Ziko hukumu na lazima zinazo wajibishwa na eda ambazo tunazibainisha kama ifuatavyo:
Mosi: Eda ya talaka/kuachwa:
Atakapo kuwa mwanamke anamkalia eda mume wake, eda ya kuachwa. Basi ama kuachwa kwake huko kutakuwa ni talaka rejea au talaka baini. Angalia:
(A) Akiwa anakaa eda kutokana na talaka rejea, eda yake hiyo inaandamiwa na hukumu zifuatazo:
1. Uwajibu wa maskani (makazi) uko juu ya mume na lililo bora ni kuwa yale yale maskani ya talaka yake yakiwa yanachukuzana nae. Na hakuna kizuizi chochote cha kisheria kinacho mzuia kukaa eda humo na mfano wa hilo.
2. Uwajibu wa kupata gharama za kujikimu kwa aina zake; yaani chakula, nguo na mengineyo. Pasina kuangalia ni mjamzito au si mjamzito, hayo ni kwa sababu ya kusalikia kwa mamlaka/utawala wa mume juu yake. Na kufungika kwa mke chini ya hukumu yake kwa sura ya kumkinikia kumrejea muda wa kuwa bado yumo ndani ya eda.
3. Kunamuwajibikia mke kulazimikiana na maskani yake, asitoke humo ila kwa dharura. Na dalili ya hukumu tatu hizi, ni kauli yake Allah Ataadhamiaye: “WAWEKENI HUMO HUMO MNAMO KAA NYINYI KWA KADIRI YA PATO LENU, WALA MSIWALETEE MADHARA KWA KUWADHIKI. NA WAKIWA WANA MIMBA, WAGHARIMIENI MPAKA WAJIFUNGUE…” [65:06]
Na amesema Atukukiaye: “…MSIWATOE KATIKA NYUMBA ZAO, WALA WASITOKE WENYEWE, ILA WAKIFANYA JAMBO LA UCHAFU ULIO WAZI…” [65:01]
4. Kunamuharimikia kujitokezea kwenye posa za wanaume, kwa kuwa yeye bado amefungika na mume wake na yeye ndiye mwenye haki zaidi kwake kuliko hao wanaume wengine: “…NA WAUME ZAO WANA HAKI YA KUWAREJESHA KATIKA MUDA HUO, KAMA WAKITAKA KUFANYA SULUHU…” [02:228]
(B) Akiwa anakaa eda kwa sababu ya kuachwa kwa talaka baini, naye wakati huo ama atakuwa ni mjamzito au si mjamzito. Angalia, akiwa ni mjamzito, talaka hiyo inaandamiwa na hukumu zifuatazo:
1. Uwajibu wa maskani ya mke, uko juu ya mume, na dalili ya hili ni kauli yake Allah Ataadhamiaye: “EWE NABII! MTAKAPO WAPA TALAKA WANAWAKE, BASI WAPENI TALAKA KATIKA WAKATI WA EDA ZAO. NA FANYENI HISABU YA EDA. NA MCHENI ALLAH, MOLA WENU MLEZI. MSIWATOE KATIKA NYUMBA ZAO, WALA WASITOKE WENYEWE, ILA WAKIFANYA JAMBO LA UCHAFU ULIO WAZI…” [65:01]
2. Kupata chakula kwa aina zake tofauti na dalili ya hili ni kauli yake Allah Atukukiaye: “…NA WAKIWA WANA MIMBA, WAGHARIMIENI MPAKA WAJIFUNGUE…” [65:06]
3. Kulazimikiana na nyumba anamo kalia eda, asitoke humo ila kwa haja, kama vile kuhitajia kujipatia chakula na mfano wa hilo. Au anahitajia kwenda kuuza vitu/bidhaa zake ili apate chumo humo na kukawa hakuna mtu wa kumuangalia na kumtimizia mahitaji yake hayo. Au alikuwa ni muajiriwa katika kazi fulani na wala hapati ruhusa ya kukaa nyumbani kwake mpaka kwisha kwa eda yake. Au alikuwa analazimika kujiondoshea upweke wake kwa kwenda kuongea kwa jirani yake. Hakuwi ni haramu huko kutoka kwake nyumbani mwake kwa ajili ya mambo kama hayo.
Ama dalili ya kuzuia kutoka pasina haja, ni kauli yake Allah Atukukiaye: “…MSIWATOE KATIKA NYUMBA ZAO, WALA WASITOKE WENYEWE…”
Ama dalili ya kujuzu kutoka kwa haja: Imepokewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-amesema: Alitalikiwa haloo yangu (mama mdogo/mkubwa), basi akataka kwenda kuishughulikia mitende yake, mtu mmoja akamkataza kutoka. Basi akamuendea Mtume-Rehema na Amani zimshukie-(Mtume) akasema: “Kwani usitoke, toka ukaitengeneze mitende yako, kwani hakika wewe huenda ukatoa sadaka au ukafanya wema”). Muslim [1483]-Allah amrehemu.
Na akiwa si mjamzito, talaka yake itaandamiwa na yote yaliyo tajwa katika kipengele kilicho pita, ILA gharama za kujikimu kwa aina zake zote; yaani chakula, mavazi na mengineyo. Hayo hayamthibitikii na hakika kinacho muwajibikia kupata ni maskani tu na kunamuwajibikia kuyalazimu. Na dalili ya hili: Ni kile kisa cha Fatimah Bint Qaysi pale alipo talikiwa na mume wake talaka moja iliyo kuwa imebakia: Kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia: “Huna matumizi ila uwe mjamzito”. Abu Daawoud [229]-Allah awarehemu.
Pili: Eda ya kufiwa:
Akiwa mwanamke anakaa eda kutokana na kufiwa na mume wake, zimepasa kwa upande wake hukumu zifuatazo:
1. KUMUONEA MAJONZI MUMEWE: Kwa kujizuia na mionekano ya pambo na manukato. Kwa hivyo basi,
F Asivae nguo zenye rangi nzuri, yenye kuvutia,
F Asijipake wanja,
F Asitumie chochote katika rangi za kujirembea; yaani asipake rangi ya mashavu na midomo wala poda.
F Asijipambe kwa pambo lolote, liwe ni la dhahabu, fedha au mengineyo.
Akifanya lolote katika haya, basi atapata dhambi. Dalili ya hayo, ni kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Si halali kwa mwanamke anaye muamini Allah na siku ya mwisho, kumuonea majonzi maiti zaidi ya siku tatu. Ila kwa mume, (atamuonea majonzi) kwa miezi minne na siku kumi”. Bukhaariy [5024] & Muslim [1486-1489]-Allah awarehemu.
Hadithi hii imefahamisha uharamu wa mwanamke kutomfanyia majonzi asiye mume, na uwajibu wake kwa mume kwa muda wa miezi minne na siku kumi. Na Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ameruhusu kudhihirisha huzuni na ameamrisha kufanya taazia ndani ya siku tatu tu. Kwa sababu nafsi haziwezi kuwa na subira ndani ya siku hizo na kuficha huzuni.
Imepokewa kutoka kwa Ummu Atwiyah; Muanswari-Allah amuwiye radhi-amesema: “Tulikuwa tukikatazwa kumuombolezea maiti zaidi ya siku tatu ila kwa mume miezi minne na siku kumi. Wala tusipake wanja, wala tusijitie manukato, wala tusivae nguo za rangi rangi ila nguo za mfumo. Na tuliruhusiwa wakati wa kutwaharika, atakapo koga mmoja wetu kutokana na hedhi yake, kutia kipande kidogo cha manukato. Na tulikuwa tukikatazwa kusindikiza jeneza”. Bukhaariy [307] & Muslim [938]-Allah awarehemu.
2. KUNAMUWAJIBIKIA KULAZIMIKIANA NA NYUMBA ANAMOKALIA EDA: Asitoke humo ila kwa haja kama zile tulizo tangulia kuzitaja kwa yule akaae eda ya kuachwa. Imepokewa kutoka kwa Zaynab Bint Ka’ab Bin Ujrah: Kwamba Furai’ah Bint Maalik Bin Sinaan-nae ni dada yake Abu Said Al-Khudriy-Allah amuwiye radhi-alimwambia kwamba yeye alikwenda kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kumuomba arejee kwao kwa Baniy Khudrah. Na kwamba mume wake alitoka kwenda kuwatafuta watumwa wake walio toroka, hata alipo kuwa karibu na kurudi, akawakuta, wakamuua. Anasema: Nikamuomba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-nirudi kwetu, kwa kuwa mume wangu hakuniachia maskani anayo yamiliki wala matumizi. Mtume wa Allah akasema: “Naam”. Anasema (Furai’ah): Nikaondoka zangu, hata nilipo kuwa katika chumba (au msikitini), Mtume wa Allah akaniita – au aliamuru niitwe, nikaitwa – akasema: “Umesemaje?” Akasema (mpokezi): Nikamkariria kile kisa nilicho kwisha mtajia kuhusiana na suala la mume wangu. Akasema (Mtume): “Kaa katika nyumba yako mpaka muda umalizike”.
Anasema: Basi nikakaa eda humo kwa miezi minne na siku kumi.
Anasema: Uthman-Allah amuwiye radhi-alipo kuwa khalifa, alinitumia ujumbe wa kuniita, basi akaniuliza juu ya hilo, nikamuelezea. Naye akalifuata na akahukumu kwalo”. Tirmdhiy [1204], Abu Daawoud [2300] & wengineo-Allah awarehemu.
Ama yale wanayo yasawirisha wengi katika watu awami (watu wa kawaida, wasio na maarifa ya hukumu za sheria), ya kwamba hakumjuzii mueda (mwanamke aliye edani) kuzungumza na mtu yeyote. Na kwamba hakumjuzii mtu yeyote kuisikia sauti yake, madai hayo hayana asili/msingi wowote katika dini. Na hakika si vinginevyo, hukumu ya kuzungumza ndani ya eda na nje ya eda, ni moja.
vi. Ufupilizo katika hukumu za eda:
Mpetwa petwa (mukhtasari) wa maneno, ni kwamba aina zote za eda zinashirikiana katika baadhi ya hukumu, ambazo ni:
F Uharamu wa kutoka kwenye makazi anamo kalia eda mwanamke ila kwa haja.
Halafu tena mwanamke anaye kaa eda ya kufiwa anapwekeka na hukumu ya peke yake, nao ni ule wajibu wa kumuonea majonzi marehemu mume wake. Na hilo ni kwa kujiepusha na manukato na pambo kwa namna tuliyo tangulia kuielezea.
Kama alivyo na hukumu pweke, mueda wa talaka rejea na yule wa talaka baini akiwa ni mjamzito, wajibu wa kupata maskani na aina zote za matumizi.
Na anapwekeka mueda wa talaka baini kama si mjamzito, na wajibu wa kupata maskani tu, bila ya baki ya matumizi mengine.
vii. Hitimisho:
Tunakhitimisha somo hili la eda kwa kubainisha suala muhimu, nalo ni ule uharamu wa wanawake kuwaombolezea wasio waume; yaani ndugu/jamaa zao, wanawake na wanaume. Huo ni uombolezaji mbaya unao chukua sura kongwe ya jahilia ambapo mwanamke hulazimu kuvaa nguo nyeusi. Au kuvaa nguo inayo shabihiana na nyeusi, kama bluu kibichi (dark blue) ili kuonyesha huzuni yake kwa jamii. Pia hujiepusha kwenda kwenye sehemu za hadhara, kujitokeza kwenye misimu ya sikukuu na minasaba yake. Mwanamke atabakia katika hali hiyo kwa mwaka mzima au zaidi kidogo.
Hakika mlazama (lazima ya taklifu) huu, haukuwa ila ni upingaji wa wazi wa amri ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-iliyo kuja katika hadithi yake sahihi, iliyo wazi: “Si halali kwa mwanamke anaye muamini Allah na siku ya mwisho, kumombolezea maiti kwa zaidi ya siku tatu ila kwa mume miezi minne na siku kumi”. Bukhaariy [5024] & Muslim [1486-1489]-Allah awarehemu.
Na imepokewa kutoka kwa Zainab Bint Abi Salamah amesema: Niliingia kwa Zainab Bint Jahshi-Allah amuwiye radhi-pale alipo fiwa na kaka yake. Basi akaagizia manukato, akajitia kisha akasema: Wallah mimi sina haja na haya manukato ila tu ni kwamba mimi nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Si halali kwa mwanamke anaye muamini Allah na siku ya mwisho, kumombolezea maiti kwa zaidi ya siku tatu ila kwa mume miezi minne na siku kumi”.