NGUZO ZA UDHU

Faida

Kabla hatujaanza kuzielezea na kuzibainisha nguzo za udhu moja baada ya nyingine kama zilivyotajwa ndani ya Qur-ani Tukufu, ni vema kujiuliza nguzo ni nini ?

Makusudio ya neno Nguzo hapa ni yale mambo ambayo dhati na hakika ya udhu unayategemea kiasi ambacho likikosekana au kupungua moja miongoni mwao, udhu huwa ni batili kisheria.

Hiyo ndiyo maana na muradi wa nguzo na zifuatazo sasa ndizo hizo nguzo za udhu kwa utaratibu; ambazo ni sita :

  1. NIA : Hii ndio nguzo ya kwanza ya udhu. Neno “nia” lina maana mbili; maana ya kilugha na maana ya kisheria. Nia katika lugha ya kawaida ni MAKUSUDIO na katika lugha ya kisheria ni MAKUSUDIO YA KITU/JAMBO HALI YA KUAMBATANISHA KITU/JAMBO HILO NA KITENDO CHAKE.

Na nia hukaa moyoni mwa mtu. Dalili/ushahidi wa kufaradhiwa nia ni kauli ya Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – “Hakika (kusihi kwa) amali kumefungamana na nia na kila mtu (atalipwa) kwa mujibu wa nia (yake) ……” Al-Bukhariy na Muslim.

Kwa kuwa udhu ni ibada na kwa kuwa nia ndiyo hupambanua baina ya ibada na ada; ikaonyesha kuwa hili sasa ni tendo la ibada kama josho la wajibu na hili ni tendo la ada kama josho la unadhifu. Basi kwa mantiki hii ikawa ni lazima udhu uambatane na nia. Namna ya nia ni mtu kusema moyoni mwake :

“Nawaytu Fardhal-udhui” au
“Nawaytu Raf-al Hadath” au
“Nawaytu istibihatas-swalaat”

Nia Huletwa wapi na mawakati gani ? Nia huletwa wakati wa kuosha fungu/sehemu ya mwanzo ya uso, kwa kuwa hapo ndio mwanzo wa udhu yaani udhu unaanzia hapo na yaletwayo kabla ya hapo huhesabika kama maandalizi ya kuingia ndani ya udhu.

2. KUOSHA USO MZIMA/WOTE kwa kufuata kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu : “BASI OSHENI NYUSO ZENU …”[5:6]

Kuosha uso mzima ndio nguzo ya pili ya udhu. Uso huoshwa mara moja tu kwa kuitegemea kauli ya Mtume : “Udhu ni mara moja moja”. Ama kule kuosha mara ya pili na ya tatu ni suna.

Imethibiti riwaya kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu –Rehema na Amani zimshukie – alitawadha mara moja moja na akasema : “Huu ndio udhu ambao Allah haikubali swala ila kwao” Na akatawadha (tena) mara mbili mbili na akasema : “Huu ndio wa wa mtu ambaye Allah atampa ujira mara mbili” Na akatawadha (tena) mara tatu tatu na akasema : “Huu ndio udhu wangu na udhu wa mitume kabla yangu, basi atakayezidisha (zaidi ya) hivi au kupunguza, (huyo atakuwa) amechupa mipaka na kufanya dhuluma”

Uso ni upi ? Kisheria uso huanzia maoteo/mameleo ya nywele za kichwa mpaka chini ya kidevu, huo ni urefu, na upana wake ni tokea ndewe moja ya sikio hadi nyingine.

Eneo lote lililo katika mipaka hiyo, ndio huitwa uso katika sheria. Na ni wajibu kuosha kila kilichoota ndani ya mipaka hiyo kama nyusi, kope, sharubu na ndevu. Ndevu huoshwa nje na ndani zikiwa chache. Ama zikiwa ni nyingi zilizoshindamana kiasi cha kutokuona ngozi basi inatosha kuosha juu yake tu.

3. KUOSHA MIKONO HADI VIFUNDONI kwa kuitikia kauli ya Mola Mtukufu : “….NA (osheni) MIKONO YENU MPAKA VIFUNDONI …” [5:6]

Imelazimu maji yaenee vema katika nywele na ngozi. Ukiwepo uchafu chini ya kucha ukayazuiliya maji kupenya ndani au pete iliyobana isiyoruhusu kupenya maji, udhu hautasihi bali utakuwa ni batili. Imepokelewa na Imam Muslim kwamba mtu mmoja alitawadha na akaacha (kuosha) sehemu ya kucha mguuni. Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akamuona na kumwambia : “Rudi ukatawadhe vizuri (kwa ukamilifu).

4. KUPAKAZA MAJI SEHEMU YA KICHWA kwa kuitekeleza kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu : “…NA MPAKE VICHWA VYENU …” [5:6]

Mapendeleo ya kupakaza maji ni kuupitisha mkono uliorowa maji kichwani. Na namna ya kupakaza ni kama ilivyothibiti katika hadithi sahihi iliyopokelewa na Abdallah ibn Zayd kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipakaza (maji) kichwa chake kwa mikono yake, akaipeleka mbele halafu akairudisha nyuma. Alianzia sehemu ya mbele ya kichwa chake kisha akaipeleka kichogoni, kisha akairudisha pale mahala alipoanzia”

5. KUOSHA MGUU HADI VIFUNDONI kwa kulishika neno lake Mola Mtukufu “…NA (osheni) MIGUU YENU MPAKA VIFUNDONI …”[5:6]

Inampasa mwenye kutawadha ahakikishe anaosha sehemu yote iliyoainishwa katika sheria. Asiache sehemu yeyote ile iliyo chini ya kucha.

Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar –Allah awawie Radhi – amesema : Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – alibakia nyuma yetu safarini, kisha akatudiriki, tukaanza kutawadha na kupaka maji miguu yetu. Mtume akalingana kwa sauti ya juu : “Adhabu kali ya moto itawathibitikia wenye kuacha kuosha visigino, (akasema hivyo) mara mbili au tatu.

6. MPANGO/TARATIBU. Kutungamanisha baina ya viungo hivi vinne vya udhu kwa namna ilivyokuja ndani ya Qur-ani Tukufu, ndiyo nguzo ya sita.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema : “ENYI MLIOAMINI! MNAPOTAKA KUSWALI, BASI OSHENI NYUSO ZENU NA MIKONO YENU MPAKA VIFUNDONI, NA MPAKE (maji) VICHWA VYENU, NA (osheni) MIGUU YENU MPAKA VIFUNDONI” [5:6]

Utaratibu ndio mojawapo ya faida tunazozipata kutokana na aya hii na pia utaratibu unapatikana kutokana na utendaji wake Bwana Mtume kwani yeye hakutawadha ila kwa kuzitungamanisha nguzo, moja ikifuatiwa na mwenziwe kama ilivyothibiti katika hadithi nyingi sahihi.

Kwa hivyo imempasa mwenye kutawadha mwenye kutawadha aanze na kuosha uso, kisha aoshe mikono, halafu apakaze kichwa maji na amalizie na kuosha miguu.

Mambo sita haya ndiyo yanayoitwa nguzo za udhu. Kusihi ama kutokusihi kwa udhu wa mtu kunategemea sana utekelezaji wake.

Akiyatekeleza yote kama itakiwavyo udhu wake ni sahihi na akiacha mojawapo ya mambo sita haya, udhu wake ni batili. Udhu ukiwa batili basi kuwa batili swala ni aula zaidi, kwa kuwa udhu ndio msingi wa swala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *