NUKTA ZA KUZINGATIWA KATIKA MAS-ALA YA TAYAMAMU.

Kabla hatujaanza kuzungumzia mambo yanayotengua tayamamu ni vema tukaziangalia kwanza nukta kadhaa muhimu katika suala zima la kutayamamu.

Nukta zenyewe ni hizi zifuatazo:

1. KUTAYAMMAMU BAADA YA KUINGIA WAKATI WA SWALA

Yeyote ambaye zimepatiakana kukamilika kwake sababu zinazomuhalalishia kutayamamu badala ya kutawadha au kuoga, haimuelei na kumjuzia kutayamamu kwa ajili ya swala ya fardhi ila baada ya kuingia wakati wa swala hiyo.

Ni lazima kutayamamu huko kuwe ndani ya wakati na sio nje yake. Huo ndio utaratibu unaopatikana katika kauli yake Bwana Mtume- Rehema na Amani zimshukie: “Popote pale mtu katika umati wangu itakapomdiriki swala, basi na aswali.” Bukhaariy ” Popote inaponidiriki swala hupangusa (hutayamamu) na kuswali” Ahmad.

Riwaya mbili hizi tulizozitaja zinafahamisha kwamba kutayamamu huwa wakati wa kuidiriki swala, na kuidiriki swala hakupatikani ila baada ya kuingia wakati wake hiyo swala husika. Haya ndiyo mafahamisho na eleweko la hadithi mbili hizi, elewa !

2. KUTAYAMAMU KWA KILA SWALA YA FARDHI:

Kisheria mtu huruhusiwa kuswali kwa tayamamu moja swala moja tu ya fardhi na tayamamu moja swala nyingi awezazo za suna ikiwa ni pamoja na swala ya jeneza (maiti) ijapokuwa swala hii si suna bali ni fardhi ya kutoshelezeana kama tutakavyokuja kuona katika masomo yetu yajayo.

Kauli ya jumla tunaweza kusema:

  • Tayamamu moja – Fardhi moja
  • Tayamamu moja – Suna nyingi

Kwa mantiki hii, mtu akitaka kuswali atayamamu tena hata kama tayamamu yake ya kwanza haijatenguka.

Maelekezo haya yanaihusu swala ya fardhi inayoswaliwa ndani ya wakati (ADAA) au ile inayoswaliwa nje ya wakati wake (KADHAA).

Haya ndiyo mafundisho ya Bwana Mtume – Rehema na amani zimshukie – yanayopatikana katika riwaya iliyopokelewa na Ibn Umar – Allah awawiye radhi – amesema (Ibn Umar katika kuelezea tayamamu ya Mtume) “akitayamamu kwa kila swala hata kama hakuhuduthi”. Al-Baihaqiy.

3. KUTAYAMMAMU HUWA NI BADALA YA JOSHO LA FARDHI KAMA KUNAVYOKUWA BADALA YA UDHU.

Mtu anapopatwa na mojawapo ya mambo yanayomuwajibishia josho la kisheria. Rejea somo la nne kipera/kipengele cha nne na akawa hawezi kutumia maji kwa sababu tulizokwishazielezea katika masomo yaliyotangulia au hakuweza kupata maji mahala alipo, basi tayamamu itamtoshelezea josho hilo.

Tunakusudia kusema kuwa atayamamu badala ya kuoga na kupata ruhusa na uhalali wa kuyafanya yale yote aliyokuwa haruhusiwi kuyafanya kisheria.

Hivyo ndivyo tunavyofahamishwa na tamko la Mwenyezi Mungu Mtukufu : “……NA MKIWA NA JANABA BASI OGENI NA MKIWA WAGONJWA AU MMO SAFARINI, AU MMOJA WENU AMETOKA CHOONI AU MMEINGILIANA NA WANAWAKE, NA HAMKUPATA MAJI, BASI KUSIDIENI (tayamamuni) UDONGO (mchanga) ULIO SAFI …..” [5:6]

Kadhalika hayo ndiyo maelekezo yanayopatikana kutokana na riwaya iliyoipokelewa na Imraan Ibn Huswayn – Allah awawiye radhi amesema: tulikuwa safarini pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu – rehema na amani zimshukie, (Mtume) akawaswalisha watu (maswahaba). Tahamaki huyo ni mtu amejitenga, Mtume akamuuliza, “Ni lipi lililokuzia kuswali?. Akajibu : Nimepatwa na janaba na hakuna maji (ya kuoga), (Mtume) akamwambia: “ Tumia mchanga, hakika huo unakutosha” Bukaariy na Muslim.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *