Inampasa muumini kuwa mtulivu na makini awapo ndani ya swala. Hii ni kwa sababu haijuzu kuitekeleza ibada kwa harakati (matendo) za haraka haraka; zenye kutoa sura tu ya ibada.
Elewa utekelezaji wa ibada bila ya kuwa makini na mtulivu unaweza kukupelekea kufanya makosa ndani ya ibada husika.
Mfano wa wale wanaozifisidi na kuziharibu ibada zao kutokana na haraka zao zisizo na msingi na upungufu wa sharti na nguzo.
Ni kama mfano wa mgonjwa aliyepewa dawa na tabibu (daktari), akamueleza jinsi ya kutumia na kiasi cha kutumia.
Mgonjwa huyu akayapuuza maelekezo ya tabibu wake, akazidisha au kupunguza kipimo cha dawa.
Hili ni kosa kubwa na baya linaloweza kumgharimu huyu mgonjwa maisha yake au siha (afya) yake.
Dawa ikimdhuru au isipomsaidia (isipomponya), mgonjwa huyu aseme dawa hii mbaya au haifai. Au aseme tabibu yule hajui kazi yake?!
Tabibu na dawa wote hawapaswi kulaumiwa, bali wa kulaumiwa ni nafsi yake mwenyewe kwa kuyakhalifu maelekezo ya tabibu wake ambaye ndiye mjuzi wa dawa.
Angalia ewe mwenye kughafilika, ndani ya swala unakuwa mbele ya nani?
Unanong’ona na kuwasiliana na nani? Hebu ona haya kunong’ona na Mola wako kwa moyo ulioghafilika na kifua kilichosheheni wasiwasi wa shetani na fikra za matamanio mabaya. Hivi huamini kuwa Allah Mola Muweza anaichomozea siri yako?
“(Allah) ANAJUA KHIYANA YA MACHO NA YAFICHWAYO NA VIFUA (nyoyo)”. [40:19]
Hukubali kuwa Allah anauangalia moyo wako na kuyajua yote yaliyomo?
Kwa nini basi unajidhihirisha kuwa unaswali kwa kuyafanya matendo ya swala na ilhali ukweli wa mambo huswali?! Unamdanganya nani, elewa hudanganyi ila nafsi yako.
FAIDA (MATUNDA) ZA SWALA.
Hakika ni ukweli usio na shaka ndani yake kwamba swala kamili, swala iswaliwayo kwa namna airidhiayo Allah:-
Huutia nuru ya twaa moyo wa mja.
Huiweka sawa na kuirekebisha tabia.
Humfundisha mja wajibu na adabu za uja kwa Bwana Mlezi wake.
Hii ni kutokana na utukufu na ukubwa wa Allah unaopandwa moyoni mwake na zoezi zima la swala.
Swala humvika mtu taji la tabia njema kama vile ukweli, uaminifu, kukinahi, unyenyekevu, upole, uadilifu na wema.
Swala humuelekeza mja kwa Mola wake na humuonyesha mja njia ya kumfika Mola wake.
Swala humfanya akipatwa na jambo limtatizalo aone hana msaada ila kukimbilia ndani ya swala.
Akiamini kuwa humo ndimo umo msaada wake:
“ENYI MLIOAMINI! JISAIDIENI (katika mambo yenu) KWA SUBIRA NA SWALA, BILA SHAKA ALLAH YU PAMOJA NA WANAOSUBIRI”. [2:153]
Swala humfanya mja amuone Mola wake yu pamoja naye po pote alipo na analiona kila alitendalo, kulisema au hata kulifikiria.
Hisia hizi humfanya kumcha na kuogopa kumuasi Allah, kwa hivyo swala kwake inakuwa ni askari wa kumchunga.
Swala huitakasa nafsi yake na hapo ndipo utamuona mtu aswaliye vilivyo hana sifa ya uongo, khiyana, shari, ghadhabu, kibri na uadui. Hapo ndipo itakuwa imethibiti juu yake kauli ya Mola wake isemayo:
“…BILA SHAKA SWALA HUMZUILIA (huyo mwenye kuswali na) MAMBO MACHAFU NA MAOVU…” [29:45]
Lau waislamu wa leo wangelizihifadhi swala zao kwa kuziswali katika nyakati zake zilizowekwa na sheria.
Wakazisimamisha na kuzitekeleza kama alivyowaamrisha Mola wao.
Bila shaka yo yote bishara ya Allah ingelitimia kwao, wangelikomeka na mambo machafu na maovu.
Wangeliepukana na majanga mbali mbali yanayotokana (yanayosababishwa) na madhambi na matendo yao maovu ya uasi kwa Bwana Muumba wao:
“…NA KAMA WANGALIFANYA WALIYOAMBIWA INGALIKUWA BORA KWAO NA YANGEKUWA YANATHIBITISHA ZAIDI (Uislamu wao). NA (ingekuwa hivyo) TUNGEWAPA MALIPO MAKUBWA KUTOKA KWETU. NA TUNGEWAONGOZA NJIA ILIYONYOOKA (ya kuwafikisha peponi)”. [4:66-68]
NANI MWENYE KUSWALI NA KUSIMAMISHA SWALA? (SIFA ZA MWENYE KUSWALI KIKWELI).
Mtu mwenye kuihifadhi na kuiswali swala itakiwavyo, mtu huyo:-
Hawi mzinifu na wala haijui kabisa zinaa:
“HAKIKA WAMEFUZU WAUMINI AMBAO KATIKA SWALA ZAO HUWA NI WANYENYEKEVU. NA AMBAO HUJIEPUSHA NA MAMBO YA UPUUZI. NA AMBAO (nguzo ya) ZAKA WANAITEKELEZA. NA AMBAO TUPU ZAO WANAZILINDA. ISIPOKUWA KWA WAKE ZAO AU KWA (wanawake) WALE ILIYOWAMILIKI MIKONO YAO YA KUUME. BASI HAO NDIO WASIOLAUMIWA” [23:1-6]
Hawi mla riba na wala haitambui riba kwa sababu:
“HIKI NI KITABU KISICHOKUWA NA SHAKA NDANI YAKE; NI UWONGOZI KWA WAMCHAO ALLAH”. [2:2]
Ni kina nani basi hao wacha-Mungu?
“AMBAO HUYAAMINI YASIYOONEKANA (Maadamu tu yamesemwa na Allah na Mtume wake) NA HUSIMAMISHA SWALA NA HUTOA KATIKA YALE TULIYOWAPA. NA AMBAO WANAAMINI YALIYOTEREMSHWA KWAKO, NA YALIYOTEREMSHWA KABLA YAKO NA WANAAMINI (kuwa iko) AKHERA”. [2:3-4]
Kwa kuwa mwenye kuswali ni Mcha-Mungu na anaiamini Qur-ani, vipi umtazamie kula riba na ilhali tayari imeshamshukia kauli ya Allah:
“ENYI MLIOAMINI! MSILE RIBA, MKIZIDISHAZIDISHA; NA MCHENI ALLAH ILI MPATE KUTENGENEKEWA. NA OGOPENI MOTO AMBAO UMEWEKEWA WENYE KUKANUSHA AMRI ZA ALLAH (Na katika hizo ni huku kutokula riba)”. [3:130-131]
Hawi mtu mwenye mfundo na kinyongo na wala hawi hasidi. Vipi atajasiri na kuthubutu kuyafanya hayo na ilhali anayaamini yaliyoteremshwa kwa Nabii Muhammad?! Mola wake anamwambia:
“…NA ANACHOKUPENI MTUME BASI POKEENI, NA ANCHOKUKATAZENI BASI JIEPUSHENI NACHO. NA MUOGOPENI ALLAH; KWA YAKINI ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU”. [59:7]
Na miongoni mwa aliyotukataza Bwana Mtume:
“Msibughudhiane, msihusudiane na wala msikatane pande kwa uadui, na kueni ndugu enyi waja wa Allah. Na wala si halali kwa muislamu kumuhama nduguye muislamu zaidi ya siku tatu”. Anas
Hawi mzito kutekeleza haki za watu na wala hachupi mpaka katika mali ya mtu. Ataanza vipi kuyafanya hayo na ilhali swala inamfanya ayaamini yaliyoteremshwa kwa Mtume, ambayo ni pamoja na :
“WALA MSILIANE MALI ZENU KWA BATILI NA KUZIPELEKA KWA MAHAKIMU ILI MPATE KULA SEHEMU YA MALI YA WATU KWA DHAMBI NA ILHALI MNAJUA (kuwa si haki yenu)”. [2:188]
Hawi muongo na wala hajui kuongopa. Vipi atasema uongo na ilhali swala inamfanya kuwa muumini na kusema uongo si sifa ya muumini:
“WANAOZUA UONGO NI WALE WASIOZIAMINI AYA ZA ALLAH; NA HAO NDIO WAONGO”. [16:105]
Hawi mwenye kupoteza/kuzuia/kunyima haki za wazazi, watu wake wa nyumbani, jamaa na jirani zake. Atajasiri vipi kuyafanya hayo na ilhali swala inamfinyanga kuyaamini yote aliyoshushiwa Nabii Muhammad, ambayo ni pamoja na:
“MWABUDUNI ALLAH WALA MSIMSHIRIKISHE NA CHO CHOTE. NA WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI, NA JAMAA NA MAYATIMA NA MASIKINI NA JIRANI WALIO KARIBU NA JIRANI WALIO MBALI, NA RAFIKI WALIO UBAVUNI (mwenu)…” [4:36]
Haachi kuwaangalia na kuwasadia mayatima, masikini na wasiojiweza wengine. Atathubutuje kuwatupa watu hao na ilhali Qur-ani anayoiamini inamwambia:
“JE, UMEMUONA (unamjua) YULE ANAYEKADHIBISHA DINI (asiyeamini malipo ya akhera)? HUYO NI YULE ANAYEMSUKUMA YATIMA. WALA HAJIHIMIZI KUWALISHA MASIKINI (wala hawahimizi wenziwe). BASI ADHABU ITAWATHUBUTUKIA WANAOSWALI. AMBAO WANAPUUZA (maamrisho ya) SWALA ZAO (kama kuwafanyia wema viumbe wenzao). AMBAO HUFANYA (amali zao ili wawaone tu) RIYAA. NAO HUNYIMA MISAADA (basi swala zao hazina faida kubwa nao)”. [108:1-7]
Kwa ujumla mwenye kusimamisha swala huipenda haki na wanahaki, sambamba na kuichukia batili na wanachama wake.
Wala hamkandamizi mtu wala yeye hakubali kukandamizwa/kuonewa.
Hadhulumu na wala hayuko tayari kudhulumiwa na hawapendi madhalimu na mafisadi.
Huyu ndiye mwanadamu kamili anayejengwa na swala mara tano kila siku. Ni mtu ambaye jamii imesalimika na shari/uovu wake na inaneemeka na kunufaika na kheri/wema wake.
Ewe muislamu, swala ni mazoezi ya viungo (mwili) yanayokuweka katika hali ya siha njema. Swala ni kiungo cha mawasiliano baina yako na Allah Mola Muumba wako.
Tambua kuisimamisha swala ni miongoni mwa nembo kuu za imani na ni katika alama za kuadhimisha dini ya Allah.
Swala ni dhihirisho tukufu la uja (utumwa) wako kwa Mola wako, dhihirisho la shukurani kwa neema za Allah Bwana Mlezi wako zisizodhibitika.
Swala ndio miraji ya roho, na siri ya kimungu ambayo hawaijui hakika na ukweli wake ila wale waliozama katika elimu na ucha-Mungu.