FAIDA SEHEMU YA NNE

MILANGO MITANO YA FAHAMU.

Milango mitano ya fahamu uliyonayo hukuwezesha kumjua Allah Mola Muumba wako.

Ni milango hii pia ambayo huithibitisha imani yako iliyomo moyoni, nayo milango hii ndio chimbuko na chemchem ya elimu na maarifa uliyonayo.

Ziada ya yote haya, milango mitano hii ya fahamu hukukumbusha zile nguzo tano za uislamu ambazo juu yake umejengwa uislamu, zingatia.

Hebu tuichunguze kwa pamoja milango mitano hii ya fahamu na dhima yake katika maisha yetu ya kila siku.

 

MLANGO WA UONI (MACHO):

Mlango huu wa fahamu, mbali na kazi zake nyingine ambazo hukusaidia katika maisha yako ya kila siku, una dhima/jukumu jingine mama.

Ukiizingatia kauli hii ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “…Nimewekewa burudani (tuzo) ya macho yangu ndani ya swala…”

Nasaai

Hutoshindwa kutambua kuwa uoni (macho) hukulingania (hukuita) kusimamisha swala.

 Kauli hii tukufu ya Mtukufu Bwana Mtume ikiwa inaashiria jambo, basi si jingine bali inaashiria kuwa hakuna burudani kama swala.

Ndani ya swala ndimo mahala pekee ambamo mja hupata fursa ya kunong’ona na Allah Bwana Mlezi na Muumba wake.

Je, iko burudani nyingine kushinda hii kwa watu wenye akili ya kuelewa?!

 

MLANGO WA UGUSI (MKONO):

Mlango huu wa fahamu una faida adida (nyingi) na mchango mkubwa katika kuyafanikisha maisha yako ya kila siku.

Ni mikono ambayo hukuwezesha kushika, kubeba, kutoa, kupokea na…na…Ukiachilia mbali faida na manufaa haya, mlango huu wa fahamu ugusi (mkono), una dhima nyingine kuu.

Dhima hii ikitekelezwa vema huchangia kwa asilimia tisini na tisa kama sio mia moja kuboresha hali ya maisha ya jamii ya kiislamu.

Mkono una dhima mama ya kukulingania wewe kutoa zaka na sadaka katika vile ulivyoruzukiwa na Allah Mmiliki halisi wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo humo.

Hebu tuitegee sikio la usikivu kauli hii ya Allah:

“YULE ANAYETOA (zakah, sadaka na vinginevyo) NA KUMCHA ALLAH. NA KUSADIKI JAMBO JEMA (akalifuata) TUTAMSAHILISHIA NJIA YA KWENDA PEPONI”. [92:5-7]

Hiyo ndio faida na jazaa ya aliyeutumia vema mlango huu wa fahamu ugusi (mkono).

Akautumia mkono wake katika kutoa vile alivyoruzukiwa na Allah Mola Mruzukuji, katika kuisadia jamii na kuupeleka mbele uislamu. Amesema Allah katika amri hii ya kutoa zakkah, tusome pamoja:

“CHUKUA SADAKA (zakah) KATIKA MALI ZAO, UWASAFISHE NA KUWATAKASA KWA AJILI YA HIZO (sadaka zao)…” [9:103]

Hapana shaka kwamba uchukuaji na utoaji wa zakah hufanyika kwa msaada mkubwa wa mlango huu wa fahamu ugusi, yaani mkono. 

Ni vema ukakumbuka kwamba kutoa katika mambo ya kheri ni katika kuishukuru neema ya Allah. Ambako hakumaanishi ila kuzidishiwa neema, tusome kwa mazingatio:

“NA (kumbukeni) ALIPOTANGAZA MOLA WENU (kuwa); KAMA MKISHUKURU, NITAKUZIDISHIENI…” [14:7]

 

MLANGO WA UONJO (ULIMI):

Kama milango ya fahamu iliyotangulia, mlango huu pia ambao hukiusisha kiungo ulimi una manufaa makubwa katika maisha ya kila siku ya mja.

Mlango huu wa fahamu hukulingania kuacha kuonja kinywaji na chakula, kwa ajili tu ya kutekeleza nguzo ya nne ya uislamu (swaumu).

Hali kadhalika mlango huu wa fahamu hukulingania kuacha kusema maneno ya fedhuli na badala yake kuutumia ulimi katika kusema maneno ya kheri na uongofu.

Zaidi ya yote hayo, mlango huu wa fahamu hukulingania kumdhukuru na kumtaja kwa wingi Allah sambamba na kukithirisha kumswalia Bwana Mtume:

“ENYI MLIOAMINI! MKUMBUKENI (mdhukuruni) ALLAH KWA WINGI NA MTUKUZENI ASUBUHI NA JIONI”.    [33:41-42]

Ni kheri kwako ikiwa utakumbuka kwamba KUMKUMBUKA ALLAH ni KUJIKUMBUKA wewe mwenyewe, amini ukitaka:

“BASI NIKUMBUKENI (kwa kunishukuru kwa hii neema niliyo kuneemesheni ya kukuleteeni Mtume, nami) NITAKUKUMBUKENI NA NISHUKURUNI WALA MSINIKUFURU”. [2:152]

 

MLANGO WA USIKIVU (MASIKIO):

Mlango huu wa fahamu una mchango mkubwa sana katika kufanikisha mawasiliano yako ya kila siku na wanadamu wenzako, sambamba na viumbe wengine.

Hukuwezesha wewe kusikia yasemwayo na wenzio; yote mema na mabaya, yenye madhara na manufaa.

Kama ambavyo huwawezesha wengine kusikia ujumbe, maoni, ushauri, nasaha na maonyo kutoka kwao.

Mbali na manufaa haya ya mlango huu wa fahamu, ambao hulihusisha sikio katika utendaji kazi wake.

Mlango huu una dhima kuu ya kukulingania kwenda kufanya ibada ya hijah na kuliitikia tangazo la ibada hiyo.

Sikio ndio hukukumbusha kauili/agizo la Allah kwa Nabii Ibrahim-Amani imshukie:

“NA (tukamwambia) UTANGAZE KWA WATU KHABARI ZA HIJAH, WATAKUJIA (wengine) KWA MIGUU NA (wengine) JUU YA KILA MNYAMA ALIYEKONDA (kwa machofu ya njiani) WAKIJA KUTOKA KATIKA KILA NJIA YA MBALI”. [22:27]

 

MLANGO WA KUNUSA (PUA):

Mlango huu wa fahamu ni kiungo muhimu sana kinachotoa mchango mkubwa sana katika uhai wa kila siku.

Kiungo hiki ndio njia kuu ya kuingiza hewa safi mwilini na kuitoa nje ile chafu.

Kadhalika humsaidia mwanadamu kuweza kutofautisha harufu za vitu mbali mbali vizuri na vibaya.

Ukiyaweka kando manufaa haya ya mlango huu wa fahamu, utaona kuwa mlango huu wa kunusa una dhima nyingine.

Mlango huu hukulingania kuvuta pumzi za kumpwekesha Allah Mola Mwenyezi kwamba kila pumzi inayoingia au kutoka mwilini mwako, itoke au iingie nawe ukiwa katika hali na mazingira ya tauhidi.

Pumzi yako isitoke au kuingia mwilini mwako ikakupa uhai wa kimwili tu bila ya kukupa uhai wa kiroho.

Kadhalika mlango huu wafahamu unakukumbusha kisa kilicho sheheni elimu, hekima, busara na nasaha njema.

Hiki si kingine bali ni kile kisa cha Mtume wa Allah Yousuf Ibn Ya’akuub-Amani ya Allah iwashukie, pale mzee Ya’akuub aliposema:

“NA ULIPOONDOKA MSAFARA (katika Misri) BABA YAO (huku Shamu) ALISEMA: NASIKIA HARUFU YA YUSUFU; LAU SI KUWA MNAITAKIDI NIMEHARIBIKA AKILI (mngenisadiki. Allah alimfanyia muujiza huo wa kusikia harufu ya ile kanzu ya mwanawe kabla haijafika)”. [12:94]

 

Kwa ujumla swala tano za fardhi unazowajibika kuzitekeleza kila siku, daima zinakukumbusha hakika na ukweli usiopingika wala kuepukika.

Swala tano hizi hukuambia kila siku kwa ulimi wa matendo ya kwamba sasa umelikaribia kaburi lako masafa ya siku moja, hivyo zidisha maandalizi.

Na swala ya Ijumaa mpaka Ijumaa nyingine inakueleza kuwa mpaka Ijumaa hiyo ya pili tayari umekwisha upoteza umri wako kwa kipindi cha juma zima.

Yaani tayari siku saba zimekwisha pungua katika umri wako.

Na Ramadhani ya mwaka jana mpaka hii ya mwaka huu inakukumbusha kuwa tayari umeshaponyokwa na mwaka mzima katika umri wako ambao hauujui ni miaka mingapi.

Kwa kuukiri ukweli huu, hebu tuizingatie kwa pamoja kauli hii ya Allah:

“NAAPA KWA ZAMA (zako ewe nabii Muhammad). KUWA BINADAMU YUMO KATIKA KHASARA. ISIPOKUWA WALE WALIOAMINI NA WAKAFANYA VITENDO VIZURI, NA WAKAUSIANA (kufuata) HAKI NA WAKAUSIANA (kushikamana) NA SUBIRA”. [103:1-3]

Ewe mwenye kuswali ni vema ukakumbuka na kukiri kuwa hakika Allah Mola Mwenye hekima na utukufu amekuwekea vitu/mambo maalumu.

Ambayo yanakufahamisha na kukuashiria juu ya mauti na mwisho wa uhai huu.

Vinakukumbusha ufufuo, kiyama, hisabu, adhabu, tuzo (thawabu) na bila ya kusahau kukumbusha juu ya neema au adhabu za kabri.

Maisha na amali zako katika ulimwengu huu wa mpito na mtihani ndio yatakayoamua ama kaburi lako liwe ni bustani ya pepo au liwe ni shimo la jahanamu.

Huu hapa usingizi (kulala) ni dalili ya wazi juu ya mauti, tusome kwa mazingatio:

“ALLAH HUTAKABADHI ROHO WAKATI WA MAUTI YAO. NA ZILE (roho) ZISIZOKUFA (bado, pia Allah anazitakabadhi) KATIKA USINGIZI WAO. BASI HUZIZUIA ZILE ALIZOZIKIDHIA MAUTI (alizozihukumia kufa) NA HUZIRUDISHA ZILE NYINGINE MPAKA (ufike) WAKATI ULIOWEKWA. BILA SHAKA KATIKA HAYA YAMO MAZINGATIO KWA WATU WANAOTAFAKARI”. [39:42]

Lakini kwa huzuni na khasara kuu, sisi hatutafakari, hatuzingatii na wala hatuyatii akilini kama kwamba (Allah atulinde na hali hiyo) tumekuwa katika wale ambao:

“WANAJUA HALI YA DHAHIRI YA MAISHA YA DUNIA, NA WAMEGHAFILIKA NA AKHERA, JE, HAWAFIKIRI KATIKA NAFSI ZAO (wakaona kuwa): ALLAH HAKUUMBA MBINGU NA ARDHI NA VILIVYOMO NDANI YAKE ILA KWA HAKI NA KWA MUDA ULIOWEKWA? NA KWA YAKINI WATU WENGI HAWAKUBALI YA KWAMBA WATAKUTANA NA MOLA WAO”. [30:7-8]

 

TUJIFUNZE NA TUKUBALI: Kuwa

“SIKUWAUMBA MAJINI NA WATU ILA WAPATE KUNIABUDU”. [51:56]

Tukubali au tukatae, swala ndio ibada mama, ibada nyingine zote zinaitegemea.

FAIDA YA SWALA: SEHEMU YA NNE

MILANGO MITANO YA FAHAMU.

Milango mitano ya fahamu uliyonayo hukuwezesha kumjua Allah Mola Muumba wako.

Ni milango hii pia ambayo huithibitisha imani yako iliyomo moyoni, nayo milango hii ndio chimbuko na chemchem ya elimu na maarifa uliyonayo.

Ziada ya yote haya, milango mitano hii ya fahamu hukukumbusha zile nguzo tano za uislamu ambazo juu yake umejengwa uislamu, zingatia.

Hebu tuichunguze kwa pamoja milango mitano hii ya fahamu na dhima yake katika maisha yetu ya kila siku.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *