ADABU / TARATIBU ZINAZOFUNGAMANA NA HALI YA KUKIDHI HAJA

Ni vema kwa mwenye kukidhi haja akategemea mguu wake wa kushoto na kuusimamisha/kuunyoosha mguu wa kulia, hivi ndivyo anavyotakiwa akae wakati wa kukidhi haja.

Hekima ya ukaaji huu ni kuifanya haja itokee kwa wepesi kama vile unavyomimina kilichomo ndani ya chupa kwa kuinamisha upande upande.

Kadhalika anatakiwa wakati wa kukidhi haja asiangalie juu, utupu wake wala kile kimtokacho. Pia ni karaha kuzungumza wakati anakidhi haja.

Imepokelewa na Ibn Umar –Allah amuwie Radhi – kwamba mtu mmoja alipita ilhali Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehma na Amani zimshukie – akikidhi haja ndogo, (mtu yule) akamtolea salamu, (Mtume) hakumjibu. Muslim.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Said – Allah amuwie Radhi – amesema ; Nimemsikia Mtume – Rehma na Amani zimshukie – akisema :

“Wasitoke watu wawili wakaenda kukidhi haja, hali ya kufunua tupu zao huku wakizungumza, hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hulichukia hilo” Abu Dawood na wengineo.

Maelezo : Inakisiwa/Inapimiwa juu ya maneno (mazungumzo) mambo mengine kama vile kula, kunywa na kuchezeachezea utupu (uchi).

Kustanji/kuchamba kwa kutumia mkono wa kushoto : Anatakiwa mwenye kukidhi haja atumie mkono wake wa kushoto kusafisha mahala ilipotokea najisi kwani ni karaha kutumia mkono wa kulia.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Qatadah – Allah amuwie Radhi – kutoka kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – amesema :

“Anapokojoa mmoja wenu, basi asiishike dhakari yake kwa mkono wa kulia na wala asistanji/asichambe kwa mkono wa kulia”.

Kadhalika miongoni mwa adabu, anatakiwa mwenye kukidhi haja mawandani; nje ya jengo lililoandaliwa kwa kukidhia haja (chooni), atafute mahala pa faragha palipo mbali na watu.

Watu wasimuone wala kusikia harufu ya choo chake au sauti ya mashuzi yake. Imepokelewa kwamba Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa anapotaka kwenda kujisaidia huenda mbali mpaka mtu asiweze kumuona. Abu Dawood na Al-Tirmidhiy.

Vile vile anatakiwa asiisege/asiipandishe nguo yake ikiwa ni shuka/msuli mpaka akurubiapo ardhi, sio anaanza kuvua nje kabla hajaingia ndani.

Afanye hivyo kwa ajili ya kuusitiri utupu wake, jambo ambalo limeamrishwa na sheria.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *