Tunapozizungumzia sherehe zetu za harusi leo na tukazipima kwa mizani ya sheria tutaona ni namna gani furaha na sherehe zetu zinavyopingana na mafundisho ya dini yetu. Sherehe zetu leo zimekusanya mambo mengi sana ambayo ni kinyume kabisa na sheria.
Chimbuko la mila/tamaduni hizi potofu ni kile kijulikanacho kama “usasa na kwenda na wakati’ sambamba na ule uigaji pofu usio na uoni wala uchambuzi wa jema na bya bali muhimu ni kuiga tu ili mtu aonekane anakwenda na wakati na ameendelea.
Miongoni mwa mila na mambo yasiyokubalika tuliyoyazua katika sherehe za harusi zetu ni kupiga kibao kata. Kibao Kata ni ngoma inayowajumuisha pamoja wanamume na wanaweke nje ya nyumba yenye harusi.
Huwekwa uwanjani meza kubwa katikati ya watu, kisha akapanda juu ya meza hiyo mwanamke akiwa kajifunga kibwebwe na wakati mwingine hupanda pamoja mwanamume na mwanamke. Unajua kinachofanyika ju ya meza hiyo ?
Kinachofanyika hapo na kushuhudiwa na jicho la kila mwenye kuona ni kile kisichoridhiwa na Mwenyezi Mungu, ni kile kinachoitia aibu jamii na kumvua utu wa mtu.
Ngoma hupigwa na jimama na jibaba hilo kuanza kukata viuno kwa njia ya fedheha bila hata chembe ya soni wala haya. Sambamba na midundo na viuno hivyo hufanyika pia kile kinachojulikana kama “sasambu”, hupandishwa juu ya meza sanduku/masanduku ya nguo alizonunuliwa na kuzawadiwa bi harusi na ndugu, jamaa na marafiki kisha zikaanza kusasambuliwa na kuonyeshwa mbele ya hadhira moja baada ya nyingine.
Sasambu hii huhusisha tangu kitambaa cha kichwa mpaka zile nguo za ndani ambazo kimaadili huwa hazionwi na kila mtu ila dukani tu.
Ikumbukwe kuwa mambo haya ya kibao kata pamoja na vikorombwezo vyake vyote hushuhudiwa pia na jamii chipukizi (watoto wadogo) wakaona mambo yasiyolingana na umri wao mdogo. Hebu tujiulize kwa makini;
- Tunatarajia kipi kingine zaidi ya uchafu na ufisadi kutokana na mjumuiko huu wa jinsia mbili hizi tofauti; wanamume na wanawake waliojiremba na kupendeza?!
- Tunazionyesha nguo za bi. Harusi mbile za watu ili iweje?!
- Tunapandiiza mbegu gani kwa chipukizi waliohudhuria zaidi ya kuirithi na kuiendeleza mila hii potofu huku wakiaini kuwa ndio namna sahihi ya kusherekea harusi?!
- Tunajisikiaje raha au huzuni na fedheha pale yule aliyepanda mezani anapokuwa ni mke, mama au dada yetu na sisi kushuhudia ukataji wake wa kiuno?!
Tuache ndugu zanguni, hizi ni mila na tamaduni zisizofaa, zinazochangia kwa asilimia nyingi tu kubomoa maadili mema katika jamii zetu. Harusi ni jambo jema, vipi tulitumie jambo jema hili kama uwanja wa kufanyia ufisadi na uchafu?!
Hivi tunaitazamia harusi hii iliyofanyika katika mazingira haya yaliyosheheni ghadhabu na laana za mwenyezi Mungu kuzaa matunda mema?
Ndugu zanguni, tuoane na kusherehekea harusi zetu kwa misingi na mafundisho shihi ya dini yetu ili tubarikiwe katika shughuli zetu na kupata radhi za Mola wetu Mtukufu. Kuendeleza na kuzifuata mila na tamaduni hizi ni upotevu na kumfuata shetani jambo ambalo Qur-ani imetuasa tujiepushe nalo. Tusome:
“ENYI MLIOAMINI! MSIFUATE NYAYO ZA SHETANI; NA ATAKAYEFUATA NYAYO ZA SHETANI (atapotea) KWANI YEYE HUAMRISHA MAMBO YA AIBU NA MAOVU (kama kibao kata) …………..” (24:21)
KUSUBIRI NJE YA MLANGO WAKATI BWANA HARUSI ANAPOINGIA NDANI ILI KUJUA KAMA BI. HARUSI NI BIKRA.
Athari ya ada hii mbaya bado imesalia katika ndoa za baadhi ya jamii zetu. Bwana harusi anapofunga ndoa na kisha kumchukua mkewe nyumbani kusindikizwa na jamaa hasa wanawake wa pande zote mbili; upande wake na ule wa mkewe.
Chumba cha bwana harusi hupambwa vizuri na kitanda kutandikwa shuka maalum mpya, hili si baya. Baya na la aibu lisilokubalika ni baada ya Bwana na Bi. Harusi kuingia chumbani baadhi ya akina mama husubiri nje mlangoni wakati mtu na mkewe wanapofanya tendo la ndoa.
Hawa husikiliza kwa makini iwapo bi harusi atalia kutokana na maumivu ya kuvunjwa bikira yake.
Wakishalisikia walitakalo, hapo ndipo maharusi hugongewa mlango, mlango ukishaunguliwa akina mama hawa hujitoma ndani kwa nderemo na vifijo, wakakichukua kitambaa kilicholowa na kuchafuliwa na damu wakatoka nacho nje huku wakishangilia na kukionyesha kwa watu wakisema:
“Harusi imejibu.” Ndugu zaguni, hii ni fedheha isiyo na nafasi hata kidogo katika maadili na mafundisho sahihi ya uislamu. Huku ni kumdhalilisha utu wa binadamu, kuvunja heshima na haki yake ya uwa faraghani. Qur-ani inatuambia:
“NA HAKIKA TUMEWATUKUZA WANAADAMU….” (17:70).
Tendo la ndoa ni tendo tukufu sana, kwani ndilo ambalo Mwenyezi Mungu Mtukufu amelijaalia liwe ni sababu ya kuendeleza kizazi cha binadamu, binadamu muzaane kupitia tendo hilo.
Tendo hili huhitaji faragha ya kutosha kumuaminisha kila mmoja kati ya mume na mke kwa wako peke yao tu na wa tatu wao ni yule aliywahalalishia wao tendo hilo yaani Mola wao, hapo ndipo hupatikana utulivu wa kulifanya tendo hili kwa makini, furaha na ukamilifu.
Huo ndio ubinadamu unaomtofautisha hayawani huyu binadamu na hayawani wengine katika tendo hili la kuzaana.
Kwa hivyo hairuhusiwi kabisa kisheria kuingilia kati faragha hii, kufanya hivyo hakumaanishi kingine zaidi ya kudhulumu na kunyang’anya haki ya faragha ya watu wengine.
Isitoshe kukionyesha kwa watu kitambaa chenye damu ni kumdhalilisha huyu mwanamke masikini, mwenye haki ya kujua kuwa mke ni bikira au thayibu (siyo bikira) ni mume tu na sio watu wengine. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie, anatumbia;
“Huenda mwanamume akazungumza (kwa watu) kile kinachokuwa baina yake na mkewe au huenda mwanamke (pia) akazungumza kitendo kinachokuwa baina yake na mumewe, (kama yuko afanyae hivyo) basi msifanye hivyo, kwani huo ni mfano wa shetani mwanamume aliyekutana njiani na shetani mwenzake mwanamke, akamuingilia huku watu wakiangalia.”Twabaraaniy.
Sasa ikiwa mume/mke hana haki ya kuitoa nje siri ya unyumba wao, na Bwana Mtume akamfananisha mume/mke afanyaye hivyo na shetani.
Vipi, wewe usiye mume/mke unaipata wapi ruhusa na na kibali hiki cha kukfichua na kuitoa nje siria hii ya mke na mume (bikira)?
Je, hujioni kwamba wewe ni mbaya zaidi kuliko shetani ? Tuacheni ndugu zanguni, mambo haya hayakubaliani hata na akili tu ya kawaida, seuze dini/mfumo sahihi wa maisha!