SOMO LA ISHIRINI – MANDHARI NA MUONEKANO WA WAKANUSHAJI NA MAKAFIRI.

Kuhimidiwa na kutakaswa ni kwake Allah, ambaye: “Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, naye ndiye wa Dhaahiri na wa Siri, naye ndiye Mjuzi wa kila kitu”. Ewe Mola wa haki! Mshushie Rehema na Amani Mbora wa viumbe vyako vyote; Bwana wetu Muhammad, Yeye, Aali zake na jamia swahaba wake mpaka ile siku ambayo kila nafsi italipwa kulingana na amali yake.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Limewadia juma jingine tena, kwa uwezo na mapenzi yake Allah; Mola Muumba wetu tumekutana katika jukwaa letu, sote tukiwa na lengo lile lile ambalo si jinginelo zaidi ya kukumbushana kuhusiana na siku ambayo imeshabisha hodi, tayari kuingia kwa amri yake Allah. Hiyo ni ile siku yenye vituko na vishindo vikuu. Ili asaa kupitia kukumbushana kwetu huku, tukajikurubisha kwa Mola wetu kwa kuyatekeleza yale yote aliyo tuamrisha na kuyaacha yale aliyo tukataza, ili tupate amani na salama katika siku hiyo isiyo kwepeka.

Mandhari ya wakanushaji na makafiri.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo hapo juu, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kukiangalia kipengele kingine kisomekacho:

  • Kwa nini basi, makafiri watahisabiwa ikiwa matendo yao yamepomoka (hayawapatii thawabu mbele za Allah)?

Naam, ikiwa tunafuatana pamoja katika jukwaa letu hili la Kiyama, basi ndugu mwana jukwaa hutashindwa kukumbuka ya kwamba tulilihitimisha jukwaa letu lililo litangulia hili la juma hili kwa kusema kwamba kafiri hana mema atakayo lipwa Akhera. Ni kwa hitimisho hilo basi, ndio juma hili tunajiuliza swali hilo hapo ambalo ndilo limebeba anuani ya jukwaa letu, tulirudie tena swali hilo ili tupate kuondokea hapo: Kwa nini basi, makafiri watahisabiwa ikiwa matendo yao yamepomoka (hayawapatii thawabu mbele za Allah)?

Ama tukilijibu swali kwa nini makafiri watahisabiwa na kuwekwa matendo yao kwenye mizani adilifu ya Allah ilhali ya kuwa matendo yao yameruka patupu, tufahamu na kujua kwamba kuhisabiwa huko ni kwa sababu kadhaa, miongoni mwazo ni:

  1. Kusimamisha hoja dhidi yao na kuonyesha uadilifu wa Allah kwao ili wasipate udhuru wa kujitetea mbele yake Yeye aliye muadilifu. Ni kwa ajili hiyo basi, atawauliza na kuwahisabu na si hivyo tu bali atawaonyesha pia sijila (madaftari ya kumbukumbu) zilizo sajili na kuhifadhi matendo yao. Na mizani itaonyesha ukubwa wa madhambi yao na uovu wa matendo yao.
  2. Allah atawahisabu kwa matendo yao ili kuwaumbua mbele ya kadamnasi katika siku hiyo ya hisabu na jazaa sawiya.

Anasema Shaikhul-Islaam-Allah amrehemu: “Linalo kusudiwa kwa hisabu ni kule kuonyeshwa makafiri matendo yao na kuwaumbua kwayo. Na hali kadhalika linakusudiwa kwa hisabu kuyapima matendo mema kwa yale matendo maovu. Sasa basi angalia, iwapo itakusudiwa kwa hisabu hiyo maana ya kwanza, basi hapana chembe ya shaka wao watahisabiwa kwa mazingatio hayo. Na kama itakusudiwa hisabu kwa maana ya pili, itakuwa ni kwamba makafiri watabakiwa na mema ambayo wanastahiki kuingizwa peponi kwa sababu ya mema hayo, kuishika maana hiyo itakuwa ni kosa la wazi kabisa”. [MAJ’MUU AL-FATAAWAA 04/305]-Allah amrehemu.

Imamu Ibnu Kathiir-Allah amrehemu-naye amesema: “Na ama makafiri yatapimwa matendo yao hata kama hawana mema yatakayo wanufaisha; yatakayo kaa mkabala wa ukafiri wao. Matendo yao hayo yatapimwa ili kudhihirisha uovu wao na ili kuwafedhehesha mbele ya kadamnasi”. [AN-NIHAAYAH ya Imamu Ibnu Kathiir 02/35]-Allah amrehemu.

  1. Ni kwamba makafiri wamekalifishwa (wamelazimishwa kwa njia ya wajibu) kufuata mashina (misingi) ya sharia kama ambavyo walivyo kalifishwa kufuata matawi (tanzu) zake (hiyo sharia). Ni kwa sababu hiyo basi, wataulizwa kwa waliyo acha kuyatenda na kuikhalifu katika hayo haki. Imamu Al-Qurtubiy-Allah amrehemu-anasema: “Na ndani ya Qur’ani mna dalili zinazo onyesha kwamba wao wamesemezwa kwazo (hizo tanzu za sharia) na wataulizwa kwazo na kuhisabiwa juu yake na kisha kulipwa kwa kuzinyongesha (kuacha kuzitenda tanzu hizo). Hivyo ni kwa kuwa Allah Ataadhamiaye anasema: {… Na ole wao wanao mshirikisha. Ambao hawatoi zaka na wanaikataa Akhera”. Fusswilat [41]:06-07

Basi akawakamia kwa kuzuia kwao kutoa zaka na akaeleza ya kwamba wahalifu hao wataulizwa: {Ni nini kilicho kupelekeni motoni? Waseme: Hatukuwa miongoni mwa walio kuwa wakiswali. Wala hatukuwa tukiwalisha masikini. Na tulikuwa tukizama pamoja na walio zama katika maovu. Na tulikuwa tukiikanusha siku ya malipo”. Al-Muddathir [74]:42-46

Kwa kauli yake Mola ikabainika ya kwamba washirikina wamesemezwa kwa nguzo za Imani (kuamini Uislamu), kufufuliwa, kusimamisha swala na kutoa zaka. Na kwamba wao wataulizwa juu ya utekelezaji wa hayo na watalipwa (kwa kuyatekeleza au kwa kutoyatekeleza) hayo.

  1. Ni kwamba makafiri wanatofautiana katika ukafiri wao na madhambi yao na maasia yao, nao wataingia motoni kwa kadiri ya madhambi hayo. Kwani moto una tabaka; nyingine ziko chini ya nyingine; kuna tabaka la chini na linalo lifuatia mpaka lile la chini kabisa. Kama ambavyo pepo nayo ina daraja; daraja nyingine ziko juu ya nyingine; kuna pepo ya juu na inayo ifuatia mpaka ile ya juu kabisa. Na kadiri ambavyo mtu anakuwa na ukafiri zaidi na upotovu topezi ni kwa kadiri hiyo hiyo atakuwa na adhabu kali zaidi. Na baadhi ya makafiri watakuwa kwenye tabaka la chini kabisa la moto na miongoni mwao ni wanafiki: “Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini kabisa motoni, wala hutompata yeyote wa kuwanusuru”. An-Nisaa [04]:145

Anasema Sheikhul-Islaam; Ibnu Taimiyah-Allah amrehemu: “Adhabu ya ambaye yamekithiri maovu yake, ni kubwa zaidi kuliko adhabu ya ambaye yamekuwa machache maovu yake. Na atakaye kuwa na mema, atapunguziwa adhabu kama ambavyo Abu Twaalib (ami yake Mtume aliye mlea) atakuwa na adhabu pungufu kuliko Abi Lahabi (ami yake Mtume aliye mpiga vita)… Basi ikawa hisabu ni kwa ajili ya kubainisha daraja za adhabu na si kwa ajili ya kuwaingiza kwao peponi”. [MAJ’MUU AL-FATAAWAA 04/305]-Allah amrehemu.

  • Watatamani makafiri lau wangelikuwa Waislamu.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Watakapo kusanyika motoni watu wa motoni na wale alio wataka Allah pamoja nao katika watu wa Kibula (Waislamu). (Hapo) makafiri watasema kuwaambia wale Waislamu: Kwani nyinyi hamkuwa Waislamu? Watajibu Waislamu (walio motoni): Kwani (tulikuwa Waislamu). Basi watasema (wale makafiri baada ya jibu hilo la Waislamu): Basi Uislamu wenu haukukusadieni kwa kuwa nyinyi mko pamoja nasi motoni. Watasema (Waislamu): Tulikuwa na madhambi ambayo tumeadhibiwa kwa sababu ya hayo. Basi hapo Allah atayasikia hayo waliyo yasema (makafiri), aamuru kutolewa walioko motoni miongoni mwa watu wa Kibula, basi watolewe. Watatoka, makafiri watakapo liona hilo, hapo watasema: Eeh! Laiti sisi tungelikuwa Waislamu, tukatolewa motoni kama walivyo tolewa wao”. Kisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaisoma kauli yake Mola: {HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wangekuwa Waislamu} Al-Hijri [15]:02

Eeh! Furaha yao iliyoje hao Waislamu; wadau wa Tauhidi (kumpwekesha Allah katika ibada). Basi ewe ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-ijue na uitambue thamani ya Uislamu wako na si hivyo tu bali itambue pia thamani yako chini ya kivuli cha mwavuli wa Uislamu. Upende Uislamu wako, ishi na Uislamu wako na jitahidi usife ila umekufa nao ili ukakufae kaburini na kesho mbele ya Allah baada ya kwisha kukufaa na kukunufaisha leo hapa duniani.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Ewe Mola uliye umba usiku na mchana zikapatikana siku, juma, miezi na hata miaka! Tunakuomba ujaalie juma hili bali umri wetu wote ulio bakia, uwe ni faraja kwetu na kwa jamia ummati Muhammad popote pale ulipo katika ulimwengu wako. Tufungulie milango ya kheri na baraka katika matendo, kauli, nia na dhamira zetu na utuwezeshe kutenda yale ambayo humo inapatikana radhi yako na utuongoze katika njia yako iliyo nyooka. Ewe Mola wetu Mlezi tutakabalie duaa!

Hapa ndio tamati ya jukwaa letu juma hili, tunamuomba Allah Mola Muumba wetu amnufaishe na jukwaa hili kila anaye ingia mtandaoni na kulifuatilia jukwaa hili. Atupe nguvu waandaaji wa jukwaa ili tuendelee kukuletea jukwaa hili kila juma lipate kutuhimiza na kutusukuma kutenda amali njema zitakazo kuwa uokovu wetu katika siku inayo tisha; siku ya Kiyama.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine katika anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ قُوٓاْ أَنفُسَكُمۡ وَأَهۡلِيكُمۡ نَارٗا وَقُودُهَا ٱلنَّاسُ وَٱلۡحِجَارَةُ عَلَيۡهَا مَلَٰٓئِكَةٌ غِلَاظٞ شِدَادٞ لَّا يَعۡصُونَ ٱللَّهَ مَآ أَمَرَهُمۡ وَيَفۡعَلُونَ مَا يُؤۡمَرُونَ ٦

Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali wenye nguvu, hawamuasi Allah kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa”. At-Tahreem [69]:06

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *