Ulipo wadia mwaka wa thelathini na nane, Muawiyah akamtuma Amrou bin Al-Aaswi kukiongoza kikosi cha askari elfu sita, kwenda Misri. Amrou akaenda mpaka akapiga kambi katika nyanda za chini za Misri. Hapo akajiwa na wale walio mkhalifu Muhammad bin Abubakri na wakataka kisasi cha damu ya Sayyidna Uthmaan, akajumuika nao. Ndipo akaamua kumuandikia waraka huu gavana Muhammad:
(Ama baad, ewe mwana wa Abubakri! Iweke mbali nami damu yako, kwani mimi sipendi upatwe na ushindi wangu. Hakika watu katika nchi hii wamekongamana dhidi yako na wao ni Waislamu (watu wa amani). Basi toka humo, hakika mimi ni katika wanasihi wako).
Baada ya kufikiwa na waraka huo wa Muawiyah, gavana Muhammad haraka akamuandikia waraka Amirul-Muuminina; Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-kumfahamisha khabari hiyo na kumuomba nguvu ya ziada itakayo msaidia kupambana na Muawiyah. Sayyidna Aliy akaujibu waraka ule wa gavana wake mteule, akamuagiza akikusanye pamoja kikundi chake na akamuamrisha kuwa na subira na akamuahidi kumuongezea nguvu ya jeshi. Hapo akasimama Muhammad katika kadamnasi ya watu wake, akawahamasisha na kuwatolea wito wa kwenda vitani pamoja naye. Wakauitika wito wake watu elfu mbili, akamtawaza uamiri wao Kinaana bin Bishri, gavana akawatanguliza wao mbele. Na yeye akaliongoza kundi la askari wengine elfu mbili kwenda kupambana na Amrou. Amiri jeshi Kinaana alipo vaana na majeshi ya Shamu yakiwa yanashirikiana na Muawiyah bin Khudeiji; mwananchi wa Misri. Katika mpambano huo, wazalendo wa Misri walio watiifu kwa Imamu Aliy, waliendeshwa mbio na akauawa amiri wao Kinaana. Wapiganaji wengine walio kuwa pamoja na gavana Muhammad, walipo sikia kupigwa na kusambaratishwa kwa wenzao, wakamtupa mkono na kumuacha peke yake. Hali hiyo ikamlazimisha gavana Muhammad kujificha ili kuyanusuru maisha yake. Ama tukirudi kwa kamanda Amrou, yeye aliendelea kusonga mbele mpaka akapiga kambi katika kitongoji cha Al-Fustwaatw. Muawiyah bin Khudeij akatoka kumsaka gavana Muhammad bin Abubakri mpaka akampata mafichoni mwake, akamuua.
Khabari za kuuawa kwa gavana Muhammad zilipo mfikia mama wa waumini; Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-alipatwa na huzuni kuu juu yake na akawakumbatia watoto wake na kuwa karibu nao. Kufuatia mauaji haya haramu ya Muhammad bin Abubakri, jimbo la Misri likaangukia mikononi mwa Muawiyah na likawa chini ya utii na amri yake na kwa hivyo wananchi wa Misri wakalazimika kula kiapo cha utiifu kwake kama Amirul-Muuminina.
Ama ile nguvu ambayo iliyo pelekwa na Sayyidna Aliy kwenda kumsaidia gavana Muhammad bin Abubakri, hawa iliwafikia khabari ya kuuawa kwake wakiwa njiani kuelekea Misri. Wakavunjika moyo na wakaamua kurejea kwa Amirul-Muuminina ili kupewa maelekezo ya nini cha kufanya baada ya mauaji hayo. [TAARIKHUT-TWABARIY 02/131]
Baada ya Muawiyah kulitwaa jimbo la Misri na kuliweka chini ya mamlaka yake, akamtuma Abdullah bin Al-Hadhramiy kwenda Basra. Na wakati huo Basra ilikuwa chini ya liwali Ziyaad bin Abu Sufyaan; khalifa (mrithi) wa Ibn Abbas. Kundi kubwa la Baniy Tamim likakusanyika kwa Ibn Al-Hadhramiy, ikumbukwe kwamba hawa ndio wale walio kuwa wakitaka kisasi cha damu ya Sayyidna Uthmaan, akawaomba msaada ili kulipa kisasi hicho kwa wauaji. Dhwahaak bin Qaisi akamuinukia naye alikuwa katika askari wa Ibn Abbas, akasema: Allah ayavunjilie mbali uliyo tujia na unayo tuitia kwayo. Sisi hivi sasa tumesha kongamana kula kiapo cha utii kwa Imamu Aliy, naye amekwisha zifuta kunguwao na amesha msamehe mkosefu. Hivi wewe unatuamuru tuzitoe alani panga zetu, tupigane wenyewe kwa wenyewe ili tu Muawiyah apate kuwa Amirul-Muuminina! Hapo akainuka Abdullah bin Haazim As-salamiy akamrudi Dhwahaak, akasema: Funga domo lako! Wewe hustahiki kuzungumza hapa. Kisha akamgeukia mjumbe wa Muawiya; Abdullah bin Al-Hadhramiy akamwambia: Sisi ni wanusuru na waunga mkono wako na utakalo sema ndilo litakalo fuatwa.
Liwali Ziyaad alipo iona hali hiyo ya ubishani na upinzani dhidi yake, akaomba himaya na hifadhi kwa kabila la Azdi, nao wakamkubalia maombi yake hayo. Wakampa hifadhi na himaya yao, yeye na Bait mali yake. Ziyaad akapeleka taarifa ya kuchafuka kwa hali ya hewa kwa kiongozi mkuu; Sayyidna Aliy. Kufuatia hali hiyo basi, Imamu Aliy akamtuma kwake A’ayun bin Dhwubailah Al-Mujaashi’iy wa kabila la Tamim, ili alifarakanishe na kulisambaratisha kundi la Tamim na lile la Ibn Al-Hadhramiy. Lakini kabla mjumbe huyu wa Imamu hajafanikiwa kulitekeleza jukumu alilo pewa, akauawa kwa kuviziwa kihila. Habari ya kuuawa kwa mjumbe huyu ilipo mfikia Sayyidna Aliy, akamtuma mjumbe mwingine; Jaariyah bin Qudaamah wa kabila la Baniy Sa’ad. Bwana huyu huyoo akatoka, akaenda Basra. Alipo fika huko, akawahutubia watu wa kabila la Azdi na akawahukumia kheri kutoka kwa Amirul-Muuminina. Na akawasomea wazalendo wa Basra waraka wa Imamu Aliy, ambao ndani yale alikuwa akiwatisha na kuwakamia kwa vita vikali kuliko vile vya Jamal iwapo watamkhalifu. Wengi wa watu wa Basra wakamuitika, wakaacha kumuunga mkono Ibn Al-Hadhramiy; mjumbe wa Muawiyah. Kisha ndipo akamuendea Ibn Al-Hadhramiy, akapambana nae na watu wake mpaka akawasambaratisha, wakatimua mbio. Akamfukuza mpaka akamkamata na kumuua.
Baada ya hapo, Muawiya akawa akipeleka vikosi vita kwenye ile miji iliyo kuwa chini ya mamlaka ya Amirul-Muuminina, ili apate kuiingiza chini ya utii na utawala wake. Akampeleka Makka Yazid bin Shajarah, ili apate kuwaongoza watu wake kwenye ibada ya Hija na awalishe watu wa Makka kiapo cha utii kwake. Na wakati huo gavana wa Makka aliye teuliwa na Imamu Aliy, alikuwa ni Quthmu bin Abbas na hakuwa na nguvu ya kutosha kupambana na uchokozi wowote. Kwa minajili hiyo basi, akaona ni busara kutoingia mapambanoni na wachokozi wale ili kuepusha kumwagika bure damu ya Waislamu. Kufuatia hali hiyo ya kutokupata upinzani, Ibn Shajarah akajitwalia madaraka, akatangaza kuwapa amani watu wote ila tu yule atakaye thubutu kupambana na utawala wake. Na akamtumia ujumbe Abu Said Al-Khudriy akimuagiza kumuamrisha Quthmu kutowaongoza watu katika ibada ya swala na wala Ibn Shajarah mwenyewe pia asiswalishe. Na kwamba suala hilo liachwe mikononi mwa waumini, wao ndio wamchague Imamu wamtakaye kuwaswalisha, basi watu wakamchagua Shaibah bin Uthmaan. Yeye ndiye akawaswalisha na ibada ya Hija ya mwaka huo ikamalizika kwa salama na amani. Na wala haukupatikana upotofu katika eneo la Haram (eneo takatifu) kwa sababu ya kuyachelea makamio ya Allah Ataadhamiaye yaliyomo katika kauli yake: “… na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi tutamwonjesha adhabu kali”. [22:25]
Baada ya hapo sasa, vikawa vikosi vikizinga zinga kutoka pande zote mbili; upande wa Amirul-Muuminina na ule wa Muawiya. Na kila upande ukilenga kuwakusanya watu chini ya sauti moja na hilo halikuwa rahisi kwa upande wowote. Lakini watu wa majimbo ya Hijaazi na Yemen waliingia katika utii wa Muawiya pale alipo wapelekea balozi Busru bin Artwaa wa kabila la Baniy Aamiriy. Kufuatia ushawishi huo mkubwa wa Muawiya, halikubakia chini ya utii wa Amirul-Muuminina ila jimbo la Iraq na miji shirika ya Fursi. Na miji yote hiyo ilikuwa ikitokota kwa mizozo na kutofautiana, likawepo kundi la Imamu Aliy na wengine wakawa ni Khawaariji; hawamtaki Aliy wala Muawiya. Na likawepo kundi jingine la wanafiki; wanadhihirisha utii kwa Imamu Aliy na huku likificha uadui dhidi yake. Amirul-Muuminina akachoshwa na kukimwa kuwaongoza watu hao vigeugeu; wasio na msimamo na akawaeleza wazi hilo katika khutba zake nyingi. [AL-KAAMIL FIY TAARIKH 03/232]