MAMBO YALIYO HARAMU KWA MWENYE HEDHI

1. Kuswali. Kwa ushahidi wa hadithi hiyo ya Fatmah Bint Abiy Hubaysh tuliyoitaja hapo katika Istihaadha.

Imepokelewa riwaya kutoka kwa Fatmah Bint Abiy Hubaysh – Allah amuwiye radhi – kwamba yeye alikuwa akitokwa na istihaadha. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie- akamwambia: “Ikiwa ni damu ya hedhi, basi itakuwa ni damu nyeusi ijulikanayo. Itakapokuwa hivyo, basi acha kuswali, ikiwa ni nyingine basi tawadha na uswali, hakika si vingenevyo huo ni mshipa”. Abu Daawoud.

2. Kusoma Qur-ani na kugusa na kuuchukua msahafu kwa ushahidi tulioutaja katika yaliyo haramu kwa mwenye janaba (namba 4 na 5).

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “HAPANA AKIGUSAYE ILA WALE WALIOTAKASWA” [56:79]

3. Kukaa msikitini si kupita njia kwa ushahidi uliotajwa katika yaharamikayo kwa mwenye janaba (namba 2).

Haya yanafahamika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu : “…WALA HALI MNA JANABA, ISIPOKUWA MMO SAFARANI(mnapita njia)…”.

Miongoni mwa dalili zinazoonyesha kuwa nafsi ya kupita hakukuharamishwa, mbali na ushahidi uliopita ni hii riwaya iliyopokelewa na Imam Muslim kutoka kwa Bi: Aysha –Allah amuwiye radhi- amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliniambia: “Niletee mswala msikitini” Nikamwambia: Mimi nimo hedhini. akaniambia. “Bila shaka hedhi yako hiyo hunayo mkono mwako “.

4. Kutufu Al-Kaaba kwa ushahidi uliopita katika yaliyoharamishwa kwa mwenye janaba (namba 3).

Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – aliposema: “Kutufu al-Kaaba ni swala, isipokuwa kwamba Allah amekuhalalishieni kuzungumza ndani yake (twawafu), basi atakayazungumza na asizungumze ila la kheri”. Al-Hakim.

Imepokelewa na Bi Aysha-Allah amuwiye radhi – amesema: Tulitoka hali ya hatujidhani ila ni wenye kuhirimia hija, tulipofika sehemu iitwayo sarafu nikaanza kutokwa na hedhi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie- akaingia kwangu na il-hali nikilia akaniuliza: “Una nini, umeigia hedhini?” nikamjibu: Naam. Akaniambia : Hakika hili ni jambo ambalo Mwenyezi Mungu amewaandikia (amewafaradhishiya) mabinti wa Adam (wanawake). Fanya/tekeleza ibada azifanyazo hujaji isipokuwa usifanye twawafu katika al-kaaba”. Na katika riwaya nyingine “mpaka utwahirike”.

5. Kupita msikitini kwa sababu damu ni najisi na ni haramu kuuchafua msikiti kwa najisi na uchafu mwingineo. Ikiwa mwanamke atajiaminisha kutokuuchafua msikiti, basi anaweza kukatiza na kupita msikitini

6. Kufunga, haijuzu kwa mwenye hedhi kufunga swaumu ya fardhi au ya suna, haya ni kwa mujibu wa riwaya ya Abiya Said-Allah amuwiye radhi. Kwamba Mtume wa Mwenyezi Allah –Rehema na Amani zimshukie – alisema kuhusiana na mwanamke wakati alipoulizwa juu ya maana ya upungufu wa dini yake (mwanamke): “Je, hakuwa aingapo hedhini, haswali na hafungi?”. Bukhariy na Muslim

Atakidhi/atalipa mwenye hedhi swaumu iliyomfutu katika kipindi cha hedhi baada ya kutwahirika kwake. Wala hawajibikiwi kukidhi swala zilizompita katika kipindi hicho. Itakapokatika hedhi yake, itamuwajibikia funga hata bado hajakoga.

Impokelewa kutoka kwa Bi Muaadhah, amesema: nilimuuliza Bi Aysha –Allah amuwiye radhi–na akasema: kwa nini mwenye hedhi anakidhi swaumu na wala hakidhi swala ? Akasema: “hayo yalikuwa yakitupata tulipokuwa pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimeshukie, basi tukiamrishwa kukidhi swaumu na wala hatukuamrishwa kukidhi swala” Bukhariy na Muslim.

7. Kuingiliwa yaani kufanya naye tendo la ndoa. Haya yanatokana na kauli ya Allah: “BASI JITENGENI NA WANAWAKE WAKATI WA HEDHI (zao) WALA MSIWAKARIBIE MPAKA WATWAHARIKE. WAKISHAKUTWAHIRIKA BASI WAENDEENI KATIKA PALE ALIPOKUAMRISHENI ALLAH…” [2:222].

Muradi na makusudio ya kujitenga na wanawake ni kuacha kuingiliana nao kimwili. Imepokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Saad. Allah Amuwiye radhi – kwamba yeye alimuuliza Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie: Ni kipi kinachonihalalikia kwa mke wangu wakati awapo hedhini? (Mtume) akamjibu: “Ni halali yako kilicho juu ya ya shuka (gaguro). Abu Daawoud.

NYONGEZA KATIKA KUTAJA UMRI WA KUBALEGHE

Tunamaanisha na kukusudia kwa neno “baleghe” ule umri ambao atakapoufika mtu mwanamume au mwanamke hupata sifa ya kuwa ni mtu MUKALLAFU.

Yaani sasa anatakiwa kuyatekeleza yale yote aliyoamrishwa au kukatazwa na sheria; tangu swala, swaumu, hijah na ibada nyingenezo. Baleghe hujulikana kwa kupatikana mojawapo ya mambo matatu haya :-

1. Kujiotolea na kutokwa na manii. Hili hushirikiana msichana na mvulana yaani msichana naye hujitolea usingizini kama ajiotoleavyo mvulana.

2. Msichana kuanza kutokwa na damu ya hedhi kipindi cha mwanzo ambacho msichana anaweza kujiotelea au kutokwa na damu ya hedhi ni miaka tisa ya mwezi muandamo. Kuchelewa au kuwahi kupata hedhi hutofautiana baina ya nchi na nchi, mtu na mtu na hali za kimaisha.

3. Mvulana au msichana kutimiza umri wa miaka kumi na tano kwa mwaka wa mwezi mwandamo. Hili ni iwapo hajajitolea au kupata hedhi mpaka kufikia umri huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *