Hii ndiyo nguzo ya sita katika mlolongo wa nguzo za swala.
Na kuitadili maana yake ni kusimama na kulingana sawa baada ya kuinuka kutoka rukuu.
Kwa hiyo tunaweza kabisa kusema kuwa kuitadili ni kisimamo sawa kinacho tenganisha baina
ya rukuu na sijida.
Dalili ya Itidali:
Itidali kama mojawapo ya nguzo za swala imetajwa katika riwaya iliyo pokelewa kutoka kwa Bi.
Aisha-Allah amuwiye radhi-kwamba yeye aliielezea swala ya Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-akasema:
“Alikuwa anapo kiinua kichwa chake kutoka rukuu, husujudu mpaka (kwanza) alingane sawa
hali ya kusimama (aitadili)”.
Sharti za Itidali:
Ili Itidali iswihi, kumeshurutizwa mambo yafuatayo:
i. Kutokukusudia kwa kuitadili kutoka rukuu kitu kingine chochote zaidi ya ibada.
ii. Kutulizana katika Itidali kiasi cha kadiri ya kuleta Tasbihi moja.
iii. Asirefushe mno kisimamo cha Itidali kiasi cha kuzidi muda unaotumika katika usomaji wa Suratil-Faatihah. Hii ni kwa sababu Itidali ni miongoni mwa nguzo fupi, kwa hivyo basi hakujuzu kuitwawilisha (kuirefusha).