tulihitimishe jukwaa letu hili la baada ya Ramadhani kwa kunasihiana na nasaha zetu tunasema: Muislamu anao wajibu wa kuendelea kumuabudu Mola wake na kuthibiti katika maamrisho yake katika kuyatenda kwa kadiri ya uweza wake na hali kadhalika athibiti katika makatazo yake kwa kuyaepuka na kuacha kuyatenda. Anapaswa kuwa na msimamo katika dini yake na wala asimuabudu Mola wake vile atakavyo yeye mja bali amuabudu vile atakavyo Mola wake; asimuabudu katika mwezi mmoja tu wa Ramadhani na akamuasi katika miezi kumi na moja baada ya Ramadhani. Asimuabudu Mola wake akiwa mahala fulani na akiwa mahala pengine anamuasi; hamuabudu. Asifanye riyaa akamuabudu Mola wake akiwa pamoja na watu fulani na akiwa peke yake au na watu wengine hafanyi ibada, hilo halifai na wala halikubaliki.

Tena ni wajibu wake mkubwa kujua na kufahamu ya kwamba Mola anaye abudiwa ndani ya Ramadhani ndiye huyo huyo Mola anaye paswa kuabudiwa katika miezi mingine isiyo Ramadhani; anapaswa kuabudiwa ndani ya mwaka mzima, miezi yote, siku zote bali umri wote. Muumini anapaswa kukita mguu wake katika dini ya Allah; amuabudu Mola wake katika pande zote mbili; upande ule wa maamrisho kwa kuyatenda na upande ule wa makatazo kwa kuyaacha na kuyaepuka. Aendelee katika twaa na ibada mpaka akutane na Mola Muumba wake naye akiwa radhi naye, hili la kuendelea na ibada ndilo linalo tajwa na kauli yake Allah Mtukufu pale alipo mwambia Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie: “Basi simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wewe na wale wanao elekea kwa Allah pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo”. Huud [11]:112

Mwisho kabisa tulikunje jamvi la jukwaa letu hili na tuondoke na zawadi ya kauli zake Allah, twende tukazitafakari na kuzifanyia kazi, anasema Mola wetu: “Siku hiyo itakapo fika, hatosema hata mtu mmoja ila kwa idhini yake Allah. Kati yao watakuwamo waliomo mashakani na wenye furaha. Ama wale wa mashakani, hao watakuwamo motoni wakiyayayatika na kukoroma. Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hakika Mola wako Mlezi hutenda apendavyo. Na ama wale walio bahatika, hao watakuwamo peponi wakidumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hicho ni kipawa kisio na ukomo”. Huud [11]:105-108

Na akasema Mola: “Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi, inafunuliwa kwangu ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na mumtake msamaha, na ole wao wanao mshirikisha”. Fusswilat [41]:06

Panapo majaaliwa yake Allah tukutane katika jukwaa la Ramadhani ya mwaka 1443H/2021 huku tukimuomba kwa rehema na fadhila zake atutie katika kundi la wale ambao wanapo ambiwa huambilika, wanapo waidhiwa huwaidhika, wanapo amrishwa huamrishika, wanapo katazwa hukatazika na wanapo lisikia neno jema huliandama na wakalifuata.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *