“MWEZI WA RAMADHANI, ZIMO NDANI YAKE NEEMA ZA ALLAH KWA WAJA WAKE ZISOZO HESABIKA WALA KUDHIBITIKA”
Sifa zote njema anastahiki Allah ambaye ametuongoza katika dini hii na hatungekuwa ni wenye kuongoka lau si kuongozwa na Allah. Ee Mola wetu wa haki! Mrehemu Muhammad na jamaa za Muhammad kama ulivyo mrehemu Ibraahim na jamaa za Ibraahim. Na mbariki Muhammad na jamaa za Muhammad kama ulivyo mbariki Ibraahim na jamaa za Ibraahim. Hakika Wewe ni Mwingi wa kusifiwa na uliye Mtukufu.
Ama baadu,
Wapendwa ndugu zetu katika Imani.
Assalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.
Ndugu mfungaji-Allah akurehemu-tayari tumebahatika kuidiriki neema ya mwezi wa Ramadhani na tumo ndani yake na kwa rehema na fadhila zake Allah na kwa uwezeshaji wake tunaifunga swaumu ya Ramadhani na tunaiswali swala ya kila mwaka; Sunna ya Tarawehe. Sote tunafahamu na tunakubali ya kwamba Allah Mtukufu ameifanya swaumu ya Ramadhani kuwa ni jambo la kisheria na ametufaradhishia kufunga, ndio maana kila unapo ingia mwezi wa Ramadhani tunafunga kwa kuitekeleza amri yake Mola. Sasa basi, kama ambavyo Allah ametuwajibishia kufunga ndivyo ambavyo amemuhalalishia na kumpa ruhusa ya kula ndani ya mwezi wa Ramadhani yule ambaye hawezi kufunga kwa nyudhuru mbali mbali kama zinavyo tajwa na kauli yake Allah: “… na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini, basi na atimize hisabu katika siku nyingine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini…”. Al-Baqarah [02]:184
Ufafanuzi wa kutosha wa hawa walio ruhusiwa na Allah kula katika kauli yake tuliyo inukuu punde, unapatikana katika Sunna (Hadithi) na maelezo yake zaidi yapo kwenye fani ya Sharia (Fiq-hi) na hapa si mahala pake na wala sio lengo letu leo. Bali tumelitaja hilo ili litufikishe kwenye makusudio ya jukwaa letu la juma hili. Naam, Allah amewaruhusu walio na nyudhuru za kisheria kula katika mchana wa mwezi wa Ramadhani, lakini leo tunao vijana wetu wengi katika shuke za sekondari na vyuo hawafungi mwezi mtukufu wa Ramadhani na hawana nyudhuru za kisheria zinazo wahalalishia kula. Hali kadhaalika tunao watu wazima wengi maofisini, mitaani na majumbani mwetu nao pia hawafungi na hawana sifa za walio halalishiwa na Allah kula katika kauli yake hiyo hapo juu. Ikiwa hiyo ndio hali ilivyo kwa vijana na watu wazima wetu, haya sasa na tujiulize: NINI ADHABU YA MTU ANAYE KULA KWA MAKUSUDI KATIKA MCHANA WA RAMADHANI, TENA WAZI WAZI PASINA HAYA, AIBU WALA SONI.
Katika kulijibu swali hili, ili kila mla mchana wa Ramadhani pasina udhuru wa kisheria, atambue na aijue adhabu yake mbele ya Allah kwa kuikaidi na kuipinga kwake amri ya Mola Muumba wake. Tuanze na kuisikiliza hotuba ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ili tuwekane sawa na twende pamoja. Mtume wa Allah alitoa hotuba katika kukumbusha mauti, akaanza na kumuhimidi na kumshukuru Mola wake, kisha akasema: “Enyi watu! Kithirisheni kumkumbuka mkata ladha, kwani mtakapo mkumbuka katika dhiki, atakueneeni nanyi mtamridhia na kwa hivyo mtalipwa. Hakika mauti ni yenye kukata mipango na matumaini, na siku ni zenye kukisogeza kifo. Na hakika ndani ya kukinahi (kutosheka na ulicho nacho), umo ukwasi (kujitosheleza). Na hakika ndani ya ukati na kati, kuna kwenye kumfikisha mtu kwenye malengo yake (tosho la maisha), na hakika katika kuipa nyongo dunia kuna raha. Na kila amali ina jazaa (yake) na kila kijacho (hicho) kiko karibu”.
Naam, kupitia hotuba hii fupi ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-iliyo beba maana makubwa sana, tunaweza kuwaambia ndugu Waumini: Dunia si makaazi ya milele na sote sisi tutaondoka na kuiacha dunia kama walivyo iacha walito tutangulia ndivyo ambavyo na sisi tutaiacha kwa wengine mpaka kitakapo simama Kiyama. Na mauti yanakata mipango, kila mmoja wetu anayo mipango na malengo yake aliyo jipangia katika maisha yake, ana mipango ya muda mfupi na ile ya muda mrefu, lakini ameiacha Dunia kabla hajaitimiza yote akaimaliza. Tukadirie lau leo Allah atawafufua walio tutangulia, kisha tukawauliza kama walikamilisha malengo na mipango yao waliyo jiwekea, hakuna hata mmoja atakaye jibu kuwa aliikamilisha, mipango yake yote na malengo yake yalikatwa ghafla tena bila ya taarifa na yule mkata ladha; mauti. Na kila siku mpya (leo) inayo mjia mwanaadamu kisha ikapita na kuja siku nyingine, siku hiyo iliyo pita huwa na dhima mbili; hufanya kazi mbili, huupunguza umri wake na humsogezea kwenye mauti yake. Kwa hivyo basi, yatupasa kukiri na kufahamu ya kwamba mauti yana muda wake maalumu ulio pangwa na Allah kabla hata ya kuumbwa huyo aliye pangiwa kufa na umri wa kuishi mwanaadamu si mrefu, tujue basi: “Na kila umma una muda wake. Utakapo fika muda wao basi hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia”. Al-A’araaf [07]:34
Ni kwa kuuzingatia ukweli huu basi, ndio tunawakumbusha ndugu zetu na wenzetu wanao kula katika mwezi wa Ramadhani pasina udhuru unao wahalalishia hilo na wanafanya makusudi kula wazi wazi mbele ya wafungaji. Ikiwa wale wenye udhuru halali wa kula, lakini bado wanaambiwa wasile hadharani, seuze wao wasio na udhuru unao zingatiwa na sheria! Sasa hao ndugu zetu, wao ndio tunawakumbusha wajibu wa kurejea kwa Mola wao, wamtupe mkono shetani, walete toba kwa maasi waliyo yatenda, washikamane na ibada na twaa ya Mola wao, waamrike panapo hitaji kuamrika na wakatazike palipo na makatazo. Wayafanye hayo kabla ya kufunga msafara wa kurejea kwa Mola wao walikotoka, tena tunazidi kuwakumbusha: Rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na itekelezeni faradhi ya kufunga mwezi wenu huu kabla hamjajiwa ghafla na mkata ladha na hapo mkashindwa kujitetea. Na muogopeni Mola wenu, kwani adhabu yake ni kali na chungu na jueni ya kwamba Allah anayo mipaka yake, basi msiivuke wala kuipetuka, kwani kuipetuka mipaka ya Allah kunakuvika sifa ya udhalimu, tusome na tuzingatie: “… Na watakao ikiuka mipaka ya Allah, hao ndio madhaalimu”. Al-Baqarah [02]:229
Na tujue ya kwamba nafasi na mahala pa madhaalimu ni ndani ya moto wa Jahannamu na humo watakaa milele.
Eeeh! Ewe ambaye unaye acha kufunga mwezi wa Ramadhani pasina udhuru! Unapaswa kutambua vema ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Nguzo za Uislamu na misingi ya dini ni mitatu na juu yake (misingi hiyo, ndio) umejengwa Uislamu, yeyote atakaye acha mojawapo ya hiyo, basi yeye kwa (kuiacha) hiyo amekuwa ni kafiri iliyo halali damu (yake kumwagwa). (Nguzo hizo ni); Shahada ya kwamba hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila ni Allah, swala za faradhi na swaumu ya Ramadhani”. Abu Ya’alaa & Dailamiy na imesemwa kuwa ni SAHIH na Imamu Dhahabiy-Allah awarehemu.
Ewe ndugu yetu muislamu-Allah akurehemu-ni kheri kwako ikiwa umeshajua kwamba yeyote yule atakaye acha kufunga mwezi wa Ramadhani bila ya udhuru na ilhali anaweza kufunga; akaacha tu kwa ujeuri. Tambua huyo hataweza kuikidhi; kuilipa siku moja tu aliyo acha kufunga hata kama atafunga umri wake wote ili kuilipa na jambo haliishii hapo, bali atakuwa katika watu wa motoni. Naam, hivyo ndivyo itakavyo kuwa kwa sababu yule anaye kula mchana wa mwezi wa Ramadhani pasina kuwa na udhuru, huyo amemuasi Allah; Mola aliye amrisha ibada hiyo ya funga na kuifanya kuwa mojawapo ya nguzo za Uislamu. Tena ameikhalifu na kuipinga amri yake, haya mtu kama huyo unatarajia adhabu yake itakuwa nini, hebu tuisikie kauli yake Allah Mtukufu ili tupate kuiona na kuijua adhabu na mahala pa anaye ikhalifu amri ya Mola Muumba wake: “Na anaye muasi Allah na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Allah) atamtia motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha”. An-nisaa [04]:14
Kama ambavyo yule anaye ipetuka mipaka ya Allah, huwa mwenye kushindwa na dhalili, kwa sababu Allah Mtukufu anasema: “Hakika wanao pinzana na Allah na Mtume wake, watadhalilishwa kama walivyo dhalilishwa wale walio kuwa kabla yao…”. Al-Mujaadilah [58]:05
Na anasema tena: “Hakika wanao mpinga Allah na Mtume wake, hao ndio miongoni mwa madhalili wa mwisho. Allah ameandika: Hapana shaka Mimi na Mtume wangu tutashinda. Hakika Allah ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda”. Al-Mujaadilah [58]:20-21
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-ya kuambizana tumeambizana, ya kukumbushana tumekumbushana na tumesomeana aya za Allah kama lilivyo agizo lake Mola wetu Mlezi. Basi lililo bakia kwetu sisi ni kuzingatia na kupulika na wala tusiwe kama wale watu wa motoni ambao Allah anasema juu yao: “Na tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika”. Al-A’araaf [07]:179
Ewe ndugu yetu-Allah akurehemu-tumechagua na kuamua sisi wenyewe kuwa Waislamu, basi na tuingie wazima wazima katika Imani hiyo ya Kiislamu kwa kutekeleza nguzo zake zote bila ya kubagua kama ilivyo amri yake Allah katika kauli yake: “Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za shetani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi”. Al-Baqarah [02]:208
Ewe ndugu yetu mwema-uliye na siha njema na wala hauna udhuru unao kuzuia kufunga, Ramadhani hii ndio fursa yako ya kutubia na kurejea kwa Mola wako, ione hatari ya kuikhalifu amri ya Mola wako. Na utambue kila alilo kuamrisha ni kwa manufaa, faida na maslahi yako mwenyewe katika nafsi yako, dini yako, dunia yako na akhera yako. Iogope adhabu ya Mola wako iliyo kali na chungu, huiwezi na kuanzia sasa tia nia ya kufunga huku ukiamini Mola wako ni Mkarimu, Mrehemevu anaye furahi mno pindi mja wake anapo rejea kwake. Na hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira.
Panapo majaaliwa yake Allah tukutane juma lijalo, hapa hapa katika jukwaa letu la Ramadhani ya mwaka 1442H/2021