AB-AADH

Maana:            Hii ni kila ile suna iliyomo ndani ya swala ambayo kuacha kwako kuitenda kwa kusahau kutakupeleka kusujudu sijidat sahwu mwishoni mwa swala yako, kabla ya kutoa salamu. Suna hizi za Ab-aadh ni pamoja na:-

1. Tashahudi ya kwanza {Mwanzo}

Muradi na makusudi ya Tashahudi ya mwanzo ni ile Tashahudi inayosomwa katika kile kitako/kikazi kisichoandamiwa na salamu {kutoa salamu} Tashahudi hii hupatikana katika rakaa mbili za mwanzo za swala za Adhuhuri, Alasiri, Maghribi, na Al-Ishaa.

Ni suna iliyothibiti kutoka kwa Bwana mtume Rehema na amani zimshukie kukaa kitako baada ya sijida ya pili ya rakaa ya pili ya swala hizi tulizozitaja kwa ajili ya kuisoma tashahudi hii ya mwanzo.

Dalili/Ushahidi:

Imepokelewa kauli ya Bwana Mtume Rehemu na Amani zimshukie katika hadithi ya yule mtu aliyekuwa akiswali sivyo ndivyo:

“ — Utakapokaa katikati ya swala, basi jitulize ukae mkao wa Iftiraashi, halafu usome Tashahudi —“ Abuu Daawoud katikati ya swala.

Baada ya sijida ya pili ya rakaa ya pili ya swala husika. Halafu usome Tashahudi: Tashahudi ya mwanzo.

Dalili na ushahidi unaothibitisha usuna wa Tashahudi ya mwanzo na kwamba sio fardhi ni kwamba Mtume wa Allah Rehema na amani zimshukie aliinuka katika swala ya Adhuhuri hali ya kuwa inamlazimu kukaa kitako (cha Tashahudi ya mwanzo) (Akaendelea na swala) alipoikamilisha swala yake akasujudu sijida mbili.” Bukhaariy na Muslim

Hadithi inatueleza kwamba Bwana Mtume alisujudu sijida mbili za kusahau ikiwa ni badali ya ile Tashahudi ya mwanzo iliyoiacha kwa kusahau kukaa kitako kwa ufahamu huo basi, lau kama Tashahudi ya mwanzo ingelikuwa ni NGUZO/FARDHI bila ya shaka Bwana Mtume (ambaye ndie aliyetufundisha swala na mengineyo ya kheri) angelilazimika kuileta nguzo hiyo kwa kurudi chini, akakaa kitako akaisoma Tashahudi.

Kisha akainuka na kuendela na sehemu iliyobakia ya swala yake na wala asingeliiunga nguzo hiyo kwa kuleta zile sijida mbili za kusahau kama tunavyofahamishwa na hadithi.

Elewa hivi ewe ndugu yangu wee, na hali ya kuwa Mola wako pekee ndiye MJUZI mno wa yote na vyote.

2. Kumswalia Mtume baada ya Tashahudi ya mwanzo.

Ni suna baada ya kumaliza kuyasoma matamko ya Tashahudi ya mwanzo kama yalivyopokewa kutoka kwa mtume, kumswalia Bwana mtume kabla ya kuinuka kuiswali rakaa ya tatu. Mwenye kuswali aiunge Tashahudi yake na swala ya Mtume kwa kusema:

ALLAHUMMA SWALLI  ALAA MUHAMMAD

3. Kitako cha Tashahudi ya mwanzo.

Hizi ni suna tatu zinazofuatana pamoja lakini kila moja inajitegemea kwa mpango huu:

Suna ya kitako.

Kwanza akae kitako baada ya kutoka katika sijida ya pili ya rakaa ya pili ya swala yenye rakaa nne au tatu. Ndipo inafuatia.

Suna ya Tashahudi.

Baada ya kukaa kitako ndipo inapokuja fursa ya kuitekeleza suna ya kuisoma Tahahudi ya mwanzo. Akimaliza kuisoma Tashahudi hii ya mwanzo, ndipo inamalizia.

Suna ya kumswalia Mtume.

Mara tu baada ya kuyakamilsiha matamko ya Tashahudui, ni suna kuyaandamizia matamko hayo na swala ya Mtume.

4. Kuwaswalia Aali wa Mtume baada ya Tashahudi ya mwisho.

Ni suna thabiti kutoka kwa Bwana Mtume, kuwaswalia Aali za Mtume sambamba na kumsalia Mtume baada ya Tahahudi ya mwisho Aseme:

ALLAHUMMA SWALLI ALAA MUHAMMAD WA ALAA AALI MUHAMMAD

Hivi ndivyo ilivyokuja katika tamko la kumswalia Mtume kama lilivyo katika hadithi zinazoibainisha nguzo ya Tashahudi.

5.  Qunuut.

Suna hii huletwa katika itikadi ya rakaa ya pili ya swala ya Sub-hi/Alfajiri. Imepokelewa kutoka wa swahaba wa Mtume Anas Ibn Maalik Allah amuwiye radhi amesema:

“Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie hakuacha kuleta Qunuut katika swala ya Sub-hi mpaka alipoaga dunia.” Ahmad

Suna hii hutekelezwa kwa kumsifia Allah na kuomba dua ye yote aitakayo LAKINI ukamilifu ni kujilazimisha kuilta ile ile Qunuut iliyopokewa kutoka kwa Mtume wa Allah. Imepokelewa kutoka kwa Al-Hasan Ibn Aliy Allah awawiye radhi amesema: Alinifundisha Mtume wa Allah maneno Rehema na Amani zimshukie niyasema katika swala ya Witri.

“ALLAHUMMA-HDINII FIIMAN HADAYTA, WA AAFINII FIMAN AAFAYTA, WATAWALLANII FIMAN TAWALLAYTA, WA BAARIK LII FIMAA A-‘TAYTA, WA QINII SHARRA MAA QADHAYTA, INNAKA TAQDHII WALAA YUQDHAA ALAYKA, WAINNAHU LAA YADHILLU MAN WAALAYTA, WALAA YAIZZU MAN ADAYTA, TABAARAKTA RABBANAA WATAALAYTA” Abuu Daawoud.

Ni vema Imamu akaileta Qunuut kwa tamko la “jamii” wingi, yaani badala ya kusema.

“ALAAHUMMA-HDINII ……………. WA AFINII

Kwa tamko la “fardhi” upweke/umoja, aseme

ALLAHUMMA-HDINAA ………… WA AFINAA

Kwa tamko la “jamii” linalomchanganya na kumjumuisha yeye pamoja na maamuma wake.

Ushahidi unaoonyesha kwamba suna ya Qunuut mahala pake ni katika Itidali ni hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah Allah amuwiye radhi kwamba Mtume Rehema na Amani zimshukie alikuwa anapokiinua kichwa chake kutoka katika rukuu ya swala ya subhi kwenye rakaa ya pili, huinyanyua juu mikono yake na kuomba kwa dua hii:

ALLAHUMMA-HDINII FIIMAN HADAYTA ………… al-Haakim.

Dalili inayothibitisha kwamba mtu anaweza kuomba dua nyingine yo yote katika Qunuut kulingana na mazingira na wakti aliomo ni ile riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Abuu Raafi Nafii amesema: “Niliswali nyumba ya Umar Ibn Khatwaab swala ya sub-hi, akakunuti (akaleta Qunuut) baada ya rukuu, (akaendelea kusema) nikamsikia akisema:

“ALLAHUMMA INNAA NASTAINUKA, WA NASTAGHFIRUKA WA NUTHNII ALAYKA, WALAA NAKFURUKA, WA NU-MINU BIKA, WA NAKHLA’U WA NATRUKU MAN YAFJURUKA, ALLAHUMMA IYYAAKA NA’BUDU, WALAKA NUSWALLI WA NASJUDU, WA ILAYKA NAS-A’AA WA NAHFIDU, WA NARJUU RAHMATAKA, WA NAKHAAFU ADHAABAKA, INNA ADHAABAKA BILKUFFARI MULHAKU, ALLAHUMMA ADHHIBI-LKAFARATA, WA ALKI FI QULUUBIHIMU-RRU’BA, WA KHAALIF BAYNA KALIMATIHIM, WA ANZIL ALAYHIM RIJZAKA WA ADHAABAKA, ALLAHUMMA ADHHIBIL-KAFARATA AHLAL-KITAABI-LLADHIINA YASUDDUUNA AN SABILIKA, WA YUKADHIBUUNA RUSULAKA, WA YUKAATILUUNA AWLIYAA-AKA, ALLAHUMMA-GHFIR LILMUUMININA WALMUUMINAAT, WALMUSLIMIINA WALMUSLIMAATI, WA ASLIH DHAATA BAYNAHUM, WA ALLIF BAYNA QULUUBIHIM, WAJ-A’L FII QULUUBIHIMUL-IIMANA WAL-HIKMATA, WA THABBITHUM ALAA MILLATA NABIYYIKA, WA AWZI-‘IHUM AN YUUFUU BIL-A’HDI ALLADHII A’AHADTAHUM ALAYHI WANSURHUM ALAA ADUWWIKA WA ADUWWIHIM, ILAAHAL-HAKKI WAJA’LNAA MINHUM” Imam Abdurazaak katika Muswanaf.

FAIDA.

QUNUUT KATIKA SWALA TANO.

Ni sheria kuleta Qunuut kwa sauti katika swala tano wakati waislamu wanapofikwa na maafa/majanga mbalimbali.

Hili linatokana na riwaya ya Ibn Abbaas Allah awaridhie amesema: Alikunuti Mtume wa Allah Rehema na amani zimshukie mwezi mzima mfululizo.

(Alileta Qunuut) katika swala za Adhuhuri, Alasiri, maghribi, Ishaa na subhi, mwishoni mwa kila swala anaposema SAMI’ALLAHU LIMAN HAMIDAH ya rakaa ya mwisho: akiwaombea maangamivu, watu wa kitongoji cha Baniy Sulaym wa kabila za Ri’il, Dhak-waan na Uswiyyah, na watu walioko nyuma yake wakitikia Aamiyn.” Abuu Daawoud na Ahmad.

Kwa nini Bwana Mtume aliwaombea maangamivu watu hawa?

Kisa chenyewe kama alivyosema Imam Ahmad kinaanzia pale walipomjia Mtume wa Allah watu wa makabila haya matatu tuliyoyataja {Ri’il, Dhakwaan na Uswiyyah} na kudai kwamba wao wameukubali uislamu na wamesilimu.

Wakamuomba Bwana Mtume awape waalimu watakao wafundisha dini. Bwana Mtume akakubali na akawapa waalimu sabini (70).

Lakini kumbe hawakusilimu kweli, wakawaua maswahaba wale wote sabini.

Kadhia hii ilimuudhi sana na kumkasirisha mno bwana Mtume na kumpelekea kuuchukua uamuzi huu wa kuwaombea maangamivu watu wabaya hawa.

TANBIHI:     Sijidat Sahwu itaelezwa kwa ukamilifu na ubainifu wa kutosha katika somo la NNE Inshaallah.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *