FAIDA SEHEMU YA TATU

Hebu uchunguze na uuangalie huo mkono wako ambao unaouinua katika Takbiratul-Ihraam ndani ya swala.

Utaona kama kwamba unayakunja na kuyakata masafa marefu yaliyo baina yako na Al-Ka’aba. Bali ukifikiria na kuzivuta sawia fikra zako utajikuta kama kwamba unatupa kila kitu nyuma yako na unabakia na Allah Mola Mwenyezi pekee.

Katika hiyo Takbiratul-Ihraam unalisema na kulitamka neno hili kuu: “ALLAAHU AKBAR” na kulipiga chapa huko mbali kwenye Al-Ka’aba Tukufu.

Kwa kitendo chako hiki utakuwa umejihakikishia kuwemo kwako ndani ya swala kwa moyo (roho), mwili na maana.

Hapo utakuwa na kila sababu ya kufurahi pale ambapo Bwana Mlezi wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake anapokuelekea kwa dhati yake mara tu baada ya kulitamka kwako neno hilo kuu kuliko maneno yote.

Sasa roho yako inaogelea katika bahari ya ukarimu na utukufu, humo unamwambia Mola wako: “WEWE TU NDIYE TUNAYEKUABUDU, NA WEWE TU NDIYE TUNAYEKUOMBA MSAADA”. [1:5]

Na katika ajabu ya mambo ni kwamba Suratil-Faatihah (Al-hamdu) unayoisoma katika kila rakaa ya swala yako ina jumla ya aya saba. Kwa nini saba?!

Namba hii saba (7) inadhihiri na kujirudiarudia katika viumbe na ishara/dalili za kuwepo Allah Mola Muumba.

Miongoni mwa viumbe/vitu vinavyoangukia katika idadi ya namba (7) kama zilivyo idadi za aya za Suratil-Faatihah ni pamoja na:-

  1. Mbingu saba.
  2. Ardhi saba.
  3. Idadi ya maneno ya kalima ya Tauhidi LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU

 


Hivi: LAA (1)

 


ILAAHA (2)

 


ILLA (3}

 


LAAHU (4)

 


MUHAMMADUN (5)

 


RASUULUL (6)

 


LAAH (7)

  1. Idadi ya sifa za waumini waliofuzu iliyotajwa katika Suratil-Muumininun. Hivi:
    1. HAKIKA WAMEFUZU WAUMINI AMBAO KATIKA SWALA ZAO HUWA NI WANYENYEKEVU.
    2. NA AMBAO HUJIEPUSHA NA MAMBO YA UPUUZI.
    3. NA AMBAO (nguzo ya zakkah) WANAITEKELEZA.
    4. NA AMBAO TUPU ZAO WANAZILINDA. ISIPOKUWA KWA WAKE ZAO AU KWA (wanawake) WALE ILIYOWAMILIKI MIKONO YAO YA KUUME. BASI HAO NDIO WASIOLAUMIWA. (Lakini) ANAYETAKA KINYUME CHA HAYA, BASI HAO NDIO WARUKAO MIPAKA (ya Allah).
    5. NA AMBAO AMANA ZAO
    6. NA AHADI ZAO WANAZIANGALIA (wanazitekeleza).
    7. NA AMBAO SWALA ZAO WANAZIHIFADHI. HAO NDIO WARITHI AMBAO WATARITHI PEPO; WAKAE HUMO MILELE. [23:1-11]

 

Hebu sasa tujaribu kuchungulia na kuangalia kwa makini siri ya aya na sifa hizi tukufu na njema, ambazo zinawataja waumini waliofuzu. Aya zimeanza na kuwataja (WANYENYEKEVU KATIKA SWALA ZAO) na zinakhitimisha na (AMBAO SWALA ZAO WANAZIHIFADHI). Hebu jaribu kuchunguza mwanzo na mwisho wa sifa hizi na uzingatie.

Sasa tuendelee kuishi na tarakimu hii saba (7):-

  1. Kutufu Al-Ka’aba mara saba.
  2. Kwenda sa’ayi (matiti/jaramba) baina ya vilima Swafaa na Mar-wa, mara saba.
  3. Idadi ya siku za juma.
  4. Idadi ya rangi za upinde wa mvua.
  5. Idadi ya makundi ya watu ambao Allah atayaweka chini ya jivuli la Arshi yake siku ya Kiyama. Kama ilivypokelewa katika hadithi sahihi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:-
    1. Imamu/kiongozi muadilifu.
    2. Kijana aliyeinukia/aliyekulia katika kumuabudu Allah.
    3. Mtu ambaye moyo wake umefungamana na misikiti.
    4. Watu wawili waliopendana kwa ajili ya Allah; wakakutana juu ya pendo hilo na kutengana kwalo.
    5. Mtu aliyetoa sadaka kiasi cha kutokujua kushoto kwake kile kitolewacho na kulia kwake.
    6. Mtu aliyeitwa na mwanamke mwenye cheo na uzuri (afanye naye machafu), yeye akasema: Hakika mimi ninamuogopa Allah.
    7. Mtu aliyemdhukuru Allah faraghani yakabubujika machozi macho yake.

Bukhaariy & Muslim

Ichunguze/izingatie hadithi pale iliposema (Na mtu ambaye moyo wake umefungamana na misikiti), utaona hadithi hii ina mafungamano ya moja kwa moja na swala.

Swala kama tulivyotangulia kusema katika darsa iliyotangulia ni kiungo baina ya mja (kiumbe) na Allah Mola Muuumba wake.

Kwa mantiki hii, mtu anapokuwa haswali huwa ameyakata mwenyewe tena kwa khiari yake mawasiliano baina yake na Mola wake.

Hali hii ya kukata mawasiliano na Mola wake ni kitendo kinachoashiria kuwa yeye (mja) anajitosheleza na hamuhitajii Muumba, jambo ambalo si kweli. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema:

Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema:

“Amesema Allah Mtukufu nimeigawa swala baina yangu na mja wangu nusu mbili na mja wangu atapata akiombacho. Basi atakaposema mja:

“SHUKURANI ZOTE ANASTAHIKI ALLAH, MOLA WA WALIMWENGU WOTE”, Allah husema amenihimidi (amenisifu na kunishukuru) mja wangu.

Na atakaposema:

“MWENYE KUNEEMESHA NEEMA KUBWA KUBWA NA MWENYE KUNEEMESHA NEEMA NDOGO NDOGO”, Allah husema amenisifia mja wangu.

Na atakaposema:

“WEWE TU NDIYE TUNAYEKUABUDU NA WEWE TU NDIYE TUNAYEKUOMBA MSAADA”, Allah husema hili ni baina yangu na mja wangu na atapata mja wangu atakachokiomba.

Na mja atakaposema: “TUNGOZE NJIA ILIYONYOOKA. NJIA YA WAKE ULIOWANEEMESHA; SIO (ya wale) WALIOKASIRIKIWA, WALA (ya) WALE WALIOPOTEA”, Allah husema hili ni la mja wangu na atapata aliombalo mja wangu”.

Muslim

 

SWALA TANO.

Sote tunatambua kwamba swala za fardhi ni tano. Kwa nini tano, nini maana ya utano huu?!

 Tarakimu/nambari tano (5) inawakilisha mambo/vitu vingi.

Hebu uangalie mkono wako unaouinua ndani ya swala, una jumla ya vidole vingapi? Bila shaka utasema kuna idadi ya vidole vitano.

Vidole vitano hivi vina maana na manufaa makubwa sana kwa mtu mwenye kuyatazama mambo/vitu kwa mazingatio.

Vidole vitano hivi vinauwakilisha utano mkuu na mkubwa ukiongozwa na:-

  1. Nguzo za uislamu ni tano kama alivyosema Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano:
    1. Shahada kwamba hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah.
    2. Kusimamisha swala.
    3. Kutoa zakkah.
    4. Kufunga Ramadhani.
    5. Kuhiji kwa mwenye uwezo”.

Bukhaariy, Muslim, Tirmidhiy & Nasaai.

  1. Herufi za neno RAMADHAN (kwa Kiarabu) ambao ni mwezi mtukufu uliofaradhishwa ndani yake swaumu na kushushwa Qur-ani. Ukizihisabu herufi hizi utakuta idadi yake ni tano:

REE – MIYM – DHWAAD – ALIFU – NUUN

{RA – MA – DHWA – A – N}

Kila mojawapo ya herufi tano hizi, inawakilisha maana maalumu kama ifuatavyo:-

    1. RA – Rahmah (rehema) yaani Ramadhani ni mwezi wa rehema.
    2. MIYM – Maghfirah (msamaha) yaani Ramadhani ni mwezi ambao Allah huwasamehe waja wake kwa wingi; mwezi wa toba kama tuuitavyo.
    3. DHWAAD – Dhwamaanuun Liljannah (dhamana ya pepo) yaani mwezi huu unampa mja dhamana ya kuingia peponi kutokana na amali njema azifanyazo ndani yake.
    4. NUUN – Nuurun minal-laah (nuru itokayo kwa Allah) yaani Ramadhani ni mwezi wenye nuru kwa sababu ya kushushwa Qur-ani ndani yake ambayo yenyewe ni nuru.
    5. ALIF – Amaanun-minan-naari (amani kutokana na moto). Yaani mwezi wa Ramadhani ukitumiwa vema humpa mja amani kwa kumuepusha na adhabu ya moto.

3). Waumini wana sifa tano kama zilivyotajwa katika Suratil-Anfaal:

    1. “HAKIKA WANAOAMINI KWELI NI WALE AMBAO ANAPOTAJWA ALLAH NYOYO ZAO HUJAA KHOFU.
    2. NA WANAPOSOMEWA AYA ZAKE HUWAZIDISHIA IMANI.
    3. NA WAKAMTEGEMEA MOLA WAO TU BASI.
    4. AMBAO WANASIMAMISHA SWALA.
    5. NA WANATOA KATIKA YALE TULIYOWAPA. HAO NDIO WANAOAMINI KWELI KWELI. WAO WANA VYEO (vikubwa) KWA MOLA WAO, NA MSAMAHA NA RIZIKI BORA (kabisa huko Akhera)”. [8:2-4]

4). Hali kadhalika vidole vitano vinakukumbusha kauli yake Allah: “…ALLAH ANATAKA KUKUONDOLEENI UCHAFU, ENYI WATU WA NYUMBA (ya Mtume-“Ahlul-Bayt”) NA (anataka) KUKUTAKASENI KABISA KABISA”. [33:33]

Amesema Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Aya hii ilishushwa kwetu sisi Ahlul-Bayt; Aliy, Fatmah, Hassan na Hussein”.

Rejea tafsiri Ibn Kathiyr na Sunan Tirmidhiy.

5). Milango mitano ya fahamu (hisia) “Five Common Sense”. Kila mmoja wetu ana milango mitano ya fahamu:-

  1. Uoni (macho).
  2. Kugusa (ngozi).
  3. Kuonja (ulimi).
  4. Usikivu (masikio).
  5. Kunusa (pua).

Ni kupitia milango mitano hii ya fahamu ndipo unapoweza kuutambua ulimwengu huu na aliyeuumba; Muumba Mshindi Mwenye nguvu.

Unapoinyanyua mikono yako ndani ya swala na vidole vyako vitano, unazikumbuka neema za Allah zilizo juu yako. Unaukumbuka uwezo, hekima (busara) na utukufu wake.

Basi ni fardhi juu yako kumuhimidi, kumshukuru na kumsifia:

“NEEMA ILIYOTOKA KWETU. HIVYO NDIVYO TUWALIPAVYO WANAOSHUKURU”. [54:35]

“…KAMA MKINISHUKURU NITAKUZIDISHIENI…” [14:7]

“…NA KAMA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH, HAMTAWEZA KUZIHISABU…” [14:34]

FAIDA YA SWALA SEHEMU YA TATU

Hebu uchunguze na uuangalie huo mkono wako ambao unaouinua katika Takbiratul-Ihraam ndani ya swala.

Utaona kama kwamba unayakunja na kuyakata masafa marefu yaliyo baina yako na Al-Ka’aba. Bali ukifikiria na kuzivuta sawia fikra zako utajikuta kama kwamba unatupa kila kitu nyuma yako na unabakia na Allah Mola Mwenyezi pekee.

Katika hiyo Takbiratul-Ihraam unalisema na kulitamka neno hili kuu: “ALLAAHU AKBAR” na kulipiga chapa huko mbali kwenye Al-Ka’aba Tukufu.

Kwa kitendo chako hiki utakuwa umejihakikishia kuwemo kwako ndani ya swala kwa moyo (roho), mwili na maana.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *