Jambo lolote lile katika maisha ya kila siku ya Muislamu linaangukia kwa mujibu na mtazamo wa sheria katika mafungu yafuatayo ya hukumu:-
Faradhi/Wajibu
Sunnah
Haramu
Mubah
Makuruuh
Hizi ndizo hukumu tano zinazoitawala sheria ya kiislamu, na ifuatayo ni maana na ufafanuzi mdogo wa kila hukumu:-
Faradhi au Wajibu ni jambo ambalo mtu baleghe, mwenye akili timamu amelazimishwa na sheria kulitenda.
Mtu mwenye sifa hizo tulizozitaja akilitenda la faradhi kama vile swala, funga n.k. kwa kumtii Mola wake hupata thawabu na akiacha kutenda bila ya udhuru wowote unakubalika kisheria anastahiki kupata dhambi na adhabu ya Mola.
Sunna kwa mtazamo wa fiq-hi ni kinyume cha faradhi. Kwa hivyo basi sunnah ni jambo ambalo sheria haikumlazimisha mtu kulitenda bali imempa khiyari kutenda au kutotenda.
Mfano wa sunnah ni kama vile kuanza kutoa salamu, kuwapa sadaka masikini, kufunga Al-khamisi na Jumatatu na kadhalika.
Atakayelitenda jambo la sunnah atalipwa thawabu na atakayeacha hatopata dhambi wala kuadhibiwa.
Haramu ni kila jambo ambalo sheria imekataza kabisa kulitenda kama vile kuiba, kusema uwongo, kunywa pombe na kadhalika.
Mtu aliye baleghe na mwenye akili timamu akilitenda lililoharimishwa kwa kuvunja amri ya Mola atastahiki kupata dhambi na adhabu na akiacha kutenda haramu kwa kufuata amri ya Mola atapata thawabu.
Mubaah ni jambo ambalo sheria haikulazimisha mtu kulitenda na wala haikumkataza kulitenda. Mfano wa mubaah ni kama vile kuvaa nguo nzuri mno au kula vyakula vizuri vizuri. Hapana thawabu wala dhambi ndani yake.
Mtu akitenda jambo la Mubaah kama vile kula na akatia nia ya kupata nguvu ya kufanya ibada, atapata thawabu na kinyume chake akinuia kwa jambo hilo hilo la Mubaah kumuasi Mwenyezi Mungu basi atapata dhambi.
Makuruuh ni kila jambo ambalo linachukiza kulitenda kwa mtazamo wa sheria. Hastahiki mtu kupata adhabu ya Mola kwa kulitenda bali akiacha atapata thawabu.