THAMANI YA WAKATI…II
Fardhi za kiislamu na desturi za Uislamu zimekuja kuthibitisha thamani ya wakati na kuijali kila hatua na sehemu ya wakati. Fardhi na desturi hizi zinaamsha aina fulani ya mwamko uanomzindua muislamu juu ya umuhimu wa wakati na mwenendo mzima wa ulimwengu sambamba na mzunguko wa sayari, nyota, jua na mpishano wa mchana na usiku.
Usiku unapotoa mkono wa kwaheri na kuiachia alfajiri kubisha hodi, huinuka mlinganiaji wa Allah na kuijaza anga kwa sauti ya wito wa Allah (adhana.) Sauti hii iliyosheheni maneno matukufu kabisa huwazindua walioghafilika na kuwaamsha waliolala waamke na kuipokea asubuhi toharifu kutoka mikononi mwa Allah.
Sauti hii husema: (Haya njooni kwenye swala, haya njooni kwenye kunadi sada “kufaulu”), huzidi na kuongeza: (Swala ni bora kuliko usingizi). Nyoyo na ndimi za waumini huipokea sauti hii ya wito wa Allah kwa utii na unyenyekevu mkubwa na haraka watu kawa huamka kujitayarisha kwa ajili ya swala. Swala hii ya alfajiri huashiria kuanza kwa siku mpya na harakati zake.
Jua linapotenguka na vichwa na watu wakiwa wamezama katika shughuli za kimaisha, hurejea mlinganiaji (muadhini) kulingana kwa mara ya pili tena. Mlinganiaji huyu hushuhudia upweke/umoja wa Allah na ujumbe/risala ya nabii wake Muhammad na kisha kutoa wito wa swala, wito wa kufaulu.
Waumini wakiusikia wito huu, haraka na kwa utii uliojaa unyenyekevu huziacha shughuli zao za kimaisha. Wakaenda kusimama mbele ya Mola wao; awapaye riziki yao na Mpangaji na Msimamizi wa kweli wa mambo yao yote. Huwa mbele yake kwa dakika kadhaa wakiitupa dunia nyuma ya migongo yao. Haya yote hufanyika katika swala ya katikati ya mchana; swala ya Adhuhuri. Swala ambayo huwakumbusha kumalizika kwa asubuhi; nusu ya kwanza ya mchana na kuingia kwa nusu ya pili.
Na wakati urefu wa kivuli cha kitu unapolingana sawa na urefu wa kitu husika na taratibu jua likaanza kuelekea mazamioni hapo ndipo mlinganiaji wa Allah hulingania tena kwa mara ya tatu akiwaita waja wa Allah kuja katika nyumba ya Allah kutekeleza fardhi ya Allah, fardhi ya Alasiri.
Kuingia kwa swala hii kama kunaashiria jambo mbali na kupata radhi za allah, basi ni kumalizika kwa mchana na kuanza kwa jioni ambayo ni nembo ya makomeleo ya shughuli za mchana kutwa. Wengi miongoni mwa waja wa Allah huanza kuelekea katika maskani zao kwa ajili ya kupumzika kutokana na uchovu wa shughuli za kutafuta maisha za mchana kutwa.
Na wakati mionzi ya jua inapotoweka na kutoonekana kabisa katika pambizo za mbingu na kutoa nafasi kwa kiza cha usiku kuanza kutawala. Wakati huu kwa mara ya nne, mlinganiaji wa Allah hulingania tena, akiwaita waja wa Allah kuitekeleza swala inayoashiria kumalizika kwa mchana na kuanza kwa usiku. Hii si nyingine bali ni swala ya Maghribi ambayo huwakuta watu walio wengi wakiwa tayari wamesharejea majumbani mwao.
Na wakati yanapozama na kupotea kabisa makungu mekundu (the red of sunset) hapo ndipo husikika adhana ya mwisho. Hii ndiyo adhana ya swala ya mwisho, inayofunga siku ya muislamu, hii si nyingine bali ni adhana ya swala ya Ishaa. Wakati huu muislamu huonyesha shukrani na asante zake kwa Allah Mola Muweza wa yote na vyote.
Anamshukuru kwa kumjalia kuamka salama, kwenda na kurudi salama salimini kazini sambamba na kumuomba ulinzi na salama katika kiza cha usiku kilichomfunika. Kwa utaratibu huu wa ibada uliowekwa na Allah kwa hekima na busara zake tukufu kupitia mfumo sahihi wa maisha (Uislamu). Muilamu hupata fursa ya kuianza siku yake kwa swala; akayaunga mawasiliano yake na Mola wake kabla ya kitu kingine cho chote, eh bakhti na saada iliyoje kuishi chini ya mfumo huu! Kadhalika muislamu huzidi kuyaendeleza mawasiliano haya kila baada ya muda fulani na hatimaye huikhitimisha siku yake hii kwa swala kama alivyoianza.
Huu ndio utaratibu wa kila siku wa maisha ya muislamu, kwa kuishi na utaratibu huu muislamu anakuwa anakumbushwa na fardhi hizi ama kuanza au kumalizika kwa kipindi fulani cha siku na kumkumbusha wajibu wake kwa kipindi hicho. Na katika kila juma, muislamu hujiwa na siku ya Ijumaa. Ndani ya siku hii, waislamu huuitikia wito wa Allah, wito wa swala ya juma. Hii ni swala ambayo huwapa fursa ya kukutana pamoja, mahala pamoja na kupata ujumbe mmoja.
Hii ni swala inayoashiria kumalizika kwa siku saba zinazoitwa juma na kuanza kwa juma jipya. Swala nne za Ijumaa humaanisha kukamilikwa kwa mwezi mmoja ambapo muislamu hungojea kwa hamu na shauku kuu kuandama kwa mwezi mwandamo (Hilaal/Crescent.) Muislamu huupokea mwezi mpya kwa Tahlili, Takbiyr na dua, ambapo husikika akisema:
“ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR, AL-HAMDULILLAAHIL-LADHIY KHALAQAKA, WAQADDARAKA MANAAZIL, WAJA’ALAKA AAYATAN LIL-‘AALAMIYNA. ALLAAHUMMA AHIL-HU ALAYNAA BIL-AMNI WAL-IYMAAN, WASSALAAMATI WAL-ISLAAM, WA TAUFIYQ LIMAA TUHIBBU WATARDHWAA. HILAAL KHAYRUN WARUSHDI, RABBIY WARABBUKAL-LAAHU”.
Kumalizika na kuanza kwa mwezi mwingine, hatimaye humkutanisha muislamu na fursa adhimu fursa ya mwaka hata mwaka. Hii si nyingine bali ni mwezi mtukufu wa Ramadhan, mwezi ambao hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na kuachwa wazi kwa wale wote watakao jikurubisha kwa Mola wao kwa kufanya amali njema ndani ya mwezi huu. Milango ya moto pia hufugwa sambamba na kutiwa pingu mashetani kwa baraka ya mwezi huu mtukufu. Ili wasizichafue na kuziharibu ibada za waja wa Allah ndani ya mwezi huu mtukufu.
Ni ndani ya mwezi huu ambamo hulingania mlinganiaji mwingine, huyu hulingania kutokea mbinguni na si ardhini kama ilivyo ada kwa swala tano za kila siku. Mlinganiaji huyu hupaaza sauti kuwaambia waumini: (Jongea ewe mtaka kheri na mbalika (kuwa mbali) ewe mtaka shari) Wito huu hupatikanao ndani ya mlingano huu wa mbinguni humfanya aliyeasi kutubia upesi. Na kumzindua aliyeghafilika na kumuabudu Mola wake na kuwarejesha wote hawa kwenye uwanja wa Allah. Katika uwanja huu huzitafuta radhi na maghfirah yake kwa wasila wa ibada tukufu na kongwe, ibada ya swaumu na ibada ya kisimamo cha usiku. Ibada hii ya swaumu humkumbusha muislamu kumalizika kwa zaidi ya theluthi mbili za mwaka na kwamba kasalikiwa na theluthi moja tu ili kuukamilisha mwaka.
Baada ya muislamu kuimaliza safari hii ya roho ndani ya mwezi wa Ramadhani, hupata fursa nyingine ya safari. Hii ni safari inayohusisha roho na mwili pamoja, hii si nyingine bali ni safari ya kwenda kuitimiza na kuitekeleza nguzo ya tano ya Uislamu; nguzo ya Hijah.
Maandalizi ya safari hii huanza mara tu baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ibada hii ya Hijah huashiria kumalizika kwa mwaka wa Kiisalmu na hivyo kumfanya muislamu awe katika matayarisho ya kuupokea mwaka wake mpya. Ambayo hii ni fursa pekee ya kutathmini mafanikio na matatizo yake ya kimwili na kiroho sambamba na kuyapatia ufumbuzi/suluhisho muafaka.
Wahenga wetu wema – Allah awarehemu – walikuwa wakiziita swala tano kuwa ni “Mizani/kipimo cha siku”, Ijumaa waliita: “Mizani ya mwaka,” na waliita Hijah kuwa ni: “Mizani ya umri.” Majina haya hawakuyaleta kwa njia ya mchezo na burudani, bali yalitokana na pupa yao juu ya umuhimu na thamani ya wakati .
Ndio wakazifanya ibada hizi kuwa ni kipimo chao cha kupima utendaji wao wa kila siku, kila juma, kila mwaka na hatimaye umri wa mtu. Vipimo hivi viliwasukuma kufikiri na kuwaza kabla ya kuamua ama kutenda na kusema au kutokutenda na kutokusema jambo fulani. Walisukumwa kufanya hivyo na muongozo kutoka kwa Mtume wao – Rehema na Amani zimshukie – alipowaasa: “Unapotaka kufanya jambo lo lote lile basi (kwanza) uzingatie mwisho wake (jambo hilo). Ikiwa una kheri (yaani lina mwisho mwema jambo hilo) basi endelea (nalo) litende na ikiwa una shari (yaani lina mwisho mbaya, basi liache (usilitende).”Ibn Al-Mubaarak
Ukiayaachilia mbali yote haya, utaikuta fardhi ya Zakah ambayo katika hali nyingi hupasa mara moja kwa mwaka. Kwa kuzitekeleza ibada hizi, muislamu hubaki kuwa macho na mwenendo mzima wa wakati. Hivi ndivvyo ambavyo fardhi na ibada hizi za uislamu zinavyomsaidia muislamu kwenda sambamba na kuujali wakati wake ambao ndio rasilimali yake kuu.