Ni haramu kwa mwenye kukidhi haja kuelekea Qiblah au kukipa mgongo.
Uharamu huu ni iwapo anakidhi haja mwandani, wala hapana chenye kumsitiri wakati wa kukidhi haja yake.
Na imeshurutizwa sitara isiwe mbali nae zaidi ya dhiraa tatu za binadamu sawa na sentimeta 150 takriban.
Ikiwa jengo analotumia limeandaliwa maalum kwa ajili ya kukidhia haja (chooni), basi si haramu, bali inajuzu kuelekea na kulipa mgongo Qiblah kwa kuwa pana sitara.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Ayyuub Al-Answariy – Allah amuwie Radhi – kutoka kwa Mtume –Rehma na Amani zimshukie – amesema
“mnapokwenda chooni msielekee Qiblah wala msikipe mgongo kwa (kukidhi) haja ndogo au kubwa, lakini elekeeni mashariki na magharibi”. Al-Bukhariy na Muslim.