HEDHI

a) MAANA YA HEDHI

Hedhi katika lugha ya kiarabu, maana yake ni KUCHURIZIKA. Ama hedhi kwa mtazamo wa sheria ni DAMU YA MAUMBILE yaani damu hii ni sehemu/ni katika jumla ya maumbile ya mwanamke, mwanamke kaumbwa hivyo kwa lengo maalum.

Damu hii kutoka ndani kabisa ya tumbo la uzazi kila mwezi baada ya mwanamke kutimiza kwa uchache umri wa miaka tisa

b) DALILI YAKE

Dalili na ushahidi juu ya kuwa hadhi huwajibisha josho la kisheria ni Qur-ani Tukufu na sunnah(hadithi).

Ama katika Qur-ani ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu : “NA WANAKUULIZA JUU YA HEDHI, WAAMBIE HUO NI UCHAFU. BASI JITENGENI NA WANAWAKE WAKATI WA HEDHI (zao). WALA MSIWAKARIBIE MPAKA WATWAHARIKE. WAKISHATWAHARIKA BASI WAENDEENI KATIKA PALE ALIPOKUAMRISHENI ALLAH…” [2.222].

Ama dalili yake katika sunnah ni kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie kumwambia Fatmah Bint Abiy Hubayshi Allah amuwiye radhi-: “Itapokujia hedhi , basi acha kuswali na itakapomalizika (kutoka) basi ikoshe damu (twaharisha) na uswali” Bukhaariy na Muslim.

c) MUDA WA HEDHI:

Tunakusudia kwa ibara (Muda wa hedhi) kile kipindi ambacho mwanamke hutumika yaani huwamo hedhini.

Kipindi hiki tunaweza kukigawa katika sehemu tatu,kama ifuatavyo:-

  • Kipindi kifupi;
  • Kipindi kirefu na
  • Kipindi cha ghalibu (ada)
KIPINDI KIFUPI

Hii ndio muda wa chini kabisa wa kutoka damu ya hedhi hiki ni kipindi cha masaa ishirini na nne (24). Hii inaamaanisha kuwa mwanamke anaweza kuingia hedhini mchana na usiku wake tu, kisha damu ikakatika

KIPINDI KIREFU

Huu ndio muda wa juu kabisa wa kutoka damu ya hedhi. Hiki ni kipindi cha siku kumi na tano (15), mchana na usiku

KIPINDI CHA GHALIBU

Huu ndio muda wa ada na desturi kwa wanawake walio wengi, yaani wanawake wengi hutumika katika kipindi hiki. Huu ni muda wa siku sita au saba.

Muda wa chini wa twahara, yaani kipindi cha chini ambacho mwanamke anakuwa katika twahara ni siku kumi na tano(15). Hakuna ukomo (limit) wa wingi wa twahara kwani inawezakana kabisa mwanamke asipate hedhi kwa muda wa mwaka, miaka miwili au miaka kadhaa na hili limethibiti kwa majaribio.

Mwanamke atakapoiona damu chini ya kipindi kifupi cha hedhi yaani chini ya masaa ishirini na nne au aliiona damu baada ya kule kipindi kirefu cha hedhi, yaani baada ya siku kumi na tano, damu hii itazingatiwa kisheria kuwa ni damu ya ISTIHAADHA na sio damu ya hedhi

d) NINI ISTIHAADHA?

Istihaadha ni damu ya ugonjwa damu hii hutoka katika mshipa ulio ndani kabisa ya tumbo la uzazi. Damu hii hutengua udhu lakini haiwajibishi josho kama ilivyo kwa damu ya hedhi.

Kadhalika damu hii haitoi fursa ya kuacha kuswali na kufunga. Mwanamke mwenye maradhi haya ya Istihaadha anatakiwa aioshe damu na afunge utepe mahala itokapo, kisha atawadha na halafu aswali.

Imepokelewa riwaya kutoka kwa Fatmah Bint Abiy Hubaysh –Allah amuwiye radhi –kwamba yeye alikuwa akitokwa na istihaadha. Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukiae- akamwambia: “Ikiwa ni damu ya hedhi, basi itakuwa ni damu nyeusi ijulikanayo. Itakapokuwa hivyo, basi acha kuswali, ikiwa ni nyingine basi tawadha na uswali, hakika si vingenevyo huo ni mshipa”. Abu Daawoud.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *