RAMADHANI 1442-JUKWAA LA 05

WAISLAMU TUNAPASWA, TENA KWA NJIA YA WAJIBU, KUIJUA THAMANI YA MSIMU HUU WA KIROHO ILI TUFAIDIKE NAO”

Sifa zote njema na takasifu ni zake Allah; aliye juu na Mkuu ambaye ametuuumbia vipawa na kutuwekea ndani ya siku za ulimwengu wetu huu. Huwapa vipawa hivyo waja wake, wakivitumia vema huwa ni sababu ya kusamehewa madhambi yao, kurudufishwa kwa ujira wa matendo yao mema na kupandishwa daraja zao mbele yake. Na Yeye Allah Mtoaji wa vipawa hivyo, ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi kwa waja wake.

Na ninakiri kwa moyo na kutamka kwa ulimi ya kwamba hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah peke yake; hana mshirika katika ufalme wake, ambaye Yeye ndiye aliye sema ndani ya Kitabu chake kitukufu: “Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi…”. Al-Baqarah [02]:185

Tena ninakiri kwa moyo na kutamka kwa ulimi ya kwamba Muhammad ni mja wa Allah na Mtume wake, ambaye yeye ndiye aliye sema: “Atakaye funga Ramadhani kwa Imani na kwa kutajia ujira kutoka kwa Allah, atasamehewa dhambi zake alizo kwisha zitenda”. Tunamuomba Allah amshushie Rehema na Amani yeye, Aali, Swahaba na umati wake mzima.

Ama baadu,

Wapendwa ndugu zetu katika Imani.

Assalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

Turuhusuni tuitumie fursa hii kukupongezeni kwa kuteuliwa kwenu na Allah kuwa miongoni mwa waja wake wengi walio wafikiwa kuidiriki fursa hii yenye kima na thamani; mwezi mtukufu wa Ramadhani. Tunawapongeza kwa kufuata nyayo za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwani yeye alikuwa akiwapongeza maswahaba wake kwa munasaba wa kuingia kwa mwezi wa Ramadhani. Tunaelezwa hilo na swahaba wake; Abu Huraira-Allah amuwiye radhi: Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwabashiria (akiwapa habari njema na pongezi) maswahaba wake akisema: “Umekwisha kufikieni mwezi wa Ramadhani; mwezi ulio barikiwa. Allah amekuwajibishieni funga yake, hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na hufungwa milango ya moto na hutiwa kifungoni humo mashetani waasi. Ndani yake umo usiku mmoja tu ambao huo ni bora kuliko miezi elfu moja, atakaye nyimwa kheri zake, huyo amekula khasara”.

Naam, Muislamu unapaswa kuufurahikia na kuushangilia mwezi huu mtukufu, na ni lipi litakalo kuzuia kuufurahikia mwezi ambao hufunguliwa ndani yake milango ya pepo?! Mwezi ambao ndani yake hufungwa milango ya moto?! Kwa nini mtu mwenye siha ya akili, asiufurahikie mwezi ambao mashetani hupigwa pingu ili kumpa fursa nzuri ya kujikurubisha kwa Mola Muumba wake?!

Ndugu Muislamu-Allah akurehemu-ni kheri kubwa kwako ikiwa utakiri na kujua ya kwamba mwezi wa Ramadhani ni neema itokayo kwa Allah kuja kwa umma wa Kiislamu kila mwaka. Ni mwezi ambao Allah hueneza ndani yake na kutoa kwa wingi mno neema zake, msamaha wake na kuwaacha huru waja wake kutokana na adhabu chungu ya moto wa Jahannamu. Mwezi huo ni fursa ya upendeleo waliyo pewa umati Muhammad ili kuifufua, kuirejesha na kuikarabati Imani yao, ni fursa inayo wafinyanga kuwa wacha Mungu kama ambavyo ni fursa inayo wafundisha kuwa na subira na ukarimu. Ni fursa inayo watakasa na madhambi na kuwasafisha kutokana na taka za moyo mithili ya kiburi, ubakhili, ukukutavu wa moyo na kadhalika. Ni fursa inayo wapa Waislamu uwanja wa kushindana katika kutenda ibada mbali mbali na anuwai za khairaati.

Naam, ni kutokana na unyeti, umuhimu na ughali wa fursa hiyo ya upendeleo, ndio tunamuona Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akiwakumbusha na kuutaka umati wake kuchunga funga ya mchana wake na kisimamo cha usiku wake na kusaidiana na kuoneana huruma baina yao. Na kuwatanabahisha mambo ambayo wanapaswa kuwa na pupa ya kuyatenda ndani ya mwezi huu. Hayo ndio tunayo ambiwa na swahaba; Salmaan Al-Faarisiy-Allah amuwiye radhi-pale alipo sema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alituhutubia katika siku ya mwisho ya mwezi wa Shaabani, akasema: “Enyi watu! Hakika umesha kugubikeni mwezi mtukufu ulio barikiwa, mwezi ambao ndani yake umo humo usiku mmoja ambao huo ni bora kuliko miezi elfu moja. Mwezi ambao Allah ameifanya funga yake kuwa ni faradhi na kisimamo chake kuwa ni suna. Basi yeyote atakaye jikurubisha (kwa Mola wake) ndani yake (mwezi huo) kwa (kutenda) jambo moja la kheri, huwa (thawabu zake) ni kama mtu aliye tekeleza faradhi katika miezi mingine. Na atakaye tekeleza humo faradhi moja, huwa (thawabu zake) ni kama mtu aliye tekeleza faradhi sabini katika miezi mingine. Nao ni mwezi wa subira na thawabu za subira ni pepo na ni mwezi wa kusaidiana na ni mwezi ambao huzidishwa humo riziki ya muumini. Atakaye mfuturisha mfungaji ndani yake (mwezi huo, futari hiyo) huwa ni maghufira ya dhambi zake (huyo mfuturishaji) na kuachwa huru na moto na hupata mithili ya ujira wake (huyo mfungaji) pasina kupungua chochote katika ujira wake huo.

Maswahaba wakasema: Ewe Mtume wa Allah! Sio kila mtu ana uwezo wa kumfuturisha mfungaji. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Allah humpa thawabu hizo yule aliye mfuturisha mfungaji (hata) kwa kumpa tende moja, au funda ya maji, au konzi ya maziwa. Nao ni mwezi ambao mwanzo wake ni rehema, katikati yake ni maghufira na mwisho wake ni kuachwa huru na moto. Na atakaye mpunguzia (kazi) mtumwa wake ndani yake (mwezi huo), atasamehewa dhambi na kuachwa huru na moto. Basi kithirisheni ndani yake mambo manne; mambo mawili mtamridhisha Mola wenu Mlezi (kwa kuyatenda) na mambo mawili (mengine) lazima mnayahitajia (mna shida nayo).

Ama yale mambo mawili ambayo mtamridhisha Mola wenu Mlezi kwa kuyatenda, ni kushuhudia ya kwamba hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah (mseme: As-hadu an laa Ilaaha illal-laah) na mumuombe maghufira (mseme: Astaghfirullah). Na ama yale mambo mawili ambayo lazima mnayahitajia, ni nyinyi kumuomba Allah (akuingizeni kwenye) pepo na mjikinge kwake na (adhabu ya) moto. Na atakaye mnywesha mfungaji funda ya maji, Allah atamnywesha kwenye hodhi langu funda moja ambalo hatashikwa tena na kiu mpaka anaingia peponi”. Ibnu Khuzamah [SAHIH IBNU KHUZAIMAH]-Allah amrehemu.

Ni kutokana na Hadithi hii ndio utaisikia misikiti mingi ndani ya mwezi wa Ramadhani ikianikizwa kwa sauti za ule uradi maarufu ambao hautausikia ila ndani ya mwezi wa Ramadhani tu, hakuna muislamu anaye lipinga hilo. Makindano yapo kwenye namna ya kuuleta uradi huo, je uletwe kwa sauti yenye kusikiwa na kila mtu kama ilivyo ada ya misikiti yetu mingi au kila mtu alete peke yake kimya kimya, hapa si ukumbi wa mas-ala hayo, pulika.

Mpendwa mwana jukwaa-Allah akurehemu-tusite na kuweka kituo kidogo hapa ili tupate kuyatolea ufafanuzi mukhtasari wa mambo manne hayo ambayo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ametutolea wito wa kuyatenda kwa wingi. Tukianza na jambo la kwanza ambalo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alilo tuhimza kulitenda ni kutamka shahada (Laa Ilaaha illal-laah), ametuhimiza hilo kwa sababu mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Tauhidi (kumpwekesha Allah katika ibada) na hali kadhalika ni mwezi wa mlingano (da’awa) wa Kiislamu. Nao ndio mwezi ambao wahyi ulianza kumshukia Mtume wa Allah ndani yake, kwenye lile pango la Hiraa kwa kauli yake Allah aliye Mtukufu: “Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba…”.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kututolea wito wa kuleta kwa wingi shahada ya Tauhidi ndani ya mwezi huu, jambo hilo halimaanishi kingine zaidi ya kuyaimarisha mafungamano yetu na Allah Mola Muumba wetu na kushikamana na dini yake. Na kukithirisha kumdhukuru Allah kama ilivyo pokewa katika Hadithi isemayo: “Mwenye kumdhukuru Allah ndani ya Ramadhani ni mwenye kusamehewa na mwenye kumuomba Allah ndani yake, harejeshwi patupu”.

Naam, lengo mama na la msingi la ibada ya swaumu ni kumzawadia mfungaji uchaMngu yeye mzima; kumfinyanga kuwa mchaMngu katika hali zake zote, hali ya dhiki na raha, hali ya uzima na ugonjwa, hali ya furaha na huzuni, hali ya amani na vita, hali ya kupata na kukosa, hali ya utulivu na harakati. Kumfanya kuwa mchaMngu katika matendo na kauli zake, katika fikra na mawazo yake, katika hukumu na maamuzi yake, katika mahusiano na maamiliano yake na watu. Kwa ujumla swaumu inamjenga mja kuwa na mahusiano mazuri na mawasiliano endelevu baina yake na Mola Muumba wake, baina yake na jamii yake kwa ustawi wa dunia na akhera yake. Hiyo ndio maana na analo likusudia Allah katika kauli yake pale alipo izungumzia swaumu, tusome, tuwaidhike na tuzingatie: “Enyi mlio amini! Mmewajibishiwa swaumu kama walivyo wajibishiwa walio kuwa kabla yenu, ili mpate kumchaMngu”. Al-Baqarah [02]:183

Naam, hilo ndilo lengo mama la ibada ya swaumu kwa kauli yake Allah aliye tufaradhishia ibada hiyo, uchaMngu. Na huo uchaMngu tunaweza kuukusanya katika maneno matatu haya “maandalizi”, “jitihada/bidii” na “dhikri ya Allah”. Swahaba wa Mtume; Ubayyu bin Ka’ab-Allah amuwiye radhi-alipo ulizwa uchaMngu ni nini, alimjibu muulizaji wake kwa njia ya kumuuliza: “Je, umeshawahi kupita kwenye njia yenye miiba? Akajibu: Kwani, (nimeshapita). Akamuuliza (tena): Basi ulifanyaje (ulipo pita)? Akajibu: Nilipanya nguo na nikajitahidi (kuhepa kuchomwa na miba). Akamwambia: Basi huo ndio uchaMngu”.

Allah Mtukufu amesema:{Enyi mlio amini! Mdhukuruni Allah kwa wingi wa kumdhukuru”. Na katika Hadithi Al-Qudsiy (Mtume amesema): “Atakaye shughulishwa na dhikri (utajo) yangu kiasi cha kukosa nafasi ya kuniomba, huyo nitampa bora zaidi ya nitakavyo wapa wale waniombao”.

Na katika Hadithi Al-Qudsiy nyingine Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mimi niko kwenye dhana ya mja wangu vile atakavyo nidhania, nami niko pamoja naye pale anapo nidhukuru. Basi atakapo nidhukuru moyoni mwake nami nitamdhukuru moyoni mwangu na akinidhukuru hadharani, Mimi nitamdhukuru kwenye hadhara iliyo bora zaidi (ya ile yake). Na akijikurubisha kwangu kwa kadiri ya shubiri moja, nami nitamkurubia kwa dhiraa moja. Na akijikurubisha kwangu kwa dhiraa moja, nami nitamkurubia kwa kiasi cha pima moja. Na atapo nijia akitembea, nami nitamwendea wangu wangu”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Ewe ndugu mfungaji-Allah akurehemu-fahamu na ujue ya kwamba, kumdhukuru Allah kwa kusema “Laa Ilaaha illal-laah”, hiyo ndio huitwa “Tahalili” na hiyo ndio kalima (neno) ya Tauhidi ambayo inaitwa kwa majina haya; “kalima ya Ikhlaaswi”, “kalima ya taq-wa (uchaMngu)”, “kalima njema” na “wito wa haki”. Na kuhusiana na kalima hiyo, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia: “Neno bora nililo pata kulisema mimi na Mitume walio nitangulia ni {Laa Ilaaha illal-laah wahdau laa shariika lahuu, lahul-mulku walahul-hamdu wahuwa ‘alaa kulli shain qadiiru} – Hapana afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah peke yake, hana mshirika, ufalme wote ni wake na Yeye ni Muweza wa kila kitu”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.

Naam, kwa mukhtasari huo ndio wito wa kwanza wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika hadithi ya kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ama jambo la pili, ambalo ni “Istighfaari” – ambako ni kumuomba Allah msamaha wa dhambi kupitia mlango wa toba. Kuielekea kadhia hii ya kumuomba msamaha Allah baada ya mwanaadamu kuteleza na akatenda dhambi kwa kuwa hilo ndilo umbile lake. Lakini umbile si tu kutenda dhambi, bali pia ni kukiri kosa na kuomba msamaha, kwa muktadha huo basi, kutenda dhambi kisha usiombe msamaha, jambo hilo halipungui kuwa ni kulikana umbile lako la asili.

Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Masoud-Allah amuwiye radhi-amesema: Ndani ya kitabu cha Allah zimo aya mbili ambazo hizo mja hatendi dhambi, kisha akazisoma na akamuomba Allah msamaha, ila Allah Mtukufu atamsamehe. (Aya mbili hizo ni):

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَنْ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَى مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ١٣٥ [آل عمران: 135]

{Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Allah na wakamuomba msamaha kwa dhambi zao – na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Allah? – Na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua}”.Aali Imraan [03]:135

Na kauli yake Yeye aliye Mtukufu:

وَمَنْ يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّهَ يَجِدِ اللَّهَ غَفُورًا رَحِيمًا١١٠ [النساء: 110]

{Na anaye tenda uovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akaomba maghufira kwa Allah, atamkuta Allah ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu}”. An-nisaa [04]:110

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Atakaye leta Istighfari (omba msamaha) kwa wingi, Allah Mtukufu atampa faraja kwa kila huzuni (itakayo msibu), na kwa kila dhiki (atampa) njia ya kutokea na atamruzuku kwa namna asiyo itazamia”.

Na Allah Mtukufu amesema katika kubainisha ubora wa Istighfaari na tumsikilize: “Nikasema: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe. Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo. Na atakupeni mali na wana, na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito”. Nuuh [71]:10-12

Naam, ndugu mfungaji-Allah akurehemu-tuendelee na ufafanuzi mdogo wa yale mambo manne ambayo Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ametutolea wito wa kuyakithirisha ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kupitia hadithi yake ambayo tumeinukuu mwanzoni mwa jukwaa hili. Tayari tumekwisha yaona yale mawili ya mwanzo ambayo tukiyafanya tutakuwa tumemridhisha Mola wetu Mlezi. Sasa kwa auni na uwezeshi wake Allah tuanze kuyatolea ufafanuzi mambo mawili ya mwisho, ambayo sisi hatuna ukwasi nayo, tunayahitajia mno. Tunasema:

Na ama mambo mawili ambayo hatuna budi nayo, ni sisi kumuomba Allah pepo yake na atukinge na adhabu ya moto wa Jahannamu; kila mmoja kati yetu anataka kuingia peponi na wala hakuna anaye taka kutiwa motoni. Ndio maana Mtume wa Allah akasema hatujikwasii na mambo hayo, lazima tunayahitajia. Hili la kumuomba Allah ndani ya Ramadhani au nje yake, kumuomba akupe au kumuomba akukinge na jambo/kitu fulani. Hilo ni amri yake Mola na kwa kuwa ni amri itokayo kwake basi bila ya chembe ya shaka kuomba dua ni ibada na kuacha kuomba ni madhambi na wala hakupungui kuwa ni kumuambia Allah kwa ulimi wa hali mimi sina shida kwako kwa chochote. Na kusema hivyo ni ujeuri na kiburi kwa Muumba. Hivi ndivyo anavyo sema Allah kuhusiana na kumuomba katika mlolongo wa aya zinazo itaja ibada ya swaumu ya Ramadhani: “Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitika (najibu) maombi (dua) ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka”. Al-Baqarah [02]:186

Na akasema Yeye Mwenye enzi na utukufu: “Na Allah hakuwa wa kuwaadhibu nawe umo pamoja nao, wala Allah si wa kuwaadhibu na hali ya kuwa wanaomba msamaha”. Al-Anfaali [08]:33

Ndugu mfungaji-Allah akurehemu-elewa ya kwamba katika kuupokea mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hupokea rehema nyingi za Allah ambazo hizo ndizo huwa sababu ya pepo kufunguka kwao. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Inapo ingia Ramadhani, hufunguka milango ya pepo na hufungwa milango ya moto na mashetani hutiwa pingu”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Sote kwa pamoja kama waumini tunapaswa kujua na kuelewa thamani ya msimu huu wa kiroho ambao ndani yake Allah husamehe madhambi na huwapandisha daraja waja wake mbele zake. Kwani ni kwa kuitambua tu thamani yake ndio tunaweza kunufaika na msimu huo wa kheri. Hebu tuione thamani ya msimu huo wa kiroho kupitia Hadithi hii ya Bwana Mtume, haya na tusome huku tukizingatia kila sentesi. Imepokewa kutoka kwa Ka’ab bin Ujrah-Allah amuwiye radhi-amesema: Alisema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Nileteeni mimbari, tukampelekea. Basi alipo panda kidato (cha kwanza) akaitikia: Aamin! Na alipo panda kidato cha pili, (pia) akaitikia: Aamin! Na (hata) alipo panda kidato cha tatu, (hali kadhalika) aliitikia: Aamin! Alipo teremka, tukamwambia: Ewe Mtume wa Allah! Leo tumesikia kwako kitu ambacho hatukuwa tukikisikia (huko nyuma). Akasema: Hakika Jibrilu-Amani imshukie-alinitokea akasema: Awekwe mbali (na rehema za Allah) yule aliye idiriki Ramadhani na asisamehewe dhambi, nikaitikia: Aamin! Na nilipo panda cha pili, akasema: Awekwe mbali (na rehema za Allah) yule uliye tajwa mbele yake na asikuswalie, nikaitikia: Aamin! Na nilipo panda kile cha tatu, akasema: Awekwe mbali (na rehema za Allah) yule aliye wadiriki wazazi wake watu wazima au mmoja wao, wasiwe sababu ya kumuingiza peponi, nikaitikia: Aamin!”. Al-Haakim-Allah amrehemu.

Ndugu mfungaji-Allah akurehemu-tukubali kwamba ni mpango na matashi yake Allah kuuteua na kuuchagua mwezi wa Ramadhani miongoni mwa miezi ya mwaka kwa hekima anazo zijua Yeye Mwenyewe, akaufanya kuwa ni bora na akatia ndani yake fursa bora kwa muumini. Ni kwa mpango huo huo na kwa hekima zake tukufu, akayapa ubora baadhi ya maeneo juu ya maeneo mengine na akazifanya nyoyo za watu ziyaelekee, ziyapende, ziyathamini na kuyatamani maeneo hayo. Na kwa muktadha huo basi, Allah aliye Mtukufu akaifanya nyumba ya awali waliyo wekewa watu kwa ajili ya ibada kuwa katika mji mtukufu wa Makka kama anavyo lielezea hilo Yeye Mwenyewe: “Hakika nyumba ya kwanza waliyo wekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka, iliyo barikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote”. Aali Imraan [03]:96

Kama ambavyo kwa mpango na utaratibu huo huo, Allah Mtukufu alivyo wateua Mitume watoa khabari njema na zile za khofu kuongoza umma mbali mbali tena akawateua mitume hao katika wanaadamu na Malaika na akawafanya bora baadhi ya mitume juu ya mitume wengine, tusome sote: “Mitume hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao Allah alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo…”. Al-Baqarah [02]:253

Na akawafanya bora baadhi ya watu juu ya wenziwao na wengine akawapa daraja kubwa, akasema Yeye aliye Mtukufu: “Na Yeye ndiye aliye kufanyeni makhalifa wa duniani, na amewanyanyua baadhi yenu juu ya wengine daraja kubwa kubwa…”. Al-An’aam [06]:165

Ni kama hivyo ndivyo Allah alivyo ufanya mwezi wa Ramadhani kuwa bora juu ya miezi mingine ya mwaka, kama alivyo sema Allah Mtukufu: “Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi atakaye kuwa mjini katika mwezi huu na afunge…”. Al-Baqarah [02]:185

Kwa hivyo basi, Ramadhani ni mwezi ambao Allah ameukhusisha na kushuka ndani yake neema ya kimungu iliyo tukufu kuliko zote, nayo si nyingine ila ni neema ya kuteremshwa Qur’ani. Si hivyo tu, bali huo ni mwezi ambao Allah ameukhusisha na ibada ya funga; haipatikani ibada hiyo ila ndani ya mwezi huo tu. Na akaifanya funga yake hiyo kuwa ni katika jumla ya faradhi na nguzo za Uislamu. Na Waislamu huupokea mwezi wa Ramadhani huku wakiwa na kumbukizi njema za neema hiyo ya Kimungu waliyo shushiwa ndani ya mwezi huo. Neema ambayo imeshushwa ili kuiletea mafanikio jamii ya wanaadamu kwa kuitoa kwenye viza vya ushirikina kuileta kwenye nuru ya Uislamu. Na pia kuitangaza nuru ya uwongofu ya mbinguni na kueneza haki, kheri, mafanikio, elimu na maarifa tangu pale wahyi ulipo anza kushuka kwenye moyo wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa zile aya za awali kabisa: “Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba. Amemuumba binaadamu kwa tone la damu. Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui”. Al-Alaq [96]:01-05

Mpendwa mfungaji-Allah akurehemu-katika kulihitimisha jukwaa letu juma hili, ni vema tusisahau ya kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhani umebeba kumbukumbu za rohoni zenye maono ya kiMngu katika ushindi na nusra ya mwanzo ambayo Allah aliwapa Waislamu katika vile vita vya Badri. Na si hivyo tu, mwezi wa Ramadhani umekhushishwa kuwa na usiku ulio mtukufu; usiku wa cheo “Lailatul-Qadri”. Usiku ambao Allah ameifanya amali inayo tendwa humo, malipo yake kuwa ni bora kuliko amali ya miezi alfu moja inayo tendwa nje ya usiku huo, uliomo ndani ya mwezi wa Ramadhani.

Naam, hakika hayo ni maana na kumbukumbu maono zinazo chochea ndani ya nafsi za Waislamu maana za upendo, furaha na ukunjufu wa nyoyo katika kuupokea mwezi wa Ramadhani kwa nderemo, shangwe, hoi hoi na vifijo. Na maana na kumbukumbu hizo huwaita wataka/watenda kheri na wale wanao taraji kukutana na Allah na nyumba ya Akhera, kujikurubisha kwa ibada na amali njema ndani ya mwezi huo. Ama wale watenda maasi, huwaita kutubia kwa Mola wao Mlezi kwa makosa na madhambi waliyo yatenda nje ya Ramadhani. Kuanzia awali ya jukwaa letu hili mpaka hapa tunapo komea, tufahamu ya kwamba mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa rehema, ni wingu la msamaha kwenye jangwa la madhambi, ni fursa ya kuachwa huru na moto. Mwezi wa Ramadhani ni muombezi wako kaburini na mbele ya Mola wako, ni muongoza njia ya peponi, ni funguo yako ya pepo ya Rayyaani.

Tenda amali njema ndani ya Ramadhani zikufae mwenyewe leo na kesho na wala usiwasahau wale waliomo makaburini ambao hawawezi tenda kutenda lakini tumaini lao ni wewe uliye hai. Wakumbuke walio kwisha kutangulia kwa kuwaombea Mungu, kuwapa hidaya thawabu za Qur’ani unayo isoma ndani ya mwezi huu mtukufu, kwa kuwatakia maghufira na kuwatolea sadaka. Ukamilifu ni wake Mola Muumba ikiwa mmenufaika na jukwaa la leo, na mapungufu ni yetu sisi waja kwa kushindwa kufikisha ujumbe wake.

Tuombe kwa unyenyekevu: Ewe Mola wa haki! Mrehemu na umsamehe kila ambaye tulikuwa naye katika Ramadhani ya mwaka jana, na Ramadhani hii hatunaye tena, yuko mbele yako akiwa muhitaji mno wa rehema zako. Mrehemu na umsamehe kila ambaye aliye pata kufunga swaumu ya Ramadhani mahala popote pale ulimwenguni. Mtakabalie kila mtenda kheri ndani ya mwezi huu na Ramadhani zilizo pita. Ijaalie Ramadhani hii kuwa ni sababu ya nusura na ushindi popote pale wanapo teswa na kudhulumiwa Waislamu duniani. Waondoshee Waislamu wote dhiki, taabu, shida, maradhi na mizozo na mahala pake ijaze faraja, raha, siha, utangamano na amani. Yaa Allah tutakabalie dua yetu!

Panapo majaaliwa yake Allah tukutane juma lijalo, hapa hapa katika jukwaa letu la Ramadhani ya mwaka 1442H/2021

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *