HIMA YA MAKURAYSHI KATIKA VITA HIVI ILIKUWA NI KUMUUA MTUME

Makurayshi wanne walifunga ahadi ya kumuua Mtume wa Allah katika vita hivi na mushrikina wenzao walilitambua hilo.

Hawa walikuwa ni Abdullah Ibn Shihaab, Utbah Ibn Abuu Waqaasw, Amrou Ibn Qamiah na Ubayyi Ibn Khalaf.

Huyu Abdullah Ibn Shihaab alimpasua Bwana Mtume katika paji lake la uso, damu zikamchuruzika kiasi cha kuzilovya ndevu zake.

Utbah Ibn Abuu Waqaasw katika harakati zake za kutekeleza ahadi aliyofunga na wenzake, yeye alimpiga Mtume wa Allah katika mdomo wake wa chini.

 Pigo la shetani huyu lilivunja jino la mbele la upande wa kulia la Mtukufu Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.

Amrou Ibn Qamiah, yeye alijaribu kuifungua ahadi aliyoifunga na wenzake kwa kumpiga tayani Mtume wa Allah.

Pigo hili lilimsababishia Bwana Mtume kuchomwa na vijimsumari viwili vilivyokuwa vimeshikilia kifuniko cha chuma alichokuwa amekivaa usoni.

Muovu huyu hakukomea hapo, bali alimpiga Bwana Mtume upanga wa bega, pigo lililomuacha akiangukia shimoni na kuchubuka magoti yake na uvumi kuenea kuwa Mtume kauawa.

Sayyidina Aliy Ibn Abuu Twaalib akamshika mkono na Sayyidina Twalhah Ibn Ubeidillah akamuinua mpaka akasimama na kulingana sawa.

Maumivu ya pigo la shetani huyu begani kwa Mtume yalimchukua mwezi mzima. Ubayyi Ibn Khalaf, yeye alimsukumiza Mtume wa Allah huku akimwambia:

“Ewe muongo utakimbilia wapi?”

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akajihami dhidi ya shetani huyu kwa kumchoma mkuki wa shingo.

Akayumbayumba juu ya farasi wake akitoa mlio mithili ya ule wa ng’ombe dume, akafia njiani wakati makafiri walipokuwa wakirejea Makah.

Uvumi wa kuuawa kwa Mtume wa Allah ukamalizika baada ya waislamu kuyakinisha kuwa yungali hai.

Hapo ndipo waislamu wakamzunguka na kumuondoshea kiwingu cha maadui waliojizatiti kumuua. Mtu wa mwanzo kumtambua Bwana Mtume alikuwa ni Ka’ab Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-kama anavyosimulia mwenyewe:

“Niliyatambua macho yake yaliyokuwa yaking’ara nyuma ya kifuniko cha chuma alichovaa usoni. Nikaita kwa sauti ya juu: Enyi kusanyiko la waislamu! Furahini, Mtume wa Allah huyu hapa. Mtume wa Allah akaniashiria kunyamaza”.

Kundi la waislamu likamkusanyikia Bwana Mtume, wakamchukua na kumpeleka katika uchochoro ulio baina ya miamba ya jabali Uhud. Bwana Mtume akajificha hapo na baadhi ya maswahaba waliojeruhiwa vibaya.

Akiwa hapo alijaribu kupanda juu ya mwamba kushuhudia mapambano yanavyoendelea, lakini hakuweza kutokana na kuishiwa nguvu kutokana na kutokwa na damu nyingi. Twalhah Ibn Ubeidillah-Allah amuwiye radhi-akambeba na kumpandisha mwambani hapo.

 

WANAWAKE WA KIKURAYSHI WAZIKATAKATA MAITI ZA WAISLAMU.

Kwa kipigo hiki kilichowashukia waislamu katika vita hivi vya Uhud, mushrikina waliona kuwa wamejilipia kisasi kutokana na kipigo kilichowapata katika vita vya Badri.

Wakaviponya vidonda vya nafsi zao kwa kuuawa Mtume wa Allah kama walivyodhania na hili likawaridhi kuwa ni ngawira tosha.

 Vita vikaanza kupoa makali yake na kuzimika harara lake. Hao mushrikina wakaanza kuondoka katika uwanja wa mapambano kurejea kambini kwao na kuanza kujishughulisha na mazishi ya watu wao waliouliwa vitani.

Wakati wanarejea kambini ndipo wanawake wao wakaitumbua nyongo ya chuki iliyomo vifuani mwao kwa kuzikatakata maiti za mashahidi.

Wakazikata pua na masikio ya mashahidi hawa-Allah awawiye radhi. Hind Bint Utbah ndiye aliyefanya unyama mkubwa kuliko wanawake wale wote.

 Yeye hakuridhika na kukata pua na masikio  ya Ami yake Mtume; Sayyidina Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib-Allah amuwiye radhi.

Huyu alijasiri kulitumbua tumbo la Sayyidina Hamzah, akalitoa ini lake na kuanza kulitafuna kwa meno yake, huku akionekana kufura kwa hasira na chuki.

Abuu Sufyaan; mumewe Hind akapita baina ya mashahidi akijaribu kuwatambua.

Alipomkuta Sayyidina Hamzah amelala chini akiwa ni miongoni mwa mashahidi, akampigapiga mfupa wa taya lake kwa kitako cha mkuki wake huku akimsimanga kwa kusema:

“Onja jazaa ya kuwakata pande jamaa zako (kuwatupa mkono)”.

Al-Hulaysi; kiongozi wa Wahabeshi alimuona akifanya kitendo hiki, akamkemea asifanye kitendo hicho cha kinyama kwa mwana wa ami yake akiwa maiti.

Abuu Sufyaan akaona amefedheheka kutokana na kitendo chake hicho cha aibu. Akamsihi   Al-Hulaysi amsitiri asiitangaze khabari hiyo mbaya inayoweza kushusha hadhi yake mbele ya watu.

 

ABUU SUFYAAN AMTAFUTA BWANA MTUME.

Hima ya Abuu Sufyaan ilikuwa ni kumkuta Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwa ni miongoni mwa waislamu waliouliwa.

Alipomkosa akaanza kuingiwa na shaka ni kweli wamefanikiwa kumuua kama ilivyotangaa masikioni mwa wengi wao kama si wote.

Akaelekea upande alikojificha Bwana Mtume na baadhi ya maswahaba wake na akaanza kupaaza sauti:

“Je, Muhammad yuko kwenu? Je, Ibn  Abiy Quhaafah (Abuu Bakri) yuko huko? Je, mnaye Ibn Al-Khatwaab?” Bwana Mtume akawakataza maswahaba wake wasimjibu, alipokosa jawabu akawaendea mushrikina wenzake na kuwaambia: “Ama watu hawa kwa yakini mmetoshewa”.

 Sayyidina Umar-Allah amuwiye radhi-kusikia kauli hiyo akashindwa kujizuia na kuamua kumjibu, akamwabia:

“Wallah umeongopa, ewe adui wa Allah! Kwa yakini Allah amekubakishia likuudhilo (likukeralo)”.

Abuu Sufyaan akiwa kama mtu anayetaka kuomba radhi kutokana na kitendo kichafu kilichofanywa na wanawake wao, akasema:

“Mtawakuta watu wenu waliouliwa wamekatwakatwa viungo, mimi sikuliamuru hilo lakini pia silioni kuwa ni baya”.

Kisha akajikosoa mwenyewe kutokana na kauli yake hii ambayo aliiona kama ni kuwanyenyekea mahasimu wake, kwa kusema:

“Ee kitendo kizuri kilioje! Hakika vita ni mghalaba (ushindani), mtukuzeni hubal{1}. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema kuwaambia maswahaba wake:

“Mwambieni Allah ndiye aliye Mtukufu kuliko vyote”.

 Abuu Sufyaan akaendelea kutamba: “Utukufu ni wetu, nyie hamna utukufu”.

Bwana Mtume akasema: “Mwambieni Allah ndiye Mola na Mlinzi wetu, nanyi hamna Mola wala Mlinzi”.

Abuu Sufyaan akaendelea kusema: “Siku ya leo ni fidia ya siku ya Badri”.

Mtume wa Allah akasema: “Mwambieni hazilingani (siku mbili hizo), wauliwa wetu wako peponi na wauliwa wenu wako motoni”. Abuu Sufyaan akapiga mayowe: “Bila shaka miadi yenu ni Badri mwaka ujao (tukutane hapo muone kazi yetu)”.

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Mwambieni, hiyo ni miadi baina yetu nasi (haina shaka)”.

________________________________________________________

{1} Huyu ni mungu-sanamu aliyekuwa ndani ya Al-Ka’aba wakimuabudu.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *