KUSTANJI/KUCHAMBA NA ADABU {TARATIBU ZA KUKIDHI HAJA}

“Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini” Hadith Tukufu

Kustanji/Kuchamba ni kusafisha na kuondoa najisi iliyotoka katika mojawapo ya tupu {uchi}mbili au zote mbili; tupu ya mbele na ya nyuma kwa kutumia maji twahara au kinachosimama memo/mahala pa maji wakati wa kukosekana maji kama vile mawe, karatasi, kitambaa, majani na kadhalika. Mchambaji ahakikishe amejisafisha vema kiasi cha kutobakia athari ya najisi iliyotoka; ikiwa ni mkojo au mavi.

Kustanji/Kuchamba baada ya kukidhi haja ni WAJIBU/FARADHI kama tutakavyoona katika kauli za Mtume – Rehma na Amani zimshukie – katika maelezo yajayo.

VITU VITUMIKAVYO KATIKA KUSTANJI

Inajuzu/inafaa kustanji (kuchamba) kwa kutumia maji mutlaq (maji halisi) ambayo ndiyo asili katika kujitwahirisha na najisi. Pia inajuzu kustanji kwa kila kitu chenye sifa zifuatazo :

  1. Kigumu (kigogofu)
  2. Chenye Kuparuza (kisichoteleza)
  3. Kinachoweza kuondosha najisi.

Vitu vyenye sifa hizi ni kama mawe, karatasi, kitambaa na kadhalika. Ni vema kustanji, mtu akaanza kwa kutumia mawe/karatasi kisha ndio akamalizia na maji. Kufanya hivyo ni kwa sababu mawe/karatasi huondosha juta (dhati) ya najisi na maji huondosha athari ya najisi bila ya kuchangayika na juta lake. Ikiwa atatumia kimojawapo baina ya mawe/karatasi na maji, basi ni bora akatumia maji kwani ndiyo pekee yenye uwezo wa kuondosha juta (dhati) na athari ya najisi, kinyume na mawe na nduguze {karatasi, kitambaa na kadhalika}.

Imepokelewa kutoka kwa Anas Ibn Maalik – Allah amuwie Radhi – amesema : Mtume wa Allah alikuwa akiingia mahala pa kukidhi haja, mimi na kijana wa rika langu tukimbebea chombo cha maji na fimbo/mkuki mfupi, basi akistanji kwa kutumia maji. Bukhariy na Muslim.

Maelezo : Fimbo/Mkuki ulikuwa ukitumika kama sitara na alama wakati wa kuswali ili mtu asiweze kupita mbele.

Imepokewa na Ibn Masoud – Allah amuwie Radhi – amesema : Mtume – Rehma na Amani zimshukie – alienda kukidhi haja na akaniamrisha nimletee mawe matatu. Al-Bukhariy.

USISTANJI kwa kutumia najisi nyingine iliyo kavu au kitu kilichonajisika tayari kwani huenda kikaizidisha athari ya najisi badala ya kuipunguza. Kadhalika ni haramu kustanji kwa kilicho chakula cha binadamu kama vile mkate au chakula cha majini kama vile mifupa. Amesema Bwana Mtume – Allah amshushie Rehma na Amani – “Msistanji kwa (kutumia) kinyesi cha wanyama wala mifupa kwani hiyo (mifupa) ni chakula cha ndugu zenu majini” Tirmidhiy.

ADABU/TARATIBU ZA KUFUATA KATIKA KUKIDHI HAJA NA KUSTANJI (KUCHAMBA)

Sheria imeweka taratibu ambazo muislamu anapaswa kuzichunga na kuzifuata wakati wa kukidhi haja na kustanji. Taratibu hizi tutazigawa katika mafungu/sehemu zifuatazo :

A. ADABU/TARATIBU ZINAZOFUNGAMANA NA MAHALA PA KUKIDHIA HAJA

Imemlazimu mkidhi haja, ajiepushe kukidhi haja katika :

  1. Njia ya watu au mahala wanapokaa, hii ni kutokana na kero na maudhi yatakayowapata. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah amuwie Radhi – kwamba Mtume – Rehma na Amani zimshukie – amesema : “Yaogopeni mambo mawili yaletayo laana” (Maswahaba) wakauliza : Ni yapi mambo mawili hayo ? (Mtume) akajibu : “Ni yule ambaye anajisaidia katika njia ya watu au kivuli chao” Muslim.
  2. Tundu iliyopo ardhini au ufa wa ukuta/kiambaza. Hii ni kwa sababu ya kumlinda na kumuepusha mkidhi haja na madhara yanayoweza kumpata. Kwani anaweza akawamo ndani ya shimo/ufa mdudu mwenye kudhuru kama vile nge au nyoka, huyu akakerwa na haja akaamua kumtokea mtu na kumdhuru. Imepokelewa kutoka kwa Abdillahi ibn Sarjisi, amesema : Amekataza Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – kukojoa katika tundu. Abuu Daawood.
  3. Chini ya mti utoao matunda. Hii ni kwa ajili ya kuyahifadhi na kuyalinda matunda yadondokayo yasipatwe na najisi. Ni mamoja ikiwa matunda hayo yanaliwa au hayaliwi lakini yana manufaa mengine kama dawa.
  4. Maji yaliyotuama (yasiokwenda). Hii ni kutokana na kichefuchefu watumiaji wa maji hayo yakiwa ni mengi yasiyoharibika na najisi na kuyanajisi yakiwa machache na hivyo kuyafanya yasifae kutumika. Imepokelewa kutoka kwa Jabir – Allah amuwie Radhi – kutoka kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kwamba (Mtume) amekataza kukojoa katika maji yaliyotuama”. Muslim.

Kunya ni aula zaidi kwa kukatazwa

B. ADABU/TARATIBU ZENYE KUFUNGAMANA NA UINGIAJI NA UTOKAJI MAHALA PA KUKIDHI HAJA

Ni Vema kwa mwenye kutaka kukidhi haja, atangulize mguu wake wa kushoto wakati wa kuingia chooni na mguu wa kulia wakati wa kutoka chooni, kama tulivyofundishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kadhalika asiingie na chochote chenye jina la Mwenyezi Mungu au jina lolote tukufu kama vile jina la Mtume au aya ya Qurani Tukufu. Bali imemlazimu muislamu kukivua kitu hicho wakati wa kuingia chooni. Pia imesuniwa kuleta dua wakati wa kuingia chooni. Pia imesuniwa kuleta dua zilizothibiti kutoka kwa Bwana Mtume kabla na baada ya kutoka chooni.

Aseme kabla ya kuingia chooni :
BISMILLAH ALLAHUMMA INNIY AUDHUBIKA MINAL KHUBUTHI WAL-KHABAITH. Al-Bukhariy na Muslim.

Na aseme baada ya kutoka :
GHUFRAANAKA AL-HAMDU LILLAHIL-LADHIY ADH-HABA ANNIYL-ADHA WA-A’AFANIY. Abu Dawood, Al-tirmidhi, Ibn Majah na Al-twabraniy.

C. ADABU/TARATIBU ZIFUNGAMANAZO NA UPANDE WA KUELEKEA WAKATI WA KUKIDHI HAJA :

Ni haramu kwa mwenye kukidhi haja kuelekea Qiblah au kukipa mgongo. Uharamu huu ni iwapo anakidhi haja mwandani, wala hapana chenye kumsitiri wakati wa kukidhi haja yake. Na imeshurutizwa sitara isiwe mbali nae zaidi ya dhiraa tatu za binadamu sawa na sentimeta 150 takriban. Ikiwa jengo analotumia limeandaliwa maalum kwa ajili ya kukidhia haja (chooni), basi si haramu, bali inajuzu kuelekea na kulipa mgongo Qiblah kwa kuwa pana sitara.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Ayyuub Al-Answariy – Allah amuwie Radhi – kutoka kwa Mtume –Rehma na Amani zimshukie – amesema “mnapokwenda chooni msielekee Qiblah wala msikipe mgongo kwa (kukidhi) haja ndogo au kubwa, lakini elekeeni mashariki na magharibi”. Al-Bukhariy na Muslim.

D. ADABU/TARATIBU ZINAZOFUNGAMANA NA HALI YA KUKIDHI HAJA :

Ni vema kwa mwenye kukidhi haja akategemea mguu wake wa kushoto na kuusimamisha/kuunyoosha mguu wa kulia, hivi ndivyo anavyotakiwa akae wakati wa kukidhi haja. Hekima ya ukaaji huu ni kuifanya haja itokee kwa wepesi kama vile unavyomimina kilichomo ndani ya chupa kwa kuinamisha upande upande. Kadhalika anatakiwa wakati wa kukidhi haja asiangalie juu, utupu wake wala kile kimtokacho. Pia ni karaha kuzungumza wakati anakidhi haja.

Imepokelewa na Ibn Umar –Allah amuwie Radhi – kwamba mtu mmoja alipita ilhali Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehma na Amani zimshukie – akikidhi haja ndogo, (mtu yule) akamtolea salamu, (Mtume) hakumjibu. Muslim.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Said – Allah amuwie Radhi – amesema ; Nimemsikia Mtume – Rehma na Amani zimshukie – akisema : “Wasitoke watu wawili wakaenda kukidhi haja, hali ya kufunua tupu zao huku wakizungumza, hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hulichukia hilo” Abu Dawood na wengineo.

Maelezo : Inakisiwa/Inapimiwa juu ya maneno (mazungumzo) mambo mengine kama vile kula, kunywa na kuchezeachezea utupu (uchi).

Kustanji/kuchamba kwa kutumia mkono wa kushoto : Anatakiwa mwenye kukidhi haja atumie mkono wake wa kushoto kusafisha mahala ilipotokea najisi kwani ni karaha kutumia mkono wa kulia.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Qatadah – Allah amuwie Radhi – kutoka kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – amesema : “Anapokojoa mmoja wenu, basi asiishike dhakari yake kwa mkono wa kulia na wala asistanji/asichambe kwa mkono wa kulia”.

Kadhalika miongoni mwa adabu, anatakiwa mwenye kukidhi haja mawandani; nje ya jengo lililoandaliwa kwa kukidhia haja (chooni), atafute mahala pa faragha palipo mbali na watu. Watu wasimuone wala kusikia harufu ya choo chake au sauti ya mashuzi yake. Imepokelewa kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa anapotaka kwenda kujisaidia huenda mbali mpaka mtu asiweze kumuona. Abu Dawood na Al-Tirmidhiy.

Vile vile anatakiwa asiisege/asiipandishe nguo yake ikiwa ni shuka/msuli mpaka akurubiapo ardhi, sio anaanza kuvua nje kabla hajaingia ndani. Afanye hivyo kwa ajili ya kuusitiri utupu wake, jambo ambalo limeamrishwa na sheria.

NYONGEZA : KATIKA KUTAJA HUKUMU ZA VYOMBO :

Vyombo ni vile vitu/vifaa ambavyo tunavyotumia katika kuwekea, kuhifadhia au kulia chakula na vitu vingine viowevu (vimiminika) kama vile maji, maziwa, juisi na kadhalika. Hivi ndivyo vyombo ambavyo tunavyokusudia kutaja hukumu ya utumiaji wake kwa mujibu wa sheria. Tutavigawa na kuviweka vyombo katika mafungu manne, kama ifuatavyo :

1. HUKUMU YA UTUMIAJI WA VYOMBO VYA DHAHABU NA FEDHA:

Vyombo vya dhahabu ni vile vyombo ambavyo malighafi (material) iliyotumika kuvitengenezea ni dhahabu halisi au fedha halisi. Vyombo hivi vinaweza kuwa ni vijiko, sahani, bakuli na kadhalika, na siyo vitu kama mikufu, bangili, hirini, haya ni mapambo ya wanawake na si vyombo.

Kwa mujibu wa sheria ni HARAMU kutumia vyombo vya dhahabu kwa aina zote za matumizi, kama vile kuvitumia kwa ajili ya kutawadhia, kunywea, kulia chakula na matumizi mengine kama haya. Mtu anaruhusiwa tu kutumia vyombo hivi kwa dharura, kama vile kukosa kabisa chombo kingine kisichokuwa cha dhahabu. Kwa dharura kama hii anaweza kutumia chombo cha dhahabu. Ruhusa hii ya dharura ni kwa mujibu wa msingi usemao :
DHARURA HUHALALISHA YALIYO HARAMU/YALIYOKATAZWA

Imepokelewa kwa swahaba Hudhayfah ibn Al-Yamaan – Allah amuwie radhi – amesema : Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu –Rehema na Amani zimshukie – akisema : “Msivae hariri wala dibaji (aina ya nguo ya thamani za hariri) na wala msinywee vyombo vya dhahabu na fedha, na wala msilie sahani zake (dhahabu na fedha) kwani vyombo hivyo ni vyao (makafiri) duniani na ni vyetu akhera” Al-Bukhariy na Muslim.

Hukadiriwa juu ya kula na kunywa matumizi mengine kama vile kunawia na kuhifadhia chakula. Ni vema ikaeleweka kuwa uharamu huu wa utumiaji vyombo vya dhahabu unamuhusu mwanamume na mwanamke.

2. HUKUMU YA UTUMIAJI WA VYOMBO VILIVYOTIWA KOWA LA DHAHABU AU FEDHA :

Tunamaanisha kwa neno KOA, ungo/muungo. Yaani chombo kisichotengenezwa kwa dhahabu au fedha kilivunjika au kilikatika, kisha yakatumika madini ya dhahabu au fedha kukiunga tena chombo kile ili kiweze kufaa kutumika.

Sheria imeharamisha kutumia chombo kilichotiwa koa la dhahabu kwa hali yeyote ile iwayo. Ni mamoja koa lilikuwa kubwa au dogo. Ama utiaji wa koa la fedha, aangalie :

  1. ikiwa koa ni dogo kwa uungaji usio wa pambo, INAJUZU/IMERUHUSIWA.
  2. Ikiwa koa ni kubwa tena ni kwa ya pambo, basi ni HARAMU/IMEKATAZWA.
  3. Ikiwa koa ni kubwa kwa sababu ya haja au koa ni dogo kwa ajili ya pambo ni KARAHA.

Na dalili/ushahidi juu ya kujuzu koa kubwa la fedha ni ile hadithi iliyopokewa kutoka kwa ‘Aaswim Al-ahwaal amesema : niliiona bilauri ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kwa Anas bin Malik na ilikuwa imevunjika, akaiunga kwa (koa) la fedha. Na Anas akasema : Nilimnyweshea Mtume wa Mwenyezi Mungu bilauri hii zaidi ya hivi na hivi.

3. HUKUMU YA UTUMIAJI WA VYOMBO VILIVYOTENGENEZWA KUTOKANA NA MADINI YENYE THAMANI KUBWA {PRECIOUS STONES}

Inajuzu kisheria kutumia vyombo ambavyo malighafi iliyotumika kuvitengenzea ni madini yenye thamani kubwa kama vile almasi, lulu, marijani (coral), yaaquti (ruby) na mengineyo. Kujuzu huku kunatokana na kutopokewa NASWI ya Qurani au hadithi kukataza vitu hivi. Na Msingi wa Fiq-hi unasema :

(ASILI KATIKA VITU NI UHALALI) maadam haikupokewa dalili ya kuharamisha au kukataza.

4. HUKUMU YA UTUMIAJI VYOMBO VYA MAKAFIRI :

Tunakusudia kwa ibara “Vyombo vya makafiri”, vyombo vinavyomilikiwa na makafiri yaani ni mali yao na wanavitumia kwa matumizi yao mbali mbali.

Sheria imeruhusu muislamu kutumia vyombo vya makafiri kwa matumizi mbali mbali. Ruhusa hii ni kwa mujibu wa hadithi iliyopokelewa na Imam Bukhariy kutoka kwa Abu Tha’alabah –Allah amuwie Radhi – kwamba Mtume –Rehema na Amani zimshukie – amesema : “Vikosheni na mvitumie kwa kulia chakula”.

Maelezo : Amri hii ya Mtume juu ya kuviosha vyombo vya makafiri kabla ya kuvitumia ni kwa ajili ya USUNA kwani inamkinika kuwa vimechafuliwa na wamiliki wake ambao ni makafiri. Pengine wamevitumia katika kunywea pombe au kupikia na kulia nguruwe na kadhalika. Inakadiriwa juu ya vyombo vitu vyao vingine kama vile nguo, samani(furniture) na kadhalika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *