MANDHARI NA VITISHO VYA SIKU YA KIYAMA.


Kuhimidiwa na kutukuzwa kunamstahikia Allah; Mola Mlezi wa viumbe wote, ambaye ametuneemesha kwa neema ya Imani na Uislamu. Na Rehema na Amani zimuendee Bwana wa ulimwengu; Mtume wetu Muhammad. Na ziwaendee pia Aali na swahaba zake kila mara na kila wakati.
Ama baad,
Mpendwa mwana-jukwaa letu.
Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!
Naam, tuendelee kuangalia, kutafakari na kuzingatia mandhari za Kiyama na vipengele vyaka kama ilivyo elezwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na mwenye Kiyama chake; Allah Mtukufu, ili asaa kwa rehema yake Mola tukaingiwa khofu na tukajawa na imani, tukafanya maandalizi yatakayo tudhaminia amani na salama katika siku nzito hiyo kabla hatujachelewa.
Naam, jukwaa letu la leo, litaendelea kuongozwa na anuani mama kama inavyo someka mbele yetu:
Mandhari na vitisho vya siku ya Kiyama.
Naam, ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaishi na kipengele kisemacho:
Nini kadiri ya urefu wa siku ya Kiyama.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-kadiri/kiasi cha muda itakayo dumu/chukua siku ya Kiyama, ni jambo lililo tajwa na kuelezwa na mwenyewe Muumba wa siku hiyo; Allah Mtukufu kupitia neno lake: “Muuliza aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea, kwa makafiri-ambayo hapana awezaye kuizuia-kutoka kwa Allah Mwenye mbingu za daraja. Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu!” Al-Ma’arij [70]:01-04
Na ufahamu ya kwamba na kipindi/muda wote huo ni katika kungojea hisabu; kuhisabiwa waja kwa amali walizo zitenda walipo kuwa kwenye nyumba ya matendo; duniani. Na pamoja na hivyo, lipo kundi jema lililo fanya ibada duniani kwa ajili ya Allah pekee, hao siku ya Kiyama itawapitia kama kiasi cha ule muda uliopo baina ya swala ya Adhuhuri na Laasiri, hivyo ndivyo utakavyo kuwa urefu wa siku hiyo kwao. Na hilo ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-pale alipo sema: “Siku ya Kiyama kwa Waumini (itakuwa) kama kadiri/kiasi cha ule muda uliopo baina ya Adhuhuri na Laasiri”. Al-Haakim [SAHIH AL-JAAMI’I – 8193]
Naam, pamoja na jazaa hiyo, wataongezewa ikramu kwa kutosimamishwa kwenye ardhi ya makusanyo kwenye jua kali. Wakati ambapo watu wengine watakuwa wakiungua kwenye jua kali lisilo na mithali, wao watakuwa katika kivuli cha Arshi ya Rahmaani wakila katika ile karamu waliyo andaliwa na mwenyewe Mfalme; Allah. Kisha watakwenda kwenye hodhi la Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wanyweshwe kwa mkono wake Bwana Mtume funda moja liwashuke kwa raha; hawatashikwa na kiu tena baada ya kunywa funda hilo.
Atakaye pendezwa kuiangalia siku ya Kiyama.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-kubali na ujue ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakaye pendezwa kuiangalia siku ya Kiyama kwa kuona kwa macho, basi na asome (sura hizi): {Idhas-shamsu kuwwirat (81)} na {Idhas-samaaun-fatwarat (82)} na {Idhas-samaaun-shaqat (84)}”. Ahmad, Tirmidhiy & Al-Haakim [SAHIH AL-JAAMI’I 6293]-Allah awarehemu.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-fahamu ya kwamba hakika si kwa jinginelo, sura tatu hizi zimekikusu mno Kiyama kwa sababu ndani yake mna maelezo ya:
Kuchanika na kupasuka kwa mbingu,
Kukunjwa kwa jua,
Kuzimwa kwa nyota, na
Kupukutika kwa sayari na baki ya fazaa na vitisho vyake vingine. Na
Kutoka kwa watu makaburini mwao na kwenda kwenye magereza (Jahannamu/motoni) yao au kwenya makasiri yao (Janna/peponi), hilo likiwa ni baada ya kupewa vitabu vyao ama kwa mikono yao ya kulia/kushoto au kwa nyuma ya migongo yao kulingana na matendo yao waliyo yatenda na kisha waambiwe wavisome wao wenyewe.
Allah Mtukufu amesema:
“Itapo chanika mbingu”. Al-Inshiqaaq [84]:01
“Mbingu itapo chanika”. Al-Infitwaar [82]:01
“Na siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu…”. Al-Furqaan [25]:25 – Basi utaziona hizo mbingu zimekuwa dhaifu, zimechanika chanika na kupasuka, kama ilivyo katika neno lake Yeye aliye Mtukufu: “Na mbingu zitafunguliwa, ziwe milango”. An-nabaa [78]:19 – Na mawingu yatakuwa ni kizuizi baina ya mbingu na ardhi.
Na kauli yake Yeye aliye Mtukufu: “Jua litakapo kunjwa”. At-takwiir [81]:01 – Amesema Ibnu Abbas-Allah awawiye radhi: “Kukunjwa kwa jua (kuliko tajwa, muradi wake ni) kuingizwa ndani ya Arshi. Na kauli nyingine ni kuondoshwa (kuzimwa) kwa mwangaza wake…. Hiyo ni kauli ya Al-Hasan na Qataadah. Twendapo basi na kauli hizo (maana itakuwa) jua litakunjwa, kisha utaondoshwa mwangaza wake na halafu litatupiliwa mbali. Allah ndiye Mjuzi mno.

Na kauli yake Yeye aliye Mtukufu: “Na nyota zikazimwa”. At-takwiir [81]:02 – Yaani: Zitakapo tapanyika. Na kauli nyingine: Zitakapo pukutika kutoka kwenye mikono ya Malaika, kwa sababu na wao watakufa. Na pamesemwa katika khabari: Nyota zimeangikwa (zimetundikwa) baina ya mbingu na ardhi kwa minyororo iliyo shikiliwa na Malaika. Na amesema Ibnu Abbas-Allah awawiye radhi: (Maana ya) kuzimwa ni kubadilika na asili ya neno hilo kuzimika ni kumiminika, na kisha kuangukia baharini. Halafu kwa pamoja nyota na bahari zitalipuka moto mkubwa.

Na kauli yake Yeye aliye Mtukufu: “Na milima ikaondolewa”. At-takwiir [81]:03 kauli hii inafanana na kauli yake: “Na siku tutakapo iondoa milima”. Al-Kahfu [18]:47 – Yaani: Imebadilika kutoka kwenye mada ya mawe na kuwa kama:
Tifutifu la mchanga,
Sufi zilizo chambuliwa,
Mavumbi yanayo peperushwa,
Sarabi (mazigazi, mangati, mangazimbwe).

Na kauli yake Yeye aliye Mtukufu: “Na ngamia wenye mimba pevu watakapo achwa wasishughulikiwe”. At-takwiir [81]:04 – Yaani: Watakapo telekezwa na wamiliki wake kiasi cha kushindwa hata kuwakama maziwa kutokana na kishindo cha siku ya Kiyama. Na hakika si kwa jenginelo, wametajwa ngamia na si wanyama wengine, kwa sababu wao ndio walikuwa mali inayo pendwa mno na Waarabu zama hizo, kiasi cha kwamba mmiliki wa ngamia wengi miongoni mwao ndiye aliye onekana mtu tajiri sana.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:
رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١
“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41
Mola wetu Mtukufu kwa rehema zako tunakuomba utupe Amani na Salama katika:
يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ …١٠٦ [آل عمران: 106]
“Siku ambayo nyuso zitanawiri na nyuso zitasawijika…”. Aali Imraan [03]:106
Hapa ndio mwisho wa jukwaa letu hili kwa juma la leo, tunatumai utakuwa umejifunza na kuelewa kitu/jambo kupitia maneno ya Allah na Mtume wake, maneno yanayo tueleza kadiri na kiasi cha urefu wa siku nzito na ngumu; siku ya Kiyama. Na kwa hivyo basi, utakuwa umetafakari na kuanza kuchukua hatua za kujiandaa na siku hiyo.
Na hali kadhalika tumekiangalia Kiyama kwa macho kama kwamba tunakiona kwa macho kupitia sura hizo tatu kama alivyo sema Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na tumezifafanua baadhi ya aya za sura hizo kwa kadiri ya kutosha jukwaa letu. Kwa anaye taka ufafanuzi wa kina, wenye kukata kiu cha msomaji makini, basi na azirejee tafsiri za Qur-ani; zile za wale Mufasirina wa mwanzo (wakongwe) na hawa wa leo, atastafidi kwa kiasi cha kutosha.
Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine katika anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.
Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.
Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:
وَمَا كَانَ رَبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَى حَتَّى يَبْعَثَ فِي أُمِّهَا رَسُولًا يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا وَمَا كُنَّا مُهْلِكِي الْقُرَى إِلَّا وَأَهْلُهَا ظَالِمُونَ٥٩ [القصص: 59]
“Na Mola wako Mlezi haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika miji yake mikuu awasomee aya zetu. Wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake wawe madhaalimu”. Al-Qaswas [28]:59

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *