Kumuhalalisha mtoto wa zinaa au mtoto wa nje ya ndoa kama ijulikanavyo leo ni miongoni mwa mila potofu na desturi mbaya zilizoenea na kutapakaa katika jamii zetu kiasi cha kuonekana kuwa ni jambo zuri linalokubalika.
Mila hii ni zao na matokeo ya mwanamume na mwanamke kuchukuana kinyumba na kuishi maisha ya mke na mume bila ya kufunga ndoa kwa mujibu wa sheria.
Pengine hili hupata baraka zote za wazazi wa pande zote mbili, upande wa mtoto wa kiume na ule wa mtoto wa kike.
Hili hufanyika pale wazee wa upande wa mtoto wa kiume wanapokwenda kwa wazazi wenzao, wazazi wa mtoto wa kike kufunga kile kinachojulikana kama “PAMVU” Baada ya pamvu kufungwa ndipo mtoto wa kiume hupata ruhusa na uhuru wa kuchanganyika na binti kama atakavyo, huku wazazi wa kiangalia na kufurahia tu bila ya kuona kuwa hilo ni jambo baya ambalo wao kama wazazi wanapaswa kulikemea na kulikataza ili kuzuia na kuepusha ufisadi na uharibufu katika jamii.
Hali hii huweza kufikia kilele cha vijana hawa kuishi pamoja kama mume na mke, na matunda ya hali hii ni kupatikana mtoto /watoto wa zinaa (nje ya ndoa).
Maisha haya ya kinyumba ni kinyume kabisa na sheria ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenyezi Mungu amelikataza jambo hili kutokana na madhara na athari yake mbaya inayoikumba jamii ya wanadamu. Tusome na tuzingatie
“………NA (mmehalalishiwa kuwaoa) WANAWAKE WEMA WA KIISLAMU NA WANAWAKE WEMA KATIKA WALE WALIOPEWA KITABU KABLA YENU. (Ni halali kwenu kuwaoa) MTAKAPOWAPA MAHARI YAO, MKAFUNGA NAO NDOA, BILA KUFANYA UZINZI (kwa mwanamke huyu na huyu), WALA KUWAWEKA (wanawake) KINYUMBA ……..” (5:5)
kwa mujibu wa aya hii ni haramu kwa mtu anayemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuishi na mwanamke kinyumba bila ya kufunga ndoa kwa mujibu wa sheria na bila ya kumpa mwanamke mahari yake.
Maisha ya kinyumba ni uzinzi usiokubalika na sheria. Baada ya watu hawa, mwanamme na mwanamke kuamua kwa khiyari zao wenyewe kumuasi Mola wao na kuzitupilia mbali sheria zake, wakaishi maisha ya kinyumba kama mtu na hawara yake bila ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu kupitia ndoa watu hawa huweza kuruzukiwa watoto katika maisha haya batili ya uzinzi.
Sasa inapofikia watu hawa kuzinduka na kutaka kufunga ndoa kwa mujibu wa sheria ili kuanza ukurasa mpya wa maisha ya ndoa.
Au inapofikia mtoto amekuwa mkubwa anataka kuolewa, ili baba apate uhalali wa kuwa walii wa binti huyu hapo ndipo hujitokeza suala lijulikanalo kama kumuhalalisha mtoto.
Tendo hili haramu la kumuhalalisha mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa (katika maisha ya uzinzi) hukamilika kwa huyu baba mzinzi kupigwa faini na kisha kumuoa mzinifu mwenziwe (mama wa mtoto).
Baada ya faini na ndoa hiyo, huyu mtoto wa zinaa hunasikishwa na baba huyu mzinifu na kutambulika na jamii husika kama mtu na mwanawe.
Baba huyu huwa na mamlaka kamili kwa mtoto huyu kama mzazi na hivyo kuwa na uhalali/ haki ya kuwa walii wa binti huyu aliyempata katika maisha ya kinyumba.
Mahari ikapokelewa, khutuba ya ndoa ikasomwa na hatimaye baba huyu asiyetambulika na sheria akamuozesha yule anayedai kuwa binti yake na wali ukaliwa.
Huku ni kuendeleza uchafu, kwa sababu kwa mujibu wa sheria huyu si baba na hivyo hawezi kuwa walii kwani mtoto yeyote anayezaliwa nje ya ndoa huwa ni wa mama, hana nasabu. Bwana Mtume Rehema na amani zimshukie – anatuasa :-
“Yeyote atakayejinasibisha na asiye baba yake (halali) na il-hali anajua kwamba si baba yake basi pepo ni haramu kwake (mtu huyu).” Bukhaariy na Muslim.
Hii ndiyo athari mbaya inayoweza kuikumba jamii ya wanadamu kutokana na kuendeleza mila na desturi hii mbaya ya kuishi maisha ya unyumba kisha kupelekea kuzaa mtoto wa zinaa.
Mtu ataozesha kwa kuamini kuwa ana haki ya kufanya hivyo, na huyu ataamini kuwa kaoa/kuolewa na hivyo kuwa ni mme/mke wa mtu.
Wakaishi katika dhana hiyo na kupata watoto huku wakiamini kuwa ni watoto wao, watu wakarithi na kurithiwa. Lo!
Masikini kumbe ukweli na haki ni kinyume cha wanavyodani au kuamini kwani kwa mujibu wa sheria huyu si baba bali ni mzinifu tu.
Kwa hivyo hana halali wa kuwa walii na kwa sababu ya kukosekana walii ambaye ni mmoja wapo wa nguzo za ndoa, ndoa haipo yaani haikusihii kisheria.
Hivyo wawili hawa mbele ya sheria si mume na meke ndio maana tunasema huku ni kuendeleza uchafu juu ya uchafu.
Vijana hawa wanazinishwa kwa sababu tu ya mtu mmoja aliyekiuka sheria na kuishi na mwana mke kinyumba yeye kafanya makosa na anasababisha watu wengine kufanya makosa wakiwa wanajua au hawajui.
Huyu ni mtu mbaya sana, atabeba mzigo wake wa dhambi zinazotokana na kitendo chake hiki chenye athari mbaya sana, atabeba mzigo wake wa dhambi zinazotokana na kitendo chake hiki chenye athari mbaya kwa jamii na pia hataepuka kubeba mzigo wa dhambi za aliowapoteza kwa kuwazinisha. Tusome
“(wanapoteza watu hivi) ILI WABEBE MIZIGO (ya madhambi) YAO KAMILI SIKU YA KIAMA, NA (pia) SEHEMU YA MIZIGO YA WALE WANAOWAPOTEZA BILA YA KUWA NA ILIMU (hao wanaowapoteza) .SIKILIZENI! NI MIBAYA MNO HIYO (mizigo) WANAYOIBEBA” (16:25) Mfasiri Mkuu wa Qur-ani Tukufu, Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatufafanulia aya hiyo pale aliposema :-
“yeyote atakayeanzisha/atakayeasisi mwendo (suna) mwema katika Uislamu, atapata ujira wake (mwendo huo) na ujira wa watakaoufuata mwendo huo baada yake (Mtu huyo) bila ya kupungua chochote katika ujira wao (watendaji) Na atakayeasisi katika Uislamu mwendo mbaya (kwa maasi aliyoyafanya) atakuwa juu yake (mzigo wa) dhambi za mwendo huo na dhambi za watakaomfuata katika mwendo huo baada yake bila ya kupungua chochote katika madhambi yao (watendaji).” Muslim.
Kukaa na mwanamke kinyumba ni zinaa ambayo ni miongoni mwa madhambi makubwa baada ya kufru, shirki na kuua na ni uchafu aliouharamisha mwenyezi Mungu Mtukufu:
‘WALA MSIKARIBIE ZINAA. HAKIKA HIYO (zinaa) NI UCHAFU (mkubwa) NA NI NJIA MBAYA (kabisa)” 17:32 Mwenyezi Mungu Mtukufu ametukataza uchafu wa zinaa ili kutuhifadhi na madhara yake sambamba na athari zake mbaya kwetu ambazo ni wazi mble ya macho ya kila mmoja wetu.
Miongoni mwa hekima/falsafa ya kuharamisha zinaa kwa aina zake zote ikiwa ni pamoja na maisha ya unyumba ni :
1. Kuchunga/kuhifadhi utukufu na heshima ya mwanadamu. Mwanadamu atofautiane na hayawani wengine; hayawani wasio wanadamu wao wana tendo la ndoa tu hawana ndoa na wigo wa tendo la ndoa kwao ni mpana sana kiasi cha kuweza kufanya tendo hilo na mama yake/baba yake.
Sasa ili kudhihirisha utukufu wa huyu binadamu juu ya baki ya hayawani wengine ndipo Mola, Muumba wake akamuwekea utaratibu mzuri ndoa.
Aoe kwanza ndipo apate uhalali wa kufanya tendo la ndoa. Mwanadamu anapoacha utaratibu huu na kuanza tendo la ndoa kabla ya ndoa, tendo lake hilo humshushia hadhi na thamani yake na kuwa kama mnyama au chini zaidi kuliko mnyama
“……. HAO NI KAMA WANYAMA BALI WAO NI WAPOTEVU ZAIDI ” (7:179)
2. Kuchunga na kuhifadhi nasabu ya mwanadamu na ukoo wake. Hayawani wasio na akili hawana nasabu wala ukoo.
Huwezi kusema mathalan : Ng’ombe huyu anaitwa Fulani bin Fulani wa ukoo Fulani. Lakini mwanadamu ni lazima kisheria atambulike nasabu na ukoo wake.
Aozwe au kuolewa kwa nasabu hiyo, kadhalika ajulikane hivyo katika shughuli zote za maisha ya kibinadamu.
Sasa watu wanapoamua kuishi kinyumba na kuzaa watoto, huko ni kujidhalilisha na kujivunjia hadhi na heshima yao na kujitangazia unyama wao na pia wana hatia ya kumpotezea mtoto aliyezaliwa nasabu na heshima yake machoni pa jamii ikiwa ni pamoja na kumkosesha haki zake za msingi kama mtoto.
Ni kutokana na athari hizi mbaya kwa jamii ndio Mwenyezi Mungu akauharamisha na kuukemea vikali uzinifu ambao ni pamoja na kuwekana kinyumba ambako huzaa haramu nyingine ya kuhalalisha mtoto wa zinaa, dhambi juu ya dhambi na uchafu juu ya uchafu.
Eeh! Ubaya uloje wa mila mbaya hizi tulizozizua na kuacha utaratibu mzuri aliotuwekea Mola Muumba wetu.
Hizi ni nasaha za wiki, kunasihika au kutonasihika hiyo ni juu yako. Amua ama kunasihika kwa manufaa ya nafsi yako na jamii kwa ujumla au acha kunasihika kwa mangamizi ya nafsi yako na jamii kwa jumla na ubebe mzigo wa dhambi zako na za jamii ikiwa ni matokeo ya ukaidi wako.