RUKHUSA YA KUKUSURU

SWALA YA MSAFIRI HUWAJE?

Allah amempa msafiri rukhsa mbili kama ifuatavyo:-

RUKHSA YA KUKUSURU (SHORTENING):

Hii ni rukhsa inayohusisha upunguzaji wa idadi ya rakaa za swala ambapo msafiri huruhusiwa kuziswali swala za rakaa nne nne kama Adhuhuri, Alasiri na Ishaa rakaa mbilimbili badala ya nne za kawaida.

Rukhsa hii hujulikana kisheria kama “QASWRU.” Rukhsa hii ya kukusuru swala za rakaa nne inatokana na kauli ya Allah:

 “NA MNAPOSAFIRI KATIKA ARDHI, SI VIBAYA KWENU MKIFUPISHA SWALA (mkikusuru)…” (4:101)

Imepokelewa kutoka kwa Ya’alaa Ibn Umayyah–Allah amuwiye radhi–amesema: Nilimuambia Umar Ibn Al-Khatwaab– Allah amuwiye radhi (kwamba Allah anasema):

 “….SI VIBAYA KWENU MKIFUPISHA SWALA (mkikusuru) IWAPO MNAOGOPA YA KWMABA WALE WALIOKUFURU WATAKUTAABISHENI….”

 Watu tayari wamo katika amani (vita hakuna, kukusuru huku ni kwa nini?) Akaniambia:

Mimi nae nilistaajabu kama unavyostaajabu wewe (leo) nikamuuliza Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-juu ya suala hili, akanijibu:

“(Rukhsa) hii ni swadaka mliyopewa na Allah, basi ipokeeni swadaka yake hiyo.” Muslim & wingeneo.

Hadithi hii ndio inayofahamisha kuwa kukusuru swala hakukukhusishwa na khofu tu pekee, bali muislamu anayo rukhsa ya kukusuru swala kwa sababu ya safari.

 

SHARTI ZA KUSIHI KUKUSURU.

Rukhsa hii ya kukusuru swala aliyopewa msafiri imeambatana na sharti ambazo anatakiwa azitimize ili kukusuru kwake kusihi.

Sharti za kusihi kukusuru ni hizi zifuatazo kama zilivyobainishwa katika vitabu vya fiq-hi:-

Dhima na utekelezaji wa swala husika viwe ndani ya swala.

Hii maana yake ni kwamba swala anayotaka kuikusuru mtu iwe imemkuta tayari yumo safarini na aikusuru humo humo safarini. Kwa mantiki hii mtu haruhusiwi kukusuru swala iliyomuwajibikia kabla hajavaana na safari. Kisha akasafiri kabla hajaiswali, basi haimjuzii mtu huyu kuiswali swala hii kwa kuikusuru.

Hii ni kwa sababu wakati swala hii ilipomuwajibikia na kuwa katika dhima yake hakuwa msafiri bado, kwa hiyo swala hii haiwezi kupewa hukumu ya safari.

Kadhalika haihusiani na rukhsa hii ya kukusuru, swala ambayo uliingia wakati wake naye akiwa safarini lakini hakuiswali mpaka akarejea mjini kwake.

Basi haitamjuzia kuiswali swala hiyo kwa kukusuru, kwa sababu wakati wa kuitekeleza atakuwa si msafiri tena na kukusuru ni rukhsa aliyopewa msafiri.

Kuvuka ukuta wa mji anaotoka au maamirisho (majengo) yake ikiwa hauna ukuta.

Kisheria mtu ataanza kuhesabika kuwa ni msafiri baada ya kuuvuka ukuta wa mji wake anaosafiri kutokea humo.

 Au baada ya kuvuka maamirisho (majengo) ya mji huo iwapo haukuzungukwa na ukuta (ngome) kama ilivyokuwa miji mingi ya kale.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa safari inaanza kwa kuvuka ukuta/maamirisho ya mji anaotoka mtu Na hapo ndipo inapoanza kutumika ile rukhsa ya kukusuru swala aliyopewa msafiri.

Imepokelewa kutoka kwa Anas Ibn Maalik Allah-amuwiye radhi-amesema:

Niliswalai Adhuhuri pamoja na Mtume–Rehema na Amani zimshukie–rakaa nne tukiwa Madina (mjini). Na alasiri tukaswali Dhul-Hulayfah rakaa mbili (Qaswra)”. Bukhaariy & Muslim

Ikumbukwe Dhul-Hulayfah ni kitongoji kilichoko nje ya maamirisho ya Madinah.

Msafiri kutonuia ukazi wa siku nne mahala anakokwenda, ukiziondoa zile siku mbili; siku ya kuingia anakokwenda na siku ya kurudi anakotoka.

Msafiri akinuia ukazi wa siku nne mahala anakokwenda, kwa nia yake hii mji huo alionuia kukaa siku nne utakuwa kisheria katika hukumu ya makazi na mahala pake pa kuishi.

Kwa mantiki hii ataandamiwa na hukumu za mkazi na sio msafiri, kwa hivyo haitamjuzia kukusuru ndani ya mji huo.

Atabakia na haki ya kukusuru njiani tu, yaani wakati wa safari ya kwenda katika mji huo au kurudi mjini kwake.

Ama atakaponuia ukazi wa chini ya siku nne, atabakiwa na rukhsa ya kukusuru mpaka atapoamua kurejea mjini kwake.

Na ikiwa msafiri huyu hajui atakaa muda gani huko ugenini ambako ameenda kwa shughuli/haja fulani na hajui ataikamilisha lini shughuli hiyo/haja yake hiyo.

Katika mazingira haya atapewa rukhsa ya kukusuru swala kwa kipindi cha siku kumi na nne tu, ukiziachilia mbali zile siku mbili; siku ya kuingia na ile ya kuondoka.

Imepokelewa kutoka kwa Imraan Ibn Huswayn–Allah amuwiye radhi–amesema:

“Nilipigana vita pamoja na Mtume wa Allah– Rehema na Amani zimshukie-na nilikuwa pamoja nae wakati wa Fat-hi Makah. Akakaa mjini Makah siku kumi na nane, haswali (katika kipindi chote hicho) ila rakaa mbili.” Abuu Daawoud

Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie-alikaa Makah kipindi chote hiki katika mwaka ule wa Fat-hi Makah kwa ajili ya kupambana na kabila la Hawaazin.

Akawa anakusuru swala, kwa sababu hakuwa akijua mapambano hayo yatamchukua muda gani hadi kumalizika na hali kuwa shwari.

Msafiri asimfuate mkazi katika swala yake, yaani asiwe maamuma anayeswali nyuma ya Imamu mkazi.

Msafiri mwenye rukhsa ya kukusuru, kwa kuiswali rakaa mbili swala ya rakaa nne hawezi kumfuata mkazi anayeiswali swala hiyo hiyo kwa kutimiza rakaa nne zote.

Angalia akiamua kumfuata mkazi huyo, swala yake itasihi na itamuwajibikia kumfuata pia katika kutimiza na hivyo kujiondoshea yeye mwenyewe rukhsa ya kukusuru.

 

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *