Mauaji ya Sayyidna Aliy

Mnamo mwaka wa 40 Hijiriya, Allah Ataadhamiaye alimpumzisha khalifa wa Mtume wake; Sayyidna Aliy, kutokana na mizozo endelevu hii na tofauti sugu hizo zilizo ugubika umma wa Kiislamu. Akamchanganya na ndugu zake mashahidi na wema, na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao! Na sababu ya kifo chake, ni kwamba walikutana watu watatu katika Makhwaariji, wakajikumbusha yale yaliyo wasibu Makhawaariji wenzao na wakaona hawawatendei haki wenzao hao walio uawa kama hawatalipa kisasi chao. Kwa hivyo basi kwa kauli moja wakaafikiana mmoja wao aende Koufa akamuue Imamu Aliy, na kura ya utekelezaji wa hilo ikamuangukia Abdurahman bin Muljim wa kabila la Al-Muraadiy. Na mwingine wa pili ambaye ni Al-Barki bin Abdillah wa kabila la Tamim, yeye aende Shamu akamuue Muawiyah. Na watatu wao ambaye ni Amrou bin Bakri wa kabila la Tamim, yeye aende Misri akamuue Amrou bin Al-Aaswi. Na wote watatu hawa wakaagana usiku ambao watayatekeleza hayo maazimio yao maovu waliyo afikiana.

Twendapo na Al-Barki yeye akaenda kwa Muawiyah, akamvizia katika swala ya Alfajiri, akampiga upanga, ukamuingia maeneo ya makalioni, lakini hakufanikiwa kumuua. Muawiyah akaamuru akamatwe na kuuawa, akauawa. Tukija kwa Amrou bin Bakri, yeye alikwenda Misri kwa Amrou bin Al-Aaswi kama walivyo kubaliana. Nyota njema ikawa upande wa bin Al-Aaswi, kwani yeye siku hiyo hakutoka kwenda msikitini kuswali swala ya Alfajiri, kwa sababu ya maradhi. Na aliye kuwa akiwaswalisha watu alikuwa ni naibu wake; Khaarija bin Hudhaafa wa kabila la Sahmiy. Muovu huyo akampiga upanga naibu Imamu kwa kumdhania kuwa ndiye gavana Amrou bin Al-Aaswi. Dhana yake ikaruka patupu, akakamatwa na kuuawa. Ama Abdullah bin Muljim, yeye akaenda Koufa, akamjongelea Amirul-Muuminina katika Alfajiri ya usiku ule ambao Makhawaariji walikongamana kutekeleza dhamira yao chafu. Na ikasadifu kuwa ni alfajiri ya mwezi saba (07) Ramadhani. Basi wakati ambapo Amirul-Muuminina akiwanadia watu: Swalaa! Swalaa! Tahamaki muovu yule akampiga upanga huku akisema: Hukumu ni ile inayo toka kwa Allah tu, na si yako wewe Aliy wala wafuasi wako. Imamu Aliy akawaambia walio kuwepo hapo: Watu wakamzingira muovu huyo, wakamtia mikononi. Imamu Aliy akamtanguliza Ja’adah bin Hubairah kuwaswalisha watu swala ya Alfajiri. Baada ya swala, Sayyidna Aliy akasema: Nafsi kwa nafsi, nikifa naye muuweni kama alivyo niua na kama nitapona, nitaangalia mwenyewe nimfanye nini. Enyi kizazi cha Abdul-Mutwalib! Sitaki mmwage damu za Waislamu kwa kisingizio cha kuuwa kwa Amirul-Muuminina. Ehee! Tanabahini! Kabisa asiuawe ila tu muuaji wangu. Angalia, ewe Hasan! Iwapo mimi nitakufa kwa sababu ya pigo hili la upanga, basi nawe mpige (muuaji wangu) pigo kwa pigo na wala usimkate kate kwa kumtenganisha viungo muuaji huyo. Kwani mimi nilipata kumsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Jiepusheni kabisa na uuaji wa kutenganisha viungo hata kama ni kwa mbwa mng’ataji”. [MAJMAU ZAWAAID 06/277]

Imamu alipo maliza kusema maneno yake hiyo, mara akaingia Jundub bin Abdillah, akasema: Ewe Amirul-Muuminina! Kama tutakukosa (ukafa) na wala hatuombi kukukosa, basi je tumbai Hasan kuwa Amirul-Muuminina? “Akajibu: Mimi sikuamrisheni na wala sikukatazeni hilo, nyinyi ni wapevu wa fikra”. Kisha akawaita wanawe; Hasan na Husein, akawaambia: “Ninakuusieni kumcha Allah na wala msiitake dunia hata kama hiyo dunia itakutakeni nyinyi na wala msikililie chochote mlicho kikosa. Na semeni kweli, muhurumieni yatima, msaidieni mpotea njia na tendeni amali kwa ajili ya Akhera. Na kuweni hasimu (wagomvi) wa dhaalimu na mnusuruni mdhulumiwa na yatendeeni amali yaliyomo ndani ya Kitabu cha Allah na wala msiiogope kwa ajili ya Allah lawama ya mwenye kulaumu”.

Kisha akamuangalia Muhammad Al-Akbar bin Al-Hunaifah, akamwambia: “Je, umeyahifadhi (umeyashika) haya niliyo wausia ndugu zako?” Akajibu: Naam (nimeyasikia). Akasema (Imamu): “Basi hakika mimi ninakuusia na wewe kama hivyo. Na ninakuusia kuwaheshimu kaka zako kwa sababu ya haki yao kubwa waliyo nayo juu yako. Na uitii amri yao na wala usikate shauri lolote kinyume nao”.

Halafu tena akawageukia Hasan na Husein, akawaambia: “Ninakuusieni kumuangalia huyu, kwani hakika yeye ni ndugu yenu shakiki na ni mwana wa baba yenu. Nanyi mmekwisha tambua ya kwamba baba yenu anampenda”. Na akamwambia Hasan: “Ninakuusia ewe mwanangu kumcha Allah, kusimamisha swala kwa wakati wake na kutoa zaka mahala pake. Na kutawadha udhu kamili kwani hakika hapana swala ila kwa twahara. Na ninakuusia kusamehe, kuzuia hasira, kuunga udugu, kumchukulia upole mtu jahili, kujifunza dini na kuthibiti katika dini. Na (ninakuusia) kuitunduwiya Qur’ani, ujirani mwema, kuamrisha mema na kukataza maovu na kujiepusha na mambo machafu”.

Baada ya kumaliza kuwausia wanawe, Imamu Aliy akaendelea kumdhukuru Allah mpaka akaiga dunia-Allah amuwiye radhi. Akakoshwa na wanawe Hasan na Husein na mwana wa nduguye; Abdullah bin Ja’afar. Akakafiniwa kwa nguo tatu zisizo na kanzu ndani yake na swala ya jeneza ikaongozwa na mwanawe Hasan.

Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-alikaa kwenye kiti cha ukhalifa kwa kipindi cha miaka minne, miezi saba na siku kadhaa. Ndani ya kipindi hicho Allah Atukukiaye alipenda kuuonjesha umma kikombe cha madhara, kwa sababu ya kukhitalifiana naye. Alifanya hivyo, ili umma uwe umeonja mambo mawili pamoja; yenye kuleta furaha na yale yenye kuleta madhara, ukata udugu na utapanyi. Kwa ajili hiyo basi, umma uweze kujichagulia lile utakalo wafikishwa na Allah.

Na katika zama za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie, Allah-utakati wa mawi ni wake-alikuwa akiufundisha umati Muhammad kwa adhabu anayo waletea haraka, ikiwa ni jazaa ya matendo fulani yaliyo tendwa. Alifanya hivyo ili kuuhadharisha umma kutokuyarudia makosa hayo, kama alivyo waadhibu kwa ushindwa katika vita vya Uhud pale Waislamu walipo legea, wakazozana katika amri na wakamuasi Mtume. Kwa darasa hilo basi, baada ya hapo Waislamu hawakuyarudia tena makosa hayo matatu, kwa sababu ya kutambua kwao kwamba hayo yanawabaidisha (yanawaweka mbali) na Allah. Na muda wa kuwa wamo katika hali hiyo, basi bila ya shaka nusra ya Allah itakuwa mbali nao. Na hali kadhaalika katika tukio hili, Allah Ataadhamiaye alitaka kuwaadhibu Waislamu wale wa mwanzo, kwa sababu ya makosa yaliyo tendwa na baadhi yao kwa khalifa wao ambaye walikula kwake kiapo cha utii, kisha wakakitengua kiapo chao hicho na si hivyo tu bali wakamuua kwa dhulma. Kwa minajili hiyo basi, ndipo Allah akawaadhibu vikali kwa kosa lao hilo, wakaadhibiwa kwa kupigana na kuuana wenyewe kwa wenyewe. Hali hiyo ikawapelekea kuchangukana, kugawika na kutokuwa na sauti moja na kukosekana kwa utii kwa viongozi wao.

Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-alipo uawa hali ya kuwa ni shahidi, watu wa Koufa wakambai mwanawe Hasan kuwa khalifa wao. Na wa mwanzo kumbai alikuwa ni Qais bin Sa’ad bin Ubaadah, alimwambia: Kunjua mkono wako nikubai kwa sharti ya kufuata Kitabu cha Allah, Sunna ya Mtume wake na kuwapiga vita wauaji. Sayyidna Hasan akasema: (Nakubali baia) kwa Kitabu cha Allah na Sunna ya Mtume wake, kwani viwili hivyo vinaleta sharti zote. Hapo ndipo watu wakambai kwa sharti hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *