KATAZO LA WIKI (JUMA LA 74)

Jamani, hayo macho uliyo pewa bure na Mola wako na ambayo wenzako wengi tu hawakupewa, Allah amewafanya kuwa ni vipofu kwa hekima anazo zijua Yeye mwenyewe, hayo tambua ni neema uliyo tunukiwa na Mola wako. Sasa kwa nini humshukuru Mola wako kwa neema hiyo?! Kwa nini unaitumia vibaya neema hiyo kwa kuangalia yale aliyo kukataza Mola Muumba wako kuyaangalia?! Hivi unapata faida gani pale unapo itumia neema hiyo kuangalia uchi wa mwenzako?! Acha, hilo halifai na tena halipungui kuwa ni kuikufuru neema hiyo ya Mola wako. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuasa: “Mwanamume asiangalie uchi wa mwanamume mwenzake na wala mwanamke asiangalie uchi wa mwanamke mwenzake. Na wala mwanamume asijifunike shuka moja na mwanamume mwenzake na wala mwanamke asijifunike shuka moja na mwanamke mwenzake”. Tirmidhiy [2793], Ibn Maajah [661] & Ahmad [03/63]-Allah awarehemu.

SWALI LA WIKI

SWALI: Mwanaadamu hupitia hatua mbali mbali katika afya yake, kwa sababu ama ya utu uzima au maradhi imefikia hawezi kuzuia mkojo, unamtoka pasina hisia. Nini hukumu ya sheria kwa mtu huyu katika utekelezaji wa ibada zake khususan swala?

JIBU: Katika jumla ya mambo maalumu ya dini ya Uislamu ambayo ni dini ya maumbile, ni kwamba hukumu zake zinachukuzana na maumbile na haja za mwanaadamu. Na miongoni mwa sura za wepesi katika hukumu za sheria ya Kiislamu, ni kwamba mtu anaye sumbuliwa na tatizo la kutokwa na mkojo (salasuli bauli); hana uwezo wa kuuzuia mkojo, swala yake inasihi kwa kufuata maelekezo yafuatayo:

  1. Asitie udhu ila tu pale anapotaka kuanza kuswali.
  2. Afunge utepe mahala unapotoka mkojo au akiweza avae kitambaa mfano wa nepi.
  3. Atwaharishe mahala unapotoka mkoja na atie udhu mpya kila anapotaka kuswali swala ya faradhi.

Ukunjufu wa mas-ala haya utaupata kwenye vitabu vya Fiq-hi.

Allah ndiye Mjuzi mno.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *