Imesuniwa kutawadha katika hali nyingi, miongoni mwa hali ambazo muislamu amesuniwa atawadhe:
1. Wakati wa kumdhukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwani Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – alikuwa akipenda kumdhukuru Mola wake katika hali ya twahara.
Ni bora ikafahamika kwamba Bwana Mtume alikuwa akimdhukuru Mola wake katika hali zote, akiwa amekaa au amesimama, akiwa ana udhu au hana, akiifanyia kazi kauli ya Mola :
“NA LIKUMBUKE (litaje) JINA LA MOLA WAKO ASUBUHI NA JIONI” [76:25].
Udhu ni silaha ya muumini, kwa hivyo ni vema saa zote akawa anatembea na silaha yake hiyo, khasa khasa wakati wa kumdhukuru Mola wake.
2. Wakati wa kulala. Zimepokelewa hadithi nyingi zinazoeleza ubora wa mtu kulala akiwa na udhu. Miongoni mwa hadithi hizo ni hii iliyopokelewa na Albaraai bin Aazib – Allah amuwie radhi – amesema :
Aliniambia Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – “Unapokiendea kitanda chako (unapotaka kulala) tawadha udhu wako wa swala, kisha ulalie upande wa kulia, halafu useme :
ALLAHUMMA INNIY ASLAMTU NAFSIY ILAYKA, WAWAJJAHTU WAJ-HIY ILAYKA, WAFAWWADHTU AMRIY ILAYKA, WA ALJA-TU DHWAHRIY ILAYKA RAGHBATAN WA RAHBATAN ILAYKA, LAA MALJAA WALAA MANJAA MINKA ILLAA ILAYKA. ALLAHUMMA AAMANTU BIKITABIKAL-LADHIY ANZALTA, WABINABIYYIKAL-LADHIY ARSALTA” Bukhariy.
3. Ni sunna kutawadha kwa mtu aliye na janaba anapotaka kula, kunywa au kulala. Imepokelewa kutoka kwa Ammaar bin Yaasir –Allah amuwie radhi – kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
“amemruhusu mwenye janaba anapotaka kula, kunywa au kulala atawadhe udhu wake wa swala (ndipo ayafanye hayo yaliyotajwa)” Tirmidhiy.
Hii ni iwapo haikumwepesikia kuoga mapema, na ikiwa ni wepesi, basi ni bora akaharakia kuoga, ZINGATIA.
4. Imesuniwa kutia udhu kabla ya kukoga josho la janaba. Imepokewa kutoka kwa Bi Aysha – Allah amuwie Radhi – amesema : Alikuwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie –
“anapotaka kukoga, huanza kwa kuosha mikono (vitanga) vyake, halafu humimina maji kwa mkono wake wa kulia na huukosha utupu wake kwa mkono wa kushoto. Halafu hutawadha udhu wake wa swala, kisha ndipo hukoga baada yake” Bukhaariy na Muslim.
5. Wakati wa kumbeba maiti. Imepokelewa katika hadithi tukufu : “Mwenye kumuosha maiti na mwenye kumbeba (pia) akoge”
6. Wakati mtu aghadhibikapo sana, ni sunnah akatawadhe kwa sababu udhu husaidia kuzima mfumuko na mchemko wa ghadhabu na humrejesha mtu kwenye hali ya utulivu.
Imepokelewa kutoka kwa Atwiyah Al-Aufaa kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – amesema :
“Bila ya shaka ghadhabu hutokana na shetani, na huyo shetani amuembwa na moto na hakika si vinginevyo moto huzimwa na maji. Basi ashikwapo na ghadhabu mmoja wenu na akatawadhe” Abuu Dawoud.
7. Ni sunna kujadidi udhu (kutawadha udhu juu ya udhu) kwa kila swala. Tunasoma katika hadithi tukufu :
“Lau si kuwaonea taabu umati wangu ningaliwaamrisha kutawadha kwa kila swala na kupiga mswaki kwa kila udhu”.
Ilikuwa ni ada ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kutawadha kwa kila swala na baadhi ya nyakati akiswali zaidi ya swala moja; yaani swala nyingi kwa udhu mmoja, yaani ule ule maadam haujatenguka.