SOMO LA NNE –02 MATUKIO MUHIMU KABLA YA KUZALIWA KWA BWANA MTUME-Rehema na Amani zimshukie.

“SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

Naam, ni juma jingine ambalo kwa uwezo wake Mola ametukutanisha tena katika darsa letu hili la Sira yake Bwana wetu Mtume Muhammad.

Ndugu mwana darsa-Allah akurehemu-tuanze kwa kumshukuru Allah Mtukufu ambaye kwa mapenzi yake makuu kwetu ametukutanisha katika darsa hili ili tupate kudarisishana dini yetu kupitia

Sira ya Mtume wa Allah. Lengo letu likiwa ni kutufanya kwanza kumjua, kumpenda na kisha kumfuata Bwana Mtume kama alivyo tuamrisha Allah. Hivyo basi tunakusihi uendelee kuwa nasi hasaa huenda Mola wetu kwa fadhila zake akaturuzuku kumjua na kumpenda yule aliye kipenzi chake na Mbora wa viumbe vyote.

Haya sasa na tuendelee na darsa letu la juma lililo pita ambamo tulianza kuyasoma yale matukio muhimu yaliyo utangulia uzawa wake Bwana Mtume, tuendelee na tukio la pili:

Kisa cha watu wa ndovu (tembo)

Ndugu msomaji-Allah akurehemu-kisa cha watu wa tembo ni katika jumla ya matukio makubwa yaliyo andamia mazazi matukufu ya Bwana Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Tukio hilo limethibiti kwa Qur-ani Tukufu na Sunna ya Mtume na likafafanuliwa na vitabu vya Sira na vile vya Tarekhe (Historia) na wamelitaja Wanazuoni wa Tafsiri kwenye vitabu vyao. Allah Mtukufu anasema:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ١ أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ٢

وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا أَبَابِيلَ٣ تَرْمِيهِمْ بِحِجَارَةٍ مِنْ سِجِّيلٍ٤ فَجَعَلَهُمْ

كَعَصْفٍ مَأْكُولٍ٥ [الفيل: 1-5]

“Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo watenda wale wenye tembo? Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika? Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi. Wakiwatupia mawe ya udongo wa motoni. Akawafanya kama majani yaliyo liwa!”. Al-Fiil [105]:01-05

Miongoni mwa ishara za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kulielekea tukio hilo:

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo toka kwenye vita vya Hudaibiya, akaenda mpaka alipo fika kwenye bonde ambalo hapo huanza mwendo wa kushuka, ngamia wake akakita magoti. Watu (maswahaba) wakasema: Amegoma! Amegoma! Akakataa kabisa kuinuka na kuendelea na safari.

Wakasema (tena): Amefanya ukaidi Qasw-waa (jina la ngamia wa Bwana Mtume)! Mtume akawaambia: “Qasw-waa hajafanya ukaidi na wala hana tabia hiyo, lakini kilicho mzuia kuendelea na safari ni kile kilicho mzuia yule tembo (wa Abraha)”. Bukhaariy-[05/388]-Allah amrehemu.

Na kuhusiana na tukio hilo, imeandikwa kwenye kitabu [السيرة النبوية AS-SIIRATUN-NABAWIYYAH] cha Abu Haatim-Allah amrehemu: “Ilikuwa katika kisa cha tembo, kwamba alikuweko mfalme katika nchi ya Yemen aliye pigana na wakaazi wake akawashinda na kuikalia kimabavu.

Asili yake mfalme huyo ni Uhabeshi, akiitwa Abraha. Huyo alijenga kanisa kubwa katika mji wa Sanaa akaliita Al-Qulais na akadai kwamba ataihamishia hapo Hija ya Waarabu. Na akaapa kwenda kuivunja Al-Ka’aba. Kusikia hivyo akatoka mmojawapo wa wafalme wa Himyari na watu wake wanao mtii, akiitwa Dhu Nafar, akapambana naye. Abraha akamshinda na kumtwaa mateka.

Alipo letwa mbele yake, Dhu Nafar akamwambia: Ewe mfalme! Usiniue! Kwani kutokuniua ni bora kwako kuliko kuniua. Akaacha kumuua na akamfunga kamba, kisha akaendelea na safari yake akiikusudia Al-Ka’aba.

Hata alipo karibia kwenye miji ya ukoo wa Khath’am, akatokewa na Nufail bin Habiib na watu wa makabila ya Yemen walio jikusanya kwake, wakapambana naye (Abraha), akawashinda na kumtwaa mateka Nufail.

Nufail akamwambia: Ewe mfalme! Hakika mimi ni mjuzi, ninaijua vema ardhi ya Waarabu, basi usiniue (huenda nikakuongoza njia). Na hii mikono yangu naitoa kwa usikivu na utiifu wangu na wa watu wangu kwako. Akaacha kumuua, akatoka nae akimfahamisha njia.

Hata alipo fika kwenye mji wa Twaifu, akatokewa na Masoud bin Mu’attab akiwa na watu wa kabila la Thaqiifu, akamwambia: Ewe mfalme! Sisi ni watumwa wako, hatuna upinzani na wewe na hakuna baina yetu kile ulicho kikusudia, hakika si vinginevyo wewe umeikusudia ile nyumba iliyoko Makka.

Sisi tutakupa mtu atakaye kufahamisha ilipo, wakampa muachwa huru wao aitwaye Abu Rughaal. Akatoka nao hata walipo fika mahala paitwapo Maghmasi (eneo lililo jirani na Makka kwenye njia ya Twaifu), akafa Abu Rughaal naye ndiye ambaye kaburi lake lilipigwa mawe.

Kutokea hapo Maghmasi, Abraha akamtuma mtu mmoja aliye kuwa akiitwa Al-Aswad bin Maqsoud kutwaa ngamia (wa watu wa Makka walio kuwa wakichunga). Watu wa Makka wakamkusanyia wanyama wakampa na akawakuta ngamia mia mbili wa (Mzee) Abdul-Mutwalib kwenye kitongoji cha Araak, nao akawaswaga.

Kisha Abraha akamtuma Hunaatwa wa ukoo wa Humeiri kwa watu wa Makka, akamwambia: Nenda ukawaulize kiongozi wao (ni nani), ukisha (mpata) mwambie ya kwamba mimi sikuja kwa ajili ya vita, ila nimekuja kuivunja nyumba hiyo (Al-Ka’aba). Hunaatwa akaenda mpaka akaingia Makka, akakutana na Abdul-Mutwalib bin Haashimu, akamwambia:

Hakika mfalme wetu amenituma nije kukuambia ya kwamba yeye hakuja kwa vita, ila kama mtaanza nyie, si jinginelo yeye amekuja kuivunja nyumba hii kisha aondoke zake. Abdul-Mutwalib akamwambia: Kwa nyumba hiyo sisi hatuna vita naye, tutamuacha yeye na nyumba hiyo. Ikiwa Allah atamuacha yeye na nyumba hiyo, sisi hatuna ubavu na hilo.

(Hunaatwa) akamwambia: Twende pamoja kwake (mfalme). Anasema (mpokezi): Akatoka pamoja naye mpaka wakafika kwenye kambi yao na Dhu Nafar alikuwa ni rafiki ya Abdul-Mutwalib, akamwendea na kumwambia: Ewe Dhu Nafar! Je, nyinyi mna uwezo wa kutukinga na hili janga lililo tujia? Akamjibu: Ana uwezo gani mtu mateka ambaye hana dhamana ya kutouawa asubuhi au jioni.

Lakini mimi nitamtuma mtu kwa Uneis; muendesha tembo, nitamuamrisha akufanyie wema auwezao kwa mfalme na akitukuze cheo na heshima yako mbele yake. Anasema (mpokezi): Akamtumia ujumbe wa wito Uneis, akamjia, akamwambia: Hakika huyu ni bwana (kiongozi) wa Makuraishi, mmiliki wa chemchem ya Makka inayo walisha watu wa nyandani na wanyama wa majabalini.

Na mfalme amewachukua ngamia wake mia mbili, basi ukiweza kumsaida naomba umsaidie, kwani hakika yeye ni rafiki yangu.

Uneis akaingia kwa Abraha, akamwambia: Ewe mfalme! Huyu ni bwana (kiongozi) wa Makuraishi, mmiliki wa chemchem ya Makka inayo walisha watu wa nyandani na wanyama wa majabalini, anaomba ruhusa ya kukuona. Nami napenda umruhusu, kwani yeye hakuja kukutia mtegoni wala kukupinga.

Basi akampa ruhusa, akaingia. Na Abdul-Mutwalib alikuwa ni mtu mtukufu, maridadi, mwenye muonekano mzuri. Abraha alipo muona akamuenzi na kumtukuza na hakupenda akae pamoja naye kwenye tandiko lake (la kifahari), akainuka akakaa kwenye busati naye akakaa hapo pamoja naye.

Abdul-Mutwalib akamwambia: Ewe mfalme! Hakika wewe umechukua mali zangu nyingi, basi nirudishie. Akamwambia: Nilipo kuona (ukiingia) ulinistaajabisha, lakini (sasa) nimekudharau. Akamuuliza: Kwa nini? Akamjibu: Mimi nimekuja kuivunja nyumba ambayo hiyo ndio dini yako na dini ya baba zako, tena ndio ngome yenu. Hukunizungumza kuhusu hiyo na badala yake unanizungumza ngamia wako mia mbili?! Akamwambia: Mimi ndiye bwana mmiliki wa ngamia hao na nyumba hii inayo mwenyewe ataizuia (isivunjwe). Akasema: Hawezi kunizuia kuivunja. Akamwambia: Basi hilo ni wewe na yeye. Abraha akaamuru apewe ngamia wake, akapewa.

Kisha akatoka Abdul-Mutwalib akawaambia Makuraishi khabari ile ya kuvunjwa kwa Al-Ka’aba na akawaamuru watawanyikie kwenye chochoro za majabalini. Abraha akapambaukiwa pale Maghmasi akiwa ameshajiandaa tayari kuingia Makka na akalipanga jeshi lake.

Akasogezewa tembo wake, akampakiza alivyo taka kuvichukua naye akiwa amesimama. Alipo mtukusa aondoke, hakutaharaki akasimama tu na alikaribia kukita chini akae kabisa. Wakampiga magongo kichwani, akagoma kwenda.

Wakaingiza magongo chini ya kwapa na miundi yake, lakini bado akagoma kwenda. Wakajaribu kumuelekeza upande wa Yemen, akaenda mbio. Wakamgeuzia upande wa Makka, akasimama. Tembo akaenda kwenye mojawapo ya majabali, hapo ndipo Allah akawaleta ndege kutokea baharini, kila ndege amechukua mawe matatu; mawe mawili miguuni na moja mdomoni.

Wanachukua mawe ukubwa wa tumba za dengu na mbaazi, wakisharuka usawa wa watu wale, huyaachia juu yao. Basi halimpati jiwe hilo mtu ila huangamia, na tukio hilo ndio kauli yake Allah Mtukufu pale alipo sema:

“Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo watenda wale wenye tembo? Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika? Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi. Wakiwatupia mawe ya udongo wa motoni. Akawafanya kama majani yaliyo liwa!”. Al-Fiil [105]:01-05

Na Allah akamshushia Abraha maradhi mwilini mwake, wakarejea mbio huku wakianguka njiani na Abraha akawa vinanyofoka na kudondoka chini vidole vyake, na kila kinapo dondoka kidole hutoka kibaba kizima cha usaha na damu. Akafika Yemen akiwa kama kifaranga cha ndege miongoni mwa walio salia katika watu wake, kisha akafa. [As-siiratun-nabawwiyah cha Abu Haatim, sah. 34-39]

Na ametaja Imamu Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-katika kitabu chake cha Sira kama alivyo nukuliwa na Ibn Hishaamu katika “As-siyar”: Ya kwamba Abdul-Mutwalib alikishika kizingiti cha mlango wa Al-Ka’aba na likasimama pamoja naye kundi la Makuraishi kumuomba Allah na kutaka awanusuru dhidi ya Abraha na jeshi lake. Abdul-Mutwalib akiwa ameshika kizingiti cha mlango wa Al-Ka’aba akasema maneno haya:

Ewe Mola wa haki! Hakika mja huzuia kilicho chake,

         Basi nawe izuie nyumba yako.

Basi usishinde kesho msalaba wao,

         Na muhali wao kuushinda muhali wako.

Na ikiwa utaawachia na kibula chetu,

         Basi amuru ulitakalo Wewe.

Kisha Abdul-Mutwalib akakiachia kizingiti cha mlango wa Al-Ka’aba na akaondoka yeye na Makuraishi alio kuwa nao, wakaenda kwenye pachipachi za majabalini. Wakajificha huko, wakisubiri kuona Abraha atafanya nini atakapo ingia Makka. Halafu tena baada ya hayo, akaelezea namna Abraha alivyo angamizwa yeye na jeshi lake. [As-siiratun-Nabawiyyah cha Ibn Hishaam]

Hilo ndilo darsa letu juma hili, tunatumai kwa uwezo wake Allah, tutakuwa tunaendelea vizuri pamoja na utakuwa umeshapata taswira ya kinacho lengwa na darsa hili.

Tumuombe Allah atupe nguvu za kuzidi kudarisishana na kuifahamu Sira ya Bwana Mtume ili itufikishe kwenye kumjua, nako kutupeleke kwenye kumpenda ambako kutatuzawadia kumfuata, na huo ndio uwokovu pekee. Allah atukutanishe juma lijalo kwa uwezo wake, tukiwa na afya tele ya mwili, akili na imani. Mpaka muda huo tunasema: Maa Salaama!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *