NENO LA AWALI

Neno la Awali

Sifa zote njema ni zake Allah; Mola Mlezi wa viumbe vyote ambaye amesema katika kitabu chake kitukufu, alicho mteremshia Mtume wake Mtukufu: “HAKIKA NYINYI MNAYO RUWAZA NJEMA KWA MTUME WA ALLAH, KWA ANAYE MTARAJI ALLAH NA SIKU YA MWISHO, NA AKAMKUMBUKA SANA ALLAH”. Ee Mola wetu wa haki! Mrehemu Muhammad na jamaa za Muhammad kama ulivyo mrehemu Ibraahim na jamaa za Ibraahim. Na mbariki Muhammad na jamaa za Muhammad kama ulivyo mbariki Ibraahim na jamaa za Ibraahim. Hakika Wewe ni Mwingi wa kusifiwa na uliye Mtukufu.

Ama baad,

Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-kwa mara nyingine tena kwa uwezo wake Allah, mtumishi na mwenza wako katika kuitumikia elimu ya dini yako, iliyo ridhiwa na Mola wako; WEBSITE UISLAMU anakuletea “UPANDE/UKURASA WA PILI WA SIRA YA MTUME WA ALLAH”. Baada ya kukuletea masomo ya Sira kwa kadiri aliyo tuwezesha Allah, sasa tunakuletea upande wa pili wa Sira hiyo ya Bwana Mtume. Katika upande huu wa pili, tunakusudia tuisome tena kwa pamoja Sira yake Mtume wa Allah sanjari na kuyaangalia MAFUNDISHO na FALSAFA zinazo patikana humo.

Mpendwa msomaji-Allah akurehemu-tambua na uelewe ya kwamba Sira ya Mtume ni miongoni mwa masomo na fani za elimu ambazo zimepewa nafasi ya mbele na umuhimu mkubwa na Waislamu wale wa kale na hata sisi wa leo. Umuhimu na nafasi ya Sira inadhihirika kutokana na kuwa kwake ni UTEKELEZAJI WA KIMATENDO wa Sharia ya Allah na ni UBAINIFU WA HUKUMU zake.

Hakika msomaji wa Sira ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-huchuma na kuvuna utekelezaji wa kiutendaji wa hukumu mbali mbali za Uislamu, zinazo bebwa na aya za Qur-ani Tukufu na Hadithi za Mtume wa Allah katika nyanja na hali tofauti tofauti za maisha, kupitia kwa Mtume wa Allah na Maswahaba wake. Pamoja na yote hayo, Sira ya Mtume wa Allah ni MAFUNDISHO yanayo lea na kukuza imani ya Muislamu na kuitakasa tabia yake. Ni KIBERITI kinacho washa ndani yake moto wa mapambano baina yake na nafsi yake, baina yake na mazingira yake, baina yake na jamii yake, baina yake na ulimwengu wake chini ya mwavuli wa maisha ya mwanaadamu bora na watu bora walio mzunguka (maswahaba). Tena ni KICHOCHEO kinacho mshakizia kuikumbatia, kuikubali na kuitekeleza haki na ni CHEMCHEM inayo mzalishia kani inayo mpa nguvu ya kusonga mbele kwenye viwanja vya matendo mema kwa mujibu wa maamrisho na maelekezo ya Allah na Mtume wake.

Tena ni kheri kwa Muislamu mwenye kumpenda Allah na Mtume wake, akatambua ya kwamba kusoma, kujifunza na kuifahamu Sira ya Bwana Mtume, kunapanda na kustawisha moyoni mwake mahaba ya Bwana wetu Muhammad. Kwa ajili hiyo basi, kumemlazimu kila Muislamu kwa nia na dhamira halisi, kutenga muda katika umri wake, kila siku au kila juma, kusoma au kusikiliza Sira ya Bwana Mtume. Tena zoezi na ada hiyo iwahusishe pia watu wa nyumbani kwake; mke, watoto na ndugu bali hata majirani zake.

Halafu tena ni vema Muislamu akatambua ya kwamba Sira ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-imezienea na kuzisheheni nyanja zote za maisha ya mwanaadamu. Kwani Sira inatusimulia na kutuelezea maisha halisi na kweli ya:

 • Kijana muaminifu, mnyoofu wa tabia kabla hajakirimiwa kupewa utume na Allah.
 • Mtume mlinganiaji anaye waitia watu kwa Allah; Mola Muumba kwa kutumia njia na mbinu bora ili ujumbe na wito wake huo ukubaliwe na kupokelewa na walengwa.
 • Kiongozi wa dola/serikali anaye ijengea na kuiwekea dola yake misingi, taratibu na kanuni madhubuti na sahihi na kuilinda na kuisimamia kwa nia na ukweli kwa kiwango kinacho idhaminia ustawi wake.
 • Mume mwema na baba mwenye huruma na mapenzi kwa familia yake, anaye simamia haki na wajibu wa kila mwanafamilia.
 • Mlezi anaye simamia malezi ya mfano ya maswahaba wake, malezi yanayo toka moyoni mwake na kuingia mioyoni mwao. Malezi yanayo wapelekea kujaribu kumuiga katika mambo madogo na hata yale makubwa.
 • Mtume rafiki wa kweli ambaye anaitekeleza vilivyo na ipasavyo haki ya urafiki, jambo linalo wafanya maswahaba wake kujikuta wakimpenda kuliko hata familia zao bali hata nafsi zao wenyewe.
 • Mpigania dini shujaa anaye pigana tu kwa ajili ya Allah, dini na waja wa Allah.
 • Kamanda mahiri, mwenye mikakati madhubuti ya vita, anaye chunga haki za binaadamu hata katika medani ya vita.
 • Mwanasiasa mkweli, aliye fanikiwa katika kuwaunganisha watu wa rika, rangi, imani na tabaka tofauti hata wakajihisi kuwa wao wote ni wamoja na hapana tofauti wala ubora wa huyu kwa yule.
 • Jirani mwema, asiye mbughudhi wala kumuudhi jirani yake.
 • Na….. na……

Kwa ujumla ni kwamba Sira ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-imehodhi na kuzienea kada na nyanja zote za maisha ya mwanaadamu; yale ya kibinafsi na hata ya kijamii. Jambo linalo mfanya Bwana Mtume kuwa ruwaza na kigezo chema kwa kila:

 • Mlingania dini,
 • Kamanda,
 • Baba,
 • Mume,
 • Rafiki,
 • Mlezi,
 • Mwanasiasa,
 • Raisi/kiongozi, na…. na……

Sote kwa pamoja tumuombe Mola wetu aturuzuku ufahamu utakao tupelekea kuifahamu na kisha kufaidika na Sira ya Bwana Mtume katika Dini, Dunia na Akhera yetu. Pia tumuombe atujaalie kuwa miongoni mwa wenye kumpenda Yeye Allah; Mola Muumba wetu na Mtume wake ili tupate kufuzu duniani na akhera.

Mtumishi wenu; WEBSITE UISLAMU.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *