Utangulizi:
- Jina la Makala:
Mpendwa msomaji na mwenza wetu katika jukwaa hili-Allah akurehemu na akudaimishe katika kheri na wema. Si kwa nguvu, ujanja, akili wala uwezo wetu, bali ni kwa uwezo wake Allah Mola Muwezeshaji wa mambo yote, ni juma jingine tunakutana tena katika muendelezo wa Utangulizi wa Makala tunazo kusudia kuanza kukuletea mfululizo wake hivi punde kwa idhini, uwezeshi na msaada wake Allah.
Leo tunapenda kukufahamisha jina tulilo kuchagulia kuwa ndilo liwe jina la utambulisho wa mfululizo wa makala zitakazo anza kukujia hivi karibuni, kwa idhini yake Mola. Makala zetu zote katika mfululizo huu, ambazo mdau na mlengwa wake ni wewe msomaji wetu na sisi waandishi wako na kila mwenye mapenzi mema na Uislamu, zitabebwa na jina hili:
“FAMILIA YA KIISLAMU; MUUNDO, MJENGO NA MPANGO WAKE KWA JICHO LA UISLAMU”
Hilo ndilo litakalo kuwa jina na anuani ya makala tunazo kuandalia, tunamuomba Allah atuwezeshe kuandika kile ambacho kitasaidia kuzijenga, kuziimarisha familia zetu na kuzilea kwa namna iliyo fundishwa na Allah na Mtume wake. Namna itakayo leta tija na matokeo mazuri kwetu sisi, familia zetu, jamii zetu, taifa letu na ulimwengu kwa ujumla wake.
- Kwa nini “Familia ya Kiislamu?”
Naam, tayari umekwisha lijua jina la makala zinazo karibia kukujia, sasa tuangalie ni kwa nini tumechagua kuizungumzia Familia ya Kiislamu na wala si mada nyingineyo?
Sababu kuu ya msingi iliyo amsha ari zetu na kutusukuma kuandika kuhusiana na Familia ya Kiislamu na hususan katika zama zetu hizi ambamo kunashuhudiwa mmomonyoko mkubwa wa maadili katika kila kaya, jamii, taifa na ulimwenguni kote. Kwa jicho letu, mmomonyoko au mporomoko huo wa maadili una uhusiano wa moja kwa moja na familia, kwa sababu familia ndio tofali la mwanzo linalo jenga na kuunda jamii au ndio chembe hai ya kwanza katika mwili wa jamii ya wanaadamu. Kwani ni kutokana na mkusanyiko wa familia kadhaa ndio huundika kijiji au jimbo/mji na kutokana na majimbo/miji kadhaa ndio huundwa dola/nchi ambayo kwa kushirikiana na nchi nyingine huunda mkusanyiko mkubwa wa jamii ya wanaadamu (ulimwengu). Kwa mantiki hiyo basi, kile kinachotoka katika familia, kiwe kizuri au kibaya hupenya na kuingia katika jamii (kijiji/mji), kisha kikasambaa mpaka katika ngazi ya taifa na kuhamia ulimwenguni kote.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-unaona namna familia ilivyo na mahusiano ya moja kwa moja na mazuri au mabaya yanayo tokea katika jamii zetu, mataifa yetu na ulimwengu wetu? Sasa basi tukiichukua familia kama “tofali la msingi” la ujenzi wa jamii, taifa bali na ulimwengu, tofali hilo likifyatuliwa kwa kiwango cha ubora kutokana na malighafi bora. Basi hapana shaka tofali hilo litakuwa imara na madhubuti katika ujenzi wa nyumba yetu “jamii/taifa/ulimwengu”. Na kutokana na uimara huo wa tofali, ni dhaahiri kuwa jengo jamii litakuwa madhubuti, imara na salama kwa wakaazi wake. Na kinyume chake, tofali likiwa duni, lililo fyatuliwa kutokana na malighafi duni, lisilo na ubora na haliko katika kiwango, kutokana na tofali hilo hatuwezi kutegemea kupata nyumba madhubuti na imara “jamii”. Kwa maneno hayo basi, tukitaka kuitengeneza jamii yetu, tunapaswa kwanza kuutengeneza vema msingi wake ambao ni familia na hiyo ndio maana ya kauli mbiu yetu isemayo: “Kutengenea kwa Familia yako, ndio kutengenea kwa jamii na taifa lako”. Na ilivyo ndivyo na sawa kusemwa, ni kwamba siku zote kutengeneza huanzia chini na sio juu, kwa sababu kusimama kwa juu kunategemea kwa asilimia zote uimara na umadhubuti wa chini. Chukua kama mfano, ghorofa lile refu unalo liona, haliwezi kusimama hata likafika hapo lilipo fika, bila ya kuwa na msingi imara na madhubuti wenye dhima ya kulibeba lisiweze kuanguka na kuwadhuru wakaazi wake au hata wapita njia.
- Lengo la makala hizi:
Baada ya kuusoma Utangulizi unao toa taswira ya Familia ya Kiislamu; muundo, mjengo na mpango wake, kisha tukafahamu jina la Makala na msingi wake, sasa ni wakati muafaka wa kujua nini lengo la makala hizi zinazo karibia kukujia.
Lengo mama la makala hizi zitakazo husika zaidi na kadhia ya Familia ya Kiislamu, ni kumjengea msomaji wake ufahamu na uelewa ya kwamba:
- Kuna mafungamano makubwa baina ya Familia kwa maana zote zinazo bebwa na neno hilo na dini. Kwani tunalazimika kufahamu ya kwamba mafungamano na matangamano ya wanandoa ambao ndio chimbuko la familia, si tu ni mafungamano na matangamano ya kimaumbile baina ya jinsia mbili, yanayo sukumwa na matamanio na matashi ya kijinsia. Lakini hayo ni mafungamano ya kidini ambayo huambatana na thawabu yakijengwa kwa namna iliyo fundishwa na mwenyewe Mola Muumba na kuelekezwa na kutolewa ufafanuzi na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie. Mtume ambaye familia yake ndio bora ya familia zote na ndiye ruwaza yetu njema, kama alivyo sema Allah Yeye aliye Mtukufu: “Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Allah kwa anaye mtaraji Allah na siku ya mwisho, na akamkumbuka Allah sana”. Al-Ahzaab [33]:21
Na hali kadhalika wanandoa huweza kupata dhambi iwapo watayajenga mafungamano yao hayo kwa kufuata akili, utashi na matamanio ya nafsi zao kinyume na muongozo wa Allah na Mtume wake. Na hivyo hivyo mahusiano na mafungamano ya wazazi na watoto wao ambao ndio tunda na zao la ndoa ambayo nayo ndio msingi wa familia inayo unda jamii na hatimaye Taifa. Mahusiano na mafungamano hayo ya wazazi na watoto wao, hayakomelei tu kwenye hisia za upendo na mapenzi ya baba na mwana au mama na mwana, bali hayo yanabeba pia hisia za upendo na mapenzi ya kidini ambayo huambatana na thawabu au dhambi (adhabu). Thawabu au dhambi inategemea na namna zitakavyo jengwa na kuelekezwa hisia hizo katika mahusiano hayo.
Uislamu; dini na mfumo kamili wa maisha ya mwanaadamu, umeiweka familia katika uzio na wigo wa utukufu na wala haukuiacha iongozwe na kutawaliwa na matakwa, matashi na matamanio ya watu. Na yote hayo ni kwa ajili ya kuifanya familia ishughulikie jambo muhimu mno la maisha ya ndoa kwa utakashi nia (Ikhlaasi) utakao itegemezea kwenye kutaraji kupata radhi za Allah aliye tuwekea mpango huo wa familia. Na kwa upande mwingine, kuogopa kujitia kwenye ghadhabu na hasira zake Mola Muumba kwa kuukhalifu utaratibu wake alio tuwekea. Na ieleweke ya kwamba utakashi nia katika uendeshaji wa familia, ni jambo linalo ipatia familia nguvu, uimara na umadhubuti na kupitia uimara huo wa familia, jamii nayo huwa imara na yenye maadili mema.
- Kuthibitisha ya kwamba Uislamu una suluhisho na ufumbuzi tosha kwa matatizo yote ya mwanaadamu na katika nyanja zake zote za hatua za maisha yake na hivyo ni kwa sababu Uislamu ni dini kamili, kama anavyo sema Yeye aliye Mtukufu: “… Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndio dini yenu…”. Al-Maaidah [05]:03
Naam, Uislamu hauwezi kukamilika iwapo hautakuwa na sheria zinazo iongoza na kuitawala familia na tena hauwi neema iliyo kamilika kama utayaacha mahusiano na mafungamano ya ndoa bila ya kuyawekea na kuyaratibia sheria zitakazo leta utulivu wa nafsi kwa kila mwanandoa. Na wala Allah hawezi kuridhia Uislamu uwe dini na mfumo wa maisha yetu kama una mapungufu katika sheria na maongozi yake. Basi ni wapi tena ambako tunaweza kupata mpango na mtungo wa familia nje ya Uislamu ambao Allah Mtukufu anasema kuhusiana nao: “Na anaye tafuta dini (mfumo kamili wa maisha) isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri”. Aali Imraan [03]:85
Hayo ndiyo yaliyo tusukuma pamoja na uchache wa maarifa yetu na ufinyu wa akili zetu, kuchukua kalamu na kuanza kuandika kuhusiana na Familia ya Kiislamu. Tutamatie hapa kwa juma hili, huku tukiitafakari kauli yake Allah Yeye aliye Mtukufu: “Enyi mlio amini! Jilindeni (ziokoeni/zikingeni) nafsi zenu na ahali (familia) zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allah kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa”. At-tahriim [66]:06
Tukutane juma lijalo katika mwanzo wa mfululizo wa makala zetu, in shaa Allah.
Ni sisi ndugu zenu katika utumishi wa dini;
WEBSITE UISLAMU.