HAKI ZA MUME

Kwanza kabisa kabla hatujaanza kuzielezea haki hizi ni vema tukatambua kuwa haki za mume kwa mkewe zinakomelea au ziko katika nafsi/dhati ya yule mke mwenyewe.

Na wala hazipindukii katika mali yake katika kipindi chote cha uhai wao kama inavyokuwa kwa mke.

Yeye mke ana haki ya nafsi na mali kwa mumewe lakini mume ana haki ya nafsi tu kwa mkewe katika kipindi cha uhai.

Haki ya mali anaipata katika kipindi cha umauti wa mweziwe tu ambayo hiyo ndiyo ijulikanayo kama haki ya mirathi.

Haki hii inamuhusu kila mmoja wao pindipo mwenziwe anapomtangulia katika maisha ya akhera.

Hivi ndio kusema kuwa mume ana haki nafsi tu kwa mkewe na wala hana haki mali kwa mujibu wa sheria toharifu.

Kwa mantiki hii mume hana haki na wala haimjuzii kisheria kuchukua au kutumia mali ya mkewe ila kwa kibali na radhi ya mkewe huyo. Mali ya mke kwa mume hukumu yake ni kama ilivyo mali ya mtu kando.

Kadhalika si halali mume kumlazimisha mkewe kujihudumia au kuihudumia familia hata akiwa tajiri namna gani.

Kwani katika uislamu hilo ni jukumu la mume na sio la mke, mke afanye hivyo kwa mapenzi na matashi yake tu na sio kwa njia ya uwajibu au kulazimishwa.

Uislamu unamtaka mume kuelewa kuwa mkewe ni mtu huru mwenye haki ya kuchuma, kumiliki na kuiendeleza mali yake.

Sambamba na kuitumia kwa maslahi yake binafsi yeye mwenyewe na familia yake kwao anakotoka au na familia yenu wewe mume na yeye mke katika mazingira ya khiari.

Hakuna kabisa mafungamano yo yote baina ya mume na mali ya mkewe katika kipindi cha uhai.

Ndoa haimpi mume kibali cha kuhodhi na kutumia mali ya mkewe bila ya ridhaa yake kwa njia yo yote ile.

Huu ndio uislamu, tukubali au tukatae utabakia hivyo hivyo na wala hauwezi kubadilishwa na matashi au mazoea yetu.

Baada ya tanbihi (uzindushi) hii, hebu sasa tuiangalie nafasi/thamani ya mwanamke katika ulimwengu huu.

Kisha ndio tuanze kuzielezea haki za mumewe zilizo juu yake, yaani wajibu wake kwa mumewe huyo.

Imepokelewa na Abdillah Ibn Amri Ibn Al-Aaswi-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

Dunia ni starehe na bora ya starehe zake ni mwanamke mwema”.

Muslim & Ahmad

Hadithi inamtaja mwanamke mwema na wala haimtaji mwanamke mzuri wa sura/umbo kuwa ndio bora ya starehe ya dunia.

Wewe miliki nyumba nzuri, shamba, magari ya kifahari, biashara kubwa , umaarufu au cheo, bado utakuwa haujastarehe kama hukumpata mwanamke mwema.

Sasa hebu tujiulize sote kwa pamoja, ni yupi huyu mwanamke mwema aliyepewa hadhi hii kuu?

Hapana shaka kama tukitafakari pamoja kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya uislamu tutaelewa kuwa mwanamke mwema ni yule anayezichunga haki za Allah Mola Muumba wake.

Na kuzipa nafasi ya kwanza kabla ya zile za mumewe hazijachukua nafasi ya tatu baada ya haki ya Mtume wa Allah. Miongoni mwa sifa za wanawake wa aina hii ni pamoja na:-

1.      Kulazimikiana na nyumba yake ili aweze kupata fursa ya kutosha ya kulitekeleza jukumu na wajibu wake kama mama na mlezi wa familia.

2.      Kutotoka hovyo nyumbani ila kwa haja maalumu inayoambatana na idhini na ridhaa ya mumewe kama kiongozi mkuu wa familia.

3.      Kuwa na moyo na ari ya kutengenea kwa hali yake na hali ya familia sambamba na kuwa na mfumo mzuri wa malezi ya watoto. Mfumo utakaozalisha wanajamii wema; baba na mama wema wa kesho.

4.      Kuwa na pupa ya kuhakikisha kuwa familia inaishi na kuifurahia hali na mazingira ya amani yatakayoiletea ufanisi na mafanikio.

5.      Kuishi ndani ya wigo wa maadili ya dini yake kwa kutekeleza maamrisho yake na kuacha makatazo ya Allah Mola Muamrishaji na Mkatazaji. Sambamba na kupanda mbegu hii njema ya maadili haya ya kidini kwa familia yake.

6.      Kukinahi na kutosheka na riziki waliyogawiwa na Allah, kwani tamaa ndio chanzo kikuu cha matatizo katika dunia hii.

Ziada ya yote haya, mwanamke hawezi kupata daraja na utukufu huu wa kuwa mwanamke mwema.

Mwenye thamani kuliko starehe zote za dunia mpaka kwanza azijue haki za mumewe; mwenza na mwandani wake katika maisha.

Hatua inayofuatia baada ya kuzijua haki hizo ni kuzitekeleza ipasavyo.

 Tena bila ya kinyongo au kuona vibaya huku akiamini kuwa huo ni wajibu wake umpasao kuutekeleza.

Na kwamba kuutekeleza wajibu wake huo ni kuitekeleza sehemu ya dini yake. Miongoni mwa wajibu wa mke ambao kwa mume ni haki ni mambo yafuatayo:-

1.      Kuipa umbele haki ya mume kuliko haki yake binfsi seuze haki za jamaa zake wengine. Hii ni kwa sababu haki ya mume kwa mkewe iko juu ya haki nyingine zote: “…NA WANAUME WANA DARAJA ZAIDI KULIKO WAO…” [2:228]

2.      Ajiandae na kuwa tayari wakati wo wote kumpa mumewe haki yake ya unyumba atakapoihitaji ila katika siku siku za hedhi au nifasi na katika hali ya maradhi.

Haijuzu kabisa kwa mwanamke muumini kumnyima mumewe haki yake hii nje ya mazingira haya tuliyoyataja (hedhi/nifasi/maradhi).

Kitendo cha kunyima mume haki yake hii humpelekea mke kuwa katika hatia ya dhambi na kulaaniwa na malaika. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:

“Mume atakapomuita mkewe kitandani, akakataa (mwanamke huyo)na mume akalala katika hali ya kumghadhibikia. Hulaaniwa (mwanamke huyo) na malaika mpaka kunapambazuka asubuhi”.

Bukhaariy & Muslim.

Na imepokewa kutoka kwa Twalqi Ibn Aliy-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

“Mume atakapomuita mkewe kwa ajili ya haja yake, basi na amuendee (amuitikie) hata kama akiwa kwenye tanuri (jikoni anapika)”.

Tirmidhiy & Nasaai

Ni dhahiri shahiri kwamba haki hii; haki ya jimaa (unyumba) ni miongoni mwa haki muhimu kabisa za mume kwa mkewe.

Kitendo cha mke kuijali, kuishughulikia na kisha kumkidhia mumewe haja yake hii ya kimaumbile kitandani.

Ni sababu kuu na nguzo muhimu kabisa ya ufanisi na mafanikio katika maisha ya ndoa. Kwa upande wa pili kuzembea kwa mke na kuipuuzia haki hii ya mumewe ni chanzo kikuu cha magomvi na mtafaruku.

Ambao mara nyingi ndio huwa sababu ya kutengana (talaka) kwa wawili hawa. Hawezi kuujua uzito wa kadhia hii ila mwanandoa, asiye mwanandoa hawezi kuona wala kuujua uzito na umuhimu wa suala hili.

Tatizo hili huweza kusababisha mume kuwa na nyumba ndogo au mke kuwa na “buzi” ikiwa mume hampi nafasi ya kushibisha kiu yake ya kimaumbile (mapenzi).

3.      Kisheria mke hana haki ya kujikurubisha kwa Mola wake kwa kufunga swaumu za suna, yaani zisizokuwa Ramadhani au zile za nadhiri ila kwa idhini ya mumewe.

Hii ni kwa sababu swaumu hii itamnyima mume haki yake ya kustarehe na mkewe wakati wa mchana.

Kwa mantiki hii ni lazima ipatikane idhini ya mume; idhini itakayoashiria kukubali kusamehe haki yake hii.

Hivi ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

“Haimuhalalikii mwanamke swaumu (ya suna) na ilhali mumewe yupo (hayuko safarini) ila kwa idhini yake. Na wala asimkaribishe mtu nyumbani kwake ila kwa idhini yake (mumewe)”.

Bukhaariy & Muslim

4.      Mke hana rukhsa kutoa nyumbani kwake cho chote kumpa yo yote ila kwa idhini ya mumewe.

Hata kama huyo anayempa ni jamaa yake huyo mume seuze jamaa zake yeye mke. Ikiwa mke atatoa bila ya idhini ya mumewe, hata kama ni kwa nia ya sadaka.

Hana atakachokipata zaidi ya dhambi na ujira/thawabu za utoaji huo zitakuwa ni katika fungu la mume.

Naam, inamjuzia kutasadaki chakula cha mumewe tu bila ya kufanya ubadhirifu. Hili ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:

“Mwanamke atakapotasadaki sehemu ya chakula cha mumewe bila ya israfu. Atapata ujira wake (sadaka hiyo) na mumewe atapata ujira wa kukichuma (chakula hicho)…”

Bukhaariy

5.      Mke hana haki ya kutoka nje ya nyumba yake, kusafiri au kufanya kazi ila kwa idhini ya mumewe.

Kadhalika hana rukhsa ya kuchanganyika na kufanya ushoga na wanawake wenziwe asiowapenda mumewe kutokana na tabia na mienendo yao mibaya.

6.      Mke akinahi na atosheke na riziki aliyoruzukiwa mumewe na Allah Mola Mwenye kuruzuku bila ya mkabala.

Asimkorofishe wala asimuudhi mumewe kwa sababu tu ya dhiki ya maisha au hali duni waliyo nayo.

Bali anachotakiwa kufanya katika hali hiyo ni kumuonyesha mumewe uvumilivu wake, akamsikizisha maneno mazuri anaporudi nyumbani jioni akitokea kazini hali ya kuwa yu taabani.

Ampe mumewe ushauri wa nini cha kufanya ili kujikwamua na hali hiyo ya dhiki iliyowagubika.

Ni lazima mke aonyeshe kuithamini taabu na uchovu wa mumewe katika kuitafuta riziki yao. Na ajiepushe kumkalifisha mumewe zaidi ya uweza wake.

Kwani kutokana na mapenzi ya mume kwake na kwa kuchelea kumuudhi mkewe, mume anaweza kujitumbukiza katika chumo la haramu kwa ajili tu ya kumridhisha mkewe.

Mke ajitahidi kuishinda nafsi yake ili asimfikishe mumewe mahala pabaya hapo.

Na amuusie kusubiri na kukinahi sambamba na kuzidisha juhudi katika kufanya kazi huku akimuomba Allah amkunjulie na kuwawepesishia riziki yao.

Kadhalika mke asiache kumtahadharisha mumewe na kuchuma kwa kupitia njia za haramu. Hii ndio iliyokuwa ada na dsturi ya wanawake wema wa zama njema za uislamu-Allah awarehemu.

Alikuwa mmoja wao akimwambia mumewe anapotoka nyumbani kwake kwenda shughulini kwake: (Tahadhari na chumo la haramu, kwani sisi tunaweza kusubiria njaa na dhara wala hatuwezi kusubiri juu ya (kuingia) motoni (kutokana na kula/kuvaa haramu).

7.      Ni wajibu wa mke kujihifadhi na kujistiri na kutodhihirisha uzuri wa mwili wake kwa mtu asiye maharimu yake ili kuchunga heshima yake, familia yake na hadhi ya mumewe:

“…BASI WANAWAKE WEMA NI WALE WENYE KUTII, WANAOJIHIFADHI (hata) WASIPOKUWAPO (waume zao) KWA KUWA ALLAH AMEWAAMRISHA KUJIHIFADHI…” [4:34]

Ni haramu mwanamke kuonyesha sehemu ya mwili wake isiyotakiwa kuonekana kisheria ila na mumewe au kumvulia nguo asiye mumewe.

Huko ni kumnyima mumewe haki yake na kumpa asiyestahiki. Jambo hili linausisha uvaaji wa nguo fupi au nyepesi zinazoonyesha rangi ya mwili.

Au zenye kubana mno kiasi cha kuliacha umbo lake zuri kuonekana na kila mwenye macho.

Ni vema mke akatambua kwamba kitendo chake hiki ni chemchem kuu ya fisadi na uharibifu katika ardhi. Imepokelewa kutoka kwa mama wa waumini (mkewe Bwana Mtume); Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema:

“Asivue mwanamke nguo zake katika nyumba isiyo ya mumewe ila atakuwa amevunja sitara baina yake na Mola wake”-Yaani atakuwa amejifedhehesha na kuvunja heshima na utukufu wake.

Ahmad, Tirmidhiy & Abuu Daawoud

 

8. Ni wajibu wa mke kumuheshimu mumewe heshima iliyochanganya huruma na upendo. Asimbughudhi mumewe kwa sababu tu ya uzuri au mali yake akiwa ni tajiri au ana hadhi kuliko mumewe huyo.

 

9. Mke anapaswa kuwa na huruma na nasaha njema kwa familia ili kuilinda dhidi ya mmomonyoko wa kimaadili.

Asijenge mazoea ya kuwatukana na kuwalaani watoto, kwani hilo litawapelekea na wao kujengeka hivyo watakapokuwa baba/mama wa familia.

Jambo dogo tu atakalofanyiwa na mumewe lisiwe ndio kifutio cha mema na mazuri yote aliyofanyiwa na mumewe huyo katika kipindi chote cha maisha yao.

 Ni lazima tukubali ukweli kuwa haya ni maumbile na tabia ya wanawake walio wengi.

 Kwamba kosa/jambo dogo tu la mumewe humfikisha kusema: (Mume gani wewe, tangu unioe sijaona jema lako hata moja, wewe nawe mwanamume katika wanamume!).

Mambo haya hayafai kwani humsafishia mwanamke huyo njia ya kwendea motoni. Imepokelewa kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliwaona wanawake ndio akthari (wengi) ya watu wa motoni, akaulizwa sababu yake ni nini. Akajibu:

 “Wanakithirisha mno laana (wanalaanilaani mara kwa mara watoto kwa jambo dogo tu) na wanakanusha wema na ihsani ya mume”. Bukhaariy, Muslim & Ahmad.

Hizi kwa mukhtasari ndizo baadhi ya haki za mume kwa mkewe au wajibu wa mke kwa upande wa mumewe.

Ni matumaini yetu kuwa kutokana na silsila (mlolongo) ya masomo haya wanandoa watakuwa kwa kiasi kikubwa wamezijua haki na wajibu wa kila mmoja wao kwa mwenziwe. Allah Mola Muumba jike na dume katika kila kitu atuwafikishe kuwa waume na wake wema wenye kupigiwa mithali mahala tuishipo-Aaamiyn.

 

One thought on “HAKI ZA MUME

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *