Hii ndio sharti ya nne na ya mwisho miongoni mwa sharti za kusihi swala.
Makusudi ya Qiblah ni Alka’aba tukufu; yaani Qiblah kiwe mbele yake makati wa kusali akielekee.
Mafaqihi; wataalamu wa fani ya fiqhi, wamekongamana na kuwafikiana kuwa inamuwajibikia mwenye kutaka kuswali kuuelekea msikiti mtukufu wa makkah ambamo humo ndimo ilimo Al-ka’aba.
Kongamano hili linatokana na kauli ya Mwenyezi Mungu mtukufu ndani ya Qur-ani:
“KWA YAKINI TUKIONA UNAVYOGEUZAGEUZA USO WAKO MBINGUNI. BASI TUTAKUGEUZA KWENYE KIBLA UKIPENDACHO BASI GEUZA USO WAKO UPANDE WA MSIKITI MTAKATIKFU (Al-Ka’aba) NA POPOTE MNAPOKUWA ZIELEKEZENI NYUSO ZENU (wakati wa swala) ULIKO (Msikiti huo) —“ [2:144]
Dalili na ushahidi wa kuelekea Qiblah ndani ya Sunnah kwamba Mtume Rehema na Amani zimshukie alimwambia swahaba aliyekuwa akimfundisha namna ya kuswali:
“Unapotaka kuswali, eneza udhu (tawadha udhu kamili), kisha elekea Qiblah na ulete takbirah”. Bukhaariy na Muslim.
Muradi wa “mtakatifu” uliotajwa katika aya na “Qiblah” katika hadithi ni Al-Ka’abah.
Mtu mwenye kuiona Al-Ka’abah hii hapa mbele yake inamuwajibikia aielekee dhati yake na asiyeiona yuko mbali kinachomuajibikia ni kuelekea tu upande iliko Al-Ka’abah kama ilivyoelezwa na aya.
Mtu asiyejua upande kilipo Qiblah na asimpate mtu wa kumuuliza kutamuwajibikia kujitahidi ndipo aswali kuelekea upande anaodhania kuwa ndio upande wa Qiblah na swala yake itakuwa ni sahihi.
Lakini itakapombainikia ndani ya swala kwamba amekosea, kwa yakini upande ule sio upande wa Qiblah pale pale swala yake itabatilika na itampasa aianze swala yake upya kwa kuelekea upande ambao ana yakini kuwa ndio Qiblah. Hukumu itakuwa ni hii hii.
Pia kama atakuwa na yakini ya kukosea hata baada ya kumaliza kuswali. Ama kosa lenyewe likiwa linatokana na dhana tu na sio yakini, basi hapana kurejea swala.