RAMADHANI HIYOOO INAKWENDA ZAKE, EWE MUISLAMU

Mstahiki wa kuhimidiwa na kutukuzwa ni Allah; Mola Muumba wetu aliye tuambia katika kitabu chake kitukufu: “Hawawi sawa watu wa motoni na watu wa peponi. Watu wa peponi ndio wenye kufuzu”. Rehema na Amani zishuke juu ya Bwana wetu Muhammad bin Abdillah, Aali zake, maswahaba wake na kila aliye itika mwito wake na kufuata maagizo yake mpaka ile siku ya hukumu ya haki.

Ama baadu,

Wapendwa ndugu zetu katika Imani.

Assalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

Tuanze kwa kumuomba Mola wetu Mtukufu atutakabalie amali zetu tulizo zitenda katika siku zilizo kwisha kwenda zake kwa kasi ya moto wa nyika na atuwezeshe kuzidisha kheri katika siku chache hizi zilizo salia za mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kisha tukumbushane ya kwamba tumo na tunaishi ndani ya kumi la mwisho la mwezi mtukufu; kumi la kuachwa huru na moto. Tayari limekwisha pita kumi la mwanzo na siku chache tu zilizo tupa kisigo limeondoka kumi la pili na sasa tunaishi masiku ya kumi la mwisho. Kama tulicheza na kuzembea katika makumi hayo, basi ni wajibu wetu mkubwa kuzinduka na kuitumia vema fursa hii iliyo bakia; kwa wale wapenzi na mashabiki wa mpira, hizi ni dakika za lala salama. Piga ua upate goli, uibuke mshindi au ufungwe upokwe pointi tatu muhimu.

Ewe ndugu mfungaji-Allah akurehemu-muombe Allah na ilhali mwenyewe ukijipinda katika kuyapatiliza masiku machache haya yaliyo bakia ya Ramadhani yako, ni kweli kuna uwezekano mkubwa wa kuja kwa Ramadhani nyingine; Ramadhani ya mwaka 1443. Lakini wewe hauna dhamana ya kuwa hai mpaka Ramadhani hiyo, ninacho taka kusema na kukukumbusha na pasina kuisahau nafsi yangu ni kwamba hii ndio Ramadhani yako uliyo tunukiwa na Mola. Ishukuru neema hiyo kwa kuhakikisha unaitumia kila siku, kila saa, kila dakika na kila sekunde ya hizi siku zilizo bakia katika kumtii na kumridhisha Mola wako ili utakapo rudi kwake umkute naye amekuridhia, unataka nini tena kingine kinacho ishinda radhi ya Allah?! Itumie fursa hii kabla haijakuponyoka, sote tunaona ni namna gani siku zinavyo kwenda mbio, ni jana tu mwezi uliandama tukaanza kufunga, mara hiyo Ijumaa ya kwanza, kisha hiyo ya pili, halafu ya tatu na sasa tunaitazamia ya nne inayo tufungia ukurasa wa Ramadhani ya mwaka 1442H. Kwenda mbio huko kwa siku kunatukumbusha kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Hakitasimama Kiyama mpaka zama zikurubiane (ziende mbio)…”. Tukiyatia akilini maneno haya ya Mtume wa Allah, ni wajibu wetu na sisi kukimbizana na zama kwa kutenda yale yanayo mridhisha Mola wetu ndani yake na kujiepusha na yote yanayo mchukiza. Tukimbizane na zama kwa kujitahidi kuingia katika kundi la wale watu wema ambao Allah anawataja kwa kauli yake tukufu, tusome kwa mazingatio: “Kwa hakika hao ambao kwa kumwogopa Mola wao Mlezi wananyenyekea. Na wake ambao aya (ishara) za Mola wao Mlezi wanaziamini. Na wale ambao Mola wao Mlezi hawamshirikishi. Na wale ambao wanatoa walicho pewa, na hali nyoyo zao zinaogopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi. Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia”. Al-Muuminuun [23]:57-61

Na wale wanao tajwa na Allah kwa kauli yake: “Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachaMngu. Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu, na Allah huwapenda wafanyao wema. Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Allah na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao – na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Allah? – Na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua. Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao”. Aali Imraan [03]:133-136

Muislamu mpendwa-Allah akurehemu-hakikisha mchana na usiku wa Ramadhani yako, unakupitia ukiwa unasoma Qur’ani, ukiwa unauamirisha msikiti kwa kurukuu na kusujudu humo. Ukiwa unaunga udugu, unatengeneza mahusiano yako na Mola wako, mahusiano yako na mkeo, mahusiano yako na ndugu zako, mahusiano yako na Waislamu wenzako. Ukiwa umekaa Itikafu humo, ukimswalia kwa wingi mno Mtume wa Allah. Ukitoka msikitini ukaenda kuwatembelea wagonjwa, wajane, mayatima na kuwasaidia kwa ulicho jaaliwa, ukatoa sadaka kuwapa masikini na mafakiri, ukawalisha watu chakula, ukasuluhisha baina ya walio hasimiana na… na…

Muislamu akishayatenda hayo, tahamaki Ramadhani hiyoo imefungasha virago, inakwenda zake kwa Mola wake ambako huko itatushuhudia kwa yote yale mema na mabaya tuliyo yatenda ndani yake. Halafu ndio inamjia muislamu furaha ya Eid. Hapa sote tunapaswa kujiuliza: NI IPI FURAHA YA KWELI YA EID? Na tena tuzidi kujiuliza: KUISHEREHEKEA KWETU EID KUNATAKIWA KUWEJE?

Kabla hatujaingia kujaribu kuyajibu maswali hayo kwa kiasi cha maarifa yetu, kwanza tuseme: Katika jumla ya mambo yanayo julikana katika sheria, ni kwamba mfanyakazi anapokwisha itekeleza kazi aliyo pewa, tena akaitekeleza kwa mujibu wa makubalino baina yake na muajiri wake. Huyo anastahiki kupewa ujira wake kamili, kwa kuitia matendoni kauli yake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Mpeni muajiriwa ujira wake kabla halijakauka jasho lake”. Na miongoni mwa mambo yasiyo na shaka ndani yake, ni kwamba mfanyakazi anaye ifanya kazi yake kwa uaminifu na ukweli unao leta tija, huyo hufurahia natija inayo tokana na kazi yake hiyo. Na furaha hiyo huonekana na kuhisiwa na kila aliye na macho. Mchukulie kuwa ni mfano yule mwanafunzi anaye jitahidi na kufanya bidii na akikesha kudurusu masomo yake, unafikiri huwaje furaha yake mwanafunzi huyo pale yanapotoka matokeo ya mtihani na akawa amefaulu vizuri. Matokeo aliyo yapata kupitia juhudi kubwa iliyo chukua muda wake mwingi. Hapana shaka furaha yake hiyo huonwa na kila mwenye macho aliye karibu naye. Qur’ani Tukufu imetupigia taswira ya furaha hiyo katika ubainifu kina na wa wazi, Allah Ataadhamiaye anasema: “Siku hiyo mtahudhurishwa – haitafichika siri yoyote yenu. Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu! Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu. Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza. Katika Bustani ya juu”. Al-Haaqah [69]:18-22

Ndugu mfungaji-Allah akurehemu-kutokana na taswira hii fasaha, tunaweza kusema ya kwamba: Atakaye funga Ramadhani kwa Ikhlasi na uaminifu, akitarajia ujira kutoka kwa Allah, akaihifadhi funga yake na akaifunga itakiwavyo, huyo atakuwa na furaha katika dunia yake na katika akhera yake. Ama furaha yake ya hapa duniani, inakuja kutokana na yeye kuitekeleza amana yake aliyo aminiwa na Allah kwa Ikhlasi na yeye akalihisi hilo kwa dhati yake na yeye mzima. Na kwamba yeye amekihifadhi kile alicho fanywa kuwa khalifa/kiongozi wake mpaka amekifikisha kwa yule aliye mpa pasina mapungufu wala kuzembea. Na furaha hiyo kuu ndio inayo muweka kwenye safu za watu watukufu.

Ama ile furaha ya akhera, hiyo basi ndio furaha ya hakika, ndio furaha ya kweli, hiyo ndio furaha iliyo tajwa na Allah katika kauli yake Ataadhamiaye: “… Na atakaye epushwa na moto na akatiwa peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu”. Aali Imraan [03]:185

Mtu kufuzu na kufaulu mtihani wa umri mzima; mtihani wa dunia, kufaulu huko kukawa ndio sababu ya kuingizwa peponi na kuepushwa na adhabu kali na chungu ya moto wa Jahannamu, hiyo furaha ambayo kila muislamu anawajibikiwa kuikimbilia ili aipate. “… Na katika hayo washindanie wenye kushindana”. Al-Mutwaffifiina [83]:26

Naam, ama juu ya namna ya kuisherehekea Eidil-Fitri, katika hili Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ndiye kiigizo chetu chema na kiongozi wetu katika ukumbi huo wa sherehe na baki ya mambo yetu mengine. Yeye aliisherehekea Eid na pia aliwaamuru maswahaba wake kuisherehekea Eid, na kushereheka kwao kuwe ndani ya wigo wa sheria ya Allah. Lililo halali limo na lililo haramu hilo halimo; hatusherehekei Eid kwa vilevi bali kwa kunywa vinywaji vya halali, Eid haisherehekewi kwa pumbao na michezo ambayo itatupelekea kupitwa na swala kwa wakati wake. Pumbao ambazo zitatufanya tusahau kumdhukuru Allah, tusahau kumswalia Bwana Mtume, tusahau kuwaombea dua wazazi wetu walio tangulia, tusahau kuwaombea dua watoto wetu ili wawe na manufaa kwetu katika dini, ulimwengu na akhera yetu na yao wao na wala wasiwe nakama kwetu. Na lengo la mambo hayo tunayo yafanya katika siku ya Eid hata tukahisi kuwa ndio tumeisherehekea sikukuu, liwe ni kutia furaha na nishati ndani ya nyoyo baada ya uchovu alio upata muislamu katika swaumu, kujizuia na vya halali na uchovu wa kukesha katika visimamo vya usiku. Na tunayafanya hayo kutokana na yale aliyo yafanya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: (Kwani siku ya Eid Abubakri Siddiq aliingia kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawakuta vijakazi wawili wakiimba kwa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi. Abubakri akawakemea kwa kusema: Hivi mnapiga zumari ya shetani nyumbani kwa Mtume wa Allah? Mtume akasema: “Waache (wafurahi), ewe Abubakri! Kwani leo, ni siku ya Eid (ni siku ya kufurahi, kula na kunywa vilivyo halali)”.

Lililo wajibu kwa muislamu katika siku ya Eid, ni kuzisafisha nyoyo kutokana na huzuni; hatakiwi mtu kuwa na huzuni katika siku hiyo na kuzitakasa na chuki na mifundo; hana sikukuu mtu ambaye bado moyoni mwake ana chuki na wenzake. Ni wajibu kusabahiana kwa nyoyo kabla ya kusabahiana kwa kupeana mikono, hakutakuwa na maana kumpa mtu mkono ikiwa ni dalili ya furaha na ilhali ndani ya mvungu wa moyo wako umejaza chuki dhidi yake, hilo halipungui kuwa ni unafiki mbaya; unafiki wa moyo. Si hivyo tu, bali katika jumla ya kusherehekea Eid, ni kuonyesha mapenzi na huruma hususan kwa watu wanyonge, mayatima, wajane, wagonjwa na walemavu bila ya kuwasahau wale waliomo magerezani. Hali kadhalika furaha ya Eidi ni kutoa kuwapa wale wenye uhitaji kwa kuitekeleza amri ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Wakwasieni (wasio jiweza) kuwaepusha na udhalili wa kuomba katika siku hii (ya Eid)”.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu kwa uchache wa maneno, Waislamu katika siku ya Eid wanatakiwa kuwa na amani na utulivu wa moyo na akili, wawe na salama katika mazingira yao, asipatikane miongoni mwao asiye na amani kwa sababu tu ya uhitaji; akakosa utulivu akahangaika huku na kule kurondea kutokana na njaa. Huyo mwenye njaa hatokuwa na utulivu wa kufanya ibada katika siku hiyo. Furaha ienee kwa Waislamu wote ili tupate kulithibitisha neno lake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Anazo mfungaji furaha mbili; furaha moja wakati wa kufuturu kwake na furaha (nyingine) wakati wa kukutana na Mola wake”.

Tulifunge jukwaa letu la juma hili, kwa kukuombeni nyinyi wadau wa jukwaa hili ilhali mkiwa mwishoni mwa ibada ya funga ambayo inadhamini kutokurejeshwa patupu kwa dua zenu. Mtuombee sisi watumishi wenu, Allah azidi kutuwezesha kwanza kuitumikia dini yake na kisha kukutumikieni nyinyi kupitia majukwaa haya ya juma hata juma na aujaalie utumishi wetu huu uwe ni kwa ajili tu ya kutaraji radhi zake Mola wetu. Na akiutakabali utumishi wetu huu, basi ujira wake uzifanye nzito mizani za masheikh na waalimu wetu walio tupokeza na kutufundisha dini hii na wazazi wetu ambao wao ndio sababu ya kupatikana kwetu kwenye ulimwengu huu baada ya Irada yake Allah Mola Muumba wetu. Na sisi kwa janibu yetu, tunamuomba Allah azitakabali ibada zenu na akuwezesheni kuwa nje ya Ramadhani namna mlivyo hivi sasa ndani ya Ramadhani. Muuthibitishie ulimwengu kuwa nyinyi mlikuwa mnamuabudu Mola wa Ramadhani na wala hamkuwa mkimuabudu Ramadhani.

Panapo majaaliwa yake Allah tukutane juma lijalo, hapa hapa katika jukwaa letu la Ramadhani ya mwaka 1442H/2021

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *