Hivi huoni kuwa udhu ambao ndio msingi wa ibada nzima ya swala kuwa ni NGUVU ya mwili, NISHATI ya roho na ni NADHAFA ya kiwili wili kwa ujumla ?
Je, huoni kuwa kuifungua swala kwa tamko lenye kudumu milele “ALLAHU AKBAR” ni nguvu ya roho inayomfanya mtu ahisi kuwa Allah ni Mkubwa kuliko wakubwa wote?
Allah ni Mtukufu kuliko watukufu wote? Hakuna Mkubwa wala Mtukufu mbele yake ila ni yeye tu.
Ni hisia hizi ndizo zilizowafanya wachawi kutotetereka na kurudi nyuma mbele ya mabavu, nguvu na vitisho vya Mungu mtu- Firauni Tujikumbushe hali ilivyokuwa: (Firauni)
AKASEMA: OH! MNAMUAMINI KABLA SIJAKUPENI RUHUSA! BILA SHAKA YEYE NDIYE MKUBWA WENU ALIYEKUFUNZENI UCHAWI. KWA HIVYO NITAKUKATENI MIKONO YENU NA MIGUU YENU KWA KUTAFAUTISHA (mkono wa kulia na mguuu wa kushoto na mkono wa kushoto na mguu wa kulia ) NA NITAKUSULUBINI KATIKA MASHINA YA MITENDE, NA BILA SHAKA MTAJUA (wakati huo) NI NANI KATIKA SISI (mimi au Mungu wake Musa) ALIYE MKALI WA KUADHIBU NA KUJIENDESHA (kuindeleza adhabu yake) “ WAKASEMA : “HATUTAKUKHITARI WEWE KULIKO ZILE ISHARA WAZIWAZI (za haki) ZILIZOTUJIA. TUNAAPA KWA YULE ALIYETUUMBA. BASI FANYA UNAVYOTAKA KUFANYA, WEWE UNAWEZA KUTOA HUKUMU INAYOHUSIANA NA MAISHA HAYA YA DUNIA TU” (20: 71-72).
Ni hisia hizi hizi zitokazo na nguvu ya kiroho izalishwayo na kukuzwa siku hata siku ndani ya swala iliyomfanya Mtume Mussa – Amani ya Allah imshukie – kutobabaika wala kuyumba wakati wafuasi wake (bani Israil ) walipokata tamaa kabisa na kuona kuwa mwisho wao umefika.
Hawana kitakachowaokoa na jeshi kubwa la Firauni linalowafukuza na mbele yao kuna habari nyekundu (Red sea). Tuitegee sikio Qur-ani ikituelezea hali ilivyokuwa .
“NA YALIPOONANA MAJESHI MAWILI (haya , watu na Nabii Musa wanakimbia, na Firauni na watu wake wanawafuatia) WATU WA MUSA WALISEMA “ HAKIKA TUTAKAMATWA”
(Musa) AKASEMA:
“ LA, KWA YAKINI MOLA WANGU YU PAMOJA NAMI, BILA SHAKA ATANIONGOZA (tuokoke sote)”…………….NA TUKAMUOKOA MUSA NA WALE WALIOKUWA PAMOJA NAYE WOTE” ( 26:61-62, 65).
Ni hisia hizi pia ndizo zilizomtia nguvu na kumuondolea wasiwasi Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipokuwa pangoni na swahibu yake Abu Bakri – Allah amuwiye radhi.
Makurayshi wamesimama mdomoni mwa pango, miguu yao inaonekena na waliomo ndani kama yanavyosikiwa maneno yao.
Hapo Abuu Bakri akitetemeka kwa khofu kuu anamnong’oneza Mtume –
“ Ewe Mtume wa Allah, lau mmoja wao atatazama chini ya miguu yake bila shaka atatuona (Mtume) akamwambia,
“ Nini dhana yako we Abu Bakri kwa wawili ambao Allah ni watatu wao?! “ Bukhariy na Muslim.
Hebu tuipe nafasi Qur-ani Tukufu:
“KAMA HAMTAMNUSURU (Mtume ) BASI ALLAH ALIMNUSURU WALIPOMTOA WALE WALIOKUFURU, ALIPOKUWA (mmoja tu na mwenziwe) WA PILI WAKE (peke yao) WALIPOKUWA WOTE WAWILI KATIKA PANGO, (Mtume) ALIPOMWAMBIA SAHIBU YAKE, “ USIHUZUNIKE KWA YAKINI ALLAH YU PAMOJA NASI” ………….” (9:40).
Ni hisia hizi ndizo zilizompa Bwana Mtume ushujaa na kutokubabaika mbele ya upanga wa Daathuuri katika vita vya Ghatwafaani.
Waislamu walipiga kambi, Mtume akawa amejitenga jpembeni amepumzika chini ya mti akiwa ameanika nguo zake zilizoloa kutokana na mvua iliyowapata.
Hapo ndipo Daathuuri mmoja wa maadui akaona amepata fursa nzuri ya kummaliza Mtume.
Akamuendea Mtume mpaka akamsimamia kichwani, upanga mkononi, Akamuamsha, Mtume na kumwambia: ni nani atakayekuzuia nisikuue, ewe Muhammad?
Mtume akamjibu: “Allah!”
Pale pale mtu yule akapatwa na kitisho na woga uliomtambaa mwili mzima na kutetemesha kiasi cha kuacha upanga umuangukie Mtume akauokota na kumuuliza hasimu yake swali lile lile:
Ni nani atakayenizuia nsikuue, ewe Daathuiru? Akajibu:
Hapana ye yote. Mtume akamsamehe.
Rejea vitabu vya sira kwa ukamilifu wa kisa hiki, ukitaka safu zilizonyooka na kukamatana nyuma ya Imam mmoja, zikisikiliza kisomo chake (Qur-ani aisomayo), zikiunyenyekea waadhi upatikanao ndani ya kisomo hicho, zikimfuata Imam wao katika harakati na vitulizano vyake.
Huoni kuwa nidhamu hii inaonyesha nguvu ya jamii iliyoungana pamoja na yenye lengo moja?
Kuna nguvu ipi ulimwenguni iliyo bora ziadi inayoweza kuilea jamii kuliko nguvu hii inayopandikizwa na swala katika nafsi ya muislamu?