KATAZO LA WIKI (JUMA LA 83)

Ubakhili/unyimi kwa upande mmoja na ubadhirifu kwa upande wa pili si katika tabia za muislamu, aslani. Allah amekuchagua miongoni mwa waja wake wengi akakunjulia riziki, unacho cha kukutosha na ziada.

Kwa nini lakini hujitangulizii akhera leo ukiwa bado hai na una uwezo wa kutoa, kwa kutoa kile kinacho isha kama utakavyo isha wewe mmliki wake, ili ukavune mbele ya Mola wako kile kinacho dumu milele pamoja nawe?! Haya kutoa hutoi na badala yake unafanya ubadhirifu, kwa manufaa ya nani?!

Ni kheri kwako ikiwa utakubali ya kwamba kutoa ni kwa manufaa/faida yako mwenyewe na kufanya ubadhirifu ni khasara na majuto yasiyo nufaisha.

Hebu ishi na neema aliyo kupa Mola wako kwa kuufuata muongozo wake huu: “WALA USIUFANYE MKONO WAKO KAMA ULIO FUNGWA SHINGONI MWAKO, WALA USIUKUNJUE WOTE KABISA, UTABAKI UKILAUMIWA MUFLISI”. Al-Israa [17]:29

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *