“LAILATUL-QADRI NI BORA KULIKO MIEZI ELFU MOJA”

Sifa na Shukurani zote njema ni zake Mola Muumba wetu ambaye Yeye ndiye aliyesema: “Hakika Sisi tumeiteremsha Qur’ani katika Lailatul-Qadri, usiku wa cheo kitukufu. Ni nini kitacho kujulisha Lailatul-Qadri? Lailatul-Qadri ni bora kuliko miezi elfu”. Ewe Mola wa haki! Mrehemu, mpe Amani na mbariki mwanaadamu kamili; Bwana wetu Muhammad pamoja na Aali zake, Maswahaba wake na wote walio muamini na kumfuata.

Ama baadu,

Wapendwa ndugu zetu katika Imani.

Assalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

Sote wana jukwaa, tunapaswa kufahamu na kukiri kwamba si kwa hila, nguvu, ujanja, akili wala uwezo wetu sisi kama wanaadamu, bali ni kwa kuwezeshwa tu na Allah Mola Muumba wetu, ndio tumo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Na hali kadhalika ni kwa uwezeshi wake tu tunaendelea na swaumu na ilhali ni wenzetu wengi tu ambao tulianza nao Ramadhani tayari wamo makaburini, tumewazika. Tukuone huku kuwemo kwetu ndani ya Ramadhani mpaka sasa ni fursa ya upendeleo tunayo pewa na Allah ili tupate kuyarekebisha na kuyaboresha mahusiano yetu naye. Na pia ni Yeye tu ndiye anaye tuwezesha kujumuika pamoja katika jukwaa letu hili la Ramadhani ili tupate kukumbushana yale yanayo husiana na mwezi huu mtukufu, huenda kwa kuyajua hayo tukaweza kuuthamini na kuuenzi mwezi huu. Kwani ni kwa kufanya hivyo tu, ndio tunaweza kuipatiliza fursa hii adhimu ambayo inaweza kuwa ndio sababu ya kutuvusha salama leo hapa duniani na hata kesho kule mbele ya Mola wetu.

Naam, zimebakia siku chache tu ili tuweze kuishi na kuwemo ndani ya yale masiku kumi ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani; masiku ambayo inatarajiwa kuwemo ndani yake Lailatul-Qadri. “Izengeeni Lailatul-Qadri katika kumi la mwisho la Ramadhani”. Bukhaariy [04/259] & Muslim [02/823]-Allah awarehemu. Huenda kibinaadamu tumezembea kuitumia vema fursa ya siku zilizo pita katika kutenda ibada ili kujikurubisha kwa Mola wetu. Ni vema sasa tukakumbushana kuhusiana na masiku haya yaliyo mlangoni, tuuone umuhimu wake kwetu ili tupate kuyapatiliza kwa kutenda anuwai za kheri ndani yake, asaa tukanadi saada. Hayo ndio yale masiku ambayo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia: “Atakaye simama katika Lailatul-Qadri kwa Imani na kwa kutaraji kupata ujira (kwa Allah), huyo atasamehewa madhambi aliyo kwisha yatenda”.

Kuhusiana na masiku hayo, Allah Ataadhamiaye anatuambia: “Hakika Sisi tumeiteremsha Qur’ani katika Lailatul-Qadri, usiku wa cheo kitukufu. Ni nini kitacho kujulisha Lailatul-Qadri? Lailatul-Qadri ni bora kuliko miezi elfu. Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo. Amani usiku huo mpaka mapambazuko ya alfajiri”. Al-Qadri [97]:01-05

Ndugu mfungaji-Allah akurehemu-sura hii ambayo aya zake tumezinukuu punde tu na wewe tayari umesha zisoma, sura hiyo inayo itwa kwa jina la usiku huo mtukufufu “Suratul-Qadri”, inatuwekea wazi ya kwamba Lailatul-Qadri – usiku wa cheo ndio bora ya siku zote za mwaka mzima. Ubora huo unatokana na kule kushushwa kwa Qur’ani ndani yake kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na kwa sababu huo ni usiku ulio barikiwa ambamo ndani yake hubainishwa kila jambo la hikima na kupitishwa, hayo ni kwa mujibu wa kauli yake Allah Ataadhamiaye: “Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa…”. Ad-Dukhaan [44]:03

Huo ni usiku wa heshima/cheo/utukufu na mipango (ukadiriaji wa mambo). Ibnu Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: “Qur’ani iliteremka katika mwezi wa Ramadhani ndani ya usiku wa cheo (Lailatul-Qadri), ndani ya usiku ulio barikiwa, kwa mkupuo mmoja kutoka kwa Allah Ataadhamiaye”.

Naam, sasa tuanze kuangalia kwa nini usiku huo ulio bora kuliko miezi elfu moja umeitwa kwa jina hilo “Lailatul-Qadri”. Usiku huo umeitwa kwa jina hilo, mosi ni kwa sababu humo Allah Mtukufu hukadiria mambo yake ayatakayo mpaka siku kama hiyo ya mwaka unao fuatia; hupanga suala la mauti kwa waja wake, umri wao wa kuishi kwa wale watakao zaliwa, riziki zao na mengineyo. Kusema hivyo ni kumaanisha ya kwamba Allah Mtukufu huyadhihirisha siku hiyo kwa Malaika wake yale mambo aliyo yakadiria tangu azali; kabla hata ya kuumbwa kwa hao wakadiriwa, kwa kuwa Yeye huyakadiria mambo mwanzoni mwake. Imepokewa kutoka kwa Ibnu Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: “Huandikwa kutoka kwenye kitabu mama yatakayo tokea katika mwaka (huo); (yaani masuala ya) riziki, mvua, uhai na mauti”.

Na pia pamesemwa, usiku huo umeitwa kwa jina hilo kwa sababu ya utukufu, cheo na heshima yake na kwa sababu matendo mema yanayo tendwa humo yana daraja kubwa na thawabu nyingi mno. Na kwa sababu mtu ambaye hakuwa na cheo/daraja wala heshima mbele za Mola wake, akiuhuisha usiku huo kwa kufanya ibada, hupata heshima, hupanda daraja na hupata utukufu mbele za Allah, kwa usiku huo mmoja tu. Hali kadhalika umeitwa kwa jina hilo, kwa sababu ya kushuka ndani yake Kitabu Kitukufu, kwa Mtume Mtukufu kwa ajili ya umma mtukufu.

Ndugu mfungaji-Allah akurehemu-kwa mukhtasari hizo ndizo sababu za usiku huo tunao utazamia ndani ya siku chache zijazo, kuitwa kwa jina la “Lailatul-Qadri”, haya sasa na tuuangalie ubora wake. Usiku huo umepata sharafu na ubora kwa sababu ya kushuka ndani yake Kitabu Kitukufu kuliko vitabu vyote vya mbinguni. Na kwa sababu kufanya ibada ndani ya usiku huo mmoja, (ujira wake) ni bora zaidi kuliko ujira wa ibada inayo fanywa ndani ya miezi elfu moja ambayo haimo ndani yake Lailatul-Qadri. Hali kadhalika ubora wake umesababishwa na kushuka kwa Malaika wengi mno ndani yake kutoka kila mbingu, kutoka Sidratul-Muntahaa (penye Mkunazi wa mwisho) na kwenye maskani ya Malaika Jibrilu. Wanateremka kutoka huko kuja ardhini, wanakuja kuitikia dua zinazo ombwa na Waumini mpaka kuchomoza kwa alfajiri. Na pia ubora wake umepatikana kwa kuwa huo ni usiku wa amani na salama, kwa hiyo usiku huo wote ni kheri tupu hakuna shari ndani yake. Amesema Imamu Dhwahaak-Allah amuwiye radhi: “Allah hakadirii/hapangi ndani ya usiku huo ila salama/amani tu. Na katika masiku mengine huhukumu na kupitisha humo balaa na salama”. Na usiku huo ni salama; shetani hawezi kufanya humo uovu/ubaya wala maudhi/kero nao ndio usiku ambao Malaika huwatolea salamu waumini waliomo misikitini wakimuabudu na kumuomba Mola Muumba wao. Na humpitia kila muumini popote pale alipo na humuamkua kwa kumwambia: Assalaamu Alayka ayuhal-muumin – Amani ya Allah ikushukie ewe muumini! Kwa mambo hayo basi, huo unakuwa ni usiku bora kuliko miezi elfu moja kama alivyo sema Allah Mtukufu katika aya tuliyo inukuu mwanzoni mwa jukwaa letu.

Kwa ubora huo tulio utaja kwa kumnukuu Allah Mwenye Lailatul-Qadri yake, Waislamu tuna haja mno ya kuushughulikia, kuuzengea na kuupania usiku huo kwa kufanya anuwai za ibada kwa upeo wa jitihada zetu. Tufanye hivyo kwa kumfuata na kumuiga yule mwanaadamu bora-Rehema na Amani zimshukie-hebu tumsikilize mama yetu; Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-akitueleza namna alivyo kuwa Mtume wa Allah katika kumi la mwisho: “Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akijitahidi kufanya ibada katika kumi la mwisho kiasi ambacho hakujitahidi nje ya Ramadhani”.

Na akasema tena: “Mtume wa Allah alikuwa linapo ingia kumi la mwisho, huhuisha usiku na akawaamsha wake zake na akafunga kibwebwe (akapania kufanya ibada”.

Na tunapaswa kuvikimbilia vipawa vyake huku tukitia akilini mwetu ya kwamba ibada ya usiku huo mmoja ni bora kuliko miezi elfu moja ambayo mtu atasimama kuswali usiku, atafunga, atapigana jihadi kwa mali na nafsi yake, na … na … Imepokewa ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwataja watu wanne katika wana wa Israili ambao walimuabudu Allah kwa miaka themanini, (katika kipindi chote hicho) hawakumuasi Allah hata kwa (kitambo cha) upepeso wa jicho. Maswahaba wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakastaajabishwa sana na hilo (kwamba kuna wanaadamu wanaweza kufanya ibada kwa muda wote huo bila ya kuasi!). (Malaika) Jibrilu akamjia Mtume, akamwambia: Ewe Muhammad! Umati wako wamestaajabishwa na ibada ya watu wale. Hakika Allah amekuteremshia kilicho bora kuliko ibada yao hiyo (ya miaka themanini bila ya kuasi), kisha akasoma: “Hakika Sisi tumeiteremsha Qur’ani katika Lailatul-Qadri, usiku wa cheo kitukufu”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafurahishwa na hilo.

Ndugu mfungaji-Allah akurehemu-hiyo ndio Lailatul-Qadri na huo ndio ubora wake. Na tambua kwamba kuipata Lailatul-Qadri ni jambo sahali na jepesi ambalo halina taabu wala shida, suala ni wewe kwanza kuwa na Ikhlasi; ukajipinda katika usiku huo kwa ajili tu kutafuta radhi za Mola wako, ukafanya ibada ya ajili yake Yeye tu. Kisha ukajitahidi kadiri ya uweza wako katika kufanya anuwai za ibada ndani ya usiku huo kwa kuzengea kupata thawabu za mwezi wa Ramadhani na kuipata Lailatul-Qadri. Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-alimuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: Unaonaje, lau itanisadifu nikaipata Lailatul-Qadri, niseme (niombe) nini? (Mtume) akamwambia: Sema: “Allaahumma innaka ‘afuwun Kariimu tuhibbul-‘afwa fa’afu ‘anniy – Ewe Mola wa haki! Hakika Wewe ni Msamehevu, Mkarimu unaye penda kusamehe, basi nakuomba unisamehe”.

Mwisho kabla ya kulikunja jamvi la jukwaa letu la leo, tukiwa tumelimaliza kumi la mwanzo na sasa tumo ukingoni mwa kumi la pili tuambizane na tunasihiane. Hapana yeyote mwenye udhuru wa kukosa kufaidika na Ramadhani, kama mtu hakunufaika na Ramadhani kupitia mlango wa swala za usiku, basi bado ana nafasi ya kufaidika kupitia mlango wa sadaka. Hakuweza kuamka usiku wala kutoa sadaka, basi asiache kufaidika kupitia mlango wa kusoma Qur-ani, kama hakuliweza hilo basi na apitie mlango wa dhikri. Na kama hakuyaweza yote hayo, basi na anufaike na Ramadhani kwa kupitia mlango wa kuuzuia ulimi wake na viungo vyake kutenda yale yanayo weza kuuchafua na kuupaka matope mwezi huu mtukufu. Atakaye ipoteza fursa hii adhimu yenye thawabu kedekede, kwa kushindwa kuitumia vema katika kutekeleza ibada mbali mbali, huyo ameupoteza mwenyewe umri wake na hapungui kuwa ameikanusha neema ya Mola Muumba wake aliyo mtunukia pasina kumpelekea maombi. Na huyo ndiye mtu aliye kula hasara kubwa kuliko zote: “…basi huyo amekhasiri khasara ya dhaahiri”. Na “…hiyo ndio khasara iliyo wazi”.

Yatutie nishati na ari ya kujitahidi kutenda kheri tunayo iweza katika mwezi huu hususan katika siku hizi chache zilizo bakia, maneno yake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-pale alipo sema: “Hakika peponi kuna vyumba ambavyo huonekanwa nje yake kutokea ndani yake na huonekanwa ndani yake kutokea nje yake. (Maswahaba) wakauliza: Ni vya nani vyumba hivyo, ewe Mtume wa Allah? Akajibu: (Hivyo ni vya) yule aliye na maneno mazuri na akalisha chakula na akadumu na funga na akaswali usiku ilhali watu wamelala”.

Ewe ndugu muislamu, uliye teuliwa na Mola wako miongoni mwa waja wake wengi kuipata neema hii ya kujiwa na mwezi mtukufu wa Ramadhani, kabisa usikubali kuichezea fursa hii hata ikaondoka nawe ukiwa hujafaidika nayo, hilo halitapungua kuwa ni utovu wa shukrani kwa Mola wako Mkarimu na pia ni kujidhulumu wewe mwenyewe. Kumbuka mwezi huu ni mgodi ulio sheheni hazina koche koche, ingia mgodini humo uchimbe madini uyatakayo kwa kiasi cha nguvu yako huku ukikumbuka kwamba Ramadhani hii ndio yako, ya mwakani ni ya Allah kwani wewe kuipata ni kwa majaaliwa yake Yeye.

Panapo majaaliwa yake Allah tukutane juma lijalo, hapa hapa katika jukwaa letu la Ramadhani ya mwaka 1442H/2021

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *