MAKALA MAALUM – VITA VYA BADRI

VITA VYA BADRI-IJUMAA, RAMADHANI 17/02 A.H. {13th MARCH/624 A.D.}
Allah Mtukufu anasema:
“NA ALLAH ALIKUNUSURUNI KATIKA (vita vya) BADRI, HALI NYINYI MLIKUWA DHAIFU. BASI MCHENI ALLAH ILI MPATE KUSHUKURU (kila wakati kwa neema zinazokujieni)”. [3:123]
Katika mwezi mtukufu wa Ramadhani vilipiganwa vita vya kwanza tangu kuasisiwa kwa dola ya kiislamu Madinah.
Hivi ndivyo vita vya Badri, vita vilivyotoa taswira ya ushindi wa Uislamu. Imepokewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisikia kwamba Abuu Sufyaan anarudi na msafara wa biashara wa Makurayshi akitokea Shamu.
Msafara huo ulikuwa umesheheni mali nyingi, Bwana Mtume akawatolea wito maswahaba wake kuutokea msafara huu, akasema:
“Huo msafara wa Makurayshi una mali zao, utokeeni huenda Allah akaufanya ngawira kwenu”.
Baadhi ya maswahaba wakawa wepesi wakaitika wito na kutoka na wengine wakawiwa uzito kutoka kwa sababu hawakujuwa kuwa kutakuwa na vita.
Na kwa kutambua kwao kwamba lengo la kutoka ni kuteka msafara na sio kupigana au kuua watu.
Abuu Sufyaan alipokaribia kufika Hijazi, akaanza kupeleleza khabari za Mtume kwa kuuliza kila msafara aliokutana nao njiani.
Mpaka akapata khabari kutoka kwa msafara mmoja ya kwamba Mtume amemtokea na maswahaba wake ili kuuteka msafara wake na kupora mali yote.
Hapo ndipo alipoanza kuchukua hatua za makusudi na za haraka za tahadhari. Akapeleka khabari Makah akiwajuliasha juu ya khatari inayoukabili msafara uliosheheni mali zao.
Kwa kawaida Makurayshi walikuwa wakifanya biashara za msimu mara mbili kwa mwaka. Biashara ya majira ya Kaskazi kuelekea nchi ya Shamu na ile ya majira ya Kusi kulekea Yemen.
Hii ndio misafara ya baishara inayotajwa na kauli tukufu ya Allah:
“ILI KUWAFANYA MAKURESHI WAENDELEE. WAENDELEE NA SAFARA ZAO ZA WAKATI WA KUSI (kwenda Yaman) NA WAKATI WA KASKAZI (kwenda Shamu). BASI NA WAMUABUDU BWANA WA NYUMBA HII (Al-Kaaba). AMBAYE ANAWALISHA KATIKA NJAA NA ANAWAPA AMANI KATIKA KHOFU”. [106:1-4]
Khabari zilipofika Makkah, watu wakajiandaa haraka haraka kwenda kuuhami msafara wao usitekwe na Bwana Mtume.
Hawakubakia nyuma katika watukufu wa kikurayshi ila wachache tu ambao walituma wawakilishi wao.
Walipokamilisha maandalizi yao na kukubaliana kuanza safari ya kwenda kupambana na waislamu ili kuulinda msafara wao.
Wanawake wao wakaanza kuimba na kupiga dufu wakiwaponda na kuwabeza waislamu ili kulihamasisha na kulishajiisha jeshi lao. Abuu Jahli ndiye aliyekuwa kiongozi wa makafiri aliyetwaa sukani ya kuliongoza jeshi hili dhidi ya waislamu. Kisha Ibilisi akajitokeza katika sura ya mtu mshauri mtoa nasaha na kuwapambia amali yao hii kwa kuwaambia:
“…LEO HAKUNA WATU WA KUKUSHINDENI, NA MIMI NI MLINZI WENU…” [8:48]
Yaani nitakuwa pamoja nanyi katika dhiki na faraja na sitokutupeni mkono mpaka nione mwisho wa kadhia hii.
 
JESHI LA WAISLAMU.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akatoka siku kadhaa baada ya kuanza kwa mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhani. Akatoka huku akiongozwa na bendera mbili;
moja ikichukuliwa na Sayyidna Aliy Ibn Abiy Twaalib na nyingine ikibebwa na Answaari. Walipokaribia kufika Badri ikawajia khabari kwamba tayari Makurayshi wamekwishatoka kuja kuuhami msafara wao kwa gharama yo yote iwayo.
Wametoka wakiwa na chakula cha kutosha na zana kamili za vita. Ni vema ikakumbukwa kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hakutoka kwa ajili ya vita, kwa hiyo hakuwa amejiandaa kivita.
Waislamu wakashitushwa sana na khabari hii, lakini imani yao isiyotetereka ikawafanya wathibiti na kusimama imara kukabiliana na lo lote litakalojitokeza.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawakusanya watu wazima miongoni mwa maswahaba wake.
Akawataka ushauri wa nini kifanyike ili kukabiliana na hatari inayowajongelea. Akawaelezea khabari iliyomfikia kuhusiana na Makurayshi na maandalizi yao kabambe katika kupigana na waislamu.
Bwana Mtume alipomaliza kuwasilisha ripoti ya hali ya mambo ilivyo, ndipo aliposimama Sayyidna Abuu Bakri-Allah amuwiye radhi-kuelezea msimamo wake kuelekea hali hiyo. Akazungumza maneno mazuri, akidhihirisha nguvu na ushujaa wake.
Akabainisha kwamba yeye yu thabiti mithili ya jabali kubwa. Alipomaliza kuelezea msimamo wake huo na kuketi chini, ndipo ikawa sasa ni zamu ya Sayyidna Umar Ibn Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi.
Naye kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake akazungumza maneno mazuri. Maneno yenye kumathilisha ushujaa wa kweli na nia thabiti katika kupambana na adui kwa gharama yo yote iwayo.
Akaonyesha shauku yake ya kutaka kukutana na Mola wake kupitia njia ya kuipigania dini yake. Na pepo ambayo upana wake ni mithili ya mbingu na ardhi kuwa ndio jazaa yake. Sayyidna Umar akaketi chini ili kutoa fursa kwa Al-Miqdaad-Allah amuwiye radhi-kuelezea msimamo wake.
Akasimama na kusema neno lake lenye kusalikia na kukumbukwa daima:
“Ewe Mtume wa Allah! Tekeleza alilokuamrisha Allah, sisi tu pamoja nawe kwa lo lote. Wallaah, sisi hatukuambii wewe kama Bani Israaili walivyomwambia Musa: Basi nenda wewe na Mola wako mkapigane, sisi tutakaa hapa kungojea nini litakalokuwa. Lakini tunachosema sisi: Nenda wewe na Mola wako mkapigane, na sisi tutapigana pamoja nanyi. Tunamuapia yule aliyekutuma kwa haki, lau ungelitupeleka Barkil-Ghimaadi (sehemu iliyo mbali na Makkah), bila ya shaka tungelikufuata. Na wala asingelibakia nyuma ye yote miongoni mwetu mpaka tulituze jicho lako na tukikunjue kifua chako kwa furaha”.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamjazi dua njema kwa maneno yake hayo mazuri yaliyosheheni ukweli na nia ya dhati. Kisha akasema:
“Nipeni ushauri enyi watu, akiwalenga Answaari kwani wazungumzaji wote waliopita walikuwa wanawawakilisha Muhajirina.”
 Hapo ndipo aliposimama Sa’ad Ibn Muaadh na kusema:
“Wallah kama kwamba unatukusudia sisi ewe Mtume wa Allah! Mtume akajibu: Ndio. Sa’ad akaanza kusema: Hakika sisi tumekuamini, tumekusadiki na tumeshuhudia kwamba dini uliyokuja nayo ndio dini ya haki. Na tumekupa ahadi na dhamana ya utii juu ya dini hii, basi tekeleza ulitakalo ewe Mtume wa Allah, nasi tu pamoja nawe. Tunamuapia yule aliyekutuma kwa haki, lau ungelituonyesha bahari hii na ukaiingia, bila ya shaka tungeliingia pamoja nawe. Na wala asingelisalia nyuma hata mtu mmoja katika sisi na wala sisi hatuoni vibaya kukutana na adui yetu kesho. Hakika sisi ni wastahamilivu vitani, wakweli katika mapambano, huenda Allah akakuonyesha kwetu litakalolituza jicho lako, basi tupeleke kwa baraka za Allah.”
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akafurahishwa mno na kauli hii ya Sa’ad, kauli ilyowakilisha msimamo wa Answaari, kisha akasema:
“Enendeni na ikupateni bishara njema, kwani hakika Allah ameniahidi mojawapo ya mapote mawili. Wallah, kama kwamba mimi hivi sasa ninayaona maanguko ya watu wale”.
Kwa kauli hii ya Bwana Mtume, maswahaba wakatambua kwamba sasa ni vita tu hakuna njia ya kuviepuka. Jua lilipokuchwa Bwana Mtume akawatuma Sayyidna Aliy, Sa’ad Ibn Abiy Waqaaswi na Zubeir kupeleleza khabari za Makurayshi.
Njiani wakakwaana na waajiriwa wawili wa Makurayshi, wakawakamata na kuwaleta mbele ya Mtume. Mtume akaanza kuwasaili: Makurayshi wako kiasi gani? Wakajibu:
Hatujui, akazidi kuwasaili: Wanachinja ngamia wangapi kwa siku? Wakajibu: Siku moja ngamia tisa na siku nyingine ngamia kumi. Bwana Mtume akasema:
Idadi ya adui ni kati ya mia tisa na alfu moja, halafu akawauliza: Ni nani katika watukufu wa Makurayshi aliyemo msafarani? Wakamtajia majina kumi na tano, Mtume akawageukia maswahaba wake na kuwaambia:
“Haya Makkah ndio hiyo imekutupieni maini yake (wanawe vipenzi) na kuwatanguliza wanamume wake bila ya kubakisha kijana au ye yote mwenye kuweza kubeba silaha ila wamekuja naye!”
Idadi ya maswahaba wa Mtume ilikuwa ni mia tatu na kumi na tatu tu. Tukirejea kwa Abuu Sufyaan tunamkuta amefanikiwa kuwakwepa waislamu na kuuokoa msafara na kufika Makkah salama.
Alipofika Makkah akawaandikia barua watu wake akiwataka warejee, kwani hakuna tena sababu ya kupigana. Akawaambia katika ujumbe wake huo:Enyi jamaa zangu!
Bila ya shaka nyinyi mlitoka kwa ajili ya kuuhami msafara wenu, na tayari Allah amekwishauokoa basi rejeeni.
Na fikra hii ya kurudi ikawa ndio fikra ya wengi miongoni mwa washirikina wale. Abuu Sufyaan pamoja na ushirikina wake, bado alikuwa ni mtu mwenye busara na uoni wa mbali.
Lakini hali haikuwa hivyo kwa Abuu Jahli, kwani yeye aliipinga kwa nguvu zote fikra hiyo, akasema: Wallah, kamwe hatutarudi nyuma mpaka tukae Badri siku tatu, tukichinja ngamia, tukilisha chakula na kunywa pombe.
Waarabu watusike na kutujua sisi ni nani na waendelee kutuogopa. Wallah hapana, haturudi mpaka Allah ahukumu baina yetu na Muhammad. Huyu Abuu Jahli alikuwa ni mtu mjinga, mpenda fakhri asiyeangalia natija ya mambo kabla ya kuyaingia.
 
MPAMBANO WAANZA.
Majeshi mawili haya yalipokutana, wa mwanzo kutimua mbio alikuwa ni Ibilisi ambaye alitoa mchango mkubwa katika kuchochea vita hivi.
Yeye alirudi kisengerenyuma mpaka safu ya mwisho kabisa, akijitenga kabisa na mushirikina aliowatia hamasa na kuwapandisha mori wa vita,huku akiahidi kuwa pamoja nao mpaka mwisho wa kadhia hii.
Akijitetea kwa kujitenga huku kwa kusema kuwa yeye anayaona wasioyaona wenziwe (Makurayshi). Huu ndio msimamo wa Ibilisi katika mambo yote, hulipamba na kuliremba jambo kisha akawapendezeshea watu hata wakaliingia kichwa kichwa.
Wakishaliingia ndio huwatupa mkono, huyoo akenda zake na kuwacheka kwa upumbavu wao wa kuyaingia mambo bila ya kutafakari.
Kamanda Mkuu wa waislamu; Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwaamuru maswahaba wake wasishambulie ila kwa amri yake. Akapanga safu na namna ya kuelekeza mashambulizi, kisha akarejea hemani kwake akiwa pamoja na Abuu Bakri. Mtume akawa anamuomba humo Mola wake ampe nusra na ushindi, akisema:
“Ewe Mola wangu wa haki wee! Ukikiacha kipote hiki cha waumini kuangamia leo, hutoabudiwa kamwe. Ewe mwenye uhai wa maisha, msimamia kila jambo tunaomba msaada kwa rehema zako”.
Yakawa mafungamano ya Mtume na kumtegemea kwake Mola wake ni kwa kiwango cha juu sana kuliko wakati mwingine wo wote.
Baada ya kuomba sana, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alirejea tena kwa maswahaba wake na kuwakhutubia. Katika khutuba yake hiyo aliwahimiza kupigana kwa nia safi (Ikhlaaswi), akawaamrisha kusubiri na kuwa na ujasiri mbele ya adui. Na akawabashiria ushindi na nusra ya Allah, akasema:
“Namuapia yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, leo mtu hatapigana nao akauawa hali ya kuwa ni mwenye kusubiri na kutarajia jazaa ya Allah. Akisonga mbele bila ya kurudi nyuma, ila Allah atamuingiza peponi”.
Bwana Mtume akawaraghibisha na kuwatia shauku ya pepo maswahaba wake. Hili likamjaza mori wa vita Umeir Ibn Al-Humaam, akasema huku akiwa na tende mkononi akizila: Shabaash, hivi kumbe hapana kizuizi kati yangu na pepo ila ni kuuliwa na watu hawa!
Akazitupilia mbali tende alizokuwa nazo mkononi, akachukua upanga wake na kujitoma katikati ya maadui. Akazivuna shingo kadhaa za adui kwa ushujaa na nguvu ya ajabu. Kisha naye akauawa-Allah amuwiye radhi yeye na wenzake wote na kila aipiganiaye dini hii mpaka siku ya Kiyama.
Kisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akachota mchanga kwa kiganja chake, akawaelekezea Makurayshi na kusema: “Nyuso zimejaa ubaya”. Halafu akawapulizia na kuwaamrisha maswahaba wake kuanza mashambulizi kama mtu mmoja. Wakawaendesha mbio makafiri wale, Allah akautambua ukweli wa waumini na kuiona ikhlaaswi yao.
Hapo ndipo ukawajia msaada kutoka mbinguni, likashuka jeshi la malaika chini ya uongozi wa Jibrili. Hapo ukawa unasikika mgongo na mchakacho wa silaha tu bila ya kuonekana wapiganaji. Mtu haoni ila kupukutika kwa vichwa tu bila ya kumuona mpigaji.
Waislamu hawakuupata msaada huu ila ni kutokana na ukweli wao na imani yao thabiti.
Ndipo Allah naye akawatekelezea ahadi yake ya kuwanusuru. Kutokana na ukweli kwamba nguvu ya mbinguni (ya Muumba) haiwezi kupambanishwa na nguvu ya ardhini (ya viumbe), ushindi ukawa ni wa waislamu.
 
VITA VYAMALIZIKA.
Vita vikamalizika baada ya kuuawa viongozi na mamwinyi wa kikurayshi, hapo wakakimbia waliokimbia na wengine wakakamatwa mateka. Mwisho mwema ukawa ni wa wacha-Mungu, nusra na ushindi ukawa ni wa waumini. Na makafiri fungu lao likawa ni fedheha na kushindwa, Allah Taala anasema:
“(Kumbukeni) MOLA WAKO ALIPOWAFUNULIA MALAIKA (akawaambia): HAKIKA MIMI NI PAMOJA NANYI, BASI WATIENI NGUVU WALE WALIOAMINI, NITATIA WOGA KATIKA NYOYO ZA MAKAFIRI. BASI WAPIGENI JUU YA SHINGO (zao) NA KATENI KILA NCHA ZA VIDOLE VYAO. HAYO NI KWA SABABU WAMEMUASI ALLAH NA MTUME WAKE. NA MWENYE KUMUASI ALLAH NA MTUME WAKE (atamuadhibisha) KWANI ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU”. [8:12-13]
 
NENO KHITAMI: DARSA NA MAZINGATIO.
Tukiwa tunaishi na tukio hili kongwe la vita vya Badri, inatupasa kuinamisha vichwa vyetu ili kuonyesha heshima zetu kwa kikundi hiki kidogo cha waumini. Maswahaba wa Mtume Mtukufu ambao wamezisadikisha kiamalia ahadi walizozichukua mbele ya Allah Mola Muumba wao.
Kipi tuwezacho kukisema kwa watu waliotoka majumbani mwao wakiamini kuwa wanakwenda matembezini tu kusikokuwa na taabu wala matata yo yote.
Hakuna vita wala mapambano, tahamaki wako ana kwa ana na kundi kubwa linalotisha, lenye uchu wa kuangamiza. Lakini pamoja na yote hayo hawakubabaika wala kutetereka kama ambavyo ingeweza kutokea kwetu.
Katika hali hiyo ngumu na kitatange hicho kisichotazamiwa, wote kwa pamoja wanamzunguka Bwana Mtume na kuonyesha utayarifu wao katika kukabiliana na hali hiyo. Wakaonyesha kupevuka kwao kiimani na kiwango cha juu cha subira wawamo katika hali ya vita.
Wakawa tayari kupambana na adui kwa gharama yo yote iwayo na kwa hali yo yote ile. Mbele yao kulikuwa na ama ushindi (nusra) au kaburi, lakini hakuna kitu kusalimu amri mbele ya adui wa Allah na Mtume wake.
Tunaweza kusema nini juu ya watu ambao katika usiku wa kuamkia mpambano wa makundi mawili yale.
Pamoja na kuitambua nguvu kubwa ya adui yao na maandalizi kabambe ya vita, bado walilala usingizi mwanana usio na mang’amung’amu.
Usingizi wao huu katika kipindi hiki cha hatari, kama unaashiria jambo basi ni kuonyesha namna gani walivyopevuka kiimani. Hili ndilo analoliashiria Allah kwa kauli yake:
“(Kumbukeni) ALIPOKULETEENI USINGIZI ULIOKUWA (alama ya) SALAMA ITOKAYO KWAKE…” [8:11]
Naam, walilala usingizi wa amani uliowaondolea kila aina ya khofu. Wote walilala na ilhali vita vi tayari mbele ya macho yao, na adui akingojea kwa uchu mkuu fursa ya kuwasagasaga. Wote walilala kama anavyolala mtu nyumbani kwake.
Wote walilala ila mtu mmoja tu, huyo hakufunika jicho lake na wala hakuuweka ubavu wake chini. Huyu alikesha katika usiku ule wa usingizi wa amani na salama. Alikesha kama mlinzi wao, akiwaombea nusra ya Allah na kuswali kwa ajili yao.
Huyu hakuwa mwingine bali ni Mtume wa Allah, akionyesha namna gani anavyowajali watu wake na jinsi kiongozi atakiwavyo kuwa kwa watu wake. Huyu ndiye Mtume ambaye Allah anatuambia juu yake:
“AMEKUFIKIENI MTUME ALIYE JINSI MOJA NA NYINYI, YANAMUHUZUNISHA YANAYOKUTAABISHENI, ANAKUHANGAIKIENI. (Na) KWA WALIOAMINI NI MPOLE NA MWENYE HURUMA”. [9:128]
Imepokelewa kutoka kwa Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-amesema:
“Tulijikuta siku ya Badri hakuna ye yote miongoni mwetu ila alilala isipokuwa Mtume wa Allah pekee. Yeye alisimama chini ya mti akiswali na kulia mpaka kulipopambazuka”.
Je, umepata kumuona au hata kumsikia tu kamanda mithili ya kamanda huyu mtukufu? Au umewahi kumshuhudia kiongozi kama huyu; Mtume aliye Mtumishi wa watu?!
Tunaweza kusema nini kwa watu ambao waliyaonea tamu mauti na dunia ikawa si kitu mbele yao pale waliposikia wito wa Mtume: “Iinukieni pepo ambayo upana wake ni sawa na upana wa mbingu na ardhi”.
Hapo kila mmoja wao akatambua kuwa hapana kinachomzuia kuingia peponi ila ni kupigana na adui mpaka auawe.
Hapo ndipo akajitoma katikati ya kundi la maadui mithili ya mshale, akifyeka vichwa kwa nguvu zake zote kuliani na kushotoni.
Mpaka anapozidiwa na kuanguka chini maiti, akiwa tayari amekwisha jihakikishia nishani ya ushahidi. Kwa hali hii, nusra ikawa jirani mno na wao mithili ya nyama na mfupa na msaada wa Allah ukawa pamoja nao.
Kwa kitendo chao hiki wakawa wametoa na kuacha darsa lenye mazingatio makubwa kwa vizazi vijavyo baada yao.
Darsa ambazo historia ya Uislamu haikamiliki bila ya kutajwa na sio kutajwa tu bali kutumika katika kuyapatia ufumbuzi na tiba sahihi matatizo yanayowazunguka waislamu leo ulimwenguni kote. Wakati tukiwa ndani ya kumbukizi za tukio hili kongwe lililosheheni suluhisho la magumu yanayowafika waislamu leo, bado
·         Uislamu ni mgeni katika ardhi za kiislamu.
·         Waislamu hawajui utukufu na thamani ya Uislamu wao.
·         Sheria na adabu za kiislamu hazijatawala ulimwengu hata katika ardhi za kiislamu.
·         Maeneo matakatifu ya waislamu yako chini ya mikono najisi ya Mayahudi waliowauwa mitume wa Allah pasi na haki.
·         Hakuna umoja wala mshikamano na udugu wa kiislamu baina ya waislamu.
·         Waislamu pamoja na wingi wao na utajiri wao, ndio jamii nyonge na dhalili duniani kote.
·         Waislamu wanamkumbatia na kumfanya kafiri kuwa ndiye mwandani wao kinyume cha waumini wenzao!
·         Waislamu wanapigana wao kwa wao kwa sababu ya fitina wanazopandikiziwa na adui.
·         Waislamu wanategemea nguvu za mashariki au magharibi kuwalinda. Wamesahau kwamba nusra haiwi na wala haitoki ila kwa Allah tu pekee.
Ndugu waislamu po pote pale mlipo katika ardhi hii ya Allah, tukiwa katika kumbukumbu ya vita hivi vya Badri ni wajibu wetu:-
Kuamini kuwa jihadi ni FARDHI YA LAZIMA. Ni ibada iliyofaradhishwa juu yetu kama ilivyofaradhishwa swaumu. Kama alivyosema Allah:
“ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA (mmefaradhishiwa) KUFUNGA (swaumu)…” [2:183] Akasema katika sura hiyo hiyo:
“MMELAZIMISHWA KUPIGANA VITA (kwa ajili ya dini)…” [2:216] Na tuamini kuwa jihadi haikomelei tu kwa maswahaba wa Mtume, bali inaendelea muda wa kusalikia Uislamu katika ardhi hii. Kwani imekuja katika hadithi tukufu: “Piganeni jihadi na mushirikina kwa mali zenu, nafsi zenu na ndimi zenu”.
Katika kipindi hiki kigumu ambacho tumezungukwa na adui kila upande kiasi cha kutokuwa na kimbilio. Ni wajibu wetu tujiunganishe na Allah Mola Mshindi asiyeshindika.
Na tukumbuke kuwa Uislamu ni imani/itikadi na mfumo mzima wa maisha kabla ya kuwa kwake ni nguvu na silaha iliyo mikononi mwetu tayari kumzima adui ye yote.
Nyoyo zetu zitakapotwaharika na ghururi za shetani na dunia na imani yetu ikaimarika kwa kutenda mambo ya twaa.
Hapo tutakuwa tumekwisha jihakikishia sababu za ushindi na nusra dhidi ya kila adui yetu. Na hapo ndipo Allah atakapotutimizia ahadi yake kongwe:
“…NA NI WAJIBU JUU YETU KUWANUSURU WALIOAMINI…” [30:47]
Mtumishi wa Umma {WEBSITE UISLAMU} inawatakia waislamu wote ulimwenguni kote kumbukizi njema na tafakari za kina zenye suluhisho za magumu yao za vita vya Badri.
 Allah awaridhie mashahidi wa Badri na wote walioupigania, wanaoupigania na watakaoupigania Uislamu mpaka siku ya Kiyama. Ewe Mola wa haki! Unusuru Uislamu na waislamu po pote pale walipo katika mashariki na magharibi ya ardhi yako, Aaamiiyn!
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *