MTAZAMO MPYA KUELEKEA DA’AWAH

Baada ya kushindwa kwa majeshi shirika (Ahzaab) na kushindwa kwa Mayahudi wa Baniy Quraydhwah, Waarabu walianza kuwa na mtazamo mpya kuielekea Da’awah.

Ikawapitia fikra kwamba wimbi hili la Da’awah ya Kiislamu lazima litakuwa na msukumo wa nguvu isiyo ya kibinadamu, hapana shaka kwamba linapata msaada kutoka kwa Allah, kwa hivyo hawataweza kamwe kushindana nalo wakalishinda.

Na kwamba hapana shaka Muhammad na wafuasi wake watakuwa katika haki, kwa hivyo ni dhahiri kuwa hatimaye ushindi na nusra vitakuwa upande wao.

Fikra hizi zilitokana na mkondo wa mambo yanavyojiri, ziliyafanya baadhi ya makabila ya Waarabu kupunguza uadui wao kuwaelekea waislamu.

Na wakati huo huo makabila mengine yakaanza kujaribu kuwa karibu na waislamu.

Hali ya hewa ya utisho na utukufu wa waislamu na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ikazagaza anga na kuzijaza nyoyo za maadui.

Mazungumzo katika baraza za watu sasa yakawa ni kuizungumzia tu nguvu ya ajabu na inayokua kwa kasi ya ajabu ya waislamu, mamlaka yao pamoja na cheo cha Mtume na nguvu tiifu inayomzunguka.

Pamoja na hali kuwa hivyo, waislamu hawakubweteka, bali waliendelea kuwa macho na silaha zao zikiwa mikononi tayari kukabiliana na adui atakayejitokeza.

Hii ni kwa sababu, walitambua fika kwamba wana maadui wengi na kwamba bado maadui hawa wanasongwa na kiu ya kutaka kulipa kisasi na kuwaangamiza.

Nafsi zao zimejaa chuki dhidi ya Da’awah hii inayo endelea kukua siku hata siku na dhidi ya kundi hili dogo linaloendelea kupata nguvu kila kukicha.

Kwa ajili hii waislamu wakawa hawana budi kuwa macho na harakati za maadui zao na kujiandaa kukabiliana na lo lote linaloweza kujitokeza.

Na ulikuwa ni wajibu wao kuwathibitishia watu ya kwamba wao wanastahiki nusra waliyopewa na Allah.

Na wawatie maadui zako fikra ya kwamba wao wana nguvu ya kupambana na ye yote miongoni mwao na wakaweza kumzuia adui pamoja na wingi na nguvu zo zote atakazokuwa nazo.

Ili lisifikirie kabila lo lote la Waarabu au Mayahudi kuushambulia Uislamu au kuwa na tamaa ya kuwashinda waislamu baada ya ushindi ule wa kishindo.

Ushindi waliozawadia na Allah kutokana na ikhlasi na juhudi yao katika dini ya Allah; ushindi wa Ahzaab na ule dhidi ya Baniy Quraydhwah.

Kumtia khofu adui:

Ni kwa sababu zote hizo, ndipo waislamu hawakuziweka pembeni silaha zao kwa kutambua kuwa mapambano ya haki dhidi ya batili bado hayajaisha.

Wala hawakulala usingizi mbele ya adui yao kwa kutegemea kuwa Allah yu pamoja nao na atawasaidia kwa nguvu zake zisizoshindwa.

Walifanya hivi kwa sababu ya kutambua kwao kuwa daima Allah hayuko pamoja na watu walioghafilika na wala hawapi msaada watu waliobweteka. Watu wasioshughulika na sababu za ushindi kadiri/upeo wa uweza wao.

Baada tu ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kumaliza kuwashughulikia Baniy Quraydhwah mwishoni mwa mwaka wa tano.

Akaanza kuwatia khofu maadui wa Uislamu kila upande, mwanzoni tu mwa mwaka wa sita. Akaanza kupeleka vikosi vya askari na wakati mwingine yeye mwenyewe akiongoza vita mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.

Aliyafanya yote haya kwa lengo la kuwatia khofu maadui zake wote; Waarabu wenzake na Mayahudi. Akitumia mbinu ya kuwasambaratisha kwa mashambulizi ya kushtukiza kabla hawajajiandaa na kujikusanya.

     Mashambulizi ya Dhwariyah:

Tarehe 10 ya mwezi wa Muharram wa mwaka huu huu wa sita {May 627 A.D.}, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma Muhammad Ibn Maslamah. Akiongoze kikosi cha askari wapanda farasi kwenda kwa Baniy Bakri Ibn Kilaab waliokuwa wamepiga kambi pande za “Dhwariyah”; mahala palipokuwa umbali wa mwendo wa siku saba kutokea Madinah kupitia njia ielekeayo Basrah.

Akawaendea, akijificha mchana na kutembea usiku mpaka akawafikia na kuwashambulia kwa ghafla.

Akafanikiwa kuwaua kumi miongoni mwao na wengine kufanikiwa kuponyoka na kukimbia.

 Akaichukua ngawira mifugo yao; ngamia mia moja na khamsini, kondoo na mbuzi alfu tatu.

Kisha akarejea Madinah siku moja kabla ya kumalizika kwa mwezi wa Muharram baada ya kuwa nje kwa siku kumi na tisa.

  IV.          Vita vya Baniy Lahyaan:

Mwanzoni mwa mwezi wa Rabiul-Awwal {Mfunguo sita – Julai 627 A.D.}, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka na kundi la maswahaba wake mia mbili akiwakusudia Baniy Lahyaan.

Hawa ndio wale wasaliti wa watu wa Rajii; Khubaib na wenzake. Hawa walikuwa wamepiga kambi katika mojawapo ya mabonde ya Hijaazi, upande wa Makkah, bonde hilo likiitwa “Fazzaan”.

Mtume akidhihirisha kuwa anaelekea Shamu ili Baniy Lahyaan wasijue makusudio yake, wakakimbia.

Akatoka Madinah akielekea upande wa Kaskazini, akakaza mwendo kuelekea njia ya upande wa Buraidi.

Hata alipokwishakuwa mbali na kudhaniwa kuwa kweli anaelekea Shamu, ndipo alipochepukia upande wa kushoto na kukaa sawa katika njia ya Makkah.

Halafu akaanza kushuka bonde na kuanza kuelekea upande wa Kusini, akiharakia Fazzaan. Pamoja na jitihada yake yote hii ya kuficha muelekeo wake, bado Baniy Lahyaan walikuwa katika hali ya tahadhari na khofu.

Walikuwa wakimchunga chunga Mtume wa Allah na kuzifuatilia kwa karibu nyendo zake.

Mtume alipofika mahala pale walipouliwa maswahaba wake, tayari Baniy Lahyaan walishajua kuwa anawafuata wao kulipa kisasi cha maswahaba wake.

Haoo wakatimua mbio na kwenda kujificha majabalini, kwa hivyo hakumkuta hata mtu mmoja. Mtume akaamua kupiga kambi hapo siku moja au mbili na akavituma vikosi vyake kila upande kwenda kuwasaka wasaliti hao.

Lakini wapi hakufanikiwa kumkamata hata mtu mmoja, akafunga azma kurejea Madinah. Lakini kabla ya kuondoka akalituma kundi dogo la maswahaba wake kuelekea upande wa njia ya Makkah chini ya uongozi wa Sayyidina Abu Bakri.

Aliwatuma kwa lengo la kuwatia khofu Makurayshi na kuwajulisha kuwa yuko njiani, wakaenda mpaka wakafika sehemu iitwayo “Kuraai-Ghamiym”.

Hapa ni mahala palipo kuwa umbali wa mwendo wa siku mbili kutokea Madinah, walipofika hapo wakageuza kurudi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawa nje ya Madinah kwa kipindi kisichopungua siku kumi na nne.

Halafu akarejea katika siku iliyokuwa na joto kali sana na alikuwa akisema:

“Tumerudi tukiwa ni wenye kutubia na Mola wetu tunamuhimidi. Ninajilinda kwa Allah kutokana na uchovu wa safari, huzuni ya marejeo na mandhari mbaya kwa watoto na mali”.

 

     V.          Vita vya Dhiy Qirdi:

 Baada ya siku kadhaa tangu kurejea kwake Madinah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka na maswahaba wake mia tano kuelekea “Dhiy Qirdi”.

Hili ni eneo lenye maji lililokuwa umbali wa mwendo wa siku moja kutoka Madinah, lilikuwa katikati ya Madinah na Khaibar.

Aliamua kwenda huko kwa ajili ya kujibu mashambulizi yaliyofanywa na Uyainah Ibn Hiswni dhidi ya mifugo ya Madinah iliyokuwa ikichunga sehemu za “Al-Ghaabah”.

Miongoni mwa mifugo hiyo, alikuwemo ngamia wa Mtume. Usiku mmoja Uyainah akisaidiana na watu wa kabila la Ghatwfaani walilivamia kundi hilo la mifugo.

Wakamuua mchungaji na kumchukua mkewe na ngamia, khabari ya uchokozi ule dhidi ya waislamu ikamfikia Salamah Ibn Al-Akwaa; mmoja wa maswahaba wa Mtume.

Yeye akachukua hatua ya kupanda juu ya jabali “Sal-i”, akaanza kupiga yowe la kuomba msaada.

Mayowe yake hayo yakapasua ngoma za masikio ya watu wa Madinah, hapo hapo ikapigwa mbiu kwa waislamu: “Ewe farasi wa Allah panda!” Kusikia mbiu hiyo, watu wakaanza kushindana kuiitikia mbiu ya Mtume wa Allah, Bwana Mtume akampa Al-Miqdaad Ibn Al-Aswad uamiri-jeshi wa kundi lililofika mwanzo. Akamwambia:

“Toka nenda kawafuatilie watu hao mpaka niungane nawe pamoja na watu wengine”.

Wakaenda shoti wakizifuatia nyayo za wachokozi wale, wakafanikiwa kuwadiriki wa mwisho mwisho, wakawaua watatu miongoni mwao.

Wakafanikiwa kuwaokoa ngamia kumi wenye mimba na wengine kumi wakaponyoka na adui.

 Huku nyuma, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatoka na maswahaba wake mia tano na kuungana na lile kundi tangulizi.

Wakakusanyika Dhiy Qirdi, lakini tayari wachokozi wale walikuwa wameshaponyoka na kujichanganya kwenye makazi ya kabila la Ghatwfaani.

Mtume wa Allah akaamua kutowafuata huko, akapiga kambi hapo siku moja, kisha huyoo akarejea Madinah baada ya siku tano.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *